
RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA NA UDURUSU WA NADHARIA ZA FASIHI
ISSA MWAMZANDI
Literary theory represents a way of thinking and a body of writing that is dedicated to the analysis of literary texts. It is a means through which literary critics come to appreciate the nature of the literary texts they seek to analyze and the methodology that informs their practice. Analyzing three 21st Century Swahili novels, this paper examines a paradigm shift: literary theory becomes the subject under examination as opposed to its conventional role where it would ideally offer systematic views of what such texts would mean. Said Ahmed Mohamed’s Dunia Yao (2006) and Nyuso za Mwanamke (2010) on the one hand, and Kyallo Wadi Wamitila’s Musaleo! (2004), on the other, represent a new kind of writing that experiments on literary theory as a subject for criticism. In these texts, we read about the tenets and practice of a variety of literary theories including Russian formalism, Saussurean and Jakobsonian structuralism, Derrida’s deconstruction, Edward Said’s post-colonial theory, and Carl Gustav Jung’s psychoanalytical theory. While this experiment that the two novelists engage in may appear elitist for the average reader at first, the paper contends that this form of writing will in the long term assist in the domestication of literary theory. Further, the three texts could greatly assist in pedagogical issues if read alongside other mandatory course books on literary theory. Utangulizi Sifa bainifu ya baadhi ya kazi za fasihi ya Kiswahili za karne ya ishirini na moja ni matumizi makubwa ya mbinu za kiuandishi za kimajaribio. Msomaji wa kazi hizi aghalabu hujikuta ameghumiwa na wingi wa urejeleo matini, uhalisia mazingaombwe pamoja na vipande vidogo vidogo vya visa ambavyo hutumika kuungia simulizi hizo zilizochupwa huku na huko (Bertoncini 2006: 93; Khamis 2003: 78). Kwa jinsi hali ilivyo riwaya hizi zinaelekea kutangaza upenuni kwamba enzi na dola ya uandishi wa kazi za kihalisia imepitwa na wakati na umefika muda wa kutoa wasaa kwa majaribio haya mapya. Ni maoni ya makala kuwa fauka ya mbinu hizi kuwa na natija pamoja na dosari zake bado kuna baadhi ya waandishi ambao bado wanaongozwa na misingi ya kihalisia. Mbali na uwezekano wa kazi hizi za kimajaribio za kuitenga sehemu ya hadhira (wakiwemo wale wasiozifahamu nadharia za fasihi) kwa kumkumbatia zaidi msomaji aliyesoma na kuzamia fani adimu za kijamii, fasihi ya karne ya ishirini na moja ni njia jarabati ya kumkomaza msomaji ashiriki kikamilifu katika kufuatilia viini vya simulizi mbalimbali anazozikuta humo. Ndani ya riwaya hizi, msomaji anapambana na fikra za wanafalsafa, wanasiasa mashuhuri pamoja na vitimvi vyao, maswala ya utandawazi na athari zake, madondoo ya vitabu vya kidini, visa(a)sili, mighani, ISSA MWAMZANDI 49 majinamizi, na hata kazi nyingine za kifasihi za wasomi watajika. Makala hii inazamia kipengele kimoja tu cha mafunzo ya nadharia za fasihi ambazo huwa muhimu hasa kwa wanafunzi wa vyuo vya ualimu na hususani vyuo vikuu pale inapowabidi wazungumzie kitaaluma kazi za fasihi. Makala imetumia riwaya ya Musaleo! (2004) ya Kyallo WadiWamitila na riwaya nyingine mbili za Said Ahmed Mohamed za Dunia Yao (2006) na Nyuso za Mwanamke (2010) kama mifano mahususi ya namna waandishi wanavyozungumzia kwa dhahiri nadharia za fasihi. Nadharia katika Uhakiki wa Fasihi: Kipi kwanza? Katika jadi ya uhakiki wa kazi za fasihi, swala mojawapo lililozingatiwa kwa makini ni iwapo wahakiki wanastahili kuzingatia kile kinachosemwa na matini ili kielezwe kwa misingi ya kinadharia au kufanya kinyume chake. Ingawa kuna kila ithibati kuwa wapo wataalamu waliofuata mojawapo kati ya njia hizo, ushahidi umeonyesha kuwa wengi wa wahakiki hupendelea kufuatiliwa zaidi kwa matini na kisha kuamua nadharia mwafaka itakayofafanua kwa uwazi kile kilichomo ndani ya matini. Said Khamis (2008) amelizungumzia hili kwa mapana na ametoa sababu ambayo naona niitaje hapa kwa kuwa inawafiki nadharia-tete inayoendelezwa na makala hii. Anasema: Nadharia zinabadilika taratibu zaidi kwa sababu mabadiliko ya nadharia mara nyingi huongozwa na mabadiliko ya mitindo na tanzu za fasihi yenyewe. Kinyume cha mambo kilichopo ni kwamba kila siku nadharia hujaribu kama inavyowezekana iwe na uwezo wa muda mrefu wa kuchambua na kuzieleza kazi za fasihi mbalimbali. Lakini, kwa upande mwingine, hakuna nadharia inayoweza kufaa katika resi ambamo utoaji wa kazi za kubuni situ una wepesi zaidi, lakini mara zote unazingatia upya na mabadiliko. Hii ina maana nadharia fulani moja au zaidi zinaweza kufaa kwa muda fulani tu mpaka pale zinapojikuta, kwa sababu moja au nyingine, zinakumbwa na matatizo ya kutoweza kuzichambua vyema kazi zinazoibuka na upya na mabadiliko. Wakati huu ndipo nadharia mpya inapohitajika. (Khamis 2008: 12) Nimemnukuu Khamis kwa mapana kutokana na kile anachokiona kama umuhimu wa nadharia za fasihi kuizingatia matini ambayo kama anavyosema daima imo mbioni kuzua mabadiliko. Katika vitu viwili hivi vinavyotegemeana, matini inayobuniwa ndiyo inayosababisha zaidi haja ya mabadiliko katika nadharia ambayo huenda ikashindwa kuzizungumzia kazi mpya za kifasihi, hususani zile za kimajaribio. Pamoja na kuwafiki hoja anayoitoa Khamis, makala inazamia nadharia-tete ambayo inahusu uhakiki wa nadharia kama msingi huo wa ubunifu wa kimajaribio ambao unahitaji uteguliwe na nadharia. Riwaya Tatu Teule kwa Muhtasari na Misingi ya Uteuzi wake Mbali na Euphrase Kezilahabi, wanariwaya Said Ahmed Mohamed na Kyallo Wadi Wamitila wametajwa kama waandishi wanaoongozwa na fikra mpya za kiuandishi, yaani uandishi wa kimajaribio ukiwemo ule wa kihalisia-mazingaombwe (Waliaula 2010: 143; Bertoncini 2006: 93; Khamis RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 50 2003: 78f). Makala inatambua kuwepo kwa sifa hizo za uhalisia mazingaombwe ndani ya riwaya miongoni mwa mambo mengi yaliyofumbatwa humo. Aidha, riwaya hizi zina sifa za kiusasabaadaye ambamo mna vipande vidogo vidogo vya simulizi zisizokuwa na muwala wala zisizochukuana vyema kama zilivyo hadithi za paukwa pakawa zinazoishilia na harusi au wahusika wanaoishi raha mustarehe. Kwa utaratibu wa sifa hizo, nimeteua riwaya husika za Musaleo! (2004), Dunia Yao (2006) na Nyuso za Mwanamke (2010) kwa kuwa zote zinaagua nadharia za fasihi kama sehemu mojawapo ya dhamira zilizomo ndani ya matini hizi. Musaleo! (2004) inajumuisha simulizi inayoenda mbele na nyuma na iliyofichama hadithi mbili tofauti na umazingaombwe usioweza kutabirika. Ni hadithi inayomsukuma msomaji mbele na nyuma na mwingiliano matini uliokithiri unaohitaji umakinifu ili msomaji apate kuelewa fikra mbinu, njama, vitimbi na hila wanazotumia wakoloni mamboleo katika kuwazuga wale wanaosimama kidete kuzitetea haki zao katika jamii. Nyuso za Mwanamke (2010) nayo inamwendeleza nguli wa kike, Nana, na jinsi anavyojinasua kimawazo kutokana na wavu wa ulimwengu wa kiume kwa kufuata kile kinachoridhiwa na moyo wake. Ni safari ya msichana, mwanagenzi wa maisha, anayeabiri kujua utu wake na sifa zinazomfafanua binafsi kama mwanamke, tofauti na wanavyotarajia wahusika wengine wa kike na wa kiume wa riwayani. Dunia Yao (2006), kwa upande wake, imesheheni mijadala ya kifalsafa inayozamia fani mbalimbali za sanaa na swala zima la ubunifu. Ninachokiona zaidi ni swala la uendelevu wa sanaa ukiwemo uhai na ufaafu wake katika kuzungumzia visa visivyowaelea watu katika ulimwengu mamboleo. Dunia, inavyosema Dunia Yao, ni bahari isiyotabirika kina chake na sanaa haiwezi kuwekewa mipaka tunapoabiri kuizungumzia. Kama ilivyoparaganyika dunia, sanaa nayo haina budi kufuata mkondo huo kwani kuifuatilia dunia kwa mstari ulionyooka kama zilivyo kazi za kihalisia ni kuishi katika njozi. Kuelewa nadharia za fasihi ni miongoni mwa njia adimu za kuelewa mafumbo ya kisanii na ya kimaisha yaliyoatikwa katika riwaya hizi. Makala imezamia baadhi ya nadharia za kifasihi ambazo zimejitokeza wazi wazi katika riwaya hizo tatu. Uhakiki wa Nadharia ya Mwigo Katika kitabu chake maarufu cha Poetics, Plato anaelezea asili na chanzo cha sanaa. Miongoni mwa mambo mengine, Plato humo anaelezea uhusiano wa karibu uliopo kati ya msanii na Mungu ambaye anachukuliwa kuwa mfalme wa sanaa zote. Hususani, Plato anamtaja Mungu wa sanaa aitwaye Muse ambaye huwapanda wasanii vichwani na kuwafanya wabubujikwe na mawazo ya kisanii pindi anapowakumba (kufuatana na Plato kama inavyofafanuliwa katika Tilak, 1993: 29). Kwa mujibu wa Plato, Mungu huyu huwapagawisha wasanii tu na kuwapa ufunuo au wahyi unaowawezesha kuwasiliana moja kwa moja na wasanii (Habib 2005: 24; Wafula & Njogu 2007: 24). ISSA MWAMZANDI 51 Kwa sababu hiyo, Plato aliwaona wasanii kama watu wenye vipaji maalum vinavyotoka kwa Mungu na kwa sababu hiyo, siyo kila mtu angeweza kuwa msanii. Katika riwaya tatu zilizoteuliwa Dunia Yao, na kwa kiasi fulani Musaleo!, inafuatilia kwa makini nadharia hii ya Plato kuhusu mwigo na imethubutu hata kumchukua mhusika wake mmoja, Muse ambaye anahusishwa na ghamidha na kariha ya utoaji wa sanaa za kiubunifu huko Ugiriki, kuwa mshirika wa kiroho wa mhusika mkuu aitwaye 'Ndi-'. Mhusika Bi Muse (wakati mwingine Mize) wa Dunia Yao anazua mjadala mpevu wa swala zima la sanaa na hulka yake kama inavyowasilishwa na Mohamed. Mhusika huyu ambaye amechukuliwa moja kwa moja kutoka kwa maandishi ya wahakiki wa Kiyunani, Plato na Aristotle, anakuwa kiunzi muhimu cha kujadili swala zima la usanii. Haya yanadokezwa ipasavyo katika riwaya hii pale Bi Muse anapoeleza asili yake. Ufunguzi wa sura ya tanounadokeza asili ya mhusika huyu, Bi Muse, ambaye ni yule yule aliyezungumziwa na Plato tangu jadi, tofauti hapa ikiwa Bi Muse ni mhusika wa hadithini. Sura inaanza hivi: “Mimi ni Muse” […] “Kwa asili hasa, Ugiriki – lakini siku hizi naishi popote. Mara nyingine hujificha katika vina virefu vya ardhi kabla sijachomoza kumzuru niliyemchagua. Na leo nimekuchagua wewe. Kwa hivyo nimechomozekea chini ya mnazi palipofukiwa kitovu chako, baada ya kupiga mbizi Bahari ya Hindi kuja kukuingia kichwani mwako…” (Mohamed 2006: 61) Sawa na anavyopendekeza Plato kuhusu namna wigo wa kisanaa unavyojiri, hapa mwandishi anaendeleza hoja hiyo hiyo ya namna Ndi- anavyosababishwa atunge kazi yake na Bi Muse. Naye ni kiumbe anayetangaza kuwa asili yake ni Ugiriki (alikotoka Plato) na hamkumbi Mgiriki pekee bali humkumba mtunzi yeyote wa kazi za kubuni. Ana nguvu za kichawi za kumsababisha msanii apagawe kama riwaya inavyodokeza: “Kwa kawaida,” aliendelea, “sina umbo maalum. Ni aina ya jeteta linalochanua jinsi andasa zangu na zako zinavyokubaliana kuchanua. Sikuzaliwa katika dhati na bayana ya mambo. Mimi ni binti wa Zeus na Mnemosyne. Asili yangu inasimamia kumbukizi na dhana tu. Ndio maana nina majina mengi kwa mujibu wa kazi yangu ya kutia ilhamu. Calliope, Clio, Erato, Euterpe, Melpomene, Polyhymnia, Terpsichore, Thalia, Urania. Hata unaweza kuniita Bi Mize, kwa jina la kikwenu. Kwani hapa nilipo nimekuja kwa sura ya kikwenukwenu, kipande samaki, kipande mtu na kipande ndege.” (Ivi: 68f) Huyu anayefahamika kama Bi Muse katika riwaya anaeleza namna anavyoweza kubadili umbo na kuwa mwenza wa kila msanii duniani. Ingawa amezaliwa na Mungu Mkuu wa Kigiriki, Zeus, Bi Muse ana uwezo wa kuwa binti wa kifalme au wa kijini kwa kuzingatia utamaduni wa msanii husika. Ndiyo sababu hapa anamwambia Ndi- kuwa akipenda anaweza kumwita Bi Mize ili afahamu kwa ukaribu nguvu zake anapomkumba. Mize au Mwanamize ni mhusika wa Waswahili anayefahamika kwa vitimvi vyake na nguvu za kiuchawi za kugeuka umbo kama inavyosemwa kwenye dondoo. RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 52 Muse, kama anavyotangaza, ana nguvu za kichawi za kumzuga mtu na kummiliki pale anapomchagua na kumfanya kuwa kiti chake. Kitendo hiki cha kupandwa na jazba na kupagawa ndicho kinachojitokeza mwanzoni mwa riwaya pale Ndi- anapoeleza namna swala zima la utunzi linavyohusiana na nguvu hizo za Muse ambapo utunzi unakua hatua baada ya nyingine hadi kukamilika kwake: Katika kubuni na kuumba – ‘Bi Muse’ anapokujia na kukuchota kwa uzuri wake – kama koja la ajabu, unatunga sauti na sauti, ileile au tofauti, na kupata silabi. Silabi na silabi, unapata neno! Neno, maneno. Ibara na sentensi. Ibara na sentensi huzaa matini. Na vyote hivyo ni sehemu muhimu ya simulizi – maandishi. (Ivi: 9) Dondoo hili linaeleza kwa muhtasari uhakiki wa ki-Plato na ki-Aristotle unaohusisha uandishi na kujazibika kwa mwandishi. Safari inayoanza na sauti au fonimu moja inakua na kupea hadi kufikia kuwa matini nzima. Inapotokea hivyo, mwandishi na mungu huyu wa sanaa, Muse, huwa kitu kimoja. Ndi- anaelekea kukiri kuwa uandishi hufatwa na ghamidha na kariha inayomjia mwandishi na wala si jambo la vivi hivi tu, chambilecho Ndi- kuwa Muse si kiumbe wa ‘sasambura turore’ au anayejitoa hadharani kuonekana. Ni kana kwamba Ndi- hushindwa kujizuia na kuhamasika kuendeleza kazi yake ya kiubunifu pale anapotawaliwa kihisia na kifikra na Bi Muse. Hujikuta tu akiongozwa asikokufahamu ingawa anavyokiri mwenyewe huwa ni wakati adimu wa kutamanika. Hii ndiyo sababu Dunia Yao inaufafanua uhusiano wa Ndi- na Bi Muse kuwa wa mke na mume wanaoliwazana na kubembelezana hadi wanapooana na kuwekana nyumbani. Ni taswira ya unganiko la kipekee ambalo hufukuza utasa na badala yake huzalisha kazi za kisanaa baada ya wahusika hawa kusuhubiana na hata kupata mtoto, yaani kazi inayotungwa. Hatua zote hizi zinaelezwa na Ndi- hivi: Ndiyo, jina lake nimekuwa nikilisikia na kulisoma siku nyingi. Kama alivyosema mwenyewe, si kiumbe wa sasambura turore. Hujifichua anapohitajiwa kwa mapenzi ya dhati au kwa kutoa msaada. Na mimi, nimefikia baleghe ya kusalitika naye. Nina haja naye. Ninamhitaji. Ninataka anisaidie. Anisaidie kuwasaidia wengine ikiwezekana. Anisaidie kuukata ugumba wa utunzi. Nina hamu kurutubisha na kutia mbolea pahala fulani. Nipate kizazi kipya cha sanaa katika ukame wa ubunifu. Nipate kurutubisha kizazi kipya cha utu katika ukame usio na utu. Ninahitajia mtekenyo wake unipandishe jazba. (Ivi: 61f) Swala la kupandwa na jazba linajitokeza pia katika Musaleo!. Katika riwaya hii, Kingunge anaonyesha kuwa uandishi wake hutokana na jazba na kariha inayomsukuma kuandika kile ambacho yeye mwenyewe hana maarifa nacho. Tunaelezwa hivi: Lakini mara hii alipomweleza mkewe uandishi wenyewe alilazimika kusikiliza kwa makini. “Mara hii ni tofauti. Inajisimulia mimi naandika tu. Ni kitu kama ndoto. Yaani kazi yangu ni kuandika yanayonijia. Ngoja niimalizapo utajua tofauti yake na nyingine…” (Wamitila 2004: 12). ISSA MWAMZANDI 53 Tofauti na riwaya ambazo Kingunge anadai amezipa majina, riwaya anayoandika kwa wakati huu ni ya kipekee na imepokea nguvu maalum asizoweza kuzidhibiti. Ni kariha ya kipekee inayomsibu na ambayo inamsukuma kuandika mambo asiyoyaelewa. Si ajabu basi anapodai kwamba riwaya hii itajipa yenyewe jina badala ya yeye kufanya hivyo (k. 10f). Nadharia za Umaumbo wa Kirusina Umuundo katika Dunia Yao Dunia Yao pia inahakiki kwa uwazi dhana za nadharia ya umuundo za uhusiano wamaneno kimfululizo na kiwimawima. Msingi unaochukuliwa na riwaya hii ni ule wa ki-Saussure, na ulioendelezwa baadaye na Roman Jakobson, unaohusiana na dhana zake za uhusiano wa ishara wimawima au kimfululizo (Eagleton 1996: 85f). Katika Dunia Yao Mohamed anatueleza hivi: Uhusiano wima wa maneno unakuhakikishia uteuzi. Uhusiano mlalo unakuhakikishia mpangilio wa kisarufi.Unatii amri za lugha au unavunja kanuni za lugha wakati mmoja. Unajenga kutoka kipashio cha chini kwenda kipashio cha juu kabisa. Au unaweza kushuka kutoka juu kwenda kipashio cha chini kabisa. Madhumuni ni kujenga maana kwa njia ya kubomoa maana. Kujenga mvuto wa kisanaa. (Mohamed 2006: 9; msisitizo wangu) Mohamed katika Dunia Yao anataja na kuzifafanua dhana mbili muhimu za umuundo ambazo anazirejelea kama “uhusiano wima” na “uhusiano mlalo” wa maneno. Mahusiano haya ya maneno, tunaelezwa, yana natija zake hasa kwa mwanafasihi. Uhusiano wima wa maneno, tunaambiwa, huhakikisha uteuzi. Swala muhimu hapa ni kujua namna uteuzi huu unavyohakikishwa kwani haujabainishwa waziwazi kwenye dondoo. Mwamzandi (2007: 71) ametoa mfano ambao kwa muhtasari unafafanua swala hili la uteuzi: mchuti kiki Abasi aliupiga teke mpira mkwaju Katika mfano huu, neno ‘teke’ limechukuliwa kama neno la kawaida au la wastani ambalo msemaji wa Kiswahili angelitumia. Maneno yaliyoandikwa kwa mlazo na ambayo yamejipanga juu na chini ya neno ‘teke’ ndiyo tunayoweza kusema kuwa yanahakikisha uteuzi unaozungumziwa na dondoo. Maneno hayo yanaeleza namna na jinsi mbalimbali za kuupiga mpira na mwanafasihi anaweza kuchangua neno mahsusi kwa kutegemea hisia maalum anayotaka kuibua kwa msomaji wake (Mwamzandi 2007: 71). Uhusiano mlalo wa maneno nao, kama unavyofafanuliwa ndani ya dondoo, una uwezo wa kuidumisha au kuivunja sarufi ya lugha, matokeo ambayo yanatokana na jinsi mwanafasihi, kwa mfano, atakavyochagua kuyapanga maneno yake katika sentensi. Katika sentensi, lugha yoyote huwa na matarajio na sheria zake za kisintaksia na kisarufi. Kwa sababu hiyo, kulibadilisha neno RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 54 moja katika sentensi na kuliweka mahala tofauti na pale panapotarajiwa na wanalugha husika kuna athari kubwa, ikiwemo ile ya kuzua maana tofauti na ile inayoweza kukubalika. Neno hilo linaathiriana kivingine na maneno mengine ya sentensi na kuzua maana mpya inayoweza kutegua uzoefu wetu wa lugha hiyo. Huu ndio ule mpangilio wa kisarufi unaoweza kutii au kuvunja kanuni za lugha na ambao unaozungumziwa na dondoo hapo juu na tunaweza kuutolea mfano huu: kitabu kizuri mtu mnene Hebu tazama sasa tunapobadilisha na kuanza na vivumishi na kisha nomino, na kuikaidi sarufi ya Kiswahili kama inavyotarajiwa: kizuri kitabu mnene mtu Ingawa maana iliyokusudiwa bado ipo, mabadiliko ya pale zilipo nomino na vivumishi kumesababisha ugeni fulani. Huu si muundo wa wastani wa Kiswahili ingawa unaweza ukakubalika katika miktadha mahsusi, ukiwemo fasihi. Huku ndiko kujenga maana kwa njia ya kuibomoa kama kunavyozungumziwa na dondoo. Uhakiki wa Kidenguzi: Nyuso za Mwanamke na Dunia Yao Mbali na kushughulikia maelezo ya kinadharia kuhusu nadharia ya udenguzi, riwaya za Nyuso za Mwanamke na Dunia Yao pia zinashughulikia zoezi lenyewe la kuchanganua maana kwa kuongozwa na fikra hiyo ya kidenguzi. Ili tufuatilie kila kinachosemwa katika riwaya hizi mintarafu ya udenguzi ni vyema tuangazie, walau kwa muhtasari, fikra kuu ya nadharia yenyewe. Udenguzi ni nadharia inayohusishwa na Mfaransa Jacques Derrida (1930-2004). Hapa nitafafanua misingi miwili tu ya nadharia hii kama ilivyofafanunuliwa na wataalamu mbalimbali (taz. Burman & McLure 2005: 284-286; Schmitz 2007: 115f). Mosi, mbinu kuu na muhimu inayotumiwa wa wanaudenguzi ni ukinzani wa jozi za maneno. Tasnifu ya Derrida kuhusu jozi hizo ni kuwa jamii za Kimagharibi zimejenga upendeleo wa wazi pale neno moja katika jozi husika daima linawakilisha utukufu au kile kinachopaniwa kufikiwa kama kitu adili huku dhana ya pili ya jozi hiyo hiyo ikiangaliwa kama ghushi, isiyo safi na ya daraja ya chini. Wanafilosofia wa awali, kama anavyodokeza Derrida, waliuona ulimwengu katika muktadha huo – jambo lililowafanya kuuona upande wa kwanza wa jozi za maneno kama unaojengwa na vitu vya kimsingi na vinavyostahili kupewa kipaumbele kama vilivyo safi, vya wastani na vilivyokamilika huku upande wa pili wa jozi nao ukifafanuliwa na vitu vilivyotandwa na utata, vyenye doa na umahuluti. Kwa sababu hiyo, usanifu wa hoja katika nchi za kimagharibi una tabia ya kuviona vitu na hali mbalimbali kwa namna ya upendeleo. ISSA MWAMZANDI 55 Pamoja na mgao huo ambao wanafilosofia wa kijadi walipania kuujenga, wanaudenguzi hulenga kufutilia mbali mipaka hiyo na kuonyesha kuwa jozi za maneno ni mfano wa sarafu moja yenye pande mbili. Udenguzi hubainisha kuwa nuru na kiza ni vitu ambavyo wanafilosofia wa kijadi wangevitenganisha kwa kupendelea nuru kuliko kiza. Kwa wadenguzi, nuru sawasawa na kiza vimechangamana na huwezi kukielewa kimoja bila kingine. Hatungeweza kumaizi kile tunachokifahamu kama nuru iwapo lugha tunayoitumia haingekuwa imeratibu ndani yake dhana ya kiza. Pili, udenguzi hushughulikia kwa pamoja jozi ya maneno yanayokinzana na wakati huo huo kubainisha itikadi kuu inayojitokeza na inayostahili kusailiwa upya. Kupitia uchanganuzi makini wa lugha ya matini, wadenguzi hudhihirisha ukinzani na utepetevu wa matini hizo. Hili ndilo linalowapelekea wadenguzi kudai kuwa matini hujiumbua na kujibomoa yenyewe na wala sio wao wanaofanya hivyo. Wanavyodai, hii ni sifa ya azali na iliyomo katika lugha kwani tangu jadi lugha imejengeka kama mfumo wenye ukinzani na unaotofautisha maana. Lugha yenyewe imejengeka kiudenguzi kwani hubainisha tofauti zilizomo ndani yake – za kimaana na za kiitikadi. Kipengele cha kwanza kinaingiliana moja kwa moja na fasiri inayotolewa na mhusika mkuu wa Nyuso za Mwanamke, Nana, pale anapotoka nyumbani kwao na kuabiri safari ndefu ya kuutafuta uhuru wake binafsi baada ya kuamua kutoroka nyumbani kwao. Anaanza somo lake la kidenguzi kwa kuzamia jozi zilizomo katika dhana mbalimbali zinazokinzana: Kwa kawaida nafsi yangu ilinifanya niamini kwamba hakuna utenganisho mkamilifu baina ya kuwepo na kutokuwepo. Sisi binadamu tupo kama hatupo au hatupo kumbe tupo. Basi, maisha ya siku hizi ni kama kuwepo ndani ya kutokuwepo au katika kutokuwepo na kuwepo. Ni hali ya kudinda ndani ya ukweli na uwongo. Au baina ya nafsi moja na ndani ya nyingi na nyingi ndani ya moja: utambulisho wetu ni wa weusi na weupe, majilio yetu ni nidhamu na machafuko. Tunavunga ndani maumbile yanayovunjwa na utamaduni wa pupa, katika dunia isiyobagua tena kati ya wema na uovu, uke na uume, kitovu na pembezoni… (Mohamed 2010: 59; msisitizo wangu). Lakini kama Derrida anavyotambua kuwa watu hupania tu kuweka mipaka kati ya vitu, mipaka hiyo kwa hakika huwa ya kufikirika na udenguzi hutuelekeza tuangalie kwa makini ukinzani unaojitokeza ndani ya matini (Carter 2006: 111). Nana anatutanabahisha juu ya jozi tofauti tofauti zikiwemo kuwepo/kutokuwepo, ukweli/uwongo, umoja/wingi, weusi/weupe, wema/uovu, uke/uume, kitovu/pembezoni ambazo tunastahili kuzifikiria kwa pamoja ili tuone namna jozi hizi zinavyojengana na kuumbuana1. Hii ndiyo sababu Nana wakati mwingine anazibadilisha jozi za maneno kama vile kuwepo/kutokuwepo hadi kutokuwepo/kuwepo, na “moja/nyingi” – “nyingi/moja”. 1 Kwa ufafanuzi zaidi wa fikra ya kidenguzi kama zoezi la uchanganuzi wa jozi za maneno msomaji anashauriwa asome makala ya Mwamzandi (2011: 1-14). Humo ataona namna maneno jozi yanavyoumbuana na pia kujengana kimaana. Aidha, ningependa kuwashukuru wahariri kwa ushauri na mapendekezo yao, hususani kuhusu sifa na hulka ya fasihi ya kiusasa-baadaye. RIWAYA TEULE ZA KARNE YA ISHIRINI NA MOJA 56 Mipaka ya jozi za maneno huwa myembamba sana na hili ndilo linaloendelezwa na Nana kwa utaratibu huu: Mkinzano unaishi ndiyo, na kwa kweli lazima uishi kwani mkinzano ndiyo maisha yenyewe. Lakini kila mkinzano una mstari mwembamba usioonekana kwa macho. Ndiyo unatenganisha mambo, lakini ni mwembamba mno kutenganisha kwa ukamilifu kitu kimoja na cha pili. Hapana kitu kimoja na cha pili, pana kimoja kinachoshibishana na kugombana na cha pili. Ndivyo dunia yetu ilivyoanza tokea mwanzo katika hali ya uwili inayotegemeana na kutofautiana […] Pana kuvuka mipaka pande mbili. Hiki cha huku kinaweza kwenda kule na cha kule kinaweza kuja huku. Nguvu za hiki zinajengwa na kile. Kuwepo kwa hiki ni sababu ya kuwepo kile. Huo ndio uwili unaotegemeana, lakini unaovunjana kwa wakati mmoja. Anayejiona ameshinda hatimaye ni yule mwenye nguvu, lakini ukitazama sana, hapana anayeshinda. Kuna kushindwa kwa wote. (Ivi: 59f) Katika dondoo hili, uwili unaozungumziwa na Derrida umekaririwa mno hapa. Kila mahali, kunatajwa kitu kimoja na jinsi kinavyosuhubiana na kuathiriana na kile cha pili. Dunia, kama asemavyo Nana, imejengwa na uwili huu wa ukinzani. Maneno ya Nana yanadokeza muktadha mahsusi unaohusu ugomvi wake na babake. Baba alidhamiria kushinda kwa kumlazimisha Nana awe chini ya mamlaka yake. Nana naye anajiona ni mtu mzima wa kujiamulia watu anaotaka kutangamana nao. Hili ndilo analosisitiza Nana katika mvutano wake na babake. Baba anapania mwanawe atangamane na watu wa aila ya juu kama alivyo yeye mwenyewe na haelekei kuufurahia uhusiano wa bintiye na Mpiga Gita (Faisal). Mwishoni, tunaonyeshwa kwamba baina ya kushinda na kushindwa, kushinda kunawavutia wengi ingawa kwa hakika hakuna mshindi. Nana anatoroka nyumbani na katika vita hivi vya baba na mwana, hakuna anayeshinda – kila mmoja anashindwa! Baadaye kidogo, Nana anatueleza waziwazi chanzo cha mawazo haya anapotuambia: Hapo nilimkumbuka Derrida na ubomozi wake anaouita (de)construction. Kila kitu lazima kiwe deconstructed. Naye hakuchukua muda kunijia katika fikra hii ya (de)construction. [...] Falsafa si mijineno tu. Si ubingwa tu wa kushindana ili mmoja amwone mwingine duni, ili yeye aonekane bingwa au gwiji. Falsafa ni maisha yenyewe. (Ivi: 60) Udenguzi au ‘ubomozi’ kama unavyorejelewa kwenye Nyuso za Mwanamke unahusishwa na usomaji uliopea wa kutazama kila neno katika jozi kwa jicho pekuzi. Usomaji huu umependelewa sana na wadenguzi wanaodai kuwa matini za fasihi zina tabia ya kuzungumzia kile zisichokidhamiria (Burman & MacLure 2005: 284f). Hii ni mianya inayostahili kufuatiliwa na msomaji ili aweze kuidengua kikamilifu matini husika. Dunia Yao, kupitia Ndi- inazungumzia hatua hii muhimu katika usomaji wa kidenguzi kwa kusema: ISSA MWAMZANDI 57 Madhumuni ni kujenga maana kwa njia ya kubomoa maana. Kujenga mvuto wa kisanaa. Ndiyo, unaweza kujenga maana hata katika mwanya mtupu. Hata ukitaka, unaweza kwa makusudi kupoteza maana kabisa kwa vivuli vya maana. (Mohamed 2006: 9) Katika dondoo hili kile kinachorejelewa kama kivuli cha maana ni ile sehemu ya pili ya neno au dhana katika jozi ambayo aghalabu huenda ikaachwa nje na isizungumziwe wazi wazi na mwandishi. Wadenguzi wanafuatilia maneno kama hayo kama linavyotarajia zoezi la kidenguzi ili kubainisha kile kisichosemwa na athari yake katika uwanja mzima wa maana (Schmitz 2007: 118;







No comments:
Post a Comment