TAMTHILIYA YA KIVULI KINAISHI
MWANDISHI:
SAID A. MOHAMED
WACHAPISHAJI:
OXFORD UNIVERSITY PRESS
MWAKA:
1990
UTANGULIZI
Kivuli Kinaishi ni tamthiliya
inayojadili na kuchambua matatizo mbalimbali yanayozikabili jamii zetu. Matatizo
hayo ni kama vile uongozi mbaya,rushwa,kukosekana kwa haki,kuwepo kwa matabaka
katika jamii,Ushirika na uzembe kazini.Kwa kutumia dhana ya Giningi mwandishi
amefaulu sana katika kujadili matatizo yao.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU: UJENZI WA JAMII MPYA
Mwandishi ameonesha jinsi jamii
ya Giningi ilivyooza.Ni jamii yenye matabaka,tabaka tawala la watu wachache
wenye navyo na wanaopenda kila kitu kiwe chao.Pili kuna tabaka la chini,hili ni
tabaka la walio wengi ambao hawana chochote,hata kile kidogo walichonacho
hunyang’anywa.(uk 18) mazungumzo kati ya Bawabu II na mkulima.
Mfano:‘’Unadhani mpunga huu unatosha hazina ya Giningi?’’
Ili kuonyesha kuwa tabaka
tawala linapenda kupata Zaidi kuliko kutoa;mkulima huyo ambaye alipata mpunga
kidogo kutokana na kukosekana kwa matrekta,mbolea waliyohaidiwa,hakusikilizwa
alipojitetea.Alihukumiwa adhabu kali.
Rushwa imeshamiri katika jamii
ya Giningi.Wafanya biashara ndio wanaotendewa haki ya upendeleo kwa sababu ya
rushwa.Bawabu II alishindwa kuwatetea walimu,wakulima na tabibu kwa sababu
hawakutoa rushwa.Katika (uk 24-25) mwandishi anaonesha jinsi kukithiri kwa
rushwa kunavyosababisha kupotea kwa haki katika jamii ya Giningi.
Kutokana na hali hii,mwandishi
anaonesha kuwa hata kuingia katika utawala wa Giningi ni lazima mtu atoe rushwa
ndipo akubalike.Kwa mfano,Mtolewa alitoa
shs. 5000/- (uk 28-29) ndipo aliruhusiwa kupita langoni.
Katika jamii ya Giningi,viongozi wamejigeuza
miungu wadogo wenye kuishi milele.Wao ndio wenye sauti ya kusema na kutoa
mawazo.Viongozi hao hawaangalii matatizo ya nchi kama vile shule kukosa huduma
bora za kuboresha elimu,hospitali kukosa dawa,n.k. Badala yake wamepoteza muda
mwingi katika sherehe za pombe na ngoma badala ya kutatua matatizo yanayowakera
wananchi.
Uozo mwingine unajitokeza
katika jamii ya Giningi ni ule wa watu kulazimishwa kusema uongo badala ya
ukweli,yaani uongo ni ukweli na ukweli uongo.Mfano tabaka tawala hudanganya
wananchi kuwa matatizo ya nchi husababishwa na vita,ukame,kupanda kwa mafuta,
n.k. (uk 98).
Pia,mwandishi ameonesha kuwa,jamii
ya Giningi maisha yake yamejaa chuki,kisasi,fujo na woga unaowaandama wananchi
wa kawaida.
Hivyo mwandishi ameonesha kuwa
ili tujenge jamii mpya yenye kuondokana na matatizo haya, lazima wananchi
wasimame imara kupingana na aina zote za dhuluma,uonevu,kupiga vita rushwa na
kuondoa matabaka katika jamii.Vilevile ameonesha kuwa,ili tujenge jamii mpya
lazima tufanye mapinduzi ambayo yatawaangamiza wagandamizaji kama vile Bi
Kirembwe.
MBINU ZA UJENZI WA JAMII MPYA
1.
Uongozi mbaya
Suala la uongozi mbaya
limewashughulisha sana waandishi wengi wa Afrika wakiwemo waandishi wa Fasihi
ya Kiswahili.Viongozi wa Afrika waliotwaa madaraka kutoka kwa wakoloni,wengi
wao wana sifa zinazofanana na Bi Kirembwe wa serikali ya Giningi.Wao
walijigeuza na kuwa viongozi wa kudumu milele na milele na hali hii imekwamisha
ufanisi wa ujenzi wa jamii mpya katika nchi za Afrika.
Nyerere aliainisha vigezo vine
vya kuleta maendeleo katika nchi changa
kama Tanzania kuwa ni Ardhi,Watu,Siasa safi na Uongozi bora, lakini
jamii ya Giningi imekosa maendeleo kwa sababu imekosa siasa safi.Imekosa siasa
safi kutokana na kukosekana kwa uongozi bora.Hivyo maendeleo ya Giningi
yamekwamishwa na uongozi mbaya wa Bi Kirembwe na wazee wenzake.
Bi Kirembwe ana hali zote za udikteta, anasema kwa niaba ya
watu,anaua watu ovyo pale wanapotaka kumpinga,anawanyima watu uhuru wa kuabudu
na badala yake wanamuabudu yeye kama Mungu.Hapendi mabadiliko – anakatalia
kwenye madaraka,ana ukatili na vitisho visivyo kifani pamoja na uchawi
uliokithiri.Kutokana na hali hiyo,amefanya kila hila na amefanikiwa kujifanya
Mungu,mchawi wa wachawi,Bwana wa Mabwana,n.k.
(uk 33-36) na (uk 56-60).
Utawala wa Bi Kirembwe umeleta
hofu na vitisho kwa Wanaginingi.Bi Kirembwe hapokei ushauri wowote ule hata
ukiwa mzuri.Anayetoa ushauri anauwa (uk 65-68) na (uk 73-75).Kama hiyo
haitoshi, Bi Kirembwe anajistarehesha kwa vileo na ngoma wakati raia wengine
wanaathirika na hali ngumu ya maisha.
Vilevile Bi Kirembwe
amejilimbikizia madaraka yote.Ni mama wa wote,ni malkia,ni mfalme,ni hakimu,
n.k.
Pia Bi Kirembwe ameshindwa
kukemea maovu yanayotendeka nchini mwake kama vile rushwa na kukosekana kwa haki,
kutokuwepo kwa demokrasia,n.k.Nchi za dunia ya tatu hususani nchi za Afrika
zimeshindwa kujenga jamii mpya kwa sababu ya kuwa na viongozi wabinafsi na wasioshaurika
kama Bi Kirembwe.Baadhi ya viongozi waliopewa madaraka na wananchi,waliwageuka
wananchi hao na baadhi yao walijitangaza kama Maraisi wa maisha.Hali hii
inasababisha bara la Afrika kushuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe mfano
Sudan,Burundi, Rwanda, Kongo, Algeria,Sierra Leone, Angola, n.k.
Hivyo mwandishi anapendekeza
kuwa,ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi mzuri.Uongozi mbaya ni
kikwazo kikuu cha ujenzi wa jamii mpya katika nchi zinazoendelea.
2.
Kufanya Mapinduzi
(mageuzi)
Kuanzia onyesho la saba na kuendelea tumeoneshwa jinsi Mtolewa
alivyoshirikiana na Wari kuleta mapinduzi katika jamii ya Giningi.Lengo kuu
lilikuwa ni kuanganisha utawala mbovu wa Bi Kirembwe.
Katika harakati za ukombozi
(kufanya mageuzi) Mtolewa aliwaunganisha Wari na kuwakomboa kifikra kwa
kuwalisha unga wa rutuba. Katika harakati hizo Mtolewa na wale Wari walikamatwa
na kuuawa lakini vuguvugu la mapinduzi walilokuwa wamekwisha pandikiza kwa
kizazi kile lilisaidia sana kuutokomeza utawala mbovu wa Bi Kirembwe.(uk
118-119) mwandishi anasema;
‘’Tunaishi Bi Kirembwe,sote tunaishi,sote tulioangamia,………Sura zetu zimo
ndani ya viwiliwili vya watoto wetu.Mawazo yetu yamo ndani ya bongo zao.Imani
na itikadi imo ndani ya maisha yao…….tunaishi,ni vivuli vinavyoishi visivyoweza
kufa,ni sauti zinazosema kimya kimya nahata kwa matamko ya wazi……’’.
Vivuli viliendelea kumsumbua Bi
Kirembwe hadi anauona mwisho wake, kwani hata viungo vyake vya mwili
vilimsaliti (uk 128).
Mfano: Macho ya Bi Kirembwe – Mimi ni
shahidi wa maovu yote uliyoyatenda ya kudidimizana kuangamiza.
Mikono
- Sisi ni mashahidi …….
Miguu
- Nami pia nilikuchukua kwenye
mienendo yako……
Kitaswira viungo vya mwili wa
Bi Kirembwe ni wale watu waliokuwa karibu sana na Bi Kirembwe kama vile wazee
na mtangazaji ambao wanamsaliti Bi Kirembwe kutokana na matendo yake mabaya.
Hali hii ilitokea kutokana na
vuguvugu la mapinduzi kupamba moto.Vizazi vipya kwa kutumia mawazo ya Mtolewa
viliendeleza mapambamano kama asemavyo mwandishi (uk 128).
‘’Sisi ni vizazi vipya Giningi,vizazi
vya walioangamia ………Vizazi vya waliodidimia ………Sisi sasa tuna kinywa
kipana….tuna uwezo wa kuamua tunavyotaka, kuamua wenyewe……….kwa maslahi ya wote………Hatutachagizwa
tena na uchawi. Tunakuja ……. Tunakuja……..’’
Pia mwandishi ameonesha jinsi Bi Kirembwe anavyogwaya na kuanza
kuhangaika kutokana na wimbi la mapinduzi kupamba moto.(uk 129),Mwandishi
anasema;
‘’Ah, hata wewe Bi
Kirembwe leo unagwaya? Unatetemeka kama…..? Unalialia kama mtoto mchanga au
mwanamke aliyefiwa na mumewe? Unahofu matokeo ya matendo yako mwenyewe…..’’
Nadharia ya kujenga jamii mpya kwa njia
ya mapinduzi inaoneshwa kutetewa na waandishi wengi. Nadharia hii inaonekana
kuwa muhimukwa sababu tabaka tawala halipendi kuachia madaraka kwa hiari hasa
katika utawala wake.
‘’Unasubiriwa kwa hamu
ndani……..Ingia na ukishaingia keti juu, usikubali kuporomoka chini . Chini kuna
udhia……..’’
Hivyo mwandishi anapendekeza kuwa,ili
tujenge jamii mpya ni lazima tufanye mapinduzi au mageuzi ya kuwaondoa viongozi
wabovu.
3.
Kujitoa
Mhanga
Bila kujitoa mhanga hakuna mapinduzi
ambayo yanaweza kufanikiwa.Mtolewa na Wari walijitoa mhanga kuleta mabadilko
katika jamii ya Giningi.Pia Mtolewa alianzisha mabadiliko makali dhidi ya Bi
Kirembwe.Aliamua kufanya hivyo baada ya kutembelewa na mizimu.
Vilevile Mtolewa alijitoa mhanga katika
kuwakomboa Wari wenzake kifikra kwa kuwalisha unga wa rutuba kama asemavyo mwandishi katika (uk 90);
‘’Hamtoweza kufahamu mpaka niwatoeni mzigo
mlio nao…..hamtatambua mpaka nikufumbueni macho na kukuzibueni masikio……’’
Mtolewa aliwafumbua macho Wari wenzake
kwa kuwalisha unga wa rutuba – elimu ambayo inamfanya mtu ajitambue na atambue
nafasi yake katika jamii na uwezo wa kuwaelimisha wenzake.
Mtolewa alijibizana na Bi Kirembwe kwa
kujiamini na bila matatizo yoyote na hii yote inatokana na moyo wa ushujaa na ujasiri
aliokuwa nao katika harakati za kutokomeza utawala mbaya wa Bi Kirembwe (uk
108).Mtolewa alijibu;
‘’Najiamini kama mchawi yeyote anavyojiamini………’’
Mwisho mwandishi ameonesha kuwa Mtolewa aliuawa na
kuangamizwa kabisa.Mtolewa alijua wazi kuwa atauawa lakini hakuogopa,bali aliendesha
mapinduzi kwa ujasiri.Hii hudhihirisha kuwa jamii mpya haitoshi kujengwa kwa
siasa safi na uongozi bora bali kuwepo kwa watu waliojitoa mhanga kufanya
mapinduzi hayo.
4.
Kuwepo
kwa Demokrasia ya kweli
Demokrasia ni mfumo wa kuendesha
serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu.Katika jamii ya Giningi
hakuna demokrasia ya kweli kutokana na uongozi mbaya wa Bi KIREMBWE.
Bi Kirembwe amebadili madaraka ya
serikali ya Giningi na kujitangaza kama mtawala wa milele. Hivyo amewanyima
wananchi wazalendo wa Giningi demokrasia.(uk 71).
‘’Ndiye mwenye
kustahiki kukalia kiti hiki daima…..kukikalia daima dawamu’’
Katika jamii ya Giningi wananchi
wananyimwa haki ya kuwachaguaviongozi wao wenyewe wanaowataka kwa kuwa hakuna
demokrasia, kwani demokrasia imetekwa nyara na Bi Kirembwe.
Vilevile Bi Kirembwe hakuruhusu
majadiliano nchini Giningi.Watu
walifundishwa kusema uongo badala ya ukweli au kulazimishwa kukubali masharti
magumu pasipo majadiliano.Mfano usiku kuwa mchana na mchana kuwa usiku.
Watu wanaoonekana kutoa mawazo ya hekima mbele ya Bi
Kirembwe,hivyo adhabu yao huwa
kifo.Mfano wa watu hao ni mkulima,tabibu na mwalimu ambao walielezea waziwazi
matatizo hayo.
Vilevile wale wazee watatu waliuawa kwa
sababu walifikiri kinyume namatakwa ya Bi Kirembwe hatakama walikuwa na mawazo
mazuri ya kuiendeleza Giningi kimaendeleo,(uk 74) kama anavyosema mwandishi;
‘’Tulidhani tutaweza kutoa mchango wetu;
tulijisemea tu, tena ndani ya nyoyo zetu kwamba sisi pia tulikuwa na sehemu ya
kutaka kuiona Giningi ya namna tofauti kama tunavyofanya.’’
Halikadhalika Mtolewa aliuawa na Bi
Kirembwe kwa sababu ya kutaka kuiona Giningi inajengwa kwa misingi ya haki na
usawa.Alionekana machoni pa Bi Kirembwe kama msaliti wa utawala wake (uk 114).
Hivyo kuwepo kwa demokrasia ya kweli
katika jamii ni mbinu moja wapo itakayosaidia ujenzi wa jamii mpya katika nchi
zinazoendelea.
5. Umuhimu
wa Elimu
Elimu ni kitu muhimu sana katika ujenzi
wa jamii mpya.Elimu inaweza kumpumbaza mtu akapumbazika,huweza kumlaza mtu
akalala nahata kushindwa kujenga jamii mpya.Kwa upande mwingine,elimu inaweza
kumuamsha mtu aliyelala usingizi akaamka na usipokaa chonjo huyo mtu aliyeamka
anaweza kufanya makubwa yasiyotegemewa katika jamii.
Katika tamthiliya hii,elimuimetumika
katika nafasi zote mbili.Elimu ilitumika kuwapumbaza Wanaginingi waamini kuwa
Bi Kirembwe ni Mungu mdogo.Giningi hakuna kubisha,unapotaka kusema lazima upate
amri kutoka kwa Bi Kirembwe.Giningi hakuna matatizo kwa mtazamo wa Bi Kirembwe.Bi
Kirembwe hakosei katika utawala wake huko Giningi.Giningi wanaendeshwa kwa
mwendo wa ngoma.Elimu hii waliipata kwa njia ya unga wa ndere (mawazo ya Bi Kirembwe)
na mawazo haya ndio yanayowafanya hata watawala wetu kuanzisha itikadi
mbalimbali ambazo kila mtu anatakiwa azifuate.
Kwa upande mwingine,mwandishi ameonesha
jinsi elimu ya kimapinduzi waliyoipata akina Mtolewa ilivyosaidia kufanikisha
kuleta mapinduzi katika jamii ya Giningi.Elimu hii ilimwezesha
Mtolewaasikubaliane na mambo ya Bi Kirembwe hata siku moja.Elimu hii ndiyo
iliyomwezesha Mtolewa kuwalisha Wari unga wa rutuba.Kupitia elimu hii ndipo
Wari walipojitambua wana nafasi gani katika jamii yao.Ndipo walipogundua kuwa
katika Giningi hakuna Amani bali kuna mateso makali.Kutokana na elimu waliamua
kufanya mapinduzi.
Kwa hiyo,mwandishi anatuonesha kuwa elimu ni kitu chenye ncha kali na
itategemea utaitumia jinsi gani, ukiitumia vizuri itakuamsha na ukiitumia
vibaya itakupumbaza akili.Hivyo elimu ni kitu kinachokata nyuma na mbele.
6.
Kupiga
Vita Rushwa
Kukithiri kwa rushwa katika jamii ya
Giningi kunakwamisha ujenzi wa jamii mpya.Bawabu II anapokea rushwa kutoka kwa
wafanyabiashara (uk 24-25).Vilevile alipokea rushwa ya Shs. 5,000/- kutoka kwa
Mtolewa ili aruhusiwe kuingia ndani
yaani aingizwe Giningi.
Kutokana na kukithiri kwa rushwa,haki
haitendeki hata kidogo.Watu wasio na uwezo wa kutoa rushwa wananyimwa haki zao
katika jamii ya Giningi na vilevile wanapewa mashtaka ya uongo ambayo hatimaye
yanawaangamiza.Mfano mzuri ni tabibu,mwalimu na mkulima.
Hivyo mwandishi anapendekeza kuwa, ili tuweze kujenga jamii
mpya yenye kufuata haki na usawa, hatuna budi kupiga vita rushwa na badala yake
haki itendeke kwa kila mmoja (raia).
7.
Kupiga
vita Matabaka
Katika tamthiliya hii,mwandishi
ameonesha matabaka ya aina mbili.Ambapo kuna tabaka tawala na tabaka tawaliwa.Tabaka tawala linawakilishwa na Bi Kirembwe,wazee,mtangazaji na Bawabu I – II.
Tabaka tawaliwa linawakilishwa na Wari
pamoja na sauti za wahenga walioangamizwa na Bi Kirembwe.Linaonewa,linanyanyaswa,linadhulumiwa,linagandamizwa
na kusingiziwa kila uovu mfano:kuuawa kwa mkulima,tabibu na mwalimu.
Katika tamthiliya hii,tabaka tawala
linanyonya,linaonea,linagandamiza na kunyanyasa tabaka tawaliwa.Vilevile tabaka
hili linawalazimisha watu wa tabaka la chini kusema uongo ni kweli na
kweli ni uongo.
Vilevile tabaka hili hutafuta kila aina
ya visingizio kuhalalisha matatizo yanayowakabili watu wa tabaka la chini kama
vile mvua,ukame,mbolea,vita,mafuta,n.k.Hivyo ili tujenge jamii mpya ni lazima
tupige vita matabaka.
8.
Ushirikina
(uchawi)
Habari nzima ya maisha ya Giningi imefungamana
na imani ya uchawi.Bi Kirembwe anafanya mambo yake kama anavyotaka kwa sababu
ya uchawi wake,anaogopwa na kuabudiwa na kila mtu.(uk 34) Mwandishi anasema;
“ Mchawi wa wachawi mjua yote ya ndani
nay a nje, ardhini na hewani, mtambua mema na maovu,mruka hewani na mwota
ndoto……”
Ushirikina kama ulivyokuwa tatizo katika
Giningi ndiyo unavyoelekea kuwa tatizo katika nchi zetu. Viongozi wetu
wanaamini kuwa wanaweza kuendelea kuwa viongozi
kwa kujizindika madawa na ndiyo maana baadhi ya viongozi hutafuta uongozi (madaraka) kwa mbinu ya uchawi.
Ni vigumu kujua dhima ya uchawi au
ushirikina katika ujenzi wa jamii mpya kwa sababu njia zake si za wazi,walio
wengi hawawezi kuona wazi yanayotendeka;isipokuwa waliozindikwa kama anavyofanya Bi Kizee kwa watoto (uk 7).
“………..haya aje mmoja hapa. Watoto
wanasogea………”
Mwandishi anaonesha kuwa jambo hili la uchawi na ushirikina lipo kama
kawaida ya mambo yote lina nafasi yake na wakati maalumu na wakati huo ukiisha
halina nguvu tena kama asemavyo Bi Kirembwe (uk 115);
“………..Tuseme uchawi wangu unaanza kupungua?..........Lakini
aaa, potelea mbali, mimi najijua ni umbo la milele………….”
9.
Nafasi ya Mwanamke katika Jamii
Katika tamthiliya hii mwandishi
amechorwa mwanamke katika pande kuu mbili,ambazo;
Kwanza amechorwa kama
mtawala wa kidikteta, atishaye watu na si kiumbe duni tena kama waandishi
wengine wanavyochora.Bi
Kirembwe amepewa nafasi na dhamana kubwa kwa Giningi. Amechorwa kama mama wa Giningi baba wa Giningi, mlezi wa Giningi, mzee
wa Giningi, mfalme wa Giningi, mchawi na hakimu wa Giningi (uk 33-35) na (uk
56-60).
Pamoja na kupewa dhamana Bi Kirembwe ametumia nafasi hii
vibaya,kwani anaitumia kwa kunyanyasa,kuonea,kugandamiza na kunyonya watu.Anashindwa
kutumia vizuri nafasi hii ya uongozi aliyopewa kuendeleza Giningi pamoja na
wananchi wake:
Kwa upande mwingine mwanamkeamechorwa
kama mwanamapinduzi,mfano mzuri Bi Kizee ambaye ameonekana wazi
kuchukia matendo maovu ya Bi Kirembwe pamoja na viongozi wengine Giningi.Amesimulia
watoto hadithi hii ili waone wenyewe matendo hayo ili waweze kurekebisha mfumo
wa aina hii wa maisha (onyesho la 1, 6, 10).
10.
Hali
ngumu ya Maisha
Katika tamthiliya hiimwandishi ameonesha
kuwa hali ngumu ya maisha huwakumba sana watu wa tabaka la chini.Watu wa tabaka
hili wana hali ngumu ya maisha kulinganisha na ile ya watu wa tabaka la juu.
Tabaka la juu hutoa ahadi za uongo kwa
tabaka la chini lakini halitekelezi ahadi hizo (uk 18);ndio maana shule hazina
vitabu,madawati,chaki,vifaa vingine,mishahara kidogo,hakuna chakula,madawa na
vifaa vingine vya hospitalini hakuna hospitalini (uk 21).Kukosekana kwa vifaa
hivi vyote kunasababisha hali mbaya ya maisha kwa watu wa tabaka la chini ambao
ndio wengi.
Kwa upande wa tabaka la juu (tawala) linaona kuwa, hali hiyo
mbaya ya maisha imesababishwa na vita vya Wanaginingi pamoja na ukame. (rejea uk 44-45).
Pia tabaka hili (tawala) linaona kuwa, hali ngumu ya maisha
inasababishwa na kushuka kwa bidhaa zetu katika masoko ya nje na kupanda kwa
bei za vifaa kutoka nje.Katika (uk 98),
kwa upande mwingine mwandishi anaonesha kuwa mvua,ukame,mbolea,vita,mafuta….vimechangia
kwa kiasi kidogo sana kuleta hali mbaya ya maisha.Ukweli ni kwamba,hali mbaya
ya maisha imeletwa na ubinafsi wa viongozi wetu,rushwa na unyonyaji
unaoendeshwa na watawala.Mtolewa kwa upande mwingine anaona kuwa,hali mbaya ya
maisha inasababishwa na kuwa na maneno mengi bila matendo.
UJUMBE
Ø Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na uongozi mzuri,tufanye
mapinduzi, tujitoe mhanga, tupige vita rushwa na tuzingatie elimu itakayowakomboa
watu kifikra.
Ø Kila jambo lina wakati wake ukiisha na jambo hilo linaisha;
kamwe wakati haulazimishi kufanya jambo la milele.
Ø Kufanya mapinduzi katika jamii si mchezo na lelemama bali
kunahitajika wapatikane ambao wako tayari kuifia jamii yao kama alivyofanya
Mtolewa.
Ø Dunia imejaa matatizo mbalimbali, hivyo lazima watu wafanye
bidii kuyatatua matatizo hayo.
Ø Tuchukie, tuyaangamize na kuyakemea maovu katika jamii,
kwani hayana faida yoyote kwa jamii.
Ø Tusipendelee urahisi katika maisha.Maisha ni mapambano,lazima
tupambane ndipo utaishi maisha mazuri.
MIGOGORO
v Mgogoro kati ya Mtolewa na Bi Kirembwe,chanzo cha mgogoro huu ni mtolewa kutaka mabadiliko kwa
kuwalisha wari unga wa rutuba ili wampinge bi kirembwe,suluhisho ni mtolewa
kuuawa.
v Mgogoro kati ya Mtolewa na Sauti za wahenga,chanzo cha
mgogoro huu ni mtolewa kuwasaliti wahenga ambao walimsomesha ,walikumlea na walimtuma giningi akafanye mapinduzi ya utawala Bi kirembwe badala yake yeye
aliungana na bi kirembwe.Suluhisho ni wahenga kumkumbusha mtolewa.
v Mgogoro kati ya Bi Kirembwe na viungo vyake vya mwili yaani
macho,mikono na miguu (mgogoro binafsi),chanzo cha mgogoro ni viungo vya bi kirembwe kushindwa kufanya
kazi na suluhisho ni bi kirembwe aliachia madaraka (alikufa).
v Mgogoro kati ya bi kirembwe na mtangazaji,chanzo cha mgogoro
huu ni mtangazaji kuanza kumpinga bi kirembwe na utawala wake,suluhisho ni bi
kirembwe kumkaba na kumuua mtangazaji..
FALSAFA
Mwandishi anaelekea kuamini kuwa palipo
na mvutano kati ya wema na ubaya,lazima wema hushinda na hivyo haki hutawala.
MSIMAMO
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi,
kwani ameonesha wazi matatizo mbalimbali yanayoikabili njamii yetu kama vile
uongozi mbaya, rushwa, dhuluma, kukosekana kwa demokrasia ya kweli, hali ngumu
ya maisha, n.k.
FANI
MUUNDO
Tamthiliya ina muundo changamano;yaani kuna visa viwili
ndani ya kimoja au tamthiliya mbili ndani ya moja.Kuna kisa cha Bi Kizee na
Watoto na kisa cha Maisha ya Giningi.
Kimpangilio tamthiliya imegawanyika katika maonyesho kumi.Onyesho
la 1, 6 na 10 yanahusu Bi Kizee na Watoto lakini maonyesho yaliyobaki yanahusu
maisha ya Giningi.Mwisho maonyesho yote yanafanya kisa kionekane kama mduara,
kwani kisa kinamalizika pale kilipoanzia tena kwa maneno yaleyale.Kuhusu
mtiririko wa matukio,msanii ametumia muundo rukia ambapo matukiohurukiana na
huenda nyuma na mbele
MTINDO
Mwandishi ametumia mtindo changamano.Kuna
mtindo wa monolojia (masimulizi) na dayolojia (majibizano).Vilevile mwandishi
amechanganya tanzu tatu katika tamthiliya hii: Ngano,Ushairi na Tamthiliya na Nafsi
zote tatu zimetumika.
WAHUSIKA
Wahusika wakuu: Bi Kirembwe, Mtolewa na
Bi Kizee.
BI KIREMBWE
Ø Mtawala mkuu wa Giningi
Ø Amejilimbikizia madaraka
Ø Ni mwakilishi wa viongozi madikteta,mfano:Anaua watu ovyo,anawanyima
watu uhuru, hapendi mabadiliko.
Ø Amejitangazia utawala wa maisha
Ø Anapenda starehe
Ø Anatumia elimu yake kuwafumba watu macho
Ø
Hafai kuigwa katika jamii
MTOLEWA
Ø Mwanamapinduzi
Ø Aliwalisha Wari unga wa rutuba
Ø Jasiri na mvumilivu
Ø Alijitoa mhanga kuifia nchi yake
Ø Mpigania haki
Ø Mtetea wanyonge
Ø Mpinga dhuluma
Ø Anafaa kuigwa katika jamii
BI KIZEE
Ø Ndiye anayesimulia habari za maisha ya Giningi
Ø Anapenda haki na usawa
Ø Anawatayarishia vijana kufanya mapinduzi
Ø Anafaa kuigwa katika jamii
BAWABU I - II
Ni wahusika wadogo na ni wawakilishi wa vyombo vya dola
ambavyo vinaendeleza rushwa na ukandamizaji wa watu wa tabaka la chini. Hivyo
hawafai kuigwa katika jamii. Wahusika wengine ni: wari, watoto, wazee, wasichana, n.k.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha iliyotumika ni lugha ya kawaida yenye
misemo,methali,tamathali za semi,taswira na picha mbalimbali.
METHALI
v Kuishi kwingi kuona mengi (uk 6).
v Unachumia juani unalia kivulini (uk 24).
v Kikulacho kinguoni mwako (uk 67).
v Majuto ni mjukuu (uk 111).
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
v Mbona tumeambiwa una hadithi tele tumesikia hazikauki kwako
kama maji ya bahari (uk 5).
v Watoto wa siku hizi………tena wana maneno makali kama chiriku
(uk 7).
v Watu wenyewe hufanya kazi kama punda…………(uk 19).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
MDOKEZO
v Subirini , subirini………
v Sawa………sawa………..sawa
v Ndiyo…..ndiyo…….ndiyo…….Sawa! Sisi ni Wari,
TANAKALI SAUTI
v Lakini…………he……….he………he………(uk 52).
v Ha…………ha……………..haaaaaaa!
v Ha, ha, ha……………ha, ha, ha, haha!
UJENZI WA TASWIRA
Ø Unga wa ndere –
Itikadi zinazomfanya mtu katika tabaka tawala akubalike na kushika miiko yaani
elimu ya kuwapumbaza watawaliwa ili waone kila kinachofanywa na tbaka tawala ni
sawa.
Ø Unga wa rutuba – elimu ya kujitambua katika jamii na
kujitambua nafasi yako na kuwa na uwezo wa kuelimisha wengine.
Ø Sauti – mawazo ya tabaka la chini lililoathirika kutokana na
utawala wa Bi Kirembwe.
Ø Kivuli kinaishi – mawazo ya kimapinduzi yaliyokwisha
pandikizwa kwa vizazi vipya ili kudai haki na usawa.
Ø Uchawi – itikadi za viongozi wasiotaka mabadiliko.
Ø Giningi – ngazi ya utawala wa juu katika jamii.
MANDHARI
Mwandishi ametumia mandhari ya
Kitanzania kutokana na kutajwa kwa miji
kama vile Unguja na Pemba.Vilevile mambo
kama rushwa,uongozi mbaya na hali ngumu ya maisha vinaashiria nchi za dunia ya
tatu kama vile Tanzania,ambapo baadhi ya viongozi hutumia vibaya madaraka yao.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu linasadifu yote yaliyomo
ndani ya kitabu.Kitaswira linaashiria mawazo ya kimapinduzi yaliyopandikizwa na
Mtolewa kabla hajauawa ambayo vizazi vipya vilivyofuata viliyatumia hadi
vikaleta mapinduzi.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui mwandishi amefanikiwa kuonesha matatizo na mbinu za
kuondokana na matatizo yanayozikumba jamii zetu.
Kifani,mwandishi amefanikiwa kuchora
wahusika katika pande mbili yaani Wana –
mapinduzi na wapinga mapinduzi.
No comments:
Post a Comment