
Uhalisia, Sanaa Faafu na Nadharia ya Usasa-baadaye
Swala jingine muhimu linaloibuliwa na riwaya zilizoteuliwa katika makala hii ni mazingatio ya kile tunachoweza kukitambua kama sanaa stahiki kwa waandishi na hadhira lengwa. Kama nilivyotanguliza hapo awali, riwaya hizi zimesheheni majaribio mengi na kwa namna zilivyoandikwa msomaji huenda akatanzwa na mbinu tata zilizomo za kiuandishi. Waandishi wa riwaya hizi wanaelekea kulitambua hilo na Dunia Yao inazamia mjadala huu wa sanaa faafu dhidi ya ile iliyopitwa na wakati, hasa kwa kuzingatia kipindi mahsusi cha kihistoria na mbinu sadifu za kuwasilishia sanaa. Kama tapo la kiuandishi, uhalisia umekuwa na uzuri wake ingawa kile kilichoonekana kitu adimu ndani ya uhalisia kimeanza kutiliwa shaka. Ndi- katika Dunia Yao anadokeza hivi: Alisita hapo. Nilifahamu amekusudia nini. Wakati wa sanaa ya uhalisia nilijua umeshapita. Kwa kweli wakati ule nilipoanza, nisingeweza kuandika vingine nje ya uhalisia. Kanuni zake zisingekubali. Nani angenichapisha? Nani angenisoma? Jambo moja muhimu lililoshikamana na sanaa wakati ule lilikuwa dukuduku la watu. Tamaa zao za dhahiri. Nusura iliyoonekana iko njiani. Ingefika kesho kama si sasa hivi. (Mohamed 2006: 71) Kama mhusika, Ndi- anaona kwamba yeye pia amekuwa katika hali ya mpito. Uhalisia aliouenzi sasa hauna nafasi kwake kwa kuwa wasomaji sasa wako tayari kuzipokea kazi zake za kimajaribio. Hapo awali, hakuwa na budi ila kutunga kazi za kihalisia na anazo sababu zake za kufanya hivyo kama inavyoelezwa katika majadiliano haya ya Ndi- na Bi Muse. Jambo la kwanza ni kuwa wasomaji wenyewe walikuwa na matarajio au dukuduku lao kuhusu kazi za fasihi ambazo walitarajiwa ziandikwe kwa mtindo huo wa kihalisia. Pili, wachapishaji nao hawangethubutu kuchapisha kazi za kimajaribio kwa kuwa wanunuzi hawangeziona za manufaa kwao. Hivyo mwandishi wa wakati huo hangekuwa na hiari ya kiuandishi ila kuwatii wachapishaji ambao waliongozwa zaidi na faida inayotokana na mauzo yao kuliko ujasiri wa kisanii wa mwandishi. Swala hili la kuthaminiwa kwa fedha kuliko waandishi limezungumziwa pia katika Musaleo! kama tatizo mojawapo linaloathiri kutolewa kwa sanaa nzuri, tena faafu. Sanaa nzuri, kama inavyoelekea kujadiliwa humo, ni ile RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 58 ambayo itakidhi haja za kibinafsi za waandishi na aila zao. Hususani, Musaleo! inalalamikia namna waandishi wanavyopunjwa na kuchezwa shere na wachapishaji. Zamda, mkewe Kingunge, analalamika jinsi mumewe anavyotumia muda wake mwingi kuandika riwaya huku akikosa namna za kuikimu familia yake. Zamda anasema: Sasa huu uandishi nao naona umekuwa kama kufungukwa na uganga. Heri siku zilizopita na hata kulipa haulipi huu! Uandishi! Uandishi! Uandishi wa nini? (Wamitila 2004: 12) Ndi- katika Dunia Yao anaelekea kupendelea fani ya usasa mamboleo au usasa wa kisasa katika maswala ya uwasilishaji wa kazi za sanaa. Sanaa, kwa mujibu wa mhusika huyu, huenda na wakati na mahitaji ya mwanadamu. Na hapo anaeleza kwa nini uhalisia ulifaa katika kipindi fulani cha uandishi kuliko uandishi wa aina yoyote na ilipodhihiri kwamba uhalisia haungeweza kushughulikia dhamira za kisasa, basi ilibidi nao utupiliwe mbali kama kinavyotarajia kipindi cha hivi leo. Ndi- anasema: “Hii ni bustani iliyopitwa na wakati,” nilimsikia akisema hatimaye, “inafanana na mantiki ya mambo ya miaka ile iliyopita. Ni bustani ya ukame na kifo. Ni ukaukivu wa mambo unaoashiria ufu wa bongo lako lisiloweza tena kusimulia kwa mantiki. Hakuna tena mantiki. Hakuna tena umajimaji wa ubichi wa mambo. Uhai haupo tena mbali na kifo, na kwa hivyo hauwezi kuwepo ukweli, ukweli. Wigo wa ukweli wa moja kwa moja haudindi tena. Na kusema kweli, tokea mwanzo haukuwepo. Iliyokuwepo ni ndoto. Ndoto ya bustani hai. Kumbe kavu na teketevu namna hii.” (Mohamed 2006: 64) Hapa, Ndi- anaulinganisha uhalisia na kifo cha kiakili, yaani kukosekana kwa ubunifu katika fasihi. Hata kile kilichothaminiwa kuwa uhalisia kiliishi katika njozi za watu na kamwe haukuwa ubunifu kama anavyodai Ndi-. Anachosisitiza Ndi- ni kuwa kuzingatia uhalisia kwa kipindi cha leo ni kuishusha hadhi fasihi. Mawazo sawa na hayo yamezungumziwa pia na Kingunge katika Musaleo! pale anapokutana na mhariri wake ili wazungumzie maendeleo ya mswada wa hadithi yake. Mhariri anabishana juu ya mwelekeo mpya aliouchukua Kingunge kwa kusema: “Wasomaji wako watalalamika sana mara hii. Mbona usitumie mtindo rahisi ambao wanaufahamu: unajua watu hawapendi mabadiliko bali huyapenda mazoea na ukale...” alilalamika mhariri. “Na hilo ndilo kosa kubwa. Maendeleo hayamo katika ukale!” (Wamitila 2004: 41) Sawa na anavyodai Ndi- wa Dunia Yao, katika Musaleo! naye mhusika Kingunge anayaona maendeleo yakiwemo katika kuhimiza kuwepo kwa majaribio katika uandishi na wala sio katika kuwa wahafidhina. Lakini je, sanaa mamboleo inayopendelewa na riwaya hizi ni ipi? ISSA MWAMZANDI 59 Waonavyo waandishi hawa wa kimajaribio uhalisia umepitwa na wakati na wamehoji kuwa sanaa kamwe haiwezi kuwekewa mipaka. Mintarafu ya riwaya hizi, sanaa nzuri ni ile itakayojumuisha mbinu za kuelezea dunia ya sasa iliyojaa miujiza na mambo mengi ambayo hayawezi kueleweka kwa njia iliyo rahisi. Uzuri wa sanaa kwao si kuyaeleza mambo yalivyo kihalisia na, chambilecho Dunia Yao, “kuzipata maana kibungabunga” (Mohamed 2006: 9). Msomaji sharti ashiriki kikamilifu katika kuzipekua maana za kazi anazozisoma na kukubali kuzugwa pale inapobidi. Sanaa nzuri kwao ni ile itakayomlazimisha msomaji kusaili ishara tofauti tofauti atakazotumia mwandishi na kisha kuzihusisha ishara hizo na muktadha wa maisha yake halisi. Hatimaye, ufaafu wa sanaa huamuliwa na namna itakavyomtumikia yule anayelengwa. Haya ndiyo mawazo makuu yanayoendelezwa katika sura yote ya tano ya Dunia Yao. Katika Musaleo! naye mhusika Kingunge anayakubali mawazo haya anaposema: “Siandiki? Naandika sana. Tena mara hii riwaya ya kisawasawa itakayojisoma yenyewe pamoja na kuyasoma maisha yetu. Naandika riwaya itakayojihakiki yenyewe!” (Wamitila 2004: 10) Kingunge, kama inavyodhihirika hapa, anashadidia wazo kuwa kitendo cha uandishi huvuka mawanda ya matini kwa kuhakiki mchakatowenyewe wa uandishi. Katika muktadha huu, riwaya za kisasa zinamaizi hali hiyo na kuhimiza wingimatini uliomo duniani – jambo ambalo wasomaji hawana budi kuliafiki na kulikubali kama dira inayochukuliwa na fasihi ya kisasa ya Kiswahili. Baada ya kuzungumzia uhalisia na ufaafu wake wa kukidhi matakwa ya binadamu, riwaya teule pia zinafafanua viunzi vilivyotumika kuzijenga. Riwaya za kisasa, kama inavyopendekezwa, zimejengwa na vipande vya ngano au simulizi fupi fupi zisizokuwa na uaushi, tofauti na simulizi kuu ambazo aliziona kama zilizopoteza uthabiti wake (Lyotard 1984: 37). Simulizi hizi hutokeza kwa muda mfupi ndani ya riwaya na hazilengi kuhodhi ukweli kama zilivyo simulizi za jadi ambazo zililenga kukongomea ukweli kama zilivyouona. Lyotard, kwa mfano, amenukuliwa na Barry (2002: 86) akisema kuwa simulizi kuu hubuniwa kwa azma ya kusawazisha ukinzani na kusababisha urajua ambao kwa hakika hauna mashiko. Mtazamo sawa na huu unachukuliwa na riwaya teule kutokana na kile anachokirejelea Baudrillard (1983: 142-156) kama “kupotea kwa uhalisi” ambapo mpaka kati ya uhalisi na kinachodhaniwa kuwa maana yake haupo. Anachodhamiria Baudrillard (ibid) ni kuwa viashiria vimepoteza uwezo wake wa uashiriaji na kwa sababu hiyo, uhalisi haurejelei chochote kilicho nje ya kiashiria bali kiashiria hutuelekeza katika viashiria vinginevyo. Maana, hivyo basi, hubakia ikiselea kutokana na wingi wa viashiria. Hii ndiyo sababu riwaya za usasa-baadaye zikakosa muungano na muumano wa hadithi tangu mwanzo hadi mwisho ingawa huo unakuwa msingi wa kuchachawiza hadithi yenyewe inayosimuliwa. Katika Musaleo! inadaiwa kwamba sanaa ya siku hizi imefanana sana na uhalisia wenyewe wa maisha na waandishi wanafuata mkondo tu wa uhalisi huo. Mawazo haya yanachukuana RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 60 na yale ya Baudrillard, anayedai kwamba mahala pa uhalisi wa siku hizi umechukuliwa na mbinu za uashiriaji au uwasilishaji wa ukweli huo (1983: 142-156). Mjadala wa Kingunge na mhariri unafafanua zaidi uhusiano kati ya uhalisia wa maisha na sanaa sadifu ya kuuzungumzia: “[...] Uhalisi wa siku hizi umevunjikavunjika hauna pa kujishikiza; hauna mshikamano imara. Hakuna njia nyingine ya kuukabili isipokuwa kwa mtindo wa uhalisi wenyewe; hujasikia mjinga hunyolewa jinsi anavyojipaka maji? Lazima tudadisidadisi kila kitu: siasa, uchumi, mapenzi hata miundo ya hadithi pamoja na hata lugha yenyewe. Hii sio dunia ya kuridhika na tulichozoea,” alisema Kingunge. (Wamitila 2004: 41) Msimulizi katika Dunia Yaoanazungumzia hili pia: Katika simulizi na mapito yake, vipandevipande – si lazima vishikane. Unavimwaga tu vipande vyenyewe kama unaatika mbegu kwenye shamba la sanaa. Unafanya hivyo kuwaacha wasomaji waunge wenyewe vipande vya maana zao, huku maneno mengine ukiyajengea vivuli ili kuwategea makusudi watafute maana zao badala ya kuzipata maana kibungabunga. (Mohamed 2006: 9) Kwa kuwa muda wa kimajaribio umefika na kazi zenye sifa hizo kukubalika na kuchapishwa, basi msimulizi katika Dunia Yao anaeleza kile kinachokuwa kiungo muhimu cha kazi kama hizi: Naam, nilikiri. Hii ndiyo itakuwa simulizi yangu mpya katika mchanganyondimi. Kipande hapa…kipande pale. Vipande vya ‘allegory’. Vipandevipande vya ngano mpya. Ngano ya tafrani-za-kileo katika usogori mpya. Aaaaa, ikiwa zamani sikukujua Bi Muse, sasa nakuhitaji mara milioni moja. Nataka niwe nawe pachapacha. Nikukumbatie unikumbatie, unikoleze ilhamu, nilimwambia. (Ivi: 68) Huu ni mdokezo unaotolewa na riwaya kuhusu kile kitakachopatikana humu. Tunatanabahishwa kuwa riwaya hii itakuwa ni mchanganyiko wa simulizi za kila aina na wingimatini wa “kipande hapa…kipande pale” (ibid.). Kwa yakini, hii ni sifa inayojitokeza katika riwaya zote tatu ambazo zimenakili kazi mbalimbali za waandishi tofauti tofauti. Mimi/Wengine, Kitovu/Pembezoni: Mazingatio ya Nadharia ya Ukoloni-baadaye Kipindi mahsusi cha kustawi kwa nadharia ya ukoloni-baadayeni katika mwaka wa 1978 baada ya Edward Said kuchapisha kitabu chake cha Orientalism (Said 1978). Nadharia yenyewe inajihusisha na mambo mawili makuu yaani ukoloni-baadaye wenyewe na kazi za kisanaa zinazouhusu. Riwaya teule zinazoshughulikiwa na makala hii zimezingatia mambo yote haya mawili kwa njia tofauti. Musaleo! inagusia mada muhimu ya Said iliyomo katika Orientalism. Riwaya inazunguzmia dhana za ‘mimi’ na ‘wengine’ – mbeya mbili muhimu zinazotofautisha Umagharibi na Umashariki. Umagharibi ulihusu nchi za Ulaya na Marekani ambazo zilihusishwa na ustaarabu pamoja na maendeleo makubwa katika nyanja zote huku Umashariki ukinasibishwa na nchi zilizokuwa na umasikini uliokithiri, maendeleo duni na ushenzi. Kile ambacho Said alikirejelea kama Orient (‘WENGINE’ katika Musaleo!) na kilicholengwa na watu wa Ulaya Magharibi kilijumuisha nchi za Mashariki ya Kati pamoja na zile za watu lugha za Kisemitiki pamoja na mataifa ya Asia Kusini. ISSA MWAMZANDI 61 Mataifa haya, na hasa yale ya Uarabuni ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ndiyo yaliyobeuliwa na kuonekana kama yenye dosari mbele ya macho ya wazungu wa Ulaya Magharibi (Said 1978: 99). Umagharibi nao ulichukuliwa kama kitovu cha ustaarabu na maendeleo ya kisayansi na kijamii. Hiyo ndiyo misingi anayoitumia mhusika Ukolongwe katika Musaleo! katika kujitofautisha na wanajamii: “Sasa kuanzia leo, na wala si kuanzia leo ni tangu zama na azali, kuna MIMI na WENGINE tu. Mimi ndimi msingi wa kila kitu. Mimi sio kama nyie!” (inasemwa alikuwa na rangi nyepesi na nywele zake zilikuwa mbuyembuye, ambazo hazikuiva) [...] Alisema mengi lakini kufupisha habari kadai rangi yake ilikuwa bora na iliashiria ubora wa akili. Ukolongwe alishikilia kuwa kauli zake ziliwekewa misingi imara na Sayansi [sic]. Inasemekana siku moja alitokeza hadharani huku ameshikilia kitabu kimoja kiitwacho The Wild Man’s Pedigree. Humo aliwasomea watu sehemu fulani aliyodai kuwa ilizieleza sifa zao. “Weusi: wasiochangamka, watulivu, wenye pua pana, wajanja, wazembe na wanaotawaliwa na ugeugeu!” Ajabu ni kwamba mwenyewe alikuwa na sifa hiyo hiyo ya kubadilikabadilika kama kinyonga. (Wamitila 2004: 26f; herufi za mlazo hivyo hivyo katika matini ya awali) Kinachohadithiwa katika riwaya ya Kingunge ni juhudi za wakoloni za kukuza uwingine kupitia maumbile kama vile rangi na nywele. Aidha, madai ya wakoloni kuwa wao ni bora yanajitokeza pia katika maandiko yao wanayoyaenzi kama vile The Wild Man’s Pedigree ambamo wanaendeleza propaganda kwamba wao ni bora kuliko wanajamii wengine. Humo, twapata Waafrika wakifafanuliwa kama wenye sifa hasi za uzembe, ujanja, kutokuwa na msimamo na hata walioumbuka kimaumbile kama inavyoashiriwa na pua zao pana. Kwa upande wao, wakoloni wanajiona kama wenye rangi bora inayoashiria akili iliyopevuka, waliostaarabika na wanaofuata maadili ya kisayansi. Pamoja na kutambua hila za wakoloni, Musaleo! inajusurisha kubainisha mbinu mbalimbali zilizotumiwa na wakoloni katika kuwatawala wenyeji Waafrika. Ukolongwe, mhusika mkuu wa riwaya ya Kingunge, kwa mfano, anapiga marufuku kile alichoshindwa kukifahamu na ambacho wenyeji walikifahamu. Pia aliamrisha watoto wafunzwe nyimbo mpya, tofauti na zile walizoziimba hapo awali. Vilevile, tunaelezwa namna alivyoiteka nyara lugha na kubadilisha maana za maneno kiasi kwamba pale panapozungumziwa ‘uhuru’ au ‘uzalendo’ wenyeji walisikia badala yake ‘kufuru’ na ‘uvundo’ mtawalia (Ivi: 26). Kwa utaratibu huo Musaleo!, kupitia kwa riwaya ya Kingunge, inaingia katika hatua ya utekelezaji wa nadharia ya ukoloni-baadaye kwa kuzingatia namna fasihi ya ukoloni-baadaye inavyoweza kuweka upenuni kwa uwazi au kwa mafumbo hila na hilaki wanazotumia watawala kwa watawaliwa (Tyson 2006: 431). Musaleo! ni zoezi la kina la uchanganuzi wa njama, hulka na athari za ukoloni mkongwe pamoja na ukoloni mamboleo wa viongozi wa zama za leo. Riwaya hii ina zoezi maalum la utekelezaji wa uhakiki wa nadharia ya ukoloni-baadaye. Humu, ukoloni mamboleo unawakilishwa na kina ‘Musaleo’ wa siku hizi, yaani viongozi, wanaotumia njama za kila aina za kuwakandamiza wale RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 62 waliowapa madaraka. Hapa na pale, riwaya hii inazungumzia kwa mafumbo namna nchi za Kimagharibi zinavyowazuga wale walioko pembezoni kama inavyobainishwa na kile kisa cha “ardhi kuwa pande kubwa lililovunjika na kuwa Godi-Wana na Huraa-Asi na mengine madogo madogo mpaka yakafikia matano” (Wamitila 2004: 89). Katika kisa hiki, kunatajwa sumaku inayozivuta ardhi mahala pamoja na yule buibui aliyesakini pale kwenye kiini ambaye aliwala nzi waliozongwa na utandu – sitiari ambazo zinafafanua mahusiano hayo ya kitovu (wenye nguvu, wakoloni au mataifa ya ulimwengu wa kwanza) dhidi ya pembezoni (wanyonge, watawaliwa au mataifa ya ‘ulimwengu wa tatu’). Nadharia ya ukoloni-baadaye haiishii katika kumlaumu mkandamizaji kama anavyodhihirisha Said katika kitabu chake Culture and Imperialism (Said 1993). Anatambua kuwa ingawa nchi za Asia, Afrika na Amerika ya Kilatini zina uhuru wa kisiasa bado zinatawaliwa na kutegemea nchi za Kizungu (Said 1993: 20). Pamoja na ukweli huo, Said anaona kwamba haifai kuzimwagia nchi za Kimagharibi lawama kwa kuwa nchi hizo zinastahili kujilaumu zenyewe kwa kutoichanganua vyema mifumo adili ya kuleta mageuzi ya dhati ya kisiasa na kitamaduni katika jamii (Said 1993: 277). Ni hapa ambapo viongozi walioshika hatamu za utawala baada ya kuondoka kwa wakoloni wakongwe waliendeleza na bado wanaendeleza uongozi wa kiimla na kuwanyanyasa wananchi wenzao. Kulingana na Said hali ilivyo baada ya ukoloni wa Kimagharibi ni aina ya mduara wa kibeberu unaoturejesha katika hali iliyokuwa wakati wa mkoloni. Bado kuna tamaa za kichoyo ambapo watu wanataka kujinufaisha kibinafsi na kuwabagua wenzao kidini, kirangi na kikabila (Said 1993: 275-276). Na hapa ndipo Nana katika Nyuso za Mwanamke anavyotaka watu waangazie kitovu na pembezoni kama chanzo cha uovu uliosakini duniani: Sikubaliani nao wanaotilia mkazo kitovu cha duara. Nguvu tunazoambiwa zimeumbwa makusudi ili wanaoishi pembezoni lazima wavutwe ndani kusujudia kitovu. Nionavyo mimi, lazima ukingo wa duara uvunjwe ili viliyomo ndani vimiminike nje na vya nje viweze kupenya ndani kutafiti kilicho ndani na kitovu chenyewe kinachotoa fikra mbaya na ovu. Bila ya hivyo walioko pembezoni maisha watajikuta wako pembezoni – wamezugwa kabisa na maneno ya kukuza njugu maganda. (Mohamed 2010: 60) Anavyoona Nana, swala la kitovu na pembezoni ni fikra potofu iliyomo vichwani mwa watu na kwa sababu hiyo wakati umefika wa kila mtu kujituma ili kuifanya dunia kuwa mahala bora badala ya kuishi kwa visingizio vya ukoloni na athari zake mbaya. Anima na Mamanchi wa Musaleo!:Wahusika katika Saikolojia Changanuzi Musaleo! imetumia mawazo ya mwanasaikolojia Carl Gustav Jung2 hasa katika ujenzi wake wa wahusika Anima na Mamanchi. Kimsingi, Jung alidai kwamba kila binadamu, awe mke au mume, 2 Carl Gustav Jung (1895-1961) ni mwanafunzi wa Sigmund Freud na kwa mujibu wa Wamitila (2003: 298) ni mwanasaikolojia anayefahamika kwa kuendeleza dhana ya ‘ung’amuzi jumuishi’ ambayo aliitumia kuelezea sehemu ya akili ya binadamu ambayo hurithiwa na kufanana kwa kila binadamu. Sehemu hii, anavyoeleza Wamitila, ndiyo ISSA MWAMZANDI 63 huwa amebeba chembechembe za hulka za jinsia tofauti na yake. Hivyo ni kusema kwamba mwanamume huwa na sifa za kike zilizofichika katika ung’amuzibwete wake na aghalabu sifa hizo hujitokeza katika umbo la msichana bikira au mwanamke mwenye sifa za kiungu na ambaye hufahamika kama Anima. Vivyo hivyo, mwanamke naye huhodhi sifa za kiume katika ung’amuzibwete wake na hudhihirika katika umbo la kikongwe mwenye busara aitwaye Animus (Carter 2006: 79). Kudhihirika kwa wahusika hawa huwa katika ndoto na ishara mbalimbali na wanasaikolojia huamini kuwa wahusika hawa huwa njia ya kuimarisha tabia ya mtu binafsi ambayo huwa imeficha mawazo na mitazamo hasi (Schmitz 2007: 200). Mawazo ya Jung yanabainika ndani ya riwaya hasa tunapozingatia uhusika wa Anima na Mamanchi na jinsi wanavyomdhihirikia Mugogo Wehu. Wote wanatokea pale Mugogo anapokunywa sumu aliyotegewa na watu wasiojulikanana kupoteza fahamu nyumbani mwake, ingawa Mugogo mwenyewe alihisi machovu na hivyo kujilaza kitandani (Wamitila 2004: 8). Yote anayoyafanya Mugogo ndani ya hadithi kwa hakika si mambo yakinifu bali yanatokea ndani ya ‘ndoto’ anayoipata katika ‘usingizi’ huu – yakiwemo kukutana kwake kwanza na Anima, na kisha, Mamanchi. Akiwa katika ndoto yake kuu, Mugogo anakutana kisadfa na Anima (Ivi: 28). Kukutana kwao kwa hakika si kwa kisadfa kama anavyodai Mugogo mwenyewe bali ni njiamaalum inayotolewa na riwaya kwa msomaji ya kuona wasiwasi na hofu zilizofichika katika ung’amuzi bwete wa Mugogo. Tangu mwanzoni mwa riwaya, tayari msomaji ameshamuona Mugogo kama mhusika anayeishi maisha yaliyojaa shauku, hofu na wasiwasi mwingi. Kwa mfano, alikuwa na yakini kuwa aliusikia mlio wa bunduki na kushuhudia kishindo cha vijana waliokimbilia huku na huko ili wazinusuru roho zao. Kisha akawaona vijana waliopigwa risasi nje ya nyumba yake ambao wanatoweka kimiujiza (Ivi: 1). Yote haya yanamfanya atoke kwa azma ya kufanya uchunguzi iwapo aliyoyashuhudia ni ya kweli. Anachohadithiwa huko nje ni tofauti na watu wanamdhania kuwa mwehu. Anashauriwa apuuze yasiyomhusu kwani hakuna aliyesikia bunduki anazozungumzia Mugogo (Ivi 6). Anaporudi nyumbani kutoka ulevini, ndipo “anapojipumzisha kitandani” (Ivi: 8) ilhali ukweli ni kuwa makali ya sumu aliyokuwa ametiliwa yalikuwa yamekolea na kumfanya apoteze fahamu. Hapo ndipo riwaya inapomdhihirisha Anima kama mhusika ambaye, katika misingi ya Jung, anajitokeza kamanjia mbadala ya kutufunulia wazi wazihofu na wasiwasi aliokuwa nao Mugogo akilini mwake. Mbali na hayo Anima wa Musaleo!, kama alivyo Anima wa Jung, pia ni mwanamke na Mugogo anaelekea kuathirika naye kimapenzi kama anavyolazimishwa akiri hilo na Mamanchi ambaye awali anajitambulisha kama “siri ya Mashamba ya Mawe” (Ivi: 22): inayohodhi vikale ambavyo hujitokeza kwa njia ya ishara na ndoto. Wahusika wake wa kisaikolojia, Anima na Animus, ni vielelezo vya visakale anavyozungumzia na ambavyo vimo katika ung’amuzi jumuishi wa kila binadamu. RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 64 “Mugogo, unamjua Anima?” Nitakosaje kumjua mtu kama huyu jamani? Alikuwa rafiki yangu wa kike; mwanamke mwenye ujasiri mkubwa na mapenzi yasiyojua kukimwa. (ibid.) Katika safari yake kwenda katika shamba la mawe, Anima anajitokeza tena – wakati huu katika umbo la mhusika Mamanchi. Katika njozi hii ambayo Mugogo anapata ufumbuzi wa mambo mengi kupitia Mamanchi, Anima sasa si msichana tena bali ni mwanamke mkongwe, mwenye busara na anayejua mambo mengi. Aidha, Mamanchi ana sifa za kiungu, sawa na zile zilizozungumziwa na Jung. Mamanchi, kwa mfano, amezaliwa akafa, akazaliwa akafa, na akazaliwa upya (Ivi: 60). Anamfahamisha Mugogo katika ziara yao ya shamba la mawe hila na vituko vinavyotumiwa na kina ‘Ukolongwe’, jina tunaloweza kulichambua kama kifupi cha ‘ukoloni mkongwe’ na kina Musaleo au viongozi wa siku hizi katika kuendeleza utawala wao wa kiimla. Weledi wa mambo alionao Mamanchi kuhusu vitimvi vya wakoloni wakongwe na wakoloni mamboleo unaelekea kumtanza Mugogo. Mapenzi na ufahamu wa Mamanchi kwake unamkumbusha uhusiano maalum aliokuwa nao na Anima kiasi cha kumfanya Mugogo ashuku kuwa Mamanchi na Anima ni mtu mmoja anapouliza: “Mbona sauti yako inafanana na ya mtu ninayemjua?” Mamanchi: Nani? Anima! Mamanchi: Anima ni mimi pia! Mimi naye ni sawa! (Ivi: 86) Kumbe Anima na Mamanchi ni wamoja ingawa wamejitokeza katika maumbo tofauti: Anima akiwa msichana huku Mamanchi akiwa ajuza. Kinachounganisha umbile lao, hata hivyo, ni msaada mkubwa unaotokana na ukweli na uthabiti wao kwa Mugogo Wehu katika kuuelewa ulimwengu unaoelekea kumtanza. Kupitia wahusika hawa, Mugogo anatoa harara zake, shida, hofu na kupata mtazamo wa maisha. Mwishoni anaporejelewa na fahamu zake, tunamwona akiwa kiumbe tofauti na vile alivyokuwa hapo awali ingawa hayo yanadokezwa kwa mafumbo na Msimulizi: Ung’amuzi wa mambo wa Mugogo Wehu umepiga hatua kubwa. Macho ambayo alishindwa kuyafungua jana ameyafungua. Ameweza hata kusema mambo kadha. (Ivi: 100) ‘Kufungua’ na ‘kufunga’ macho kunakorejelewa hapa kunahusiana na kule kuzindukana kwa Mugogo Wehu kutoka lindi la kutofahamu (kupoteza kwake fahamu) ambako kulielekea kumtia woga hadi hali ya matumaini (kufungua macho) kama inavyoashiriwa na uwezo wa ‘kusema mambo kadha’. Hitimisho hili linawafiki uhakiki wa ki-Jung kwa jinsi linavyoagua hofu, wasiwasi na jumla ya mitazamo hasi iliyofichika katika ung’amuzibwete hadi kuleta satua kwa waathiriwa, wakiwemo Mugogo Wehu. Hitimisho Mapitio ya riwaya za Dunia Yao, Nyuso za Mwanamke na Musaleo!yamebainisha wazi kwamba fasihi ni nyenzo mbadala, tena ya kiubunifu, ya kuzizungumzia nadharia za fasihi kwa njia ya ISSA MWAMZANDI 65 ukakamavu zaidi. Uaguzi wa makini wa nadharia za fasihi katika riwaya teule umeziweka kazi hizi katika medani ya kipekee ya kuzungumzia mambo ambayo yangepatikana katika matini mahususi za nadharia za fasihi. Miongoni mwa mambo mengine mengi, riwaya hizi, kwa ustadi, zimeatika mawazo ya wananadharia mbalimbali wa fasihi wakiwemo wanaumaumbo wa Kirusi, wanaumuundo, wanaudenguzi na hata wanasaikolojia changanuzi katika bunilizi za Kiswahili. Wahakiki, walimu na wapenzi wa fasihi wanaweza kuzitumia riwaya husika kama matini za kiziada katika somo la nadharia. Ingawa hivyo, kufana kwa usomaji wa riwaya zenyewe katika muktadha wa makala utamhitajia anayeelekeza somo hili la nadharia awe amesoma matini za kimsingi kuhusu nadharia za fasihi. Uteguzi wa istilahi maalum na maelezo ya kimafumbo yaliyomo ndani ya riwaya teule, kwa mfano, utafana iwapo mhakiki au mwalimu ataweza kubainisha vyanzo vyake kinadharia. Tumeona, mathalani, namna dhana za ‘mimi’ na ‘wengine’ katika Musaleo!na ‘kitovu’ na ‘pembezoni’ katika Nyuso za Mwanamke zinavyopewa maana za kipekee katika nadharia ya ukoloni-baadaye. Ni dhahiri kuwa riwaya hizi zinatangaza hadharani kwamba sanaa haiwezi kukadiriwa katika misingi ya ukale kama ilivyopendekezwa na wanafasihi wakongwe. Dunia Yao na Musaleo! zinaelekea kupendekeza kuwa fasihi faafu na iliyo hai ni ile inayompa msanii uwezo wa kueleza fikra zake kwa njia inayoyafanya mawazo yake yatiririke bila kizuizi chochote. Kwa kufanya hivyo riwaya husika zinasuta ukale unaotumiwa kulemaza fikra huru za waandishi wa kisasa kwa kutishiwa kutochapishiwa kazi zao au kusomwa. Kazi hizi kwa muhtasari zinawanasihi wasomaji wasilemazwe na fikra sawa na hizo ambazo, kwa hakika, ndizo adui wa maendeleo na kukua kwa fasihi. Makala inaafiki msimamo huo na inahimiza uandishi wa aina hii ambao hatimaye hautakuwa mgumu kwa jinsi muda unavyopita. Marejeleo Barry, Peter. 2002. Beginning Theory. Manchester: Manchester University Press. Baudrillard, Jean. 1983. Simulations. New York: Semiotext(e). Bertoncini, Elena. 2006. Globalization Unmasked in Two Kiswahili Novels. Makala ya Kongamano la Kimataifa la Jubilei ya TUKI – 2005, ed. by Seleman S. Sewangi & Joshua S. Madumulla. Dar es Salaam: TUKI, pp. 84-94. Burman, Erica&Magie MacLure. 2005. Deconstruction as a Method of Research. Research Methods in the Social Sciences, ed. by Bridget Somekh & Cathy Lewin. New Delhi: Vistaar Publications, pp. 284-292. Carter, David. 2006. Literary Theory. Reading: Cox & Wyman. Eagleton, Terry. 1996. Literary Theory: an Introduction. Oxford: Blackwell Publishing. RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 66 Habib, Rafey M.A. 2005. A History of Literary Criticism. Malden: Blackwell Publishing Khamis, Said A.M. 2003. Fragmentation, Orality and Magic Realism in Kezilahabi’s Novel “Nagona”. Nordic Journal of African Studies 12(1): 78-91. Khamis, Said A.M. 2008. Nadharia, Ubunifu, Uchambuzi na Taaluma ya Kiswahili. Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika, ed. by Nathan O. Ogechi, Naomi L. Shitemi & K. Inyani Simala. Eldoret: Moi University Press, pp. 3-23. Lyotard, Jean-François. 1984. The Postmodern Condition. A Report on Knowledge. Trans. Geoff Bennington and Brian Massuni. Minneapolis: University of Minnesota Press. Mohamed, Said Ahmed. 2006. Dunia Yao. Nairobi: Oxford University Press. Mohamed, Said Ahmed. 2010. Nyuso za Mwanamke. Nairobi: Longhorn Publishers. Mwamzandi, Issa Y. 2007. Utandawazi na Teknolojia ya Mawasiliano katika Umalenga wa Waswahili: Mfano wa Sitiari za Taarab. Kiswahili na Elimu Nchini Kenya, ed. by Kimani Njogu. Nairobi: Twaweza Communications, pp. 68-82. Mwamzandi, IssaY. 2011. Derridean Thought in Practice: an Examination of the Kiswahili Proverb. Journal of Intra-African Studies 5: 1-14. Said, Edward. 1978. Orientalism. New York: Pantheon Books. Said, Edward. 1993. Culture and Imperialism. London: Chatto and Windus. Schmitz, Thomas A. 2007. Modern LiteraryTheory and Ancient Texts: an Introduction. Malden: Blackwell Publishing. Tilak, Raghukul. 1993. History and Principles of Literary Criticism. New Delhi: Rama Brothers Educational Publishers. Tyson, Lois. 2006. Critical Theory Today. New York: Routledge & Taylor and Francis. Wafula, Richard & Kimani Njogu. 2007. Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation. Waliaula, Ken W. 2010. Uhalisia na Uhalisiamazingaombwe: Mshabaha kati ya Dunia Yao na The Tin Drum. Swahili Forum 17: 143-157. Wamitila, Kyallo W. 2003. Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Books. Wamitila, KyalloW. 2004. Musaleo!. Nairobi: Vide-Muwa
No comments:
Post a Comment