MADA YA
NNE: FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi ni moja kati ya
tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu
na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza
kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu.
Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi
Tanzu za Fasihi Simulizi
Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi
inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya
mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.
Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja
na hizi zifuatazo:
- Masimulizi/hadithi
- Semi
- Ushairi
- Mazungumzo
- Maigizo
- Ngomezi
Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi
Simulizi
SIMULIZI/ HADITHI
Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia
habari fulani. Ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na
mtiririko wake huwa mwepesi au sahili. Urefu wa hadithi hutofautiana kutoka
kitanzu/kipera kimoja hadi kingine. Kwa jumla zipo hadithi ambazo ni za kubuni na
zingine za kihistoria. Baadhi ya vipera vya utanzu huu ni:
Ngano
Hizi ni hadithi za kimapokeo
zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu
maisha. Vijipera vya kipera hiki ni:
- Istiara
– hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine
iliyofichika. Yaani hadithi nzima ni kama sitiari.
- Mbazi-
hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au
wa kumkanya mtu
- Kisa-
hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli.
Visakale
Masimulizi ya kimapokeo juu ya
wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia. Kwa
mfano hadithi za Liyongo
Mapisi
Maelezo ya historia bila kutia mambo
ya kubuni.
Soga
Ni hadithi ndogo ndogo zinazohusisha
utani na ucheshi kwa kiasi fulani. Hizi ni hadithi ambazo hutambwa katika
mtiririko wa matukio ambao huzua kicheko. Soga hudhamiria kuchekesha na pia
kukejeli.
Tarihi
Hizi ni hadithi ambazo husimulia au
zimejengwa kwenye matukio ya kihistoria. Inawezekana matukio yanayosimuliwa
yakawa ya kweli, yaani yalipata kutokea kihistoria. Hadithi hizi hutokea zaidi
katika maandishi.
Visasili
Ni utanzu unaofungamana na imani za
dini na mizungu ya jamii. Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na
mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu
asili yao wenyewe, na maana na shabaha ya maisha yao. Mara nyingi hadithi hizi
huaminiwa kuwa ni kweli tupu, na hutumika kuelezea au kuhalalisha baadhi ya
mila na madhehebu ya jamii inayohusika.
Vipera vya Ushairi
Huu ni utanzu wa fasihi simulizi
unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa
kawaida. Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani.
Nyimbo
Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Kipera
hiki kimegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea,
kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za
vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
- Tumbuizo:hizi
ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali
kama vile ngomani au harusini. Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza
watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga
kubembeleza watoto.
- Kongozi:hizi
ni nyimbo za kuaga mwaka.
- Nyimbo za dini:hizi
ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu.
- Wawe:hizi
ni nyimbo za kilimo; huuimbwa wakati wa kulima.
- Tenzi:hizi
ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha.
- Tendi:hizi
ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa, wahusika wa
tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa.
- Mbolezi:hizi
ni nyimbo za kilio au maombolezo.
- Kimai:hizi
ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini.
- Nyiso:hizi
ni nyimbo za jandoni.
- Nyimbo za vita:hizi
ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita..
- Nyimbo za watoto:hizi
ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao.
- Nyimbo za uwindaji:hizi
ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au
sherehe zao.
- Nyimbo za Taifa:hizi
ni nyimbo za kusifia Taifa au kabila.
- Nyimbo za kazi:hizi
ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima,
kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika
Maghani
Maghani ni istilahi inayotumiwa
kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa.
Kipera hiki kina vijipera vitatu
ambavyo ni maghani ya kawaida,sifonamaghani masimulizi.
Maghani ya kawaidani kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za
ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini
ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo:hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na
mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Sifo huwa na tanzu muhimu
kama vile vivugo (majigambo),pembezinatondozi.
- Kivugo:hili
ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe.
- Tondozi:hizi
ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu.
Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi,
historia au tukio fulani. Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara,
ngano, sifo na tendi.
- Rara ni
hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua; rara huimbwa au
kughanwa ikiambatana na ala za muziki.
- Ngano:hizi
ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika
kuelezea au kuonya kuhusu maisha.Ngano huwa ghani masimulizi
inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
- Sifo:hizi
ni tungo za kusifu: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika
utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.
- Tendi:hizi
ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito
kijamii au kitaifa.
Vipera vya Semi
Semi ni tungo au kauli fupifupi za
kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Baadhi ya tanzu katika
kundi hili ni:
- Methali:
Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo,
mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Mara nyingi mawazo hayo huelezwa
kwa kutumia tamathali hasa sitiari na mafumbo. Methali nyingi huwa na
muundo wenye sehemu mbili. Sehemu ya kwanza huanzisha wazo fulani, na
sehemu ya pili hulikanusha au kulikaamilsha wazo hilo. Kwa mfano; mwenda
pole hajikwai, aliye juu mngoje chini.
- Vitendawili:
Ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili iufumbue. Fumbo hilo
kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo, na mara nyingi lina
mafunzo muhimu kwa washiriki, mbali na kuwachemsha bongo zao. Vitendawili
ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha
vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile.
- Misimu:
Ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea
mazingira maalum. Msimu ukipata mashiko ya kutosha katika jamii huweza
hatimaye kuingia katika kundi la methali za jamii hiyo.
- Mafumbo:
Ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika.
Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalum, hivyo ni tofauti
na methali au vitendawili ambavyo ni semi za kimapokeo.
- Lakabu:
Haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia
kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina
haya huwa ni maneno au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbwa. Mara
nyingi majina haya huwa ni sitiari. Baadhi ya majina haya humsifia mhusika,
lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha; Mifano: simba wa yuda- Hali
Selassie, Baba wa taifa – Mwl Nyerere.
Vipera vya Maigizo
Maigizo ni mchezo ambao hutumia
watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha
na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira.
Uhakiki wa kazi za Fasihi Simulizi
Umuhimu wa Uhakiki wa Kazi za Fasihi
Simulizi
Umuhimu wa uhakiki wa kazi za fasihi
simulizi ni kubaini ubora wa kazi za fasihi simulizi, kubaini vipengele
mbalimbali vya fani na maudhui, kupima namna kazi inavyoambatana na mazingira
inamotokea, kupima kufaa na kutokufaa kwa fasihi simulizi, kubaini ukweli wa
mambo yanayoelezwa, kuangalia uhalisi wa watu na mazingira katika jamii na
kubaini umuhimu wa kazi ya fasihi katika jamii husika.
Vigezo vya Uhakiki wa Kazi za Fasihi Simulizi
Uhakiki wa kazi ya fasihi huzingatia
vigezo viwili ambavyo vimegawanyika katika vipengele mbalimbali. Vigezo hivyo
ni fani na maudhui. Katika kigezo cha fani mhakiki atazingatia muundo, mtindo,
matumizi ya lugha, wahusika na mandhari wakati katika kigezo cha maudhui
mhakiki atazingatia dhamira, migogoro, falsafa, msimamo na ujumbe.
Uhakiki wa Hadithi
Uhakiki wa hadithi kama ilivyo
katika kazi nyingine za fasihi simulizi umejikita katika kuchunguza vipengele
mbalimbali vya fani na maudhui. Vipengele vya fani ni muundo, mtindo, wahusika,
mandhari na matumizi ya lugha. Aidha kwa upande wa maudhui, vipengele vyake ni
dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe na msimamo.
Matumizi ya Semi katika Hadithi
Uhakiki wa semi katika fasihi
umejikita kuangalia usahihi wa matumizi ya vipengele mbalimbali vya lugha
katika kazi ya fasihi inayohusika. Vipengele hivyo ni misemo, nahau na mafumbo.
Vilevile uhakiki wa semi umejikita katika kuchunguza namna lugha ilivyofuzu
kigezo cha kwenda na wakati.
No comments:
Post a Comment