MADA 1 : FASIHI KWA UJUMLA
NADHARIA YA
FASIHI
Nadharia niImani au kanuni
zinazofuatwa na watu Fulani au jamii katika shughuli au jambo Fulani mahsusi.
Nadharia za fasihi ni muongozo au
kanuni zinazofuatwa na wataalamu (wanazuoni) mbalimbali wanapoteua maana halisi
ya fasihi.
Fasihi ni nini?
Fasili/Maana mbalimbali zimetolewa kuhusu dhana ya fasihi,
maana hizo ni kama:-
1. FASIHI NI KIOO CHA JAMII (MAISHA)
Kwa maana kwamba mtu anaweza akajitazama akaona taswira yake
na akajirekebisha . Fasihi hii ina udhaifu kwani kioo hakiwezi kumweleza mtu jambo la kufanya ili hali yake iwe bora zaidi
. Pia si sehemu zote takazojiona kwenye kioo(F.Mkwera , 1978)
2.
FASIHI NI HISI
Fasihi ina maana kuwa lazima pawe na mguso fulani wa
wahusika ndipo aweze kuandika na kueleza jambo fulani,’Sengo na kiango Wanasema “hisi ni kama kuona njaa, baridi,
joto, uchovu pengine kuumwa. Hapa swali la kujiuliza ni kwamba, je fasihi ina
maana moja kati ya hiyo? Uamuzi wa kutenda jambo huja wakati umeguswa. Je hizo
hisia ziko wapi? Je mtu ambaye haguswi sana
moyoni hawezi kuwa mwanafasihi mashuhuri?
Je mwanamuziki ambaye huusifu uzuri wa mwanamke anaguswa moyoni? Je mwandishi
kama Shaban Robert, E. Kazilahabi
wameguswa mara ngapi? Vile vile kivipi waguswe Zaidi ya wengine? (Sengo na Kiango) hivyo bado fasili hii ina
madhaifu
3. FASIHI NI MWAMVULI WA MTU NA JAMII NA UTU NA
MAISHA YA HADHI NA TAADHIMA.
Fasihi hii ina maana
kwamba mwamvuli humkinga mtu katika mvua na jua na fasihi huhifadhi na kukinga
amali za jamii zisiharibike maana hii ni nzuri kwani inasisitiza utunzaji wa
kile kizuri kwa maana kuwa jamii inachambua kuwa makini na kuona amali za jamii
zinazihifadhiwa. Lakini swali la kujiuliza ni kwamba jamii itasaidiwa?
Jamii haitulii kama maji katika mtungi bali hubadilika mara kwa mara kutokana na
nguvu za migongano, hivyo kitu kipya huzaliwa na cha zamani hufa kwasababu
jamii haitulii, hivyo hakuna haja ya kuhifadhi amali za jamii chini ya
mwamvuli. Zipo mila na desturi zilizohifadhiwa na makabila mengi ambazo hazina
nafasi leo. Hali ya mabadiliko ya jamii kutokana na siasa, utawala, uchumi,
elimu, sayansi na teknolojia vyote hivi katika maendeleo vitatoboa mwamvuli na
kuziharibu amali zilizohifadhiwa (Sengo na Kiango 1973)
4.
FASIHI NI SANAA YA UCHAMBUZI WA LUGHA YOYOTE
KADRI INAVYOSEMWA,INAVYOANDIKWA NA KUSOMWA
Hii ni kweli kuwa fasihi lazima itumie lugha kwani lugha
ndicho chombo muhimu kitumiwacho na fasihi na si fasihi tu bali taaluma zote hutumia lugha.Madhaifu/Udhaifu
wa fasihi hii ni kwamba maana hii imejikita katika uchambuzi wa Lugha kana
kwamba hakuna vipengele vingine vinavyochambuliwa katika fasihi zaidi ya lugha
na hii ni sawa na kusema umeme ni waya wa shaba kwa vile umeme umepita kwenye
waya huo.Na hii ni si kweli kwani Hisabati,fizikia au historia si fasihi kwa
vile tu hutumia lugha.
V:FASIHI NI KIELELEZO CHA HISIA ZA MWANDISHI JUU YA MAMBO
YANAYOMWATHIRI YEYE,KIKUNDI AU JAMII NZIMA ANAMWISHI NA KWAMBA LENGO LAKE NI
KUSTAREHESHA AU KUFUNZA WASOMAJI.
Fasihi(maana) hii ni nzuri kwa ujumla lakini mapungufu yake
ni kwamba imemuwekea mwandishi kama chanzo pekee cha uumbaji wa Sanaa na hasa
akili yake pia maana hii imetokana na
falsafa ya kidhaanifu kwa kuhusisha uchambuzi wa mambo katika fikra bila kutazama hali halisi ya maisha ya watu na
vitu.
VI:FASIHI NI CHOMBO CHA UTETEZI WA MASLAHI YA TABAKA MOJA AU JINGINE NA
KWAMBA MWANDISHI NI MTUMISHI WAKE AJIJUAYE AU ASIYEJIJUA ATAKE ASITAKE
MWANDISHI HUYU NA LENGO AU DHAMIRA FULANI ANAYOTAKA KUIONESHA.
Wasomaji wanaweza wakipenda au kuyataka maudhui ya kazi yake
na pengine jamii kufuatana na msimamo juu ya itikadi ya siasa (nap engine amali
za jamii)inayotawala kwa kipindi kile na
jinsi mwandishi anavyoanisha maandishi yake na itikadi hiyo.
Fasihi au maana hii ni nzuri sana kwani kwa kifupi ni kwamba
fasihi ni silaha nyingi zinazotumiwa na tabaka moja kutetea maslahi yake katika
mapambano ya kudumu dhidi ya matabaka mengine.
Hitimisho kwa ufupi fasihi ni taaluma inayotumia Sanaa
maalumu ya lugha.Taaluma hii ni elimu ambayo ndiyo maisha yanayofaa kufuatwa na
jamii katika maendeleo yake kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni.Ni elimu kwa sababu
fasihi huipa jamii maarifa na mbinu za kupambana na mazingira na kuondoa uozo
katika jamii kwa ujumla.
Fasihi hutuelezea uzuri wa maandishi ,maandishi ambayo
huonekana katika mashairi historia za maisha ya watu,tenzi,hadithi za kusisimua
na insha mbalimbali.
CHIMBUKO LA FASIHI NA SANAA.
Kuna mitizamo mikuu miwili ya kiulimwengu inavyotokeza
katika suala la chimbuko la fasihi .Mitazamo hiyo ni ule wa kidhanifu na ule wa
kiyakinifu.
I.MTAZAMO WA KIDHANIFU.
Mtazamo wa
kidhanifu wa misingi yake katika kudhanifu kwa hiyo hufuatana na mtazamo huu
inaaminika kuwa fasihi na Sanaa kwa ujumla kutoka kwa Mungu kwa hiyo mwanasanaa
ikiwa imekwishwapikwa na kuivishwa na Mungu huyo.
Mtazamo wa
namna hii ulijitokeza tangu zamani sana wakati wanafalsafa wa mwanzo wa kigiriki
na kinenzi kama vile Socrafes Plato na Anstolle,walipoanza kuingia katika
ulimwengu wa nadharia ya Sanaa katika uwanja wa nadharia wa fasihi/Sanaa ya
Kiswahili kuna mifano mingi ya wahakiki wa mwanzo waliokuwa na mitazamo sawa
nay a wanafalsafa hao mfano F.Mkwera
insha yake fasihi inadhihirisha uaminifu wake wa mawazo ya kidhanifu kwa
kudai “fasihi ni Sanaa ambayo huanzia kwa muumba humfikia mtu katika
vipengele mbalimbali ni hekima ambayo mtu ameshirikishwa apa kumtambua muumba wake”.
Nkwera ameungwa mkono na wahakiki wengine ambao wanasisitiza
mtazamo huu kwa kusema
“Mtengenezi
ya Sanaa huonekana kuwa ni shughuli ya kiungu yenyekumwiga Mungu ambaye ndiye
msanii wa kwanza”
John Ramadhani pia katika makala yake ya fasihi ya Kiswahili
anasisitiza kuwa.
“Zaidi ya kwamba fasihi ni hisia vile vile kitengo cha mtu cha kubaini
kazi ya Sanaa ni uigaji wa Mungu ambaye ndiye mfalme wa Sanaa zote”.
Mawazo haya ya akina Nkwera,John Ramadhani na wengineo wa
aina hiyo mwangivi tu mawazo yaiyochakaa ambayo yalikwisha kutajwa na
kushughulikiwa na wahakiki wa zamani
tuliowataja kwa msimamo huu wa kidhanifu,Sanaa au fasihi havijifinyangi kwa
jitihada zab akili za mikono ambayo mtu hana uwezo wa kuiona.
Mtazamo huu Zaidi ya kuwa umepotosha maana halisi kwa
kuchanganya Imani na taaluma,pia unajaribu kumtenganisha msanii na jamii yake
unatoa nadharia inayomwinua msanii na kufanya aonekane kuwa mtu wa ajabu aliyekaribu na Mungu kuliko watu
wengine wa kawaida.
Athari za mtazamo huu zinaonekana hata leo hii kwa baadhi ya
wataalamu wa fasihi ya Kiswahili waliojaribu lueleza maana ya ushairi wengi wao
walidai kuwa ushairi ni hekima za ajabu pamoja na mawazo ambayo yana uzito na
kustajabisha kwa hiyo hata washairi wenyewe ni lazima basi wawe na hekima na
mawazo hayo mazito ambayo aghalabu tunayaona wakiyapokea mara kwa mara kutoka kwa Mungu katika beti zao za mwanzo za
mashairi au tenzi zao.Pia tunawaona wacha Mungu hawa wakimshukuru Mungu wao kwa
kuwapa vipaji hivyo ambavyo kuwanyima wengine katika beti za mwisho za mashairi
yao.
MTAZAMO WA KIYAKINIFU
Chanzo cha fasihi kulingana na mtazamo huu si sawa na chanzo
cha binadamu wenyewe.Binadamu na mazingira yake ndio Alfa na Omega ya fasihi.
Iwe kwa kuumbwa au mabadiliko kuanzia chembe hai ambayo
imepitia maendeleo kadha ya mateuzi hata kufikiria mtu binadamu alionishwa na
kazi ili kuyabadili mazingira yake.
Katika harakati zake za kujiendeleza kiuchumi kila mara
alijaribu hiki na kile alichokiona kinafaa alikiendeleza Zaidi na kukidumisha
katika hali hii hadithi(ngano),methali,vitendawili,nyimbo,tenzi(mashairi) n.k
vyote hivyo vilitungwa na kusimuliwa kwa madhumuni ya kufunza,kukosoa,kuadhibu,kuchokoza fikra
na kuliwaza jamii baada ya kazi.
Sanaa hii ilirithishwa toka kizazi hadi kizazi kwa njia ya
masimulizi na binadamu ilivyozidi kujiendeleza kisayansi na kiteknolojia
akahifadhi taaluma hii katika maandishi.Ndiyo sababu tunasema chanzo cha fasihi
ni sawa na chanzo cha binadamu mwenyewe na jinsi binadamu alivyozidi na
atakavyozidi ndiyo taaluma hii ilivyokuwa na kuendelea.
DHIMA YA MWANAFASIHI KATIKA JAMII
Maana ya mwanafasihi/mtunzi wa kazi ya fasihi
Ni mtu yeyote anayejishughulisha na uandishi au utungaji wa
kazi za fasihi yaani fasihi andishi na fasihi simulizi.
DHIMA ZA MWANAFASIHI
1.(a).Kuelimisha jamii,Katika kuelimisha jamii mwanafasihi
huchambua na kuchochea umma kuwafumbua macho,hufichua wazo au uchafu uliomo
katika jamii,wagandamizaji kufichuliwa na wagandamizao hupewa muongozo sahihi
ili waitambue hali yao dhaifu.Mfano”Duka la Kaya”kuchambua na huchochea jamii
ili iweze kupambana na hali mbaya ya maisha.
(b).Kupiga vita kwa hali na mali mazingira yote ya ujinga,maradhi,njaa
na umaskini,Mfano mwandishi wa tamthiliya ya Hawala ya fedha anapambana
na maovu kama vile ujinga na uvivu na Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe anajali na
kupiga vita.
(c).Kukosoa jamii,Mwanafasihi anaikosoa jamii katika vipengele
mbalimbali vya maisha.Mfano riwaya ya “Duka la Kaya”inakosoa hali ugawaji mbaya
wa bidhaa muhimu nchini “Raha karaha na Mashairi ya Chekacheka”mwandishi wa
diwani hizi anaikosoa jamii ya Tanzania kwa mapana kama vile Uongozi
mbaya,kukithiri kwa rushwa n.k.
(d).Kutia hamasa na kumfanya mtu asikate tamaa,Mfano S.Kandoro
anaeleza hamasa ya wananchi waliokuwa wameungana kama “Siafu ili kumtoa nyoka pangoni”.Mwandishi
kwa hamasa amewaita waafrika njooni “au” kwetu ni kwa nini.Hivyo ni wazi kuwa
kazi hizo zinajitahidi kuendeleza mapambano dhidi ya ukoloni mkongwe na mambo
leo.
(e)Mwandisi anadhima kujenga misingi na fikra za usawa na demokrasia
miongoni mwa umma wa wakulima na wafanyakazi,Mwanafasihi huyu
huwatukuza wakulima na wafanyakazi pamoja na amali zao.
(f) Mwanafasihi hueneza mawazo na falsafa za jamii,Kwa mfano
katika shairi na ngonjera za Mathias Mnyapala ametangaza sana siasa ya ujamaa
na kujitegemea kwa kutumia ngonjera za UKUTA 1 & 2 vile vile riwaya kama
vile mfaa na utu,njozi za usiku,ndoto yandaria ,jero si kitu n.k zimetangaza
sana siasa ya ujamaa na kujitegemea hapa nchini Shaban Robert aliwahi kueneza
falsafa juu ya kweli kwa kiasi kikubwa katika mashairi yake.
(g)Mwanafasihi hutoa mwongozo kwa kuikomboa jamii kutoka fikra mbovu za
kugandamizwa,kunyonywa na kuonewa na kujikomboa ili iweze kupata haki na usawa,Mfano
Riwaya ya kiimbila “Ubeberu Utashindwa” na tamthiliya ya E.Mbogo “Tone la
Mwisho” G Husseni “Kinjekitile”
2.Kuburudisha,zipo kazi mbalimbali za fasihi
zinazoburudisha.Msomaji au msikilizaji wa fasihi huburudisha yaani husisimsha
mwili na akili na huvutiwa kihisia na kazi ya fasihi anayeisoma au
kusikiliza.Tabia ya msomaji au msikilizaji huweza kujengwa kutokana na mafunzo
na mifano bora ya matendo ya kuigwa anayoyapata katika fasihi.
3.Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii,Amali za jamii ni
pamoja na mila na desturimtindo wa maisha,Imani historia jiografia,visasili na
visakale ni urithi ya maarifa ya kijadi kwa mfano tiba sayansi ya kilimo,mbinu
za uwindaji,ufundi wa aina zote n.k.Amali hizo huweza kuhifadhiwa na
kuendelezwa na mwanafasihi na hivyo kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Kwa mfano tamthiliya ya Kinjikitile inahifadhi mengi kuhusu
hali ya maisha wakati wa ukoloni wa kidachi,Kurwa na Doto (farsy) ni riwaya
yenye kuhifadhi japo kwa kejeri,mila,desturi na itikadi za jadi za
waunguja,Riwaya ya Bwana Mnyombokero na Bibi Bugonoka Ntuhanalwa na Buliwali
iliyoandikwa na Anicet Kitireza imehifadhi mila,Imani,mtindo wa maisha,ufundi
na taaluma mbalimbali za jadi za wakerewe mengi yaliyoeleza humo siku hizi
hayapatikani popote isipokuwa katika riwaya hiyo vile vile Mzishi wa Baba ana
Radhi(Nkwera) kinaeleza mila na desturi za wapangwa.
Watunzi hasa nyimbo na visasili hukoleza pia shughuli za
kijadi za kiutamaduni kwa mfano Ibada,matambiko,sherehe,katika shughuli za aina
hiyo nyimbo licha ya kuwa kiburudisho hubeba ujumbe wenye kuhusiana na tukio
hilo.
4.Kudumisha na kuendeleza lugha,Kwa kadri lugha inavyotumiwa na
kufinyangwa na watunzi ndivyo inavyokuwa na kupevuka.Maneno mengi yatumiwayo
leo katika lugha mbalimbali yalibuniwa na kuenezwa na watunzi wa
mashairi,riwaya,nyimbo na tamthiliya katika Kiswahili.Mifano mizuri ni maneno
mengi yahusuyo Sanaa ya ushairi(vina, mizani, beti, mishororo, miwala,
tathlitha, takhimisa, tarbia n.k)
Katika adi ya ushairi wa kiswahili inadaiwa kuwa ushairi
ulikua ni ghala ya maneno washairi walitumia maneno magumu au yasiyokuwa ya
kawaida makusudi ili kuyahifadhi ysipotee…….katika tamduni nyingine kazi hiyo
hufanywa na kamusi na vitabu viitwavyo Hazina ya maneno kwa kuwa waswahili
hawakuwa na kamusi kazi ya kuhifadhi maneno ilifanywa na ushairi.
FASIHI NA JAMII
Fasihi ni zao la jamii. Ni zao ambalo ni chombo vilevile chs
jamii hiyo ambayo kinaweza kutumiwa kwa shari au kwa heri. Inaweza kutumiwa kusaidia
kuchonga wanajamii ili wayaangalie mazingira yao kwa udadisi na uchambuzi ili
wayarekebishe. Vile vile inaweza kutumia na tabaka fulani kuwapumbaza au kuwatia
kiwi machoni wanajamii wasiweze kuyaangalia kwa jicho pevu mazingira hayo.
Hivyo wakashindwa kuyaelewa vizuri na hivyo wasifanikiwe kuyapindua machungu
yanayowasakama.
Hivyo fasihi yapaswa kuwa chombo cha uaminifu kwa jamii
yake. Fasihi ya kweli kwa jamiihaina budi kuichambua, kuikosoa, kuielimisha na
kuiongoza jamii, kuondoa unyonge na upotofu wa aina yoyote ambao upo katika
jamii.
Vile vile fasihi inawajibika kuonyesha bila kuogopa udhalimu
wowote uliomo katika jamii na ambao unaendelea kujiimarisha na kutabiri hali
mbaya ya jamiihiyo pia lazima ionyeshe mambo yote mazuri katika jamiina
kuyasisitiza na kuwatia moyo wale wanayotenda ili waendelee kuyatenda na
kueneza uzuri huo kwa wanajamii wote.Fasihi haina budi kupinga aina yoyote ya
upotofu na kufichwa makosa yake katika jamii. Pia inapaswa kushambulia udhaifu
wowote uliomokatika jamii.
Fasihi ni mali ya jamii hivyo inapaswa kuwa mali ya jamii
kweli iweze kuleta maendeleo ambayo jamii hiyo imepanga kuyaleta. Vile vile
watu wanaokwenda kinyume na utaratibu wa jamii fasihi haina budi kuwataja wazi
wazi na kuwakemea bila kuogopa ili waweze kujirekebisha na kushirikiana na wazao katika kuzungusha gurudumu la maendeleo
ya jamii.
Ili fasihi iwe chombo kiaminifu cha jamii hiyo lazima ionye, ikosee, na kurekebisha jamii wale
wanaotenda mambo kinyume na falsafa ya jamii hiyo lazima wakosolewe. Fasihi
iwaseme wazi wazi wale wanaotenda kinyume cha matakwa ya jamii hiyo lazima
wakosolewe. Iwakosoe wale wanaofanya mambo yasiokubalika katika jamii na
inapobidi kulaanina kukemea matendo yote yasiyofuata mwenendo wa jamii
inayohusika.
Msimamo wa mwandishi ndio utakaofanya fasihi yake ambayo kwa
kweli ni fasihi ya jamii. Iwe chombo kiaminifu katika kuyapindua machungu ,
makosa hayo kimsingi kuna misimamo miwili kuhusu fasihi na jamii.Plekhenou (1957)anaitaja misimamo
hiyo:-
i)
Wapo wanaoamini kuwa Sanaa ni chombo kimoja wapokatika
harakati dhidi ya mazingira, msimamo huu unasisitiza kuwa Sanaa
isaidiwe kumsukasuka na kumwamsha mwanadamu ili apambane na mazingira machafu.
Msimamo huu unasisitiza kuwa jamii hapo kwa aili ya mwanasanaa. Mwanasanaa yupo
kwa ajili ya jamii.
ii)
Wapo wanasanaa wanaosisitiza kuwa kufanya Sanaa
kama chombo tu ni kuzalilisha mno. Sanaa si lengo si chombo Plekhenou anasema kwa kuwa watu hawa hudai kuwa
kuifanya sanaa chombo cha kufikia malengo hilo ni maalumu mno ni kuteremsha
hadhi ya Sanaa. Ili fasihi iwe na manufaa katika jamii ni hima iwe chombo
kiaminifu cha jamii hiyo, eti lazima iwe na jukumu la kuielezea, kuichambua,
kuikosoa, kuiongoza jamii katika lengo lake la kuipindua unyonge na uchafu
uliomokatika jamii. Iwe na msimamousiotetereka, usimhofu mtu, usiogope kitu,
itetee haki, ipinge na kufichua makosa yafanyikayo katika jamii, ioneshe
udhaifu wa aina zote katika jamii.
Somoro (1977) katika kusisitiza
hayo yeye alisema “Ni lazima kufahamu kuwa, ujinga wa mtu mmoja ni udhaifu wa
jamii nzima na uathiri kazi ya kila mmoja wetu……makosa ya mtu mmoja huifanya
kazi ya kila mtu kuwa nzitozaidi kuhatarisha malengo yetu na kuidhoofisha jamii
nzima. Waandishi wasione haya kuyataja makosa yanayofanyika katika jami
wanakosolewa nao wasione haya wala chuki bali wafurahi kuwa adui amegunduliwa.
Lunacharsky (1973)baada ya
kukosolewa Sanaa na kuimarika kutokana na kukosolewa huko alisema:-
“Hata kama tumezorotesha mambo
kiasi kikubwa na wakati mwingine kufanya makosa mazito, kizazi chetu
kinajivunia kwa mazito mengi tuliyoyafanya na tuko tayari kukubali hukumu za
vizazi vipya bila hofu….,”
Anasisitiza Lunacharsky hapani muhimu fasihi ipongeze watu kuwa
michango wanayofanya katika jamii, lakini isiogope kuwa hukumu wanaopotosha
jamii. Ni muhimu fasihi ieleweshe umma itusaidie umma kutambua kuwa pengine
maarifa yetu ya jana ni ujinga wa leo.
Katika kusisitiza hiloAblilatif
Abdallah anaeleza kuwa fasihi sharti izingatie na kushughulikia matatizo ya
jamii inayoshughulikia pamoja na yale ya jamii nzima ya binadamu popote walipo.
Fasihi isaidie tabaka la wanaodhuria wanyonge katika jamii yeyote kupambana na
matatizo yao yanayo wakabili.
G. Kazilahabi ameonesha kuwa
fasihi halisiina msingi yake katika jamii. Baadhi ya viini vya fasihi halisi
ni:-
- Kuielewa jamii na mazingira
yake(ya kijiografia na utamaduni).
-Kuelewa matatizo ya jamii
hiyo.
-Kuelewa ngazi za kijamii na
tofauti za kiuchumi(matabaka).
-Kutoa makosa na kuashambulia watu wa ngazi zote bila huruma.
-Kuitazama kwa uangalifu Serikali ya utawala.
Hivyo ili fasihi yetu iwe na manufaa ni muhimu waandishi waandike juu ya
matatizo waliyo na hakika nayo wasishughulikie matatizo yalyo nje ya jamii yetu
na mwandishi anayeandika matatizo ambayo yako nje ya jamii yetu atakua
anaandika nje ya jamii yake.
FASIHI KAMA CHOMBO CHA
UKOMBOZI
Ukombozi ni harakati za jamii yoyote zenye lengo la kuitoa jamii hiyo kwa
nguvu (kwa silaha) au kwa mazungumzo kutoka katika makuchaa ya watumwa
kisiasa,kiuchumi,kimawazo na kiutamaduni.Jamii inaweza kuwa ni ya kitumwa
kisiasa ikiwa haitakuwa na fursa ya kushika hatamu ya uongozi wao na badala
yake ikategemea uongozi kutoka kwa jamii nyingine jamii itaitwa ya kitumwa ,kiuchumi,ikiwa
haitakuwa na haki ya kuendesha njia mbalimbali za uzalishaji mali.Pia jamii
isiyoweza kufikiri na kuamua wala kutokuthamini mawazo yake yenyewe na badala
yake ikawa katika mgawanyiko wa ibada na itikadi za kigeni ni jamii isiyo huru
kimawazo vile vile jamii haitakuwa huru kiutamaduni ikiwa itakosa kuthamini
aminifu,uumbaji na ugunduzi wake yenyewe badala yake ikasujudu amali zilizo na
chimbuko kutoka nje.
Nyanja za ukombozi wa jinsi fasihi ya Kiswahili ilivyozitazama mpaka leo
(a)Kisiasa
Ukombozi wa kisiasa unapatikanaje?
Unapatikana tu baada ya kupiania uhuru wa bendera kuwa ndio wa kwanza
kupatikana kwa nchi ambayo iko katika harakati za kujikomboa katika maandishi
ya mengi fasihi ukweli huu unajitokeza kwa mfano katika utenzi wa uhuru wa
kwenya msanii anatuonyesha juu ya vita
vya kumngoa mkoloni kutoka katika kiti cha uongozi kwanza baada ya mwafrika
kupandisha bendera yake mambo mengine yafuatevilevile katika utenzi wa uhuru wa
Tanganyika na utenzi wa jamhuri ya Tanzania “tunaona uhuru wa bendera ukielezwa
kwa kabla ya ukombozi wa aina nyingine kufuata.
Kwa hiyo ukombozi huu mwanzo (uhuru wa bendera) husababisha uhuru wa
kisiasa wan chi kisha uhuru wa kisiasa huwa ni jukwaa la ukombozi wa uchumi na
mambo mengine,vitabu vingine vinavyozungumzia ukombozi wa kisiasa ni mzalendo,F.E.MK
Senkero) Ubeberu Utashindwa(J.K Kiimbila),Tone la Mwisho(E.Mbogo),Kinjikitile
na Mashetani(E.Hussein),Nuru mpya(R.Rufeshobya)
(b)Kiuchumi
Uhuru wa bendera ni sehemu ya mwanzo tu wa ukombozi wa jamii nchi
zinaweza kujidai ni huru kumbe uchumi wake bado ungali mikononi mwa nchi
nyingine.Nchi nyingi zinazoendelea bado ziko katika harakati hii ya kutaka
kujikomboa kiuchumi.
Waandishi wengi wa fasihi ya Kiswahili
wamezungumzia sana suala la uchumi katika (Mashairi ya Azimio la Arusha)
mwandishi anaonyesha na kushambulia unyonyaji ambao ni adui wa uhuru wetu.
Vilevile waandishi wanasisitiza kufanya kazi kama njia ya kuimaisha
uchumi.Pia wameeleza kuwa unyonyaji unaweza kukomeshwa kwa kutaifisha njia zote
za uzalishaji mali na kuwa mikononi mwa umma.
Katika tamthiliya ya “Bwana Mkubwa” (J.P Mbonde) ameonesha kuwa shabaha
yetu sisi ni kupigana na ukoloni mambo leo.Kwa sasa na kupata uhuru
kamili.Ukoloni mambo leo ni kikwazo cha ukombozi wa kiuchumi
Kwa sababu ya ulegevu wa uhuru wa kisiasa tunaweza kuwa na mali mikononi
mwetu lakini tukizembea kufanya kweli ipasavyo yaweza kufanyiwa njama na
ukoloni ndio maana upo umuhimu wa bidii katika kazi na uzalishaji wa mali kisha
linafuata swala la ulinzi wa mali hiyo.
Kuzikomboa njia za uzalishaji mali hakutoshi kwani kila hila zao
zisizoisha wakoloni wanaweza wakatupora mali hiyo tunapaswa kuwa macho.
Katika utenzi wa “Zindiko la ujamaa” mwandishianaeleza utaifishaji wa
njia kuu za uchumi na uhalali wa utaifishaji huo. Mwandishi anaonyesha kuwa
utaifishaji huo ulifanywa si kwa kuwaona wakoloni kwa dhuluma bali kama njia
moja wapo ambayo itaongeza kwenye ukombozi wa kiuchumi katika jamii. Lengo moja
ni kufuata ubinafsi ambao unarutubisha tofauti za kitabaka na badala yake
manufaa ya umma kwa ujumla yapatikanayo;
Ukombozi wa kiuchumi si utaifishaji wa njia za uzalishaji mali tu na wala
si kukomesha ukabaila na ubepari bali ni kuongeza juhudi katika kazi mbali
mbali ili kuongeza kiasi cha pato la kitaifa. Waandishi wengine wanazungumzia
ukombozi wa kiuchumi ni kama vile, “Nuru mpya” (G. R. Ruteshubya) “Mashetani”
(E. Hussein) “Sauti ya dhiki” (A. Abdallah) “Kasri ya mwinyi fuad” (Shafi Adam
Shoji) Zetu bora mkulima na wasifu wa sili binti saad(S. Robert).
C) Kimawazo
Ukombozi wa kimawazo ni uhuru wa mtu katika upeo wa fikra pasipo
kutegemea mtu mwingine. Hapa mtu aliye huru awe anajiamini mwenyewe na awe mtu
kama watu wengine. Awe mwenye uwezo wa kuwaza, kuamua na kutenda, kuchanganua
na kupanga kama watu wengine. Mtu aliye mtumwa na kimawazo anaweza kufananishwa
na mnyama wa kufugwa. Mnyama wa kufugwa daima ni masaibu na bwana wake wakati
wote huongojea amri kutoka kwa bwana wake.
Maandishi ya fasihi yanazungumziakwa upana swala hili la uhuru wa mawazo
. Katika riwaya ya “Njozi za usiku” dhana hii ya utumwa wa kimawazoipo ndani ya
watu wengi ambao wanashiria hasa baada ya maajilio ya elimu iliyokuja pamoja na
ukoloni na ikatumika kwa upotofu. Katika riwaya hii msanii anaonyesha kuwa wale
waliosoma walidharau kazi zote za mikono, walifikiri kuwa kazi za mikono,
walfikiri kuwa kazi za mikono michafu na zinafaa kwa wale ambao hawakusoma. Wao
wanfikiri kuwa kazi ya mtu aliyesoma ni kushika kalamu na kuandika tu au
kuwasimamia ambao hawakusoma.
Tangu uhuru wa Tanzania kumekuwa na harakati za kufutilia mbal
ukanganyifu wa namna hii katika mawazo ya watu. Mawazo ya namna hii ndio
yamekuwa yakiwafanya watu wengi wa hali ya chini waamini kuwa uchumi walionao
wamepewa na Mungu.
Vile vile kimawazo watu waliamini kwamba kila jambo lilitokana na
watawala wa kizungu lilikuwa ni bora kabisa. Kwa mfano hata majina yliletwa
toka Ulaya nay a kwetu ya asili kuachwa.
Haya yanajadiliwa wazi katika tamthiliya ya “Bwana mkubwa” (J. P. Mbonde)
Katika ukombozi wa kimawazo kuna swala la ukombozi wa mwanamke na swala
la dini.
Katik swala la ukombozi wa mwanamke watu wengi wanalitazama krahisi jambo
hili. Wengi wanadhani kuwa mwanamke hana haki ya kujibagua kutoka kwa wanaume
na kujipigania haki yake. Watu hawa hawaelewi ni mapinduzi gani ambayo hawa
wanapigania.
Katika fasihi ya Kiswahili Shaban Robert amepata kuwatetea wanawake
katika kazi zake mbali mbali ikiemo Diwani ya”Wasifu wa siti binti saad” na
siku ya watenzi wote.
Shaban Robert amemtazama mwanamke kama mtu asiyestahili dhima na utu kama
watu wengine wowote wale.
Katika kitabu cha “Wasifu wa Siti binti Saad” msanii au mwandishi
anaeleza wazi jinsi jamii ilivyomfanya mwanamke kama chombo cha kutunzwa
utawani ili kiwe kizuri kipate kuwavutia wanaokitafuta na baada ya kutoka
utawani kikawa mikononi mwa mwanaume kikamtegemea kwa hiyo mwanamke alikuwa ni
mtu aliyechukuliwa kama hana wajibu wowote wa maana Zaidi ya kuwa mtegemeaji.
Lakini Shabn Robert aliona kuwa ( uk 23) “Ukimdumisha mtu leo utamuona juu ya
kilele cha utukufu kesho. Dhila au dhana ililipua fataki ya utukufu katika moyo
na mtu mara kwa mara.
Mawazo ya mwandishi ni kwamba wanawake budi watazamwe katika hali zao za
maisha katika ubaya na uzuri kama wanaume. Kuhusu swala la dini linajitokeza
katika riwaya ya “Kichwa maji” ambapo mwandishi anaona dini imeanzishwa na
waoga ambao hutawaliwa na milango yao ya fahamu badalaya kutawaliwa na akili au
bongo zao.
Jambo muhimu katika kumkomboa mtu kimawazo ni kwamba ikiwa dini
itaendelea kuwepo isiwe na mtazamo duni na finyu na thari zake ambazo alikuja
nazo mkoloni akidai kuwa tamaduni zetu ni za kishenzi. Sharti elimundiyo iwe ya
kutafakari na kugeuz mfumo wa maisha ya jamii.
Katika dini pia kuna madhehebu mbali mbali ambayo kati yao kuna uhasama
mkubwa, mwislamu anadai kuwa yeye ni bora Zaidi kuliko mkristo na mkristo
anajiona yeye ni bora kuliko mwislamu. Madhehebu yote haya yamechimbuka huko
mashariki ya kati…….katika kitabu cha “Bwana mkubwa” (uk 18-19)
…………kwanini basi mlitutengnisha katika vikundi vidogo vya madhehebu
tofauti kada ya wakristo iwapo Mungu ni yule yule mmoja leo mnatueleza tuombe
kuungana, utengano alianzisha nani? na kwa faida ya nani?........mbona babu
zetu walimwabudu Mungu wao toka zamani kabla ya ujio wa wazungu.
Kwa ujumla dini imechangia kwa kiasi kikubwa sana katika kudumisha mtu
kimawazo na kumfanya atumie fahamu tu kwa hiyo katika kumkomboa mtu kimawazo
sharti suala la dini litupiwe jich kali fasihi inazidi kuona jicho lake.
(d)Kiutamaduni.
Kwa ujumla utamaduni wan chi zilizotawaliwa na ukoloni umeathiriwa sana
na ukoloni huo watu wa nchi hizo wanazipoteza kidogo kidogo thamani za
utamaduni zao.
Katika fasihi ya Kiswahili ukweli huu wa mambo tunaupata katika kitabu
cha “Njozi za Usiku” mwandishi wa riwaya hii ameelezea namna vijana wote hasa
waliosoma hawataki kabisa kusikza kuhusu mila na desturi na michezo ya wakale
wao (uk 51)
Hadi leo vijana wengi wakiwa kwao (vijijini) na ikatokea kwamba kuna
ngoma za kienyeji zinachezwa wao husimama mbali au kando wakitazama kwa dharau
mambo yanayotendeka mbele yao.Wanaamini kabisa kuwa ngoma hizo ni za kishezi
ngoma ambazo zinafaa kuchezwa na watu wasiosoma watu wasio staarabika.
Katika riwaya ya “Kichwa maji” mwandishi ameonesha jinsi isiyo ya kawaida
kwa msomi au watu wenye cheo serikalini kucheza ngoma za kienyeji lakini vijana
hao hao mwanzoni wasomi wenye mwawzo ya kisiasa wakisikia sehemu fulani kuna
mziki au disko watajitahidi sana ili wasikose kufika huko.
Kwa sasa kuna mtindo mwingine wa kupaka madawa ya kujichubua ngozi
waonekane weupe na wengine huvaa nywele za bandia au maiti ili kuficha nywele
zao za kipilipili.Huu wote ni utumwa wa kimawazo kwa upande fulani watu hawa
wanaamini kuwa uzungu ndilo shina za maarifa watu hawa hawajui kwamba kuna
wazungu wengine ni maskini zaidi hata kuliko sisi wenyewe.
Hitimisho lugha ya ukoloni mambo leo vile vile ili tujikomboe katika
nyanjo hizi ni lazima tuondoe ubinafsi, uroho wa madaraka na ulevi wa madaraka
hapa nchini.
FASIHI NI SANAA.
Sanaa ni uzuri unajitokeza katika umbo zilizosanifwa umbo ambalo mtu
hulitumia kuelezea hisia zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye
dhana maalumu.
Kazi za fasihi zipo katika nyanja zifuatazo uchoraji, ususi, fasihi,
ufinyanzi, muziki, ufumaji, utarizi na maonesho.Nyanja hizi za Sanaa zinaweza
kuonyeshwa kwenye kielelezo hiki:-
Ufumaji
|
Muziki
|
Utarizi
|
Uchoraji
|
SANAA
|
Fasihi
|
Ufinyanzi
|
Uchongaji
|
Maonyesho
|
Ususi
|
Katika kipengele cha Sanaa kinachotofautiana na kipengele
kwa umbo na matumizi. Fasihi ni kipengele cha Sanaa kinachotumia maneno kuumba
huo uzuri wa kisanaa.
TOFAUTI KATI YA FASIHI
NA TANZU NYINGINE ZA SANAA
1. Lugha
, kazi zote za kifasihi zinaundwa kisanaa kwa kutumia lugha inayotumika au
kuandikika. Lugha hiyo hubeba maana Fulani (ujumbe) kwa jamii Fulani.Hivyo lugha
ndiyo inayotufautisha fasihi na Sanaa nyingine. Kwa mfano, uchoraji kipengele
chake muhimu kalamu, rangi na kipande cha nguo au karatasi. Ufinyanzi lugha
yake ni udongo , uchongaji wa vinyago lugha yake ni gogo la mti n.k
Fasihi si maeezo ya kawaida kawaidakama
vile matangazo, taarifa ya habari au barua, fasihi ni maelezo yenye mguso
kisanaa. Kazi za kifasihi, huumbwa kimafumbo hutumia nahau au misemo , methali,
tamathali za semi, taswira na ishara mbali mbali. Kazi za fasihihufikirisha mtu
huweza kutumia akili ili aweze kugundua kazi ya kifasihi aliyosoma au kuisikia
kuwa ina maana gani.
2. Wahusika,kazi
yoyote ya fasihi inakuwa na wahusika wake ambao matukio mbali mbali yanayohusu
jamii huwazungukia wahusika ni watu ama viumbe, waliokusudiwa wawakilishe tabia
za watu katika kazi za fasihi. Kwa upande mwingine wahusika ni muhimu sana
katikakutoa na kufikisha dhamira kwa hadira iliyokusudiwa na mwandishi.
3. Mandhari,
kazi ya fasihi inakuwa na mandhri ambayo huonyesha tukio linaponyika.
Mandharihiyo inaweza kuwa ya kubuni au ya kweli.
4. Utendaji,
utendaji hasa katika fasihi simulizi hushirikisha fanani na hadhira kwa wakati
mmoja. Vile vile utendaji humfanya fanani aweze kuonyesha baadhi yamatendo
katika usimulizi wake.
5. Fani
na maudhui,kazi za fasihi zina sehemu mbili yaani fan na maudhui na
sehemu hizi zinafungamana. Maudhui ni kile kinachosemwa na fani ni namna
kinavyosemwa. Kazi nyingine za Sanaa vile vile zinafanikisha ujumbe kwa hadhira
lakinimbinu na vifaa vinavyotumika ni sehemu ya fasihi. Kwa ujumla kazi za
kifasihi, fani na maudhui yake ni hali ya juu sana ukilinganisha na Sanaa nyinginezo.
KWA VIPI FASIHI NI SANAA ?
Usanaa wa fasihi hujitokeza
katikavipengele mbali mbali kama ifuatavyo:-
1.
Mtindo, Sanaa kaitka fasihi
hujidhihirisha katika namna kueleza jamii (mtindo) katika kueleza jambo
kunakuwa na aina fulani ya kiufundi ambao mwanafasihi huutumia katika kufikisha
ujumbe kwa jamii yake. Taarifa ianyotolewa inaweza kufichwa katika fumbo,
shairi, kitendawili, tamthiliya au hadithi.
2.
Muundo (mpangilio maalumu wa matukio)
katika kazi ya fasihi, matukio yanapangwa kiufundi ili yaweze kuwasilishwa
vizuri kwa jamii husika. Matukio hayapangwi ovyo ovyo tu bali yanakuwa na
mpangilio maalumu.
3.
Utenzi mzuri wa lugha iliyojaa nahau,
misemo, methali, tamathali za semi, taswira na ishara mbali mbali
unaonyesha wazi usanaa wa fasihi. Lugha itumikayo katika fasihi ni ya kisanaa.
Ni lugha iliyopambwana inayokusudiwa kuibua hisia za namna Fulani ka hadhira
yake. Lugha hiyo inaweza kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia hamasa
au kushawishi. Matumizi ya lugha yak ya aina tofauti, kuna tamathali za semi,
misemo, nahau, methali. Lugha ya wahusika hasa lahaja zao, uchaguzi wa
msamiati, miundo ya sentensi, ufundi wa kutoa maelezo hasa ya wahusika ya
mandhari na matukio, uteuzi wa lugha yenyewe itumiwayo.
4.
Uundaji wa wahusika, wahusika huwa
na tabia zinazotofautiana kati yao.
Wanaundwa kiufundi sana na msanii anaweza kuamua anataka wahusika
wanaowakilisha tabia na matendo fulani tu katika jamii na kwa hiyo atawaumba
wahusika hao ili kukamilisha nia na lengo lake.
Katika kutofautisha tabia na hali za
wahusika, mwandishi analazimika kutumia mbinu ya kuwapa majina wahusika wake.
Wahusika wanaweza kuumbwa kinafsi au kiakili na kimwili. Kutokana na ujenzi wa
aina hii mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha
mabadiliko yake kila anapokutana na mazingira tofauti.
5.
Mandhari, fasihi hujengwa katika
mazingira maalum. Mandhari husaidia sana kujenga hisia inayokusudiwa na
mwandishi. Mandhari yanajengwakiufundi na mwandishi ili yasaidie katika kujenga
kazi nzima ya fasihi.
MASUALA YA KIITIKADI NA DHANA YA UDHAMINI KATIKA KAZI ZA FASIHI
Maana ya Itikadi
Itikadi ni Imani ya watu au jamii Fulani
juu ya kitu Fulani. Itikadi kisiasa ni mfumo wa mawazo na Imani ambao umewekwa
na tabaka tawala/ tawaliwa au tabaka lolote lenye nguvu katika jamii
inayohusika ikiwa na lengo la kulinda, kutetea na kuendekeza matakwa na maslahi
yake. Utaratibu huo unaambatana na umilikaji wa njia kuu za uchumi na umilikaji
wa mapato ya ziada yatokanayo na jasho la wazalishaji mali hizo, vymbo vya
kitaalumakama vile elimu na nyenzo zisaidiazo kuimarisha itikadi kama vile dini
vinatumika kutetea utaratibu uliowekwa na tabaka tawala.
Kimsingi kuna mitazamo miwili ya kiitikadi:-
i)
Itikadi inayotetea na kulinda maslahi ya watu
wchache tu katika jamii (utumwa, ukabaila na ubepari)
ii)
Itikadi inayotetea na kulinda maslahi na matakwa
ya watu wengi katika jamii (ujima na ukomunisti).
Vile vile tunapojadili juu ya itikadi katika fasihi na usemi kwa ujumla
pia tunaongelea juu ya utabaka uliopo katika jamii inayohusika . Kuna matabaka
ya aina mbili:-
a)
Tabaka tawala
b)
Tabaka tawaliwa
Tabaka linamiliki vyombo vya dolana
kwa kutumia vyombo hivyo na kwa kutumia waandishi, tabaka tawala linaunda,
linaendeleza na kutetea maslahi yake.
Vile vile tabaka tawala lina nguvu
za kiakili na za kielimu kwa manufaa yao. Mwandishi kwa ujumla hawezi kuepukana
na mfumo huo wa kitabaka. Tabaka Fulani huwa dhamini waandishi kwa njia mbali
mbali.
UDHAMINI
Ni hali ya watu au shirika Fulani kutoa fedha kwa ajili ya
kugharimu kitu fulani . Mdhamini au wadhamini ni kundi la watu wenye shabaha
zinazofanana wenye kusimama kama ufadhili wa mradi fulani. Katika fasihi hawa
ni wale wanaosimamia makundi maalumu kipropaganda na kiitikadi.
AINA ZA UDHAMINI
Kuna udhamini wa aina
mbili:-
i)
Udhamini wa ushawishi
ii)
Udamini wa nguvu
UDHAMINI WA USHAWISHI
Ni aina ya udhamini ambao mdhamini huwashawishi na
kwanunuawaandishi au wasanii. Matokeo yake ni kwamba msanii anafungwa na
matakwa ya mdhamini.
UDHAMINI WA NGUVU
Huu ni udhamini unaotumia vyombo vya dola kama vile jeshi,
polisi, magereza n.k.Hakuna hiari katika udhamini wa nguvu, kila kitu
kinaendeshwa kama vile mashine tu. Kwa ujumla mwandishi akidhaminiwa kwa nguvu
za serikali huwa kama kasuku aimbaye na kuutukuza mfumo wa maisha uliopo katika
jamii hata kama roho na moyo wake viko mbali sana na mfumo huo. Lakini msanii
anapodhaminiwa kutetea umma, lazima kutakuwa na madhara yake katika jamii yake
inayohusika.
Mwandishi wa fasihi katika kila nchi atakuwa na udhamini
unaolingana na mazingira yake kwa mfano katika nchi ya Tanzania, mwandishi
anaweza kuandika kwa udhamini wa jamii yake inayohusika.Mdhamini anaweza
kuwamtu binafsi mwenye fedha, shirika, chombo cha serikali, chama Fulani au kundi
la mataifa kwa ushirikiano. Pia mdhamini ni mwakilishi wa wenye mamlaka juu
yake, kwa mfano katika serikali yaTanzania chuo kikuu ni mwakilishi wa serikali
na serikali ni mwakilishi wa tabaka tawala. Hivyo msanii anayedhaminiwa na chuo
kikuu ambacho ni combo cha serikali hatimaye anajikuta anafanya kazi ili
kuendeleza maslahi ya tabaka tawala.
SABABU ZA UDHAMINI
Ø
Uhaba wa fedha kwa waandishi za kuendeshea
shughuli zao za uandishi katika uandishi wa kazi za fasihi. Pesa zinahitajika
kwa ajili ya kununulia karatasi, kalamu, uchapaji n.k.
Ø
Kulinda na kutetea maslahi yawadhamini wao. Hii
inatokea zaidi kama mdhamini ni wa tabaka tawala. Kama tabaka linalo tawala ni
la mabepari kazi za fasihi zitatetea tabaka hilo.
Ø
Kujulikana au kuipendekeza. Baadhi ya waandishi
hudhaminiwa kwasababu ya kutakakujulikaa na kwa upande mwingine mdhamini
anawadhamini waandishi kwa lengo hilo.
Ø
Kupata fedha za haraka. Hawa huandika vitabu
vyenye kujaa wahusika wakuu, mafundi wa kufanya mahaba, kutumia madawa ya
kulevya na kufanya mapenzi kwa kutumia mipira ya kiume na kike bila kujali
stahana utamaduni wa jamii yake. Mwandishi anachojali hapa ni pesa na sio
matakwa ya jamii yake.
Ø
Kulazimishwa na tabaka tawala. Waandishi
hawawanakubali udhamini huo kwakuogopa udhabiti wa kazi zao na tabaka tawala.
Waandishi hawa wakikataa udhamini huo kazi zao zitadhibitiwana kupigwa marufuku
zisisomwe au kuchapishwakabisa.
ATHARI ZA
UDHAMINI
1.
Mwandishi anayedhaminiwa anatakiwa kuandika yale
tu ambayo mdhamini wake anayataka. Msanii hatakuwa na hiari au uhuru wa
kuandika kitu chochote na kwa njia anayotaka. Kwa kudhaminiwana tabaka tawala
kamwe mwandishi hawezi kudharau umma ili ujitambue kuwa unagandamizwa.
2.
Mapana ya uandishi wake kidata, kigiografia na
kimaudhui huamuliwa na mdhamini na kutegemea mahitaji yake na kiwango cha fedha
alichonacho mdhamini.
3.
Ufafanuzi wa data na maudhui ya kazi ya fasihi
lazima ulingane na mtazamo wa itikadi ya mdhamini.Hii ina maana kuwa mwandishi
wa kazi ya fasihi hawezi kufanya ufafanuzi wa data na maudhui mwenyewe bila
kumshirikisha mdhamini.
4.
Matokeo ya uandishi wa kazi za fasihi mara
nyingi ni mali ya mdhamini na hutumia kuendeleza maslahi yake mabayo sio lazima
yalingane na malengo ya mwandishi.
5.
Wasanii au waandishi wengi kutokana na kudhaminiwa
huanza kuandika kazi zao kwa kupenda pesa hii huwafanya waandishi kuwa makasuku
kwa sababu ya kuandika yale tu yasemwayo na mdhamini wake bila kuyafanyia
uchambuzi wa kina.
6.
Udhamini hukuza utabaka katika jamii, hapa
tunakuwa na tabaka lenye nacho (mdhamini) na tabaka la wasionacho (msanii)
mdhamini humnyonya msanii.
7.
Kuzuka kwa fasihi pendwa (riwaya ya pendwa).Hapa
waandishi kwa lengo la kupata pesa za haraka huandika riwaya pendwa ambazo zina
soko kubwa hapa nchini hasa kwa vijana na wakati huo huo riwaya hizo hazifunzi
lolote jamii Zaidi ya kuburudisha.
8.
Udhamini huchochea rushwa, hii ni kwa sababu
waandishi wengi wanataka udhamini huo na matokeo yake wale wanapata udhamini
huo lazima watoe chochote (rushwa) kwa mdhamini.
UMUHIMU WA UDHAMINI
1.
Husaidia waandishi chipukizi katika kuchapisha
kazi zao.
2.
Husaidia waandishi katika kufanya utafiti wa
mambo mbalimbali yatakiwayo katika Sanaa hiyo ya fasihi.
3.
Husaidia kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa kukuza
taaluma ya uandishi.
UHURU WA
MWANDISHI
Dhana ya uhuru wa mwandishi ni pana sana.
Kwanza uhuru wa mwandishi uko katika utashi,Bila utashi mwandishi
atakuwa mwoga na mwepesi wa kukata tamaa.Atayumbishwa haraka kutoka kwenye
msingi wa falsafa yake na Imani aliyo nayo juu ya mabadiliko yatokeayo katika
jamii.Makombora ya wahakiki na wanasiasa huweza kumyumbisha, lakini kwa
mwandishi mwenye utashi makombora hayo humkomaza.
Baadhi ya waandishi walionyesha utashi wao katika Afrika ni
Ole Sanyika na Ngugi wa Thiongo “waandishi hawa wameshambuliwa sana na
wahakiki, lakini misimamo yao ni ile ile vile vile wamewahi kufungwa na
walipotoka kifungoni hawakubadili misimamo yao na wamekuwa hivyo kwa sababu ya
utashi wa falsafa zao katika fasihi ya kiswahili, waandishi wenye utashi wapo
na msini wa kuwepo kwao ni kutoyumbishwa na matamshi ya jukwaani na wahakiki
ambao hawajapevuka.
Pili,uhuru wa mwandishi umo katika kuwa na falsafa moja
inayoeleweka,Falsafa ifanyayo na maandishi ya mwandishi moja yawe na kitu
kijulikanacho lengo.Waandishi waliotajwa hapo juu yaani Ole Sanyika na Ngugi wa
Thiongo ndio wanaongoza kuwa na falsafa zao zinazojulikana. Katika fasihi ya Kiswahili
tunaona waandishi wachache wenye falsafa zao inayojulikana wengi tulio nao
wanaandika kufuatana na jambo fulani au tukio la wakati huo bila kulinganisha
leo ataandika juu ya mapenzi, kesho juu ya upelelezi na kesho kutwa mapinduzi
mwishowe anakuwa na orodha ndefu ya vitabu visivyokuwa na lengo.
Waandishi wachache tulio nao ambao wameelekea kuwa na falsafa
inayoongza maandishi yao ni kama Shaban Robert, G.Kezilahabi na Mohamedi
Suleiman.Bila kuwa na falsafa maalumu ni rahisi kwa mwa mwandishi kuyumbishwa.
Tatu, uhuru wa mwandishi umo katika kuitawala vema Sanaa yake,kama unaandika riwaya na
hujui misingi ya Sanaa ya aina hiyo atajikuta katika kikwazo,utajikuta uhuru wa
kisanaa unaweza kujaribu, lakini kazi utakayoitoa itakuwa hafifu.Kazi nzuri ya
kisanaa ni ile inayounganisha vema ubunifu na uhalisia.Mwandishi akielemea sana
katika ubunifu anazua matatizo mengine kazi ngumu aliyonayo mwandishi ni katika
kupata barabara msitari huo.Mwandishi mwenye vitabu vingi anaweza kuwa na
kitabu kimoja tu kilichoupatia vema mstari huo katika fasihi ya Kiswahili
waandishi walioupatia msitari huo tunao.Ebraim Hussein,Penina Mhando,Mohamed
Suleiman, C.G Mng’ong’o na J.A.Safari.Msanii anayeweza kuitawala vema Sanaa yake anaunganisha vizuri Sanaa na
maudhui yake.
Mwisho uhuru wa mwandishi umo katika lugha anayotumia msanii
atawale vema Sanaa yake nilazima ujue lugha anayotumia.Lugha ndicho kiungo
maalumukati ya Sanaa na kazi ya kifasihimwandishi kama hajui vema lugha
anayotumia atajikuta hana uhuru wa kukisema anachotaka kwa hiyo lugha ndiyo
nguzo ya nne katika uhuru wa mwandishi, waandishi wa Kiswahili waliokwisha kutajwa wanakitawala Kiswahili
sanifu,Kiswahili sanifu ndiyo msingi
wa fasihi ya Kiswahili.
Ni kweli kuna uhuru wa mwandishi?
Uhuru wa mwandishi ni nini?
Ni ile hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi katika
kutoa mawazo au hisia zake kwa jamii.Ni uhuru wa kuandika na kulikosoa tabaka
lolote katika jamii bila kupata matatizo yoyote.
Mwandisihi ni nani?
Ni mtu yoyote atumiaye muda wake mwingi kuandika na kuzungumzia jamii yake kwa njia
ya maandishi.
Je kuna uhuru wa mwandishi?
Kwa ujumla uhuru wa mwandishi ni uhuru ikiwa hakufaulu
kudhuru tabaka tawala hii ni kwa sababu suala la uhuru wa mwandishi ni la
kitabaka na lilianza pale jamii ilipogawanyika katika matabaka kwa maana hii
uhuru wa mwandishi unaamuliwa na tabaka tawala
Kuanzia enzi za utumwa, maandishi ya liyovumbuliwa fasihi
andishi ya mwanzo ilikuwa ya wateule wachache tu na wenye vyeo vyao.Hao
mabwana, wamwinyi na mabepari walihakikisha kila mbinu hutumika ikiwemo ya
udhibiki wa maandishi kuendeleza na kulinda utawala wao.
Naye B.Goya (1974-78) anasema kwa maandishi hana
uhuru kwa vyovyote vile kwa sababu yeye ni tokeo la jamii Fulani kila jamii ina
mipaka yake ambayo mtu hatakiwi kukiuka kwa vyovyote vile mwandishi huyu
amebanwa na mipaka hiyo asivuke.Pindi avukapo mipaka hiyo atapambana na jamii
hiyo (tabaka tawala) vitabu vya mwandishi huyo vitapigwa marufuku au vitabu
vikitolewa havitanunuliwa au serikali itavikusanya na kuvifanyia mipango
mwingine katika Afrika kuna mifano mingi
ya udhibiki wa waandishi mfano mzuri ni mwandishi maarufu wa Kenya Ngugi wa Thiongo
ambaye kazi zake hasa ya “Ngaahika Ndeenda”(I will marry when I want)-
Nitaolewa Nitakapotaka, Ilimgombanisha na vyombo vya dola hadi akawekwa
kizuizini, Ngugi wa kwanza kufichua siri za mfumo wa kibepari kwa watu wanyonge
aliliuzi tabaka tawala la jamii yake ambalo halikusita kutumia udhibiki na
vyombo vyake vya Mabavu.
Baada ya uhuru vitabu vingi sana viliandikwa kwa kudhibitisha
maandishi mbalimbali uliojitokeza waziwazi E.Kazilabi aliandika riwaya “Rosa
mistika”(1971) kitabu hiki kilipigwa marufuku kisitumike mashuleni na wala
kisiuzwe waziwazi madukani.Ilidaiwa kuwa waliokipiga marufuku kuwa kilikiuka
maadili ya jamii kwa kueleza mambo ya aibu kwa wazi.Sura ya kumi ndiyo hasa
ilitolewa mfano wa uchafu wa kitabu hiki.Udhibiti huo ulifanywa na Wizara ya
Elimu na ulizusha maswali mengi kwa wasomaji.Wasomaji walianza kujiuliza, Je si
kweli uchafu uelezwao katika “Rosa mistika” umo ndani ya jamii ya Tanzania? Je
upotofu na uongozi mbaya ulifuchuliwa na riwaya hiyo hii si upo kati yetu? Kwa
baadhi ya wasomaji ilielekea kuwa suala la uchafu wa maelezo yatokeayo kitandani
baina ya wakuu wa chuo na wanafunzi wake lilitumika kama kisingizio tu cha
kudhibiti ukweli wa masuala mengine nyeti yaliyowagusa viongozi wakilishwa na
watu kama vile Bwana Maendeleo Deogratius anayeshiriki katika kuwaharibu vijana.
Vitabu vingine ambavyo havieleweki vinasema nini, maudhui,
falsafa na ujumbe wa mwandishi ni mashetani(E.Hussein) “Aliyeonja
Pepo”(F.Topan) na “Ayubu” Paukwa theatre Association.Na hivi viko kwa kukwepa
mkono mrefu wa tabaka tawala.
DHIMA YA UHURU WA MWANDISHI.
1. Mwandisshi atakuwa huru
kuikosoa jamii au tabaka lolote litakaloenda kinyume na utaratibu wa jamii bila
matatizo.Mwandishi atakuwa huru kuonyesha dhuluma, ukatili na ujangili
unaofanywa katika jamii na tabaka lolote bila matatizo yoyote.
2. Kukiwa na uhuru wa
mwandishi, msanii atakuwa na falsafa inayoeleweka pamoja na utashi (wake).Hii
itamfanya mwandishi awe na msimamo unaoeleweka.Msimamo wake utamaidia kuifundisha na kuielimisha
jamii bila uoga.Ataijiulisha jamii hali yake na ataonesha jamii njia za kufikia
haja na kutatua matatizo ya jamii bila uoga
3. Mwandishi atakuwa huru kutoa
mwongozo katika jamii kwa kuikomboa jamii kutoka katika fikra mbovu za
kugandamizwa, kunyonywa na kuonewa na tabaka tawala ili jamii ipate haki na
heshima bila woga wa kuliondoa tabaka ambalo ndilo lenye mamlaka yote katika
jamii.
4. Uandishi wa kikasuku
hupungua, waandishi au wasanii huacha tabia ya kuwa vipaza sauti vya tabaka
fulani katika jamii, wasanii makasuku huandika mambo bila kufikiri na
kurudiarudia mawazo yaliyokwisha semwa
na wanasiasa majukwaani bila fikra mpya kwa hali hii hupotosha jamii.Hivyo
kunapokuwa na uhuru wa mwandishi wa kutosha hali hii haiwezi kutokea kwa sababu
mwandishi ataandika mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii na hataweza
kujikomba au kujipendekeza kwa tabaka tawala lenye mamlaka yote katika jamii.
5. Kunapokuwa na uhuru wa
mwandishi fasihi inakuwa chombo cha kuikomboa jamii kiuchumi,kisiasa,
kiutamaduni na kifikra (kimawazo) katika jamii ya kitabaka fasihi ni mali ya
tabaka tawala na hutumia fasihi kutetea na kulinda maslahi yao.Hivyo inapokuwa
mali ya jamii nzima inatumiwa na jamii hiyo katika kuwakomboa wanajamii wote.
6. Kunapokuwa na uhuru wa
mwandishi, mwandishi anakuwa huru kuichokoza na kuisukasuka (kuichochea) jamii
bila matatizo yeyote. Mwandishi atachokoza jamii ya wakulima na wafanyakazi
kufikiri ili waweze kulichunguza tabaka tawala kwa jicho pevu na kutoa
hadharani uozo uliopo katika kunyonywa, kupuuzwa,kuonewa, kugandamizwa na
kunyanyaswa na tabaka tawala
7. Mwandishi atakuwa huru
kuelimisha na kuishauri jamii katika mambo muhimu yanayojitokea katika jamii
bila woga.Mwandishi ataishauri jamii kuhusiana na mambo kama vile afya, elimu
na ichague mambo gani yanafaa kuhifadhiwa na yapi hayafai vile vile msanii
anakuwa huru kuirekebisha jamii bila woga kwa kuangalia yapi ni mazuri na yapi
ni mabovu yanayotendeka katika jamii
No comments:
Post a Comment