MADA YA TANO: USIMULIZI
Usimulizi
ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani.
Katika mada hii utajifunza juu ya taratibu za usimulizi wa matukio kupitia njia
kuu mbili za masimulizi, yaani kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Pia
utaweza kujifunza juu ya mbinu mbalimbali za usimulizi.
Usimulizi wa Hadithi
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu
mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia
hutegemea namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa
msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya
maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio
fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya
kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye
yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.
Usimulizi wa Habari
Taratibu za Usimulizi wa Matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni
kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi
msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao
kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika
usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
- Aina ya tukio
– msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa
mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
- Mahali pa tukio –
ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha
ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa
kutaja hata jina la mtaa.
- Wakati –
katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni
asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa
ngapi.
- Wahusika wa tukio –
ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri
wao n.k.
- Chanzo cha tukio –
kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
- Athari za tukio –
athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi
wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
- Hatima ya tukio –
msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio
kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni
ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa
hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi
hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
- Utangulizi
– sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia
na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio
huwa ni maneno machache kiasi yasiyozidi aya moja.
- Kiini –
kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika,
muda, mahali na athari za tukio.
- Mwisho –
mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio
linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo
ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo
amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate
kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali
inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi,
utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji
atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo
ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao
unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha
habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano,
yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa
unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.
No comments:
Post a Comment