DIWANI YA CHUNGU TAMU
MWANDISHI: THEOBALD MVUNGI
WACHAPISHAJI: TPH
MWAKA: 1985
UTANGULIZI
Chungu Tamu ni diwani
iliyoandikwa na Theobald Mvungi miaka ya 1980.Katika diwani hii mwandishi
anaimulika jamii na kuichunguza kwa makini.Anakosoa na kutoa mapendekezo ili
wananchi waondokane na machungu yanayowaandama na kuonja utamu ambao
utawafikisha kwenye kheri.Katika diwani hii mwandishi ameonesha dhahiri jinsi
Uchungu na Utamu vinayotangamana katika harakati zote za maisha ya mwanadamu.Kwa
ufupi,diwani hii ni kipaza sauti kinacholia kwa sauti kali kuujulisha ulimwengu
juu ya uchungu unaoiandama jamii yetu ya Tanzania .
MAUDHUI
DHAMIRA KUU; UJENZI YA JAMII MPYA
Suala la ujenzi wa
jamii mpya limezishughulisha fikra za
wanafasihi wengi hapa Tanzania .Jamii
endelevu ni jamii mpya ambayo haina ubaguzi,matabaka,uongozi mbaya,yenye
kufuata misingi ya haki na usawa.Jamii iliyojikomboa katika Nyanja zote yaani kiuchumi,
kisiasa,kiutamaduni na kifikra.Wanafasihi
wa Afrika wanaitaka jamii hiyo ijengwe kwa kufuata misingi ya haki na usawa kwa
kila mtu. Wanafasihi wa Afrika wameonesha dhahiri kuwa jamii iliyoachwa na
wakoloni ilikua zimeoza na hivyo zinahitajika juhudi kubwa ili kuondoa uozo
huo.
Nchini Tanzania suala
la jamii endelevu lilianza mara tu baada
ya kupata uhuru na kuimarishwa zaidi wakati wa Azaimio la Arusha. Watanzania
walitaka wajenge jamii yenye kufuata misingi ya haki na utu,jamii isiyokuwa na
matabaka,jamii yenye viongozi waliotakasika, jamii yenye demokrasia ya kweli,jamii
isiyo na unyonyaji wa aina yoyote ile,jamii
ambayo hatamu za uongozi zingekuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi,jamii isiyo
na dhuluma ya aina yoyote,n.k.Hadi mwandishi anaandika diwani hii anaonyesha
kuwa jamii bado haijafanikiwa kuifikia
lengo la kujenga jamii mpya.
Mwandishi ameonesha vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya
na endelevu hapa nchini na mbinu za kujikwamua kutoka kwenye vikwazo hivyo.Mwandishi ametoa mapendekezo ambayo anaamini kuwa endapo
jamii itayafuata itafanikiwa kuijenga
jamii mpya na endelevu.Mbinu hizo ndizo dhamira ndogo ndogo
za diwani hii kama ifuatavyo;
1. KUPINGA DHULUMA
Dhuluma ni tendo lisilo la haki,tendo la uonevu,ukatili
au uovu. Dhuluma hupingana na haki.Suala la dhuluma hurudisha nyuma maendeleo
ya jamii na hivyo ni kikwazo kikubwa cha ujenzi wa jamii endelevu.Suala la
dhuluma limemshughulisha sana mwandishi wa diwani hii,katika shairi la “Chatu
na kuku” Katika ubeti wa mwisho mwandishi
anasema;
Basi babu akatua,
Funda
akajimezea,
Mimi tama
imejishikia,
Huzuni
imenisaliti,
Kwa chatu
kukosa dhati,
Ndipo
nikapanga hizi beti,
Ziwe kama
ndiyo hati
Ukumbusho wa
huyu dhulumati.
Katika shiri la “Chatu na Kuku”, mwandishi amelijenga
kitaswira kuonesha jinsi wakoloni (chatu) walivyoingia Afrika na kuendeleza
dhuluma.Chatu amewakilisha wakoloni na
kuku anawakilisha wananchi (Waafrika)
walioonyonywa na kudhulumiwa na wakoloni. Mayai ya kuku yanawakilisha mali ghafi waliyodhulumu wakoloni kutoka
hapa Afrika.
Katika shairi la“Chanzo
ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha jinsi ulanguzi unavyosababisha
dhuluma katika jamii.Mwandishi ameonesha kuwa chanzo cha ulanguzi ni upungufu
wa bidhaa muhimu,tamaa,pamoja na uzembe toka kwenye vyombo vya dola. Ulanguzi
husababisha rushwa,magendo na hivyo
haki haitendeki katika jamii.
Mwandishi
anasema;
“Mianzo tukiijua,
Mipango tujipangia,
Kamwe pasiwe na njia,
Ulanguzi kurudia,
Iwe tu twahadithia,
Mithili historia”.
Katika shairi la
“Kademokrasia Katoweka”mwandishi anasema;
Ya msiba atayetamka,
Udikteta waja haraka,
Mtemi na walomzunguka,
Wawatia raia
mashaka,
Dhuluma
yatangazwa fanaka.
Mwandishi anaonesha jinsi wananchi wanavyodhulumiwa
demokrasia yao ya kutoa maoni yao hadharani.Demokrasia inapokosekana,dhuluma ya
kutawala kwa mabavu huendelezwa.
Katika shairi la “Wengine
Wabaki Taabuni”,mwandishi
anajadili juu ya dhuluma wanayoiendesha wakubwa dhidi ya watu wa tabaka la
chini.Ameonesha kuwa majambazi wanayo idhini ya kufanya kila jambo kwa
wanyonge,kwani hayo majambazi hulindwa na wakubwa.Anaendelea kueleza kuwa dhuluma
inayoendeshwa na majambazi hapa nchini ni njama za walinzi (vyombo vya dola).Mwandishi Anasema;
“Majambazi
wanayo idhini,
Kufanya
lijalo akilini,
Na
hawataingia nguvuni,
Ma’na walinzi
wamo njamani,
Tabu yaanzia
kileleni.”
Mwandishi
anaeleza kuwa tabu inaanzia kileleni
maana yake ni tabu au dhuluma inaanzia kwa wakubwa.Hivyo ili tufanikishe
suala la ujenzi wa jamii mpya ni lazima
tujitoe mhanga kupambana na kila aina ya dhuluma katika jamii.
2. KUFANYA KAZI KWA BIDII
Uzembe na kutowajibika
ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya jamii yoyote ile.Jamii yoyote
ile yenye viongozi wazembe,viongozi wasiowajibika au wananchi wasiojua wajibu
wao daima itabaki nyuma kimaendeleo.Mwandishi anaitaka jamii yetu ijue umuhimu
wa kazi na kuwajibika katika suala zima la maendeleo. Mashairi kadhaa katika
diwani hii yanasisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya
jamii.Katika shairi la “Daktari askari”.Mwandishi anasema;
Saa moja jioni Landova inaingia,
Majeruhi sita na waganga pia,
Majeruhi vibaya wanalalama,
Waganga wao na sisi kazi tukaanza,
Hakuna kuamkiana au sijui nini.la,
Wagonjwa wengi misuli walikatika,
Wengine risasi walichimbiwa ,
Tukawekea damu,
Wa kushonwa,tukawashona,
Wakupasua ,tukapasua.
Katika shairi la “Daktari Askari”,mwandishi anaonesha jinsi
waganga wanavyojua umuhimu wa kuwajibika katika kazi yao ya utabibu. Ameonesha
kuwa wale waganga waliwahudumia majeruhi kwa bidii wakati wa vita.Hivyo kila
mtu anatakiwa kuwajibika kama wale waganga ndipo tutaweza kulisukuma mbele
gurudumu letu la ujenzi wa jamii endelevu.
Katika shairi la “Chanzo
ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha utekelezaji na uwajibikaji mbovu
unavyosababisha rushwa, magendo na ulanguzi katika jamii yetu Katika shairi
hili mwandishi ameonesha dhahiri kuwa uzembe toka kwenye vyombo vya dola ndio
umechangia uwajibikaji kuwa mbovu.Mwandishi anasema;
“Chombo hiki kuzembea,
Chanzo kilichozidia,
Magendo kuyatetea,
Watu kuwasaidia,
Chombo kilididimia.”
Katika shairi la “Wimbo
Wake Hotubani” wandishi anaonesha utekelezaji mbaya wa maazimio unavyochangia kuzorota kwa
maendeleo ya jamii yetu.Katika shairi hili,mwandishi ameonesha kuwa viongozi
wetu wametuna ofisini na shambani hawaingii, wanatumia madaraka vibaya,maagizo
ni midomoni bila utekelezaji, kila siku-mchana kutwa wanakunywa na kulewa, n.k.Utekeleaji
wao uko kwenye hotuba,Mwandishi anasema;
“Cheo kiko
mkononi,
Agizo li
mdomoni,
Mchana kutwa
ndotoni,
Wimbo wake
hotubani,
Raia kazi
fanyeni.”
Katika shiri la “Wengine
Wabaki Taabuni”,mwandishi anaonesha jinsi uzembe kazini,kutowajibika
ipasavyo,usaliti pamoja na rushwa unavyorudisha nyuma utekelezaji mzuri wa
maazimio tunayojiwekea.Mwandishi anaitaka
jamii ifahamu na kutambua umuhimu wa kazi na wajibu wa kila mmoja katika
jamii ndipo tutaweza kufanikisha kuijenga jamii mpya.
3. UONGOZI MBAYA
Suala la uongozi mbaya
limekuwa tatizo sugu kwa nchi nyingi za Afrika.Waandishi
wengi wameonesha jinsi ambavyo viongozi wengi walioshika madaraka baada ya
mkoloni kuondoka walivyoteka nyara uhuru uliopatikana,kwa hiyo mabadiliko
yakawa rangi ya ngozi tu,kwani wananchi wengi waliendelea kuteseka katika
umasikini wao.Katika shairi la “Tishio la Binadamu”mwandishi anasema;
Mashindano ya silaha,yamekuwa ni
mchezo,
Wakubwa waona raha,kwa silaha
waundazo,
Mabomu yaso na siha,ndiyo yawapa
uwezo,
Urusi na Marikani,dunia mwaipa adha.
Mwandishi anakemea juu
ya uongozi unaotumia mabavu, Mfano mzuri mwandishi anakemea nchi za Urusi na
Marekani ambazo ni wanachama wenye kura ya VETO kwenye umoja wa Mataifa
zinavyotumia mabavu kuzikandamiza nchi zisizo na nguvu kisilaha. Mwandish
anasema;-
“Kuyasujudu
mabavu, mwadai tusilotaka,
Maoni yetu
chakavu, sawa nguo ya miaka,
Ni pengi penye
makovu, nchi zilivyopasuka,
Mabomu
yateketeza,waundaji mwafurahi!”
Shairi la “Chini
ya Mti Mkavu” mwandishi analaani uongozi unaoendeleza dhuluma katika
jamii.Anakemea juu ya uongozi mbaya usiojali maslahi ya wengi,uongozi usiopiga
vita umaskini hapa nchini, n.k.
Katika shairi la “Wanajua
Kuvumilia”,mwandishi analaani ahadi za uongo zinazotolewa na viongozi
wetu.Ameonesha kuwa viongozi wetu hawasemi ukweli bali uongo ndio umetawala
midomo yao.Katika shairi hili mwandishi analaani vibaya viongozi ambao hawafiki
vijijini kwa wananchi waliowachagua ili
kujionea hali halisi ya maisha wanayoshi.Mwandishi anasema:-
“Afadhali
kuimba ukweli,
Wimbo mchomo
mkali,
Wimbo,
unalilia hali,
Ya vijiji
vilivyo mbali,
Kwa wale
wasio kauli.”
Katika shairi la “Udongoni”
mwandishi anawakumbusha viongozi wajibu wao katika jamii.Mwandishi anasema:-
“Lanikumbusha
wajibu,
Kujenga si
kuharibu,
Naahidi
kujaribu,
Kulinda
tulichojenga.”
Mwandishi anaona kuwa Uongozi bora ni msingi mkubwa katika
ujenzi wa jamii mpya hivyo anaiasa jamii kupiga vita Uongozi mbaya ili kujenga jamii endelevu hapa nchini.
4.
KUWEPO NA DEMOKRASIA YA KWELI
Demokrasia ni mfumo wa
kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu wenyewe.Demokrasia
inahitajika sehemu yoyote ile ili kuwaruhusu wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru
bila wasi wasi au kikwazo chochote.Katika shairi la“Mjanja yu Mashakani”
mwandishi anasema;
Kumezuka
mkatao,miaka ya themanini,
Watu wafanya
jutio,hawasemi chinichini,
Hawasemi tena
ndio,haitoki midomoni,
Wamevumilia
sana,mwisho wa uvumilivu.
Mwandishi
anajadili kuhusu mfumo wa demokrasia
ambao umejitokeza miaka ya 1980 kote ulimwenguni.Mfumo huu ni ule wa kupinga
sera ya chama kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi (mageuzi).Katika
shairi hili mwandishi anaonesha kuwa mfumo wa vyama vingi umewaamsha wananchi
wengi kutoka usingizini na kuanza kutetea haki zao.Hata hivyo,mwandishi
anaonesha kuwa wale viongozi waliojilimbikizia madaraka na vyeo mbali mbali
wamehofia sana mfumo huu na hivyo hufanya kila mbinu ili kuudidimiza.Viongozi
wanaong’ang’ania madaraka ndio wanaohofia mfumo huu.
Shairi la “Kademokrasi
Kametoweka”linapinga uongozi mbaya barani Afrika.Mwandishi ameonesha
kuwa demokrasia inapopokonywa na viongozi wachache,udikteta huota mizizi na
kuung’oa huchukua muda mrefu.Hali hii inasababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe
katika baadhi ya nchi barani Afrika.Mfano wa nchi hizo ni Jamuhuri ya Watu wa
Kongo,Uganda,Burundi,Sierra Leone,n.k.Utawala wa nguvu hurudisha nyuma maendeleo
ya bara la Afrika na nchi nyingine za ulimwengu wa tatu ambako hakuna demokrasia
ya kweli.Mwandishi anasema:-
“Barani mabavu
yatumika,
Dikteta
asijeanguka,
Na majungu
pia ayapika,
Udikteta pasi
shufaka,
Nasimulia ya
Afrika
Mwandishi anaonesha kuwa mabavu yanatumika ili
kumlinda dikteta asije akaangushwa kwa kufuata mfumo wa demokrasia ya kweli.Madikteta
hao hutumia vyombo vya dola kama vile polisi, jeshi,magereza na mahakama ili
kutetea maslahi yao.Kwa ujumla anatoa pendekezo kuwa, ili tuweze kujenga jamii mpya hatuna budi kujenga na
kudumisha demokrasia ya kweli katika harakati zetu za maisha.
5.KUPIGA VITA MATABAKA
Matabaka ni hali ya watu
kuishi kufuatana na madaraka walionayoya,uchumi na siasa n.k.Msanii ametumia
vielelezo halisi kufikisha ujumbe kwa jamii.Katika shairi la “Wimbo
wake
Hotubani” mwandishi anasema;
Magavana majimboni,
Wasambazao nchini,
Wapewa kubwa idhini,
Na watune ofisini,
Wasoingia shambani,
Kwa sifa madarakani.
Mwandishi anadhihirisha
matabaka yaliyopo nchini mwetu. Magavana
wanawakilisha tabaka la juu (viongozi) na punda na ngamia wamechorwa kitaswira
kuwakilisha wananchi wanyonge wanaoteswa na kunyanyasika.
Katika shairi la “Wengi Wabaki Taabuni” mwandishi anasema;
Mesikia kilio gizani,
Jamaa apita
njiani,
Ghafla
akakabwa kooni,
Kapigwa
kabari ya kihuni,
Yaitwa demokrasi
guni.
Mwandishi anaonesha
kuwa,kuna matabaka ya aina mbili katika jamii yaani tabaka la wachache
wanaofurahia maisha na tabaka la wengi wanaoteseka taabuni.
Kwa ujumla mwandishi ameonesha kuwa mgawanyiko wa watu katika
matabaka huleta utengano katika jamii.Ili tuweze kufaulu kuijenga jamii mpya
(endelevu) hatuna budi kupiga vita matabaka yaliyoshamiri katika jamii.Lengo
liwe kuijenga jamii yenye kufuata misingi ya haki na usawa.
6.KUEPUKA VITA
(UHASAMA)
Vita husababisha
uhasama katika jamii.Huleta ugomvi na kutokuelewana miongoni mwa watu.Vita
hurudisha nyuma maendeleo ya jamii.Vita huleta athari mbaya katika jamii.Mfano
vifo,umasikini,ugumu wa maisha.Katika shairi la “Tishio la Binadamu”,mwandishi anasema:-
“Mashindano
ya silaha,yamekuwa ni mchezo,
Wakubwa
wanaona raha,kwa silaha waziundazo,
Mabomu yaso
na silaha,ndiyo yanawapa uwezo,
Urusi na
Marekani, dunia mwaipa adha”
Mwandishi anaitahadharisha
dunia kuwa vita kuu vinanukia.Hii ni kutokana na uhasama uliopo kati ya nchi na
nchi pamoja na utengenezaji wa silaha kali kutoka Urusi na Marekani.Kutokana na
hali hii dunia nzima sasa iko mashakani juu ya vita.Mwandishi anaendelea
kueleza kuwa mashindano ya silaha yamekuwa ni mchezo na nchi kubwa zinaona
fahari kuzitengeneza.Hivyo mwandishi anaitaka jamii itakayojengwa iepukane daima na suala la vita.
7.SUALA LA MAPENZI
Mwandishi amejadili
aina mbali mbali za mapenzi katika diwani hii kama ifuatavyo;
Mosi,mapenzi ya mtu na nchi yake.Haya mapenzi tunayaona katika shairi
la “Daktari
Askari” ambapo tunona kuwa,wakati wa vita kati ya Uganda na Tanzania
raia,wanajeshi,manesi,n.k.walijitolea kwa moyo wa dhati kwenda kupigana ili
kuikomboa nchi yao.Mapenzi haya ni ya kweli na dhati.Mapenzi ya Iddi Amini Dada
kwa nchi yake hayakuwa ya dhati ndiyo maana alitumia mabavu kuiongoza nchi
yake.
Pili,Mapenzi mengine
kati ya mtu na nchi yake yanapatikana katika shairi la“Ngulu Wapaona”Katika
shairi hili msanii anaonesha umuhimu wa kuwa na
mapenzi na kwenu (nchi yako) hata
kama ni porini. Msaanii anamtaka kila mtu kuthamini kwao hata kama kuna karaha.Anaonesha
kuwa kwenu ni kwenu na ukuthamini na
kukuheshimu kwa raha na Baraka.
Tatu,mapenzi kati ya
mwanamme na mwanamke.Mapenzi haya mwandishi ameyagawa ktika makundi makuu mawili ya mapenzi ya dhati na yale ya udanganyifu.Mashairi
yanayoongelea mapenzi ya dhati ni yale ya “Daktari Askari”,“Thomas
na Doto”,“Manzese Mpaka Ostabei”pamoja na lile la“Takukumbuka Daima.”
Mashairi yanayoongelea mapenzi ya udanganyifu
ni kama vile “Usiwe Mwonja Asali”, “Fikra za Waungwana”.
Mapenzi ya dhati ni ya
kuheshimiana,Mapenzi yasiojali hali au kipato cha mtu. Mapenzi ya uaminifu.
Mapenzi kati ya Daktari Adam na Eva katika shairi la “DaktariAskari”
yalikuwa ya dhati, bila kujali kwao au utaifa.Hali kadhalika mapenzi kati ya Thomas
na Doto yalikua ya dhati bila kujali
rangi au taifa.Na mapenzi kati ya Mashaka na Dorothy yalikuwa ya dhati bila
kujali pesa au utajiri. Mapenzi ya dhati husababisha uvumilivu katika
maisha.Mapenzi ya dhati huzaa matunda mema katika ndoa,yaani hujenga ndoa za
uaminifu.Hivyo mapenzi ya dhati huzaa ndoa za kudumu,ndoa zisizojali
rangi,utajiri,utaifa au hali ya mtu.Ndoa za uaminifu zilizotokana na mapenzi ya
dhati Katika diwani hii ni zile kati ya daktari
Adam na Eva, pamoja na ile ya Mashaka
na Dorothy.
Mapenzi ya udanganyifu
nayo pia huzaa ndoa za udanganyifu na mara nyingi ndoa hizo huwa hazidumu.Katika
shairi la “Usiwe Mwonja Asali”,msanii
anaonesha jinsi mapenzi ya udanganyifu yanavyosababisha uchumba wa
udanganyifu.Msanii anaishauri jamii kuwa ukiwa na mchumba msiwe na tabia za
kujamiiana ovyo,bali mpaka mtakapooana.
Katika shairi la “Fikra
za Waungwana” mwandishi anadhihirisha wazi jinsi mapenzi ya udanganyifu
yanavyosababisha ndoa za ulaghai. Mwandishi anasema:-
“Mume
wangu nakupenda, Joseph amenikuna,
Nimekula naye
tunda, ninampenda sana,
Na usifanye
inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa
mpango, kwako na kwake Joseph.”
Kwa ujumla mwandishi anaitaka jamii yetu idumishe mapenzi
na ndoa za dhati.
5.
NAFASI YA MWANAMKE PAMOJA NA UHURU WAKE KATIKA JAMII.
Mwandishi amemchora
mwanamke katika nafasi mbali mbali kama ifuatavyo;
Mosi,amemchora kama mwanamapinduzi na jasiri.Katika
shairi la “Daktari Askari”mwanamke ameoneshwa akifanya kazi za kimapinduzi
sawa na zile za mwanamme.Mwanamke anapigana vita ili aikomboe nchi yake.
Pili,mwanamke amechorwa
kama mtu mwenye mapenzi dhati katika jamii.Katika shairi la “Manzese
Mpaka Ostabei” linamwonesha Dorothy akiwa na mapenzi ya dhati kwa
Mashaka . Hali kadhalika katika shairi la “Daktari Askari linamwonesha Eva akionesha
mapenzi ya dhati kwa Daktari Adam.
Tatu,mwanamke amechorwa kama kiumbe laghai, asiye mwaminifu
hususani katika suala a mapenzi na ndoa. Haya yote tuayoyaona katika shairi la “Fikra za Waungwana”.
Mwisho,mwanamke amechorwa kama mzazi na mlezi katika jamii.Katika shairi
la “Manzese mpaka Ostabei”,mwanamke amechorwa kama mzazi na mlezi na hii nafasi
inawakilishwa na Dorothy ambaye alimzaa mtoto na kumlea baada ya kuolewa na
Mashaka.
Kuhusu uhuru wa
mwanamke,msanii ameleta mjadala juu ya uhuru wa mwanamke,uhuru wa kuolewa na
wanaume wawili kama afanyavyo mwanaume kwa kuoa wake wawili au zaidi.
Katika shairi la “Fikra
za Waungwana” mwandishi anasema;
“Mume wangu
nakupenda, Josefu amenikuna
Nimekula naye
tunda, nampendelea sana,
Ila usifanye
inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa
mpango, kwako na kwake Josefu.”
Msanii anajadili
dhamira hii kupitia mhusika Anna.Katika
shairi hili, Anna ana mume wake (Nania) lakini kwa upande mwingine anampenda
Josefu ambaye ni mume wake wa pili. Anna
haoni sababu ya kutokuwa na wanaume wawili.
Msanii anaonesha kuwa
uhuru anaoutaka Anna ni wa kuishi au kuwa na wanaume wawili na huo ndio msimamo
wa Anna.
Hata baada ya kesi yake kupelekwa mahakamani,Anna alibaki na msimamo
huo huo.Hali kadhalika majaji walishindwa kutoa hukumu,kwani hakuna sheria
inayozuia mwanamke kuwa na wanaume wengi kama walivyo wanaume ambao huwa na
wanawake wengi.
Lakini swali la
kujiuliza ni kuwa, je mwanamke ana haki
ya kuwa na wanaume wawili katika jamii?,Hakuna sheria inayomzuia mwanamke kuwa
na wanaume wawili lakini mila na desturi ndiyo zinazomzuia mwanamke kuwa na
waume wawili. Hivyo ni kutokana na kasoro hizo ndiyo maana anapinga kasoro
hizo,kudai uhuru wake wa kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja kama
mwanaume anavyooa wake wawili au zaidi kwa wakati mmoja. Hivyo anaishauri jamii
kuona inaweka wazi sharia zinazohusiana na suala hili.Majaji walishindwa
kuhukumu kesi ya Nania- hii ni kwasababu hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia
mwanamke kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja.
UJUMBE
v Ni lazima tujitoe mhanga ili kutetea
wanyonge
v Dhuluma,unyonyaji,kutowajibika pamoja
na uongozi mbaya ni baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya.
v Mashindano ya kutengeneza silaha kwa
mataifa makubwa huhatarisha amani duniani.
v Demokrasia ya kweli ndiyo njia pekee
ya kuendeleza mfumo wa mageuzi hapa nchini na katika nchi nyingine za ulimwengu
wa tatu.
v Mgawanyiko wa watu katika matabaka
husababisha kukosekana kwa umoja na mshikamano katika jamii.
v Mapenzi ya dhati yanahitajika katika
jamii na ni lazima yadumishwe. Mapenzi ya ulaghai yapigwe vita kwa hali zote.
v Suala la mapenzi na ndoa waachiwe
wawili wanaopendana na si maamuzi ya wazazi.
FALSAFA
Ø Mwandishi anaamini itikadi
itakavyowatetea wanyonge, yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Analaani
wizi, dhuluma,udikteta,unyonyaji na kila aina ya uovu.Vile vile anatetea uhuru
katika mapenzi na ndoa.
MSIMAMO
Ø Mwandishi wa diwani hii ana msimamo
wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mbali mbali yanayozikumba jamii zetu na
mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi
mbaya, ulanguzi, dhuluma,rushwa,n.k pamoja na namna ya kuyatatua matatizo hayo.
FANI
MUUNDO
Katika ushairi,muundo
ni umbo,ploti pamoja na mjengo wa ushairi.Muundo hupatikana kwa kuangalia idadi
ya mistari kwa kila ubeti wa shairi linalohusika.Katika diwani hii msanii
ametumia miundo changamano.Miundo mikuu iliyotumiwa na mwandishi ni ;
·
Tarbia
(mistari minne kwa kila beti) pamoja.Mashairi yaliyotumia muundo wa tarbia ni Chungu Tamu” “Tishio la Binadamu”, “Chini ya
Mti Mkavu’,“Mjanja yu Mashakani” “Radi ya Kiangazi” ,“Shairi la Udongoni,Fikra
za Waungwana” ,“Mfereji wa Maringo,) pamoja na lile la “Takukumbuka Daima,’)
·
Sabilia
(mistari mitano na kuendelea kwa kila ubeti).
Mashairi yaliyotumia muundo wa sabilia ni kama vile:- “Daktari Askari”,“Chanzo ni Wenye Kauli” ,
“Wimbo Wake Hotubani”, “Wengine Wabaki Taabuni”, “Ngulu Wapaona, “Chungu na
Tamu” “Usiwe Mwnja Asali”,“Thomas na Doto”,“Manzese Mpaka Ostabei” pamoja
na shairi la “Wosia”.Mashairi mengine yaliyobakia yametumia muundo wa tarbia
kwa baadhi ya beti na nyingine muundo wa sabilia.
MTINDO
Mtindo ni upekee wa
mwandishi katika kazi yake.Upekee huo huweza kumtofautisha mwandishi mmoja na
mwandishi mwingine. Katika ushairi, kuna aina mbali mbali za mitindo kama vile
mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na mtindo unaofuata kanuni za
usasa. Mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo hutawaliwa na urari wa
vina na mizani, muwala, mara nyingi kuna mfanano kwa kila kituo, huweza
kuimbika, n.k. Mtindo unaofuata kanun za ushairi wa kisasa haufuati au
haufungwifungwi na kanuni za ushairi wa kimapokeo. Hakuna urari wa vina,
mizani, ufanano wa kituo, kuimbika, n.k.
Diwani ya Chungu Tamu
ina mashairi yaliyotumia mtindo changamano,yaani mtindo unaofuata kanuni za
ushairi wa kimapokeo na ule unaofuata kanuni za
ushairi wa kisasa.Hii ina maana kwamba,mshairi anayakubali mashairi ya aina
zote mbili (kimapokeo na kisasa).
Vile vile mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi kwa baadhi
ya mashairi.Katika mashairi ya “Chatu na Kuku”, “Daktari
Askari” “Thomas na Doto” na “Manzese Mpaka Ostabei”.Mwandishi ametumia
mtindo huu ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyokusudia.
MATUMIZI YA LUGHA
Aina ya lugha iliyotumika
ni sanifu yenye misemo,nahau na methali, tamathali za semi,mbinu nyingine za
kisanaa pamoja na ujenzi wa taswira.Lugha ya kishairi yenye uchaguzi maalum wa
maneno (diction) imetumika.
MISEMO, NAHAU NA METHALI
·
Imetumiwa
na mwandishi kwa lengo la kuwasilisha ujumbe kwa jamii husika. Mfano:-
Ø Sasa mwaleta shari (msemo) – uk 7
Ø Umoja ni nguvu (methali) –uk 6
Ø Kuvaa masulupwete (msemo) – uk 48
Ø Ndoa ni fumbo (msemo) – uk 42
Ø Usinawe kwa ulimbo (msemo) – uk 42
Ø Mapenzi hayana mipaka (msemo) – uk 40
Ø Utajichimbia kaburi (msemo) – uk 9
Ø Lakini haikutiwa chumvi mitaani (msemo) – uk
12
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
Ø Maoni yetu chakavu,sawa nguo ya miaka
(uk 2)
Ø Macho yao mekundu mithili wavuta
bangi (uk 6)
Ø Kwa msikilizaji husisimua mithili
filamu za wachunga ng’ombe
Ø Shaba kama maji (uk 12)
Ø Kichwa chake kama cha kifutu (uk 38)
Ø Mwili ukamjaa harara kama jini
lililokosa mbuyu (uk 41)
Ø Tumbo lake kubwa kama pipa (uk 50)
Ø Kichwa kidogo kama cha chatu (uk 50)
Ø Mweusi kama kiatu cha jeshi (uk 50)
Ø Utaonekana kama kinyago cha kuchonga
(uk 12),n.k.
TASHIHISI
v Kifo kimeniita (uk 4)
v Njaa inawasaliti (uk 6)
v Kicheche pia ameapa (uk 7)
v Huzuni imenisaliti (uk 10)
v Katika ile baridi kali,mabomu ya
mikono,yakatubusu miguuni (uk 16)
v Vichaka vikawakaribisha (uk 38)
v Taa za waka kwa maringo (uk 44)
v Jiji lasema hali ngumu (uk 44)
v Mapenzi hayana mpango, yakikanywa
zaidi,hayana akili ati (uk53)
v Mioto ikapasua anga (uk 11), n.k.
SITIARI
§ Ushairi ni sukari tamu (uk 1)
§ Utoto ni kito (uk 2)
§ Yeye alisema dunia ni raha na tabu
(uk 2)
§ Umaskini ni mzigo (uk 11)
§ Wote weusi wawa mkaa (uk 45)
TAFSIDA
·
Usiwe mwonja
asali (uk 37)
·
Walipenda faragha
(uk 51)
·
Dora
ana kitu tumboni (uk 54)
·
Nimekula
naye tunda (uk 56)
TABAINI
v Kuwaza na kuwazua
v Lakini usikubali raha tu, kumbuka na
karaha (uk 13)
v Aponya aua (uk 17)
KEJELI
·
Nyie
yawafalia,mfanyakazi ya kuchoma na kuuza mkaa (uk 45)
·
Wa
Manzese atakulisha taka (uk 52)
·
Jina
lenye ugonjwa wa kaka (uk 52)
·
Iweje
binti shibe aende kwa omba omba (uk 52)
DHIHAKA
Ø Ati mchumba, mchumba siye Baraka (uk
52)
MBINU NYINGINE ZA
KISASA
TAKRIRI
Ø Mateka, mateka wapenzi (uk 22),
Ø Adamu, machozi (uk 20)
Ø je je, je….je nyingi (uk 43),
Ø Mateka, Mateka, wapewa (uk 22)
Ø Tukanyata, tukanyata tukakaribia
Mbarara (uk 16)
MDOKEZO
Ø Je je je…je nyingi (uk 43)
Ø Si mganga wa tunguli…(uk 14)
Ø Sijui yaah yaah…(uk 44)
Ø Sijui Mashaka…(uk 53)
Ø Kati yao huyu…!(uk 51)
Ø Profesa Idd Amin…(uk 19)
Ø Ikawa nakupenda lakini…
NIDAA
·
Ati
mie mzee1!
·
Ghafla
mwewe huyu!
·
Umeshituka!
·
Mwauzunika
nini!
·
Kwa
hamu ya umoja!
TASHTITI
v Hujisikia wezi wakiomba Mungu kabla
ya kwenda huko waendako? (uk 13)
v Wewe mwana –kibarua, hujioni? (uk 49)
MJAZIO
Ø Twaona wanaopelekewa chai, mikate,
karanga, mayai…(uk 13)
Ø Ndugu mwenyekiti nadhani, labda,
pengine, ningependekeza, kwa maoni yangu, kwa mfano tungeliweza….(uk 15)
ONOMATOPEA(TANAKALI
SAUTI)
·
Lo!
(uk 4)
·
Loooo!
(uk 20)
LUGHA YA KIINGEREZA
·
Movement
order (uk 14)
·
Surrender
(uk 17)
·
Doctor
where College? (uk 18)
·
Life
President? (uk 19)
·
-Good
Doctor (uk 19)
·
My first fiancé
(uk 20)
·
But this is war
sir (uk 20)
·
Look Adam. My
parents are dead. I am alone (uk 23)
·
Sir
is that a request or an order? (uk 24)
·
Two
doctors fighting for no reason (uk 25) n.k.
TAFASIRI YA MOJA KWA MOJA
Ø Fomu wani (uk 48)
UJENZI WA TASWIRA
Mwandishi ametumia
baadhi ya taswira ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyoiandika. Baadhi ya
taswira hizo ni kama vile:-
v Chatu (uk 2)…..Inawakilisha
wadhulumaji (wakoloni)
v Kuku (uk2)……Inawakilisha wadhulumiwa
(Waafrika)
v Vifaranga (uk 9)….Inawakilisha mali
ghafi
v Mjanja (uk 25)….Viongozi wanaoshikilia
mfumo wa chama kimoja
v Watwana (uk 25)….Wananchi wanaotaka
mabadiliko au uongozi mbovu
v Ngulu (uk 33)….Vijiji, sehemu isiyo
na maendeleo, sehemu iliyosahaulika
v Zabibu (uk 42)…..Msichana au mwanamke
MANDHARI
Kitabu hiki
kiliandaliwa miaka ya 1980. Na matukio yanayosimuliwa katika kitabu hiki
yanazungukia nchi za Afrika ya Mashariki hususani Tanzania na Uganda. Hata
hivyo, maudhui ya kitabu hiki yanasadifu kipindi hiki cha sasa katika nchi yoyote ile ulimwengu wa tatu.
JINA LA KITABU
Jina la diwani hii“Chungu Tamu’’ linasadifu yaliyomo ndani ya
kitabu. Msanii ameonesha kuwa, baada ya kupita katika machungu na kuamua
kupambana nayo ndipo utamu utafuata. Anaitaka jamii itumie kila mbinu kupambana
na vikwazo vinavyokwamisha jamii isiweze kuupata utamu (ujenzi wa jamii mpya
endelevu).Aidha msanii anaonesha kuwa katika maisha,uchungu na utamu
havitengamani.Vile vile msanii ameonesha dhahiri kuwa, wananchi wa kawaida
ambao ndio wazalishaji wanakula “Chungu” lakini viongozi ambao si wazalishaji
wanakula “Tamu”.
KUFAULU KWA MWANDISHI
KIMAUDHUI
Mwandishi ameongelea
masuala ambayo yanaisakama jamii yetu katika wakati huu tulio nao. Ameonesha
mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala zima la ujenzi wa jamii mpya.
KIFANI
Mwandishi amefaulu
kutumia miundo changamano,mitindo changamano,lugha ya kishairi pamoja na ujenzi
wa taswira.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
v Lugha imejaa taswira kwa kiasi
kikubwa na hivyo msomaji wa kawaida hawezi kuambulia ujumbe wowote.Hivyo
amewanyima baadhi ya wasomaji uhondo wa kazi yake.
v Msanii metumia lugha ya Kiingereza
(kigeni) katika baadhi ya mashairi.Huu ni udhaifu wa mwandishi,kwani anakinyima
Kiswahili sanifu nafasi ya kuenea.Vile vile kwa mtu asiyefahamu Kiingereza
atashindwa kupata ujumbe.
No comments:
Post a Comment