TAMTHILIYA YA NGUZO MAMA
MWANDISHI:
PENINA MUHANDO
WACHAPISHAJI:
DUP
MWAKA: 1982
UTANGULIZI
Tamthiliya ya Nguzo
Mama aliyoandikwa na Penina Muhando inayasawiri na kuyaelezea matatizo
mbalimbali yanayowakabili na kuwaelemea wanawake wengi wa Tanzania na Afrika
kwa ujumla. Wanawake wengi wamekuwa wakinyanyasika kwa kunyanyaswa na kuteswa
na waume zao.Mwandishi anathibitisha
hayo kwa kutueleza maisha waliyokuwa wakiishi wanawake wa Patata.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU: UKOMBOZI WA MWANAMKE
Mwandishi wa kitabu hiki cha Nguzo Mama anaelezea na kuonesha juhudi mbali mbali zifanywazo na
wanawake katika kujikomboa kutoka minyororo ya utumwa wa mwanaume na manyanyaso
mazito anayoyapata kutoka kwa mwanaume na jamii nzima inayomzunguka. Mwandishi,
baada ya kusawiri maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika na manyanyaso
anayoyapata kama vile kupigwa, kufanyishwa kazi kuliko uwezo wake, mfano :-
kulima peke yake, kufua, kuosha vyombo,
kukusanya kuni n.k., anaamua kutumia kipaji chakekuelezea jinsi gani mwanamke
anaweza kujikomboa.
Katika kitabu cha Nguzo
Mama,mwandishi anawaonesha wanawake wa Patata wahangaikavyo
katika kujikomboa.Ukombozi huo umegusa nyanja zote za maisha yaani kisiasa,
kiuchumi na kijamii.
Kiuchumi,katika kujikomboa wanawake wa Patata wanaamua kuanzisha
miradi mbalimbali ambayo itawawezesha kujipatia fedha kwa ajili ya maendeleo.
Miradi ikashamiri sehemu zote za Patata.
‘’..........Miradi tutatilia mikazo, miradi
ya kila aina vilabu vya pombe, maduka ya khanga, ushirika wa kushona, kupika,
hoteli na mengi........’’(uk 52).
Bi Pili yeye akaamua kuanzisha kilabu cha pombe ili
aweze kujikomboa kwenye maisha magumu yanayomkabili.
‘’Kaamua Bi Pili, Pombe kujipikia, na
kilabuni kuiuza
Pesa akipata, Pesa msema kweli
Na nguzo mama itasimama’’ (uk 14).
Mwandishi anaonesha umuhimu wa pesa katika kujikomboa
kwa wanawake,kwani pesa ndio hasa iletayo maendeleo stahiki.Hali kadhalika Bi
Moja na wenzake nao wakajiunga na kuanzisha viwanda vyao vya kufuma mapambo ya
nyumbani.
‘’Kutokea Bi Moja,Na lake jipya kiwa nda
kuanzisha
Mapambo ya nyumbani kufuma
Mapambo akiyauza na pesa kujipatia
Itakuwaje nguzo mama isisimame’’ (uk 17).
Kijamii, wanawake wa Patata wamehamasika kwa kuanzisha
vikundi vya akina mama, ambavyo vitasimama imara kutetea maslahi yao na
kusaidiana wao kwa wao katika kujikomboa.Mfano mzuri ni kikundi lcha kina Bi
Nne, yeye alikuwa kiongozi wa umoja huo akiwahamasisha wanawake wenzake ili
waweze kuinua ‘’nguzo Mama’’
‘’Bi Nne anapiga makofi nao
Anasimama na kutoa hotuba
Nguzo mama hoyee’’ (uk 11).
Bi Nne naye hakuwa nyuma katika kazi yake ya ualimu.Akaanzisha
Umoja wa Walimu, nia ikiwa kuwasaidia kutatua matatizo yao mbalimbali
yanayowakabili katika ufundishaji, Bi Nne anawashauri walimu wenzake kuanzisha
umoja huo ili kwanza waanze na matatizo
yao yanayowakabili katika hatua ya kujikomboa kama wanawake.
‘’Kutokea Bi Nne, wenzake wengi
Makubwa hawakujitakia, vizuri walishauri
Tuanze na yetu matatizo, Ndani yah ii yetu kazi
Kazi yetu ya kufunza vyema kuichapa
Vigingi vikitokomea,
vyema vijana watafunzika
Wakifunzika wote Patata
‘’Nguzo Mama itasimama’’ (uk 20).
Hapa mwandishi anaonesha elimu kama njia moja wapo
itakayoweza kuwakomboa wanawake pale aliposema;
‘’Vigingi vikitokomea, vyema vijana
watafunzika, wakifunzika wote Patata nguzo mama itasimama’’
Mwandishi pia anaonesha ushirikianao wa jamii nzima,
wanawake kwa wanaume kutasaidia sana katika kuleta ukombozi wa mwanamke na
mwanamke peke yake, abadani hatoweza kusimamisha ‘’Nguzo Mama’’
‘’Bi Nane ‘’Tushirikishe wanaume pia. Nguzo mama ina faida kwa wote
Tuite na watoto wote faida kwa wote –
wao taifa la kesho’’
Kwa hiyo, mwandishi licha ya kuonesha
utakiwaji wa jamii nzima katika ukombozi wa mwanamke, pia anaonesha faida za
ukombozi huo hazitamlenga mwanamke tu bali na jamii nzima inayomzunguka
mwanamke.
Pia umoja nao unaoneshwa kama njia itakayowezesha
wanawake waweze kujikomboa.
‘’Bora tufanye mikutano
Labda na maandamano
Maazimio tuyatangaze
Tukupambeje maua’’ (uk 7).
Mikutano kama ilivyo kawaida yake
ingewezesha kuwapasha watu wengi zaidi juu ya ukombozi wa mwanamke na
manyanyaso wapatayo. Hivyo watu wengi wangehabalishwa katika uwanja wa siasa.
Nafasi za uongozi kwa wanawake ni moja kati ya njia ambazo zingemwezesha
mwanamke kujikomboa.
Katika tamthiliya hii, mwandishi
anaonesha juhudi mbalimbali zifanywazo na wanawake wa Patata katika kuchukua uongozi wa Serikali.
‘’.........Akina mama watapewa vyeo, orodha
tumeshapanga. Tutapata mawaziri, mameneja, mabalozi na kadhalika. Wengine
tayari wameshapata kama mnavyofahamu’’ (uk 52).
Baadhi ya wanawake ambao walipata
uongozi ni Bi Nne ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya vyeo.
‘’He! Kweli
nimekumbuka looo!
Nimechelewa
mkutano wa kamati ya vyeo
Na mimi ndiye mwenyekiti, si mnajua
tunavyokazana kuwaombea mabibi vyeo maana wanasahauliwa. Lazima tufanye huo
mkutano’’ (uk 42).
Bi Tatu yeye alikuwa mwenyekiti wa
kamati ya malezi bora
‘’My God ! Mmeona! Tena Shangazi mwenyewe
ndiye mwenyekiti wa malezi bora’’ (uk 50).
Ukombozi wa fikra pia umeoneshwa kama
tatizo linalowasumbua wanawake wa Patata. Mfano anamuonesha Bi Nane dhidi ya
madai aliyoambiwa. Bi Nane hasa alipokubaliana na kila kitu alichoelezwa na Bi
Nne.
DHAMIRA NDOGONDOGO
1. UONGOZI MBAYA
Mwandishi wa tamthiliya hii, anaanza kwa
kuonesha umuhimu wa kiongozi katika jamii yoyote ile. Pia anaonesha kiongozi
kama mtu aliyeshikilia jamii anayeweza kuipeleka jamii anayeweza kuipeleka
jamii yake kwenye neema au mdomo wa samba kutegemeana na uongozi wake
atakavyokuwa anaupeleka.
‘’........Tena kwetu sie kiongozi huongoza
njia
Aweza kuwapeleka kwenye neema
Au mdomoni kwa samba........’’ (uk 22).
Lakini viongozi hao, wengi wao
wamekuwa wakizipeleka jamii zao kwenye mdomo wa samba,kwani viongozi hao hutumia
uongozi kama dhana ya kuonesha wao ni watu watukufu na walio kwenye daraja la
juu katika jamii.Wakiamuawatakavyo bila kufuata miongozo iliyopo katika uongozi huo.
‘’ Bi Nane akawaza
Kumbe kazi hii ya uongozi au
uwenyekiti
Inampa mtu
uwezo wa kufanya
Mambo kinyume cha
kawaida......’’ (uk 24).
Mwandishi anaonesha uongozi mbovu kama ndio chanzo cha
matatizo yanayoikabili jamii ya Wanapatata. Viongozi kama akina Bi Nne na Mwenyekiti
wa Kamati ya Mashauri,wanaoneshwa kama viongozi wabovu wanaosababisha kuwa na
matatizo katika jamii ya Patata.
‘’ Lahaula! Kumbe ndio maanawatu
wengi wanaulilia uwenyekiti,kwani ni rahisi kazi yake,kiholela mambo
kujifanyia,masikini Patata si ajabu kumbe vurugu kutapakaa’’ (uk 25).
Mwandishi anaonesha vurugu
zinazoisonga Patata kuwa zimechangiwa na uongozi mbovu.Udikteta pia unaoneshwa
kuwa ni zao la uongozi mbovu uliopo kwenye jamii ya wana Patata.Viongozi kama
mwenyekiti wa kamati ya mashauri wamechorwa kama madikteta,wanaotumia uongozi
wao watakavyo,wajisikiavyo kutoka mioyoni mwao au vile waambiwavyo na watu wao
wa karibu bila kufuata misingi na
miongozo waliyowekewa na katiba ya jamii zao. Mwenyekiti wa kamati ya mashauri
anatumia vitisho kumlazimisha Bi Nane kusemaasichokijua ili mradi tu yeye ni
kiongozi.
Pia mwenyekiti anaonesha udikteta
wake pale alipotaka kuamua kesi aliyosikiliza upande mmoja tu wa mashtaka,tena
maelezo hayo kapewa wakati mshtakiwa hayupo.
‘’........Vipi mtu atakubali kutoa ushauri
kutumia vitisho!
Kufuatilia maelezo ya mshtaki peke
yake
Tena yaliyoelezwa wakati mshtakiwa
hakuwepo
Vipi mtu atamshauri mshtakiwa
Bila kujua mawazo yake’’ (uk 24).
Pia mwandishi anaonesha udikteta
uliokithiri unavyoitawala jamii ya Patata, yaani mtu mmoja anaweza kuamua
maamuzi yanayotakiwa kufanywa na kamati nzima. Tena ajifanyiaye mambo bila kushirikisha kamati hiyo.Mfano ni pale
mwenyekiti wa kamati ya mashauri walipokaa na kuunda kamati ya watu wawiliili
wamshitaki Bi Nane.
‘’ ....Vipi
watu hawa, wawili, moja, mbili kujifanya wao kikao.
Katiba gani inasema mwenyekiti peke
yake
Awe na kikaocha kuamua mashauri
Au asaidiane na mtu si mwanakamati
Mwenyekiti na mshtaki kuwa kikao?!
Sijapata kusikia, hiki ni kikao cha
hila.
Kusema sitajisumbua, kimya
akijikalia’’ (uk 24).
Mwandishi anaendelea kutuonesha
maajabu ya uongozi mbaya wa wanaPatata
ulivyokithiri,kwani wale viongozi walikuwa wanategemewa ndio haohao wanaofanya
mambo ya ajabu.
‘’Na ajabu kupita yote
Vipi mwenyekiti bila kamati
Akatoa ushauri katika mashtaka?’’ (uk 25).
Hapa msimulizi alikuwa anaendelea
kutuonesha jinsi mambo yalivyo mabaya hapo Patata.
Kwa wema na huruma
‘’Mwanangu mie sijui labda kamuulize
Bi Nne’’ (uk 54).
Chizi anamshangaa Bi Saba, kwani
licha ya kuwa kiongozi hajui hata
ninimaana ya Nguzo Mama. Chizi
anaendelea kusema;
‘’Lakini juzi kachaguliwa katibu
Sijui wa kamati gani ile. Nimesahau’’
(uk 55).
2. DHULUMA
Mwandishi amejadili tatizo la dhuluma lilivyoigubika jamii yetu ya
leo.Katika tamthiliya yake ya Nguzo Mama anajaribu kutuonesha jinsi jamii ya
Patata, kama zilivyo jamii nyingine, ilivyooza kwa dhuluma,hasa kwa wanawake
wajane pindi tu wanapofiwa na waume zao.
Katika
tamthiliya ya Nguzo Mama,mwandishi anatumia mhusika wake Bi Saba kuonesha jinsi
ganiwanawake wengi wa Kiafrika wanavyodhulumiwa mali na ndugu za waume zao
pindi tu wanapofariki. Bi Saba baada ya tu ya kufiwa, shemeji yake walikuja na
kugawana vitu vya Bi Saba pasipo kumuachia hata kitu. Watoto nao walichukuliwa,
wakimwacha Bi Saba masikini akihangaika huku na kule bila mafanikio.
‘’ Haa!
Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda!
Hata
sufuria! Nitalala wapi na nitapika wapi jamani?’’ (uk 43).
Mwandishi
anaendelea kueleza uozo wa dhuluma ndani ya Patata ilivyoletamatatizo na huzuni
kwa wanaodhulumiwa huku wakikosekana watu wa kuwasaidia, hakuna mtu wa kumsaidia mwenzak, dhuluma imetapakaa kila
mahali Patata.
‘’Akalia
Bi Saba tena akalia, hana wa kumsaidia
Mumewe kafa
nduguze wamekuja juu,
Pesa
wamechukua senti tano haikubaki
Vyombo na
nguo zote wakagawana
Roho
ikampasuka Bi Saba kuwaona hao ndugu
Walivyogombania mali wasiyochuma
‘’Kiti
hiki changu’’ Mie lile jembe’’
‘’Mie
suruali hizi’’ ili mradi ilikuwa zogo’’ (uk 43-44).
Mwandishi
pia anaelezea juu ya dhuluma, kwa kitu au mali uliyoichuma kwa jasho lako
mwenyewe,ukahangaika huku na kule kutafuta mali hiyo lakini mwisho wanakuja
wachache kukudhuluma mali hiyo. Mfano Bi Saba.
Uongozi
mbaya pia umesababisha kuondoka kwa demokrasia kwa watu wa Patata, kwani wachache wenye madaraka ndio wanaoonekana
kupewa kipaumbele kuzidi wenzao, wanaowaongoza.Mfano ni pale Chizi alipokuwa
anamuuliza Bi Nne akimwonesha kuwa yeye ni mtu mkubwa na anapewa kipaumbele
zaidi. Anasema;
‘’.......Lakini
bibi yangu aliniambia
Binadamu
wote sawa, lakini wengine ni sawa zaidi.
Na
huyu ni mmoja wa hao’’ (uk 58)
Pia
mwenyekiti wa kamati ya mashauri hafuati
demokrasia inayotakiwa kwa kumlazimisha na kumpa masharti yaliyo kinyume
kabisa na katiba,yenye kuonesha udikteta uliokithiri usiofuata na unaoepuka kabisa
demokrasia .
‘’
Jambo la pili nakueleza kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya mkutano bila
kibali cha ofisi hii. Na ofisi hii lazima iletwe kumbukumbu za mikutano yote
iliyofanyika hapa Patata. Sheria hii ipo na inajulikana kwa hiyo urudi ufuate
mashauri yangu’’ (uk 25).
Viongozi wa
Patata wanaoneshwa pia viongozi
wasiopenda kuwajibika katika kufanya kazi za kuliletea taifa lao
maendeleo yao, wawapo tu! Kazi kuongea maneno yasiyotekelezwa. Mfano ni Bi
Tatu, yeye ni kiongozi wa malezi bora lakini ameshindwa hata kulea watoto wa
kaka yake anayehangaika mtaani (chizi). Pia anashindwa hata kujishughulisha
kufanya vijibiashara.
‘’My God!
Mmeona! Tena Shangazi mwenyewe ndiye mwenyekiti wa kamati ya malezi bora yeye
mwenyewe hafanyikazi…..’’(uk 50).
Licha ya
kuwa viongozi wa Patata hawapendi kuwajibika, lakini pia wanaoneshwa kama
wasiokuwa na elimu, na wasiojua nini kinaendelea hata kwenye uongozi wao.Chizi
anasema;
‘’…..Siku moja nikamwendea, labda niwe kweli chizi
‘’Shikamoo’’
‘’Marhaba’’ Bi Saba nieleze.
Nini kitu
Nguzo Mama, naona hapa Patata mambo yamevurugika, kila ninakogeuka nasikia
nguzo mama, Nguzo Mama kitu gani? Vizuri, alijibu.
Yeye
alihangaika huku na kule ili ajiletee maendeleo yake naya watoto wake, lakini
bado mumewe alipofariki nduguze wakaja
na kumdhulumu jasho halali.
‘’Atawaambiaje
watu hawa,
Kuwa vyote
walivyochukua Zaidi ni jasho lake
Watoto wake
wapenzi mwenyewe aliwalea
Wakati wao
baba mnatindi akiyachapa
Na pesa kwa
pombe kuangamiza
Pesa ya
ndugu yao iliishia chooni’’ (Uk 44)
Hivyo mwandishi anaitaka jamii kupinga
dhuluma ili kuleta maendeleo.
3. ELIMU
Katika tamthiliya
hii elimu inaoneshwa kama jambo la muhimu sana kwenye maendeleo ya jamii yoyote
ile.Mwandishiameonesha kuwa kila nyumba ya mafanikio au maendeleo yoyote yale
kuna elimu. Bi Nne anakubaliana na ukweli huu pale alipokuwa anasisitiza somo
la ushonaji liingizwe kwenye mitaala ya wanafunzi mashuleni ili waweze
kujifunza kushona vitu mbalimbali kama mapambo na nguo. Kisha wauze wapate
maendeleo.
‘’……….Pia
somo la ushonaji litatiliwa mkazo mashuleni. Kila shule italifundisha ili
watoto wetu wajue kushona, wavae vizuri na kupamba nyumba zao vizuri’’ (uk
18).
Bi Nane
naye anaonesha na kuthibitisha ukweli juu ya umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya
jamii ya Patata. Yeye anaonesha kuwa kama watu hawatapata elimu, basi hata
maendeleo hawatayasimamisha yakasimama.
‘’…….Tuvitoe
vigingi vile vituzuiavyo
Kazi yetu ya
kufunza vyema kuichapa vigingi vikitokomea, vyema vijana watafunzika
Wakifunzika
wote Patata.
Nguzo Mama
itasimama’’ (uk 20).
Ukosefu wa elimu nao unaoneshwa kama tatizo kubwa kwa
jamii ya Patata linalosababisha kukosekana kwa maendeleo na kuwakomboa
wanawake. Viongozi wanaoneshwa kama watu wasiokuwa na elimu, wasiojua hata
kinachoendelea kwenye uongozi wao. Mfano ni pale Chizi alipomuuliza Bi Saba
ambaye ni kiongozi kuhusu maana ya Nguzo Mama. Lakini Bi Saba anaonekana hajui
chochote kuhusu Nguzo Mama. Baada ya Chizi kumuuliza Bi Saba anajibu;
‘’Mwanangu
mie sijui labda kamuulize Bi Nne’’.
Yaani Bi
Saba anaonekana mtu asiye na elimu kabisa, kwani hajui hata jambo alifanyalo,
Chizi anaendelea kutuhabarisha kuhusu Bi Saba,
‘’Lakini
sijui kachaguliwa katibu sijui wa kamati gani ile. Nimesahau’’ (uk 55)
Elimu
pia inaoneshwa ilivyopana na katika hayo mapana yake ya kila sehemu ina umuhimu
wake. Elimu ya malezi, kama zilivyo elimu nyingine, inaonekana kuwa na umuhimu
mkubwa sana katika jamii hasa ikizingatia kwenye kipindi hiki ambacho magonjwa
ya ajabu yanayoizunguka jamii kama vile Kisonono, Kaswende na Ukimwi. Hivyo
mwandishi anasisitiza kuwepo na elimu ya malezi itakayowasaidia vijana na
wanawake hasa wale wanaotupa watoto kwenye mapipa na vyooni. ‘’……….Pia
wasichana kutupa watoto kwenye mapipa, kuna semina wiki ijayo kuzungumzia swala
hili, ni aibu kubwa sana kwetu’’ (uk 52).Sharti wapate elimu ya malezi
waache tabia hiyo.
4.
USALITI
Ni tendo la kuchonganisha watu kwa
kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka huku ili wapate kugombana .Kama tafsiri
ya usaliti ilivyo, Mwandishi amefanikiwa kuonesha suala la usaliti kwa ustadi
mkubwa,pale alipowachora wahusika wake kama wasaliti. mfano ni pale walimu
walipomsaliti mwenzao Bi Nane kwa kutoa siri za vikao wanavyovifanya na
kumpelekea Bi Nne,ambaye anaonekana kama adui wa Bi Nane.
‘’……..Tena Mwenyekiti mimi
nilikwambia hao walimu wengine hawampendi huyu Bi Nane, yeye tu ndiye
anayejiweka kimbelembele kama wanampenda mbona walimu hao hao wanatoka wanakuja
kunieleza mipango yao? Sema basi tukusikie’’ (uk 22-23).
Matokeo ya usaliti huu yalimuweka
pabaya Bi Nane, kwani alisongwasongwa na kuhangaishwa na uongozi wakimtuhumu
kama msaliti na mvuruga Amani anayetaka kusimamisha maendeleo ya Patata.
‘’Lahaula!
Sawa hawajakaa makubwa yakawakuta!
Barazani wakaitwa mashtaka kuyajibu’’ (uk 20).
Mwandishi anaendelea kutuonesha
usaliti ulivyosababisha Bi Nane kuingia kwenyematatizo pale mwenyekiti
alipokuwa anamuhoji.
‘’Kwa kifupi ni kwamba, tumepata habari
kwamba wewe umeanzisha kikundi cha kupinga juhudi za wenzetu hapa Patata za
kusimamisha Nguzo Mama. Tena kikundi hicho cha walimu watupu kinabagua wasio
walimu. Tena kikundi hicho kimekuwa kikifanya mikutano kupanga njama za
kuchafua juhudi za wenzenu’’ (uk 21).
Mwandishi pia ameonesha
dhamira yenye kufanana na usaliti japokuwa kitafsiri sio usaliti.
5.
UMASIKINI NA MAGONJWA
Umasikini
ni hali ya kukosa mali, yaani mtu kutoweza kukidhi haja ya mahitaji yake ya
kila siku. Kuishi chini ya kiwango kinachotakiwa.Umasikini ni tatizo kubwa linalozisumbua nchi za dunia ya
tatu,limejadiliwa kwa kina na mwandishi.Patata ni moja ya jamii za watu
masikini wasioweza kujimudu kimaisha wahangaikao huku na kule kusaka riziki
bila mafanikio. Jamii ya Patata inaonekana ikisumbuliwa na shida chungu nzima.Bi
Tano shida zimemwandama, watoto wake wanapata tabu, hata hela ya kuwanunulia
nguo hana sembuse chakula. Watoto wake siku nyingine wanashinda na njaa wakiangalia
siku inavyopita, jua likitokea mashariki kuelekea magharibi.
‘’Taabu,
taabu! Taabu!
Watoto
wangu hawana chakula
Hawana
nguo, hawana chakula
Watoto
wanashinda na njaa.
Wanalala
na njaa’’ (uk 40).
Hali
kadhalika Chizi naye anaonesha hali hii ya umasikini pale anapolalamika kuumwa
na njaa na njaa yenyewe inaonekana si ya siku moja tu bali ni muda mrefu, kwani
anaelezea kuwa njaa hiyo huwa haijimuisha.
‘’Labda
tuite njaa
Kama hii
inayomuuma
Njaa
kamwe haimuishi’’ (uk 31).
Mwandishi
pia anaelezea umasikini ulivyotawala Patata kiasi ambacho watu wanashindwa hata
kubadili nguo,yaani wao wamekuwa na nguo za ‘’kauka nikuvae’’.
‘’Bi Pili : Nimeifua mchana huu, asubuhi si
nilidamkia shambani…..’’(uk 36).
Mumewe bwana
Sudi anajibu,
‘’Kelele!
Sasa mimi nitavaa nini
Utaikausha
kwa moto hiyo nakwambia
Mimi nataka kurudi, nilikotoka
nimeacha pombe kafiri unATAKA WENZANGU WAIMALIZE!
Kausha hiyo
nguo haraka kabla sijakupiga’’ (uk 36).
Mwandishi
katika kuonesha umasikini ulivyoibuka Patata anazichunguza na kuzifichua sababu
zinazoleta umasikini huo.Moja kati ya sababu hizo ni uvivu na kutojituma katika
kufanya kazi.Wananchi wa Patata ni wavivu na hawajitumi.Wanawake wapo tu
wanapiga soga huku miguu waitandaza kwenye mikeka.Mfano Bi Moja yeye asilani
yumo ndani tu anashinda utadhani mwali anayefundwa.Kutwa domo akilipiga tena
huku miguu kainyosha , na kamwe hutamwona jasho likimtoka akifanya kazi.
‘’Mwenzenu
miye nashangazwa na maneno ya Bi Moja
Hiyo dhahabu
na fedha, na huu wake uturi
Wapi
atavipata, kumbe ndani anashinda
Miguu
kainyosha na domo kujipigia
Kamwe
sijamuona, akilitoa jasho kazi kujifanyia
Wapi niambie
inapatikana fedha na dhahabu
Bila kazi
kufanyia, niende na mie Chizi
Nyingi
nikajitolee’’ (uk 47-48).
Kama ilivyo
kwa wanawake wa Patata, wanaume ikiwa ni mara mbili yao kutwa nzima kiguu na
njia, wanaume hawajui hata jembe linashikwa vipi.Wao ni pombe tu,pombe na wao,
kutwa nzima wanashinda vilabuni, wakinywa na kupiga zogo tu mara hiki mara
kile. Uvivu umewajaa hawataki kabisa kujishughulisha.Kazi zote wamewaachia wake
zao hata zile za kuihudumia familia.Hata kile kidogo kinachozalishwa na wake
zao basi huwapokonya.
‘’Huyu Bi
Pili rohoni anasikitisha, Atakufa masikini hohehahe kama mie, Lakini
ninashangaa kala nini bibi huyu, Walahi sijaona mwingine hodari kumpita lakini
yule wake mume, nini kamlisha kazi zote afanya yeye bi Pili, matunda yote ale
Bwana Sudi.
Jasho lake
Bi Pili laishia kilabuni,huyu wake bwana Sudi Matindi anayatandika usiku na
mchana siku moja nitamuuliza Bwana Sudi, Dawa gani aliyompa Bi Pili na mie
nikabahatika mke kujipatia awe kama Bi Pili ambaye taabu yote atakubali, watoto
anizalie na pia anilelee, chakula anilimie na pia anipikie.Nguo anifulie na
pombe anipatie.Nikipata yote haya!
Kama ilivyo shilingi yenye pande mbili,ndivyo kila
mwenye umasikini maradhi nayo hayaeshi.Jamii ya Patata inaoneshwa kama jamii
yenye kusumbuliwa na maradhi mbalimbali hasa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
‘’……Nimeishi
siku nyingi, Na mengi nimeyaona, ugonjwa wa kaputula na ule wa magunia
Pia
kipindupindu vile vita vya mdachi.
Na yule
Nduli Amini Lkini ya Patata.
Sijui niite
vita au ugonjwa’’ (uk 31).
Umasikini
pia umeoneshwa wakati Bi Moja alipokuwa anamdai mume wake fedha za kununulia
khanga (Shabani).
‘’Nimekwambia
mie hela sina sasa unataka nikaibe?’’ (uk 35).
6.
UVIVU NA UZEMBE
Uwajibikaji
ni hali ya kufanya jambo pasipo hiari,yaani unalazimika kulifanya.Tofauti na
ilivyo kawaida kwa watu wa jamii ya Patata wenyewe wamekuwa si wawajibikaji,yaani
hawawajibiki ipasavyo katika kufanya kazi.Wananchi wa Patata wanaoneshwa kama
watu wavivu wasiopenda kujituma katika kufanya kazi.Dhamira hii,mwandishi anaonesha
uvivu na uzembe kama chanzo
kilichosababisha kufifia na kushindwa kuinua Nguzo Mama.Mfano mzuri ni pale
wanawake wa Patata waliposhindwa kuinua ‘’Nguzo Mama’’. Mfano Bi Moja yeye
anaacha kuinua na kuvuta Kamba na kuanza kuongea na Bi Tano kuhusu khanga. Kwa
muktadha waliokuwepo wasingepaswa kuzungumzia mambo hayo.Bi Tano anamuelekeza
kuwa zinapatikana kwa Mwarabu na pia anamtahadharisha kuwa anapaswa kuziwahi la
sivyo zitakwisha.Mara Bi Moja anaondoka na hapo Bi Nane anashituka na kuuliza,
‘’ Sasa jamani Bi Moja anakwenda wapi tena!!
Bi Moja
akiwa mbali anajibu,
‘’Aaa jamani
nitarudi lakini khanga hizi sizikosi’’ (uk 34).
Bi Sita naye anaoneshwa kama mwanamke asiye
muwajibikaji na asiyejali umuhimu wa kazi za maendeleo, kwani naye baadaye
anaacha kuvuta kamba na kumfuata mwanaume eti kwasababu alimkonyeza ili amfuate
licha ya umuhimu uliopo kwenye kuinua ‘’Nguzo
Mama’’.
‘’……Mara anatokea Maganga, Bi Sita anamfuata wanachekeana. Maganga
anamfanyia ishara amfuate’’
Bi Tano anaona yanayofanyika upesi
anaacha kamba na kuwafuata’’ (uk 38).
Bi Tatu
naye kwake Nguzo Mama si mali kitu Zaidi
ya mume na sherehe,hivyo anawasusia wewnzake kamba na kutimkia kwenye Volvo lililomfuata na kuelekea
kwenye pati ambayo kwake yeye ni muhimu Zaidi kuliko Nguzo Mama.
‘’Jamani mie
naondoka mnaiona Volvo hiyo imenifuata mie’’. Anaendelea kusisitiza ‘’Siyo
utani ndugu nyangu,Tunakwenda kwenye pati na mume wangu leo saa moja lazima
nipalilie unga kwa baba watoto wangu ati. Nitakula nini’’ (uk 41).
Hata
viongozi nao wanaonekana wababaishaji waliojaa maneno matamu mdomoni lakini pasipo
uwajibikaji kwa vitendo.Bi Nne kama kiongozi naye anaondoka kwenye kazi muhimu,
kazi ya vitendo itakayowezesha maendeleo ya mwanamke kupatikana na kwenda
kwenye vikao,kazi ya kupiga soga bila utekelezaji.
‘’Hee!
Kweli nimekumbuka. Loo!
Nimechelewa
mkutano wa kamati ya vyeo na mimi ndiye mwenyekiti……’’ (uk 42).
Kwa
kutowajibika huko wanawake hao wa Patata wakasababisha kushindikana kuinua kwa
‘’NguzoMama’’, nguzo ambayo ni egemeo
lao la maendeleo.Na ndiyo ufunguo ambao ungeweza kuwaondoa kwenye minyororo ya
utumwa na ukandamizwaji wa siku nyingi. Lakini kutowajibika
kukawakosesha.Mwandishi pia anaonesha
ugumu wa maisha wa watu wa Patata unavyotokana na kutowajibika kwao.Bi Moja
anaonekana kama mwanamke asiyejishughulisha na kazi yoyote ile kutwa yumo ndani
tu katulia,kwa hali kama hii ya kutowajibika
ndiyo hasa chanzo cha umasikini.
‘’Mwenzenu
mie nashangazwa na maneno ya Bi Moja
Hivyo
dhahabu na fedha na huo wote uturi
Wapi
ataupata, kumbe ndani anashinda
Miguu
kuinyosha na domo kujipigia.
Kamwe
sijamuona akilitoa jasho kazi kujifanyia…….’’ (uk 42).
7. MAPENZI NA NDOA
Katika
tamthiliya ya ‘’Nguzo Mama’’ mwandishi
anaelezea mapenzi yasiyokuwa ya kweli, yanayojali pesa na usaliti kati ya
wanandoa.Mfano ni Maganga (mume wa Bi Tano) na mkewe Bi Tano,Maganga anaonekana
kutokuwa na mapenzi ya kweli kwa kumsaliti mkewe na kumchukua Bi Sita.
‘’Wee
Bi Sita mshenzi, unanichukulia mume wangu hivihivi kimachomacho’’ (uk 39).
Usaliti huu wa mapenzi unaleta sononeko la moyo kwa Bi
Tano. Pia unaleta hali ngumu kwa familia ya Bi Tano, kwani watoto wanalala njaa
kwa kukosa chakula na mahitaji muhimu kwa kuwa Maganga (baba yao) anamaliza
pesa zote kwa wanawake.
Mwandishi pia anaonesha mapenzi yanayoendeshwa na pesa
kuliko utashi wa mtu na mtu, mfano ni pale Bi Tatu alipowaambia wenzake
alipofuatwa na mumewe.
‘’Sio utani ndugu yangu, Tunakwenda kwenye
pati na mume wangu leo saa moja usiku, lazima nipalilie unga kwa baba watoto
wangu ati, nitakula nini’’ (uk 44).
Pia anaonesha suala la mwanaume kuwa na mke zaidi ya
mmoja lisivyokubaliwa na wanawake na jinsi gani wanavyohangaika kulibadilisha
suala hili.
8.
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA
JAMII
Katika tamthiliya ya Nguzo Mama
mwanamke amechorwa katika nafasi tofauti kama ifuatavyo;
Kwanza amechorwa kama chombo cha
starehe kilichopo kwa ajili ya kustarehesha wanaume.Mwandishi ameonesha kuwa mwanamke anatumia mwili wake kama
bidhaa iuzwayo sokoni na kumpatia faida.Mfano ni Bi Sita ambaye ni changuidoa.
“Mwenzio nautafuta huo muda siupati.
Laiti ningeupata wengi zaidi kunasa.
Kwani mmoja, wawili wanafaa kitu gani?”
(uk 29).
Pili,Mwanamke pia amechorwa kama
jasiri anayejitoa mhanga kuusema ukweli.Mwandishi anamuonesha Bi Nne anayeamua kumwambia ukweli
mwenyekiti juu ya kutokubaliana kwake na maamuzi aliyoyatoa.
“Sikubali Mwenyekiti kama nashtakiwa
haki ninayo ya kutoa maelezo vile ninavyotaka.
Nitaeleza kwa maandishi nakala
wanaohusika wote nitawapa.Kesho nitakuletea ahadi ninaweka,ukishasoma maelezo
yangu ukae ukihukumu.Lakini kabla ya hapo sipokei hukumu wala ushauri” (uk 29).
Tatu,Mwanamke amechorwa kama kiumbe
duni kisicho na thamani wala uwezo wakufanya jambo lolote katika jamii. Katika kijiji cha Patata wanaume waliwadharau na kuwabeza
wanawake wakiwaona kama watu wasiokuwa wakamilifu (uk 46).
Nne,Mwanamke amechorwa kama uvumilivu
nao umeoneshwa kama sifa ya mwanamke kwenye tamthiliya hii.Mwanamke anaonekana kutokata tamaa katika juhudi zake za
kuinua Nguzo Mama licha ya ugumu
unaowakabili (uk 11).
Tano,Mwanamke amechorwa kama mtu
anayekandamizwa na asiyepewa haki zake za msingi.Mfano ni Bi Saba alipodhulumiwa vitu vyake na nduguze mumewe
na kuambiwa hana haki ya kurithi vitu vya marehemu mumewe (uk 43).
Sita,Mwanamke amechorwa kama mtumwa wa
mumewe.Hii inaonekana pale Bwana Sudi
alipokuwa anamtumikisha mkewe Bi Pili kufanya shughuli zote za nyumbani na
shambani yeye akiwa anakunywa pombe tu (uk 49).
Saba,Mwanamke anachorwa kama kiongozi wa familia ndiye
aikuzaye jamii, kama
hapatokuwepo na mwanamke katika jamii, hakuna jamii itakayoweza kuwepo. (uk
44-45)
UJUMBE
·
Umoja ni
nguvu utengano ni udhaifu
· Kwa kila jambo la maendeleo jamii nzima (yaani wanawake,
wanaume,wazee,vijana na watoto) lazima washirikiane.
· Ulevi ni adui wa maendeleo.
· Uongozi bora ni muhimu katika kufikiamalengo.
· Malezi bora ni muhimu katika familia
· Wanawake wanafanikiwa kujikomboa siku watakayoamua kuungana
na kushirikiana
·
Wanawake
nao wapewe nafasi za uon gozi.
MIGOGORO
v Mgogoro
kati ya Bi Pili na mumewe (Bwana Sudi),Chanzo cha mgogoro wao ni pesa.Bwana Sudi anataka kuchukua
pesa za mkewe alizouzia pombe.Suluhisho ni Sudi kumpiga mkewe baada ya kukataa
kumpatia pesa hizo.
v Mgogoro
kati ya Bwana Sudi,Shaba na Totolo,Chanzo ni baada ya Shaba na Totolo kumtetea Bi Pili mke wa
Sudi asipigwe na mumewe.Suluhisho ni Shaba na Totolo kumwacha Bwana Sudi
aendelee na matusi juu yao,kwani waligundua kuwa alikuwa amelewa.
v Mgogoro
kati ya Bi Tano na Wanakikundi,Chanzo
ni kutonunuliwa kwa vitambaa.Suluhisho ni kugawana vitambaa hivyo kwa kila
mwanakikundi akauze kivyake.
MSIMAMO
Msanii ana msimamo wa
kimapinduzi kwa kuyatolea macho matatizo yanayowakabili wanawake katika kujikomboa
na vipi wafanye ili waweze kujikomboa.
FALSAFA
Msanii
anaamini kwamba ili wanawake wajikomboe
lazima wawe na msimamo,maelewano,pamoja na umoja na ushirikiano pasipo
wivu wala kubaguana.
FANI
MUUNDO
Msanii ametumia muundo wa moja kwa moja.Tamthiliya hii
imeanza kwa kuonesha jinsi nguzo mama ilivyolala na harakati za kina mama kashika
na kunyanyua nguzo mama. Mchezo umegawanyika katika sehemu nne.
MTINDO
Msanii ametumia mtindo wa
dayolojia na masimulizi.Vilevile ametumia lugha ya kishairi ili kuleta mvuto
katika mchezo wake.Pia msanii ametumia nyimbo na mianzo ya hadithi za fasihi
simulizi. (uk 3).
MATUMIZI YA LUGHA
MISEMO/ NAHAU
v Utakiona cha mtema kuni (uk 42).
v Watoto ni taifa kesho (uk 55).
v Utakufa kibudu (uk 22).
v Akachanganya ulimi {uk 57).
v Dume Malaya si dume roho yako kusumbua (uk 40).
METHALI
v La mgambo likilia lina jambo (uk 45).
v Aso mwana aeleke jiwe (uk 45).
v Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu (uk 33).
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
v Anatembea kama kapigwa bumbuazi (uk 9).
v Sikilizeni na sauti kama ndege nyikani (uk 30).
v Wanaswagwa kama mbuzi (uk 44).
v Amevaa kama mkulima wa bara (uk 24).
TASHIHISI
Ø Hasira zikampanda Bi Nane (uk 8).
SITIARI
v Mbwa mume wako
anayefuata wanawakeovyo.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
TAKRIRI
v Wakajaribu ,wakajaribu (uk 5).
v Mwachie! Mwachie! Mwachie! (uk 8).
v Toka! Toka! Toka usirudi tena (uk 8).
v Akaenda, akaenda, akaenda (uk 40).
MDOKEZO
v Wakavuta…….wakavuta……….(uk 35).
v Siku moja ………ngojeni niwaoneshe (uk 49).
v Ee ndiyo malezi ya watoto wetu………(uk 52).
v Hebu tutazame kwanza kwanini hawasogei….(uk 58).
TANAKALI SAUTI
v Lu lu lu lu lu lu lu lu lu! (uk 2 na 18).
v Ai ai ai ai ai ai ai ai ai ai! (uk 2).
MATUMIZI YA KIINGEREZA
v My God (uk 32, 49,
50).
LUGHA ZA MATUSI




WAHUSIKA
Bi Moja
v Mke
wa Shabani
v Hakuwa
na msimamo katika kusimamisha Nguzo Mama.
v Alikuwa
na tama.
v Hafai
kuigwa na jamii.
Bi Pili
v Mke wa Sudi
v Alinyanyaswa na mume wake.
v Ni mvumilivu katika matatizo.
v Ni mlezi bora wa familia.
v Anafaa kuigwa na jamii.
Bi Tatu
v Ni mpenda starehe.
v Hapendi kazi ambazo hazina mshahara.
v Anambembeleza mume wake kwa kuogopa kuachwa.
v Hafai kuigwa na jamii.
Bi Nne
v Ni mtu asiyependa maendeleo ya wenzake.
v Ana wivu, mbinafsi, mfitini na ana chuki binafsi.
v Hafai kuigwa na jamii.
Bi Tano
v Ni mke wa Maganga.
v Ana hasira sana.
v Hakumpenda Bi Sita.
Bi Sita
v Alikuwa kahaba na alikuwa anatembea na waume za watu.
v Ni mkorofi na hakupenda ushirikiano.
v Hafai kuigwa.
Bi Saba
v Alifiwa na mume wake.
v Ni mlezi swa watoto.
v Ni kiumbe duni kwani shemeji zake walimnyang’anya mali zake
zote na hata watoto baada ya mume wake kufa.
Bi Nane
v Alipenda ushirikiano na swenzake.
v Alikuwa na elimuya kutosha.
v Alipenda kuelimisha wenzakekatika shughuli za maendeleo.
v Hakuwa na chuki na mtu.
v Anafaa kuigwa.
Chizi
v Ni mpenda demokrasia.
v Alipiga vita uoga.
v Ni mfichua maovu yaliyoko katika jamii
v Anaonesha wazi matatizo yanayosababisha wanawakekushindwa
kujikomboa.
v Anafaa kuigwa na jamii.
Mwenyekiti
v Ni mtu mwenye uongozi mbaya
v Anapenda kusiliza majungu na fitina.
v Anawachukia wanawake wasomi.
v Hafai kuigwa na jamii.
MANDHARI
Mandhari ya tamthiliya hii ni ya kubuni lakini yanasawiri
maisha ya vijijini na kiasi maisha ya mjini,kwani mwandishi ameonesha mandhari
ya vilabuni,uwanjani na nyumbani.Mandhari yaliyooneshwa yanaoana sana na nchi
za Kiafrika vile Tanzania,kwani unyanyasaji na ugandamizwaji wa wanawake wa
Kitanzania ni sawa kabisa na wale wa Patata.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu Nguzo
Mamalinasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki.Kitaswira “Nguzo Mama” ni
umoja wa wanawake Tanzania (U.W.T) ambao uliundwa kwa lengo la kuwatetea,
kuwalinda na kuwapa haki na maendeleo wanawake sawa na wanaume.Tamthiliya hii
inaonesha harakati za wanawake wa Patata wakiwemo wakulima,wasomi,waalimu,makahaba
na wanaungana kuimarisha umoja na maendeleo yao.Wanafungua miradi mbalimbali
kama vile kushona,kupika pombe,pamoja na tofauti zilizopo kati yao kama vile
uzembe,majungu,fitina na kutoelewana.
KUFAULU
NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Kimaudhuimwandishi
amefaulu kwa kiwango cha juu katika maudhui yaliyomo ndani ya mchezo huu,kwani
amefaulu kutueleza matatizo yaliyowapata wanawake wengi wa Kiafrika
hususani Tanzania.
Kifani,mwandishi
ametumia lugha rahisi inayoeleweka,lugha ya kishairi inayofurahisha pia na
nyimbo zinazoburudisha. Hivyo kufanya mchezo usichoshe.
KUTOFAULU
Kimaudhui,mwandishi
ameshindwa kutueleza hatma ya
wanawake wa Patata na jamii nzima baada ya kushindwa kuinua nguzo mama.
Kifani,matumizi ya lugha ya matusi ni udhaifu wa mwandishi,kwani
matusi ni lugha isiyotakiwa katika jamii.
No comments:
Post a Comment