JINA LA DIWANI: KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI GORA HAJI
WACHAPISHAJI: TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani inayozungumza juu ya mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja
na suala zima la ujenzi wa jamii mpya.Katika diwani hii,mwandishi ametoa
maadili na maonyo mbali mbali pamoja na mbinu mbalimbali za kufuata ili
kufanikiwa katika suala zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
MAUDHUI;
DHAMIRA KUU-Ujenzi wa jamii mpya
Mwandishi amejadili
dhamira ya ujenzi wa jamii mpya katika kazi yake.Mwandishi ameonesha vikwazo
mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini, Vikwazo hivyo ni
kama vile uongozi mbaya,rushwa,tamaa, ukosefu wa elimu, ukoloni mamboleo, n.k.
Katika kujadili
dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia mbalimbali ambazo jamii inapaswa
kuzitumia katika suala zima la ujenzi wa jamii mpya hapa nchini,hizo
ndizo dhamira ndogo ndogo;
1.
Uongozi Mbaya
Mwandishi ameonesha kuwa Uongozi bora
unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta ufanisi mzuri katika utendaji na
utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwani Uongozi mbaya unasababisha kushindwa
kufikia malengo.Kutokana na uongozi mbaya ndiyo maana jamii hufikia kufanya
mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika uongozi mpya ili kuijenga
jamii kwa upya.
Katika shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi anaongelea
juu ya mapinduzi yanayofanywa na tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala.mwandishi
anasema;
‘’kimbunga mji wa
siyu,kilichowahi kufika,
Si kwa yule wal
huyu,ilikuwa patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi
kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika’’.
Mwandishi ametumia mji
wa Siyu kama kielelezo kizuri kwa
jamii yeyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi wabaya/wabovu na
kuleta viongozi bora.Katika mapinduzi hayo mwandishi amefafanua kuwa wananchi wengi
ndio wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi la “Madanganyo”
mwandishi anazungumzia jinsi uongozi mbaya unavyowadanganya wananchi na jinsi unavyowaathiri
na kuwakera wananchi.Wananchi hushiriki katika shughuli za uzalishaji mali
(miradi mblimbali) lakini matunda ya jasho lao huliwa na wachache.Wachache hao
husahau wale waliosulubika katika uzalishajina na mtokeo yake wananchi
wanaishia kuishi maisha ya taabu.Katika Ubeti wa 6,msanii/mwandishi anasema;
“Mlitupigia mbiu,
tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, kwa
mapanga na mashoka,
Manufaa kwa wakuu,
wadogo yetu mashaka,
Wezeni kutukumbuka, mjue nasi wenzenu.”
Shairi la “Wenye
Vyao Watubana” mwandishi amejadili namna matajiri jinsi
wanavyowagandamiza,kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote yaani maskini.Mwandishi
anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii.Hii ni kutokana na
uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi hawachukui
tahadhari yeyote ile.Katika ubeti wa 7,mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga,kwa
lodi wa darajani,
Kujitolea mhanga,kwa
bei hawezekani,
Mvao wake wa kanga,ni
shilingi elifeni,
Wakubwa tuteteeni,
wenye vyao watubana.”
Shairi la “Kibwangai”
linajadili dhana ya usaliti wa viongozi
wetu kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi
wanavyowachagua viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au
wakishashika nyazfa wanageuka na kuwasaliti wananchi waliowachagua.Katika ubeti
wa 7,msanii anasema;
“Kibwangai lipoona, ni mtu
kakamilika,
Akaanza kujivuna,na
dharau kuzidiya,
Wala hakujali
tena,wenzake walowambiya,
Akahisi hawi nyani,umbo
lile litadumu.”
Katika Shairi hili
manii ametumia taswira ya Kibwangai kuwakilisha viongozi
wasaliti na nyani kuwakilisha wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai yaani watawaliwa.
Katika shairi la “Hili
Mnatutakiya”,mwandishi
anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi ,jeshi n.k namna vinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa
kuwalinda raia na kuwashughulikia wahalifu.Katika ubeti wa 1,msanii anasema;
Twasema
kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu mkatubwaga,hasa
ukiangaliya,
Hao wezi mwafuga,wazidi
kutuibiya,
Hakuna
watendewalo,ndipo wakapamba moto.
Msanii ameonesha kuwa
vyombo hivyo ndivyo vinavyowalinda
wezi,majambazi na matapeli.
Kwa ujumla msanii wa diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya
lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
2.
Kupiga vita rushwa
Rushwa ni kikwazo
kimojawapo kinachokwamisha kujenga jamii kwa upya.Kutokana na rushwa kuota
mizizi katika jamii haki hupotea bali wachache
wanafaidi matunda ya nchi na wengine
wanaendelea kuumia.Katika Shairi la “Rushwa” mwandishi anasema;
“Rushwa kajenga kambi,na
kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi,mkaidi
hashindiki,
Tumzushiyeni wimbi,
isiwe kutuhiliki,
Tumchimbie handaki,rushwa
tukamzikeni.”
Katika ubeti huu,mwandishi
anatuonesha kuwa lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki na usawa vitawale
kwani kupiga vita rushwa ni njia pekee itakayosaidia kujenga jamii mpya ambayo mwandishi
ameipendekeza.
3.
Umuhimu wa Elimu
Ili tuijenge jamii mpya ni lazima watu wapate
elimu na waelimike bila kujali umri wala jinsia.Mwandishi anawahimiza wazee
kujiunga na kisomo chenye manufaa ili wafute ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.Katika
shairi la “Kisomo cha Maarifa” ubeti wa 2,Msanii anasema;
Kisomo cha
manufaa,tusomeni kwa haraka,
Isiwe
tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
Roho si
inochakaa,mwili ndio hupayuka,
Tusomeni kwa
haraka,kisomo cha maarifa.
katika shairi hili
mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu wazima kwa
sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya maendeleo.
Mwandishi anaonesha
kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha zoezi zima la ujenzi wa jamii
mpya kwani bila kuwa na wasomi katika jamii kama hii yetu zoezi la
ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
4.
Kupiga vita ukoloni mamboleo
Ukoloni mamboleo ni kitendo
cha nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini kimaamuzi inatawaliwa na nchi
nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya
uchumi hapa nchini.Na ili tuweze kufanikisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini
hatuna budi kupiga vita ukoloni mamboleo.Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi
anaonesha jinsi ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa nchini.Ukoloni
mamboleo unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na kuwanufaisha
matajiri au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
“Ambao ni
matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri,
salama kujipatiya,
Walokuwa
mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye
Chuwi gani?
Mwandishi ameeleza
kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi zinazoendelea.Hivyo
mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia) hizo na tuupinge
ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii mpya.
5.
Umuhimu wa kujitawala
Ili tuweze kujenga
jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja zote za kifikra,kisiasa,kiutamaduni
pamoja na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “Mwandishi anaeleza kuwa ili tuweze kujitawala ni lazima tuepukane na unafiki,vibaraka
(wasaliti),tusikate tama na tudumishe amani. Katika ubeti wa 3 msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe,
wasiwe wenye kuzuzuka,
Tamaa uwakatishe,
yasiwe wanayotaka,
Katu wasiwawezeshe,
wabakiye kuzuzuka,
Washindike mahusuda,wasopenda
bara letu.”
Katika shairi la “Kujitawala” Mwandishi anaeleza umuhimu wa
kujitawala kwa jamii yoyote ile.Mwandishi anaonesha kuwa, kujitawala ni pale
umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa au
kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa
1 Msanii anasema:-
“Kujitawala si kwema,kuliko
kutawaliwa,
Kujitawala ni umma,kila yao kuamua,
Kujitawala si kama,ulanguzi na rushwa
Katika shairi hili la ‘kujitawala’
mwandishi anaonesha faida mbalimbali za kujitawala kama vile kuwepo kwa demokrasia,
kuwepo umoja naushirikiano,kuwepo haki na usawa,amani hudumishwa,vile vile mila
na desturiza nchi zinadumishwa.Hivyo mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii
mpya ni lazima tujitawale kisiasa,kiuchumi,kiutamaduni na kifikra.
6. Umuhimu wa kazi na kuwajibika
Kazi ni nguzo muhimu
sana ya ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi amesisitiza umuhimu wa kazi na kuwajibika.katika
shairi la “Kazi” Mwandishi anatuonesha kuwa kazi ndio msingi wa maendeleo.
Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na tuepukane na njaa. Ubeti wa 1,mwandishi anasema;-
“Pesa huletwa na kazi, ni njia zipitiayo,
Hutopata matumizi,iwapo kazi hunayo,
Hata njaa hukuhizi,uvivu na angamiyo’’
Katika shairi la “Uokolewe”,mwandishi anasisitiza umuhimu
wa kudumisha umoja na mshikamano ili kuinua uchumi wetu. Anasisitiza umuhimu wa
kufanya kazi kwa bidii na kutumia
vyema rasilimali zetu ili kuinua uchumi wetu.
Katika shairi la “Dumizi” mwandishi anakemea tabia ya baadhi ya watu kukaa bila kazi
(uvivu) na kuanza maisha ya kunyonya.Hivyo
mwandishi anapiga vita unyonyaji unaofanywa na baadhi ya watu.
Hivyo msanii aniasa jamii kujihusisha na ukulima, uvuvi,
utalii na viwanda ili kujenga jamii kwa upya.
7.
Mapenzi na ndoa
Katika diwani hii,mwandishi
ameonesha kuwa mapenzi yamegawanyika katika pande kuu mbili ambazo ni;Kuna
mapenzi ya kweli na mapenzi ya udanganyifu.
Katika shairi la “Usimpige
Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga mke wake na vile
vile mwanaume hatakiwi kumwekea mkewe
masharti magumu.
Shairi la “Hongera”
mwandishi anawaonya wanandoa (bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana
wawapo nyumbani. Amewapa kila mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za (4-5) mwandishi anasema:-
4- “Bi
arusi yangu shika, uyatie akilini.
Muumeo akifika, anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
Hongera!
5- “Bwana arusi sikia,
ukiwa kwako nyumbani,
Maneno ya kutupia,hayafai asilani,
Kauli njema tumia, na lugha iwe laini,
Hongera”
Katika shairi la “Sifa
ya Mke” msanii anaonesha kuwa
sifa kubwa ya mwanamke ni tabia na wala
si sura.Sifa ya tabia njema humpa mwanamke taadhima,huruma,utiifu na
hata uhodari. Anaeleza kuwa mwanamke anapaswa
kuwa mtulivu,asiwe kiruka njia, asiwe na
ufedhuli wa aina yoyote,uovu, n.k.
Katika shairi la “Sitaki”mwandishi
anakemea mapenzi ya udanganyifu yaliyoshamiri katika jamii zetu kwa wakati huu.
Mwandishi anasema:-
“Rabi sinipe mapenzi,hakuna wa
kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi,ni
wachache duniani,
Penzi la siku
hizi,kuhadaana nyoyoni,
Mapenzi yamepotea, sasa
ni adimu sana,”
Ni kweli mapenzi ya
siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina pamoja na
udanganyifu.Mwandishi anaitaka jamii kutambua kuwa mapenzi ya pesa si mapenzi
ya kweli hivyo ni vyema yapigwe vita.
8. Maonyo na maadili mema katika maisha
Mwandishi amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu
kuhusiana na harakati mbali mbali za maisha.Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni
kielelezo kizuri kinachofaa kufuatwa na kizazi hiki.Maadili na maonyo haya ni
ya muhimu sana katika maisha.Maadili hayo ni kama vile:-
(a)Malezi bora katika
jamii ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msingi bora wa maisha.Katika shairi la“Vijana wa Zanzibar” Mwandishi
ameonesha matendo ambayo vijana wa siku hizi
wanayatenda ambayo si mazuri pia
ni ya kusikitisha.vijana wa siku hizi hawana utii,ni wajeuri, ni wadanganyifu,ni
majambazi na pia hudharau mila na desturi zetu za asili na kukimbilia tamaduni
za kigeni.Katika ubeti wa 2 msanii
anasema:-
“Mwawacha yenu ya hapa,ambayo
yako mazuri,
Kutii na kuogopa,mwaona
hakuna kheri,
Mwayavamia kwa pupa,kwa
kedi na ujeuri,
Mila zetu za fakhari,wacheni
kuzipotosha.”
Kulingana na ubeti huu
mwandishi anaonesha kuwa suala la malezi bora ni muhimu sana katika jamii ili
kuwaandaa vijana wetu kuendana na mazingira wanamoishi.
Kwa ujumla, katika suala la malezi mwandishi anaifundisha
jamii kuwa,samaki mkunje angali mbichi.
b)Umuhimu wa
kuwathamini wazazi
Mwandishi ameonesha
kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi.Katika shairi la “Wazazi”
msanii ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao
ya mtoto; hivyo mtoto hatakiwi kuwakasirikia,kuwaudhi wala kuwachikiza bali
anatakiwa kuwa na mapenzi nao.Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni kumpa chakula, mavazi,malezi mema pamoja na
elimu.Katika ubeti wa 4 msanii anasema;
“Wakatafuta walimu,kukupatia
ujuzi,
Wakakufunza elimu,pamoja
na matumizi,
Sasa ni mtu timamu,waendelea
na kazi,
Usiwaudhi wazazi,hiyo
ndiyo yako ngao”
Katika shairi la “Ulezi
Kazi” Mwandishi ameonesha jinsi mama (wazazi) wanavyohangaika kubeba
mimba hatimye kuzaa na kuanza kazi ya ulezi wa mtoto hadi anapofikia umri wa
kujitegemea. Mwandishi anaonesha kuwa wazazi hupata taabu na shida mbalimbali
katika ulezi wao.Hivyo mwandishi anashauri wazazi wathaminiwe na wapewe heshima
zote wanazostahili.
c)Kuepukana na umbea
Umbea ni ile tabia ya
kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii si nzuri,kwani
huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika shairi la “Wacha
Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na badala yake
ijishughulishe na shughuli za uzalishaji mali.Madhara ya umbea ni kama vile
majungu,uchochezi,n.k. Umbea pia husababisha utengano baina ya ndugu au
marafiki.Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
“Wacha kupika majungu,na kuleta
uchochezi,
Kuwajaza walimwengu,kasumba
zile na hizi,
Hicho kimoja kifungu,huletesha
ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi,huvunja
mafanikiyo.”
Katika shairi la “Hayafai
Mitaani” mwandishi anaionya
jamii kuwa si jambo la busara au zuri kusambaza au kupeleka taarifa ya jambo fulani
sehemu ambayo haihusiki.Anaona kuwa ni busara sana endapo jambo fulani limefanyikia
sehemu fulani liishie huko huko lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu
isiyohusika.Si tabia nzuri kupeleka mitaani kwa watu wasiohusika. Katika ubeti
wa 2 unasema:-
“Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani, mitaani kufikisha,
Kwani siri ya mwituni, si vyema kuelewesha,
Ya kunini huishia kunini.”
Hivyo mwandishi
anatushauri kuwa jambo moja likitendeka sehemu moja ni bora liishie katika
sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
(d)Kuepukana na udokozi
(tabia ya wizi)
Udokozi ni ile hali ya
kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au kunyang’anya.Katka shairi
la ‘Paka’mwandishi
anakemea tabia hii kwani si nzuri.Tabia
hii ipo miongoni mwa wanajamii.Mwandishi anaonya kuwa tabia hii huhatarisha
maisha ya wahusika yaani wenye tabia hii.Mwandishi amemtumia paka kuwakilisha
watu wenye tabia hiyo.Aidha mwandishi anaendelea kuelezea kuwa tabia hii husababisha uchokozi,ugomvi pamoja na chuki katika maisha.
(e)Umuhimu wa shukrani
katika maisha
Mwandishi anaieleza
jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu mwingine.
Katika shiri la “Punda” mwandishi
ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo na shukrani kwa wenzao ple wanapotendewa
mema.Mwandishi ameonesha kuwa mwandamu asiye na shukrani hata umfanyie wema kiasi
gani hawezi kutoa shukrani.Ameelezea kuwa mtu asiye na shukrani ni vyema kuachana
naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa. Anasema;
“Punda hakumbuki wema,hata
kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na
maji anufaike,
Katu haiwi salama,
shukrani zake mateke,
Ndiyo tabia ya punda,kurusha
rusha mateke,
Kuchunga akikushinda, muwachiye ende zake.”
Katika ubeti huu,mwandishi
anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa fadhila au jambo jema.
UJUMBE
Ø Dhana potofu ya kudhani bila ya kuwa
na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa sababu hupotosha ukweli wa mambo.
Ø Mapenzi na ndoa ya dhati ni muhimu
katika jamii zetu
Ø Ukoloni mamboleo, uongozi mbaya,rushwa
na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
Ø Maadili mema na maonyo ni njia pekee
ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.
FALSAFA
Mwandishi anaamini
kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msimamo
na mwenendo bora wa maisha na anatetea
misingi ya haki na utu katika jamii.
MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi
una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo kwa kudhani tu bila kuwa
na misingi ya kisayansi.
FANI
a)Muundo
Mwandisha ametumia miundo
tofauti katika diwani hii kama vile;
Ø Tarbia (mistari 4) katika shairi la Kisomo cha manufaa,
Ø Tathlitha(mistari 3) katika shairi la “Kujitawala” (uk 7-8).
Ø Takhimisa (sabilia) – mistari 5 na kuendelea katika
shairi la “Punda” na shairi la “Bahati”.
b)Mtindo
Mtindo uliotumika ni
ule unaofuata kanuni za kimapokeo yaani urari wa vina na mizani pamoja na
mpangilio wa beti.Karibu mashairi yote yana vina vya kati na mwisho isipokuwa katika
mashairi ya “Kimbunga”,“Dumuzi’, “Madereva”,“Chuwi” yana
nusu mstari katika kituo.
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi ametumia
lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja yenye mafumbo na taswira mbali
mbali pamoja na tamathali za semi kidogo
na misemo kwa kiasi.
d)TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
Ø Kwenye shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
·
Ufedhuli
na uovu kama yake mazoea.
·
Awe
kama malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi ametumia
mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali,machafu,matusi kwa kutumia tafsida.Mfano
shairi la “Nyang’au”linahusu tamaa,Paka” linahusu wizi, shairi la “Dumuzi” linakemea uvivu,n.k.
Mbinu Nyingine za
Kisanaa
Takriri
Mwandishi ametumia
takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8) neno kujitawala
limerudiwarudiwa.
Matumizi ya Taswira
Mwandishi ametumia
taswira nyingi kama vile;
Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi
wasaliti
Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi
waliosalitiwa
Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni
mamboleo, n.k.
Jina la Kitabu
Jina la Kitabu Kimbunga halisadifu yale yaliyomo ndani
ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili katika kitabu
hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya kimaisha.Asilimia kubwa ya
mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo na maadili katika maisha.
Kufaulu kwa
Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu ;
Ø Kutoa maadili mema na maonyo katika
jamii
Ø Kujadili dhamira ya ujenzi wa jamii
mpya
Ø Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata
ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani
Ø Ametumia lugha rahisi, mafumbo,
taswira, n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Ø Baadhi ya maadili aliyoyajadili
katika diwani hii ameyajadili kidhanifu,ni sawa na yale tunayoyapata
makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii mpya
Ø Vile vile amejadili masuala
mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu.Kama vile masuala ya kipaji (uk
38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani
v Mwandishi ametumia lahaja ya Unguja badala ya Kiswahili sanifu
ivyo ni vigumu kueleweka kwa watu wote.
v Diwani hii ni ya hali ya chini sana
katika muundo,mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya kisanaa.
No comments:
Post a Comment