KISWAHILI
KIDATO CHA PILI
MADA
YA KWANZA: UUNDAJI WA MANENO
Uundaji wa maneno ni ujenzi au
uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa maneno mapya husaidia
kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano. Uundaji wa
maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na
maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa mfano tunayo maneno mapya,
kama vile ufisadi, uwekezaji, ukeketaji, ujasiriamali na mengine mengi kutokana
na mabadiliko ya kijamii.
Kutumia Uambishaji
Kubainisha Mofimu katika Maneno
Uambishaji wa maneno ni kitendo cha
kupata maneno kwa kubandika Mofimu kwenye kiini cha neno, uambishaji kutokea
kabla ya kiini cha neno au mzizi wa neno. Mfano kiini pig- unaweza kuunda
maneno kama inapiga, anayepiga, mpigaji, amepigika nk.
Mofimu zinazobadilika kwenye kiini
cha neno huitwa Viambishi.
Katika lugha ya Kiswahili viambishi
hutokea kabla na baada ya kiini cha neno.
Mfano
Wanapendana = Wa-na-pendan-a kiini
cha neno ni-pend-.
Mofimu zilizobadilisha baada ya
kiini –an-na-a viambishi vinavyotokea kabla ya kiini cha neno huitwa viambisha
awali au tangulizi. Viambisha vinavyotokea baada ya kiini cha neno huitwa
viambishi tamati au fuatishi.
Example 1
Angalia mifano ifuatayo:
Neno
|
Viambisha Awali
|
Kiini Viambisha
|
Tamati
|
Unapendelea
|
u-na-
|
-penda
|
el-e-a
|
Waliongozana
|
wa-li-
|
-ongoz-
|
an-a
|
Analima
|
a-na-
|
-lim-
|
-a
|
anayeiimbisha
|
a-na-ye
|
-imb-
|
-ish-a
|
Dhima za Mofimu
Bainisha dhima za mofimu
Baadhi ya dhima za uambishaji ni
kama ifuatavyo:
- Kuonyesha upatanisho wa usanifu maana ya maneno
yanayozalishwa kutofautiana katika msingi wa kusanifu tu, lakini uhusiano
wa maneno hayo hutokana na kiini au mzizi wake uleule.Mfano;Fundisha
kiini chake ni fund. Unaweza kuzalisha maneno mengine kwa kutumia
mzizi/kiini kilichopo kama vile fundishana, mafundisho, mfundishaji,
fundishwa, fundishana.
- Uambishaji huonyesha nafsi
- Uambashaji huonyesha njeo (muda)
- Uambishaji huonyesha urejeshi
- Uambishaji huonyesha ukanushi
- Uambishaji huonyesha hali mbalimbali za kitenzi
Vitenzi vikiambishwa huweza
kujenga/kuunda/kuzalisha vitenzi vingine au nomino.
Example 2
Mfano
Vitenzi
|
Kiini
|
Nomino
|
Vitenzi
|
Cheza
|
-chez-
|
Mchezaji, mchezo
|
wanacheza/atamchezea
|
Piga
|
-pig-
|
Mpigaji, Mpiganaji
|
watanipiga, aliyempiga/wanaompiga
|
Uambishaji
hutumika kuzalisha viwakilishi na vielezi.
Neno (Kiwakilishi)
|
Kiini
|
Kielezi
|
Huyu, Huyo
|
Hu
|
Humu, humo
|
Wangu, wako,wake
|
wa
|
|
Hii, hizo, hiki
|
hi
|
Viambishi awali vina dhima ya
kudokeza nafsi, njia, idadi urejeshi na ukanushi.Mfano:
Hawakulima
- Ha-, kiambishi cha ukanushi
- Ku-, kiambishi njeo/wakati
Viambishi tamati vina dhima
mbalimbali hudokeza hali ya utendekaji, ukamilishaji au kimalizio cha neno na
kauli za matendo kama vile kutendwa, kutendewa,kutendeka nk.
Dhima:Ukanusho, kutendeana, agizo na
mtendwa, ukamilisho, usababishi.
Mfano 3
Neno
|
Viambishi Tamati
|
Anapiga
|
-a
|
Wanapigana
|
-an
|
Asipigwe
|
-w
|
Amempigisha
|
-ish-
|
Viambishi tamati vina dhima ya
kutambulishwa mapema/nomino zilizoundwa kutokana na vitenzi.
Neno
|
Kiini
|
Viambishi Tamati
|
Piga
|
pig-
|
-o
|
Mchezo
|
chez-
|
-o
|
Mtembezi
|
tembe-
|
-z-i
|
Mfiwa
|
-fi-
|
-us-a
|
Kutumia Mnyumbuliko
Mazingira yanayosababisha Mahitaji ya Maneno Mapya
Elezea mazingira yanayosababisha
mahitaji ya maneno mapya
Mnyumbulisho ni neno linalotokana na
neno nyumbua. Kunyumbua kitu ni kuvuta, kuongeza urefu wa kitu hicho.
Kunyumbua katika lugha ya Kiswahili
ni kuongeza vinyumbulishi katika katika kiini ili kupata msamiati mpya. Hivyo
basi, mnyumbulisho ni njia mojawapo na inasaidia kuunda maneno kwa njia ya
kunyumbulisha.
Viambishi vinapochukuliwa katika
kiini cha neno, basi neno hilo huwa limenyumbulishwa. Kwa mfano neno lima kiini
chake lim- huweza kunyumbulishwa na kupata maneno mengine mpya, kama lim-ishwa,
lim-ia, lim-w-a.
Pia maneno ya mnyumbulisho yanaweza
kuundwa kwa kuongeza viambishi kwenye shina, kwa mfano:
Neno
|
Kiini
|
Shina
|
Maneno ya Mnyumbuliko
|
Elekea
|
elek
|
eleka
|
Elekeana, elekea, elekwa, elekesha
|
Shikishana
|
shik
|
shikisha
|
Shikishana, shikisha, shikishaneni
|
Kwa ujumla tunawaza kusema kuwa maneno
ya kawaida hunyumbulika. Hivyo kiini/mzizi au shina moja huweza kuzalisha
maneno mengine mengi ambayo yanatokana na msingi mmoja wa maana.
Dhima ya Uambishaji na Mnyambulikoa wa Maneno
Dhima ya uambishaji ni kuleta
upatanisho wa kisarufi, kuonesha idadi na umoja na wingi katika ngeli za
majina, kuonesha njeo na kuonesha urejeshi pamoja na hali mbalimbali kwa
uambikaji wa viambishi kabla ya mzizi wa neno. Aidha dhima ya mnyambuliko ni
kuonesha matokeo ya tendo na kuzalisha kauli mbalimbali kwa kupachika viambishi
baada ya mzizi wa neno.
Kuunda Maneno mbalimbali kwa kutumia
Mnyambuliko
Unda maneno mbalimbali kwa kutumia
mnyambuliko
Uundaji wa maneno mbalimbali kwa
kutumia mnyambuliko hufanyika kwa kupachika viambishi baada ya mzizi wa neno na
hivyo kulifanya neno husika liweze kuonesha matokeo mbalimbali ya matendo
pamoja na kuzalisha kauli mbalimbali za matendo.
Zoezi 1
Unda maneno mbalimbali kwa kutumia
mnyambuliko
Kutumia Maneno ya Mnyambuliko katika
Miktadha mablimbali
Tumia maneno ya mnyambuliko katika
miktadha mablimbali
Maneno ya mnyambuliko hutumika
katika miktadha mbalimbali ambapo miktadha hiyo hujitokeza katika kauli
mbalimbali za vitenzi. Kauli hizo ni kauli ya kutenda, kauli ya kutendwa, kauli
ya kutendewa, kauli ya kutendea, kauli ya kutendeka, kauli ya kutendesha, kauli
ya kutendana, na kauli ya kutendama.
Zoezi 2
Tumia maneno ya mnyambuliko katika
miktadha mablimbal
MADA YA PILI: MATUMIZI YA LUGHA KATIKA
MIKTADHA MBALI MBALI
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo
wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida
mbalimbali za jamii inayohusika.
Rejesta
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta
kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na
uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande
mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha
fasaha, mfano katika elimu, mahakamani na kadhalika.
Kuwasiliana kwa kutumia Rejesta
Rejesta za Mitaani
Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa
magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka
kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo. Mfano wa maneno yanayotumika
sana mitaani ni kama vile “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke) n.k. Kwa ujumla
lugha ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani
ambayo yanaeleweka kwa wazungumzaji wenyewe.
Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo ya kwenye shughuli
maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum
zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu
kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli
maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
- Maofisini au mahali popote pa kazi
- Mahakamani
- Hotelini
- Hospitalini
- Msikitini
- Kanisani n.k
Mazungumzo ya mahotelini yana
utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Nani wali kuku?
B: Mimi
Chai moja wapi?
B: Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza
“Nani wali kuku”, ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”.
Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni
tofauti na lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza usahihi ili
kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano 1
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio
la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za
Tanzania?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa
kitabu cha sheria za Tanzania na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi: Ulichukua muda
mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi: Sijui.
Kimsingi hii ni hali ya kawaida
kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama
hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka,
wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa
maelezo.
Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale
mawasiliano yasiyo rasmi, ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au
mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
- Vijana wenye rika moja,
- Wazee wenyewe,
- Wanawake wenyewe,
- Wanaume wenyewe,
- Mwalimu na mwanafunzi,
- Meneja na wafanyakazi wake,
- Mtu na mpenzi wake, n.k.
Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa
rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu
wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
Mfano 2
Mfano:
'Basi, Master jana wikiendi ilikuwa
kibaridi sana. Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga.
Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa noma kila
mzamiaji. Alikuwa mnoko kishenzi. Akatema mkwara mbuzi, nikajibu kwa
mkwaradume....akabloo mimi ndani’.
Maana ya Maneno
- Wikiendi – Mwisho wa wiki
- Kibaridi –tulivu
- Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa
- Zinga la Mnuso –sherehe kubwa
- Saiti –sehemu
- Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni
ametulia pembeni
- Noma – Hatari
- Mnoko kishenzi – kinaa sana
- Mkwara mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja
unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili.
Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.
Dhima za Rejesta
Katika kipengele cha utambulisho wa
kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha
miongoni mwa watumiaji wake au kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii
husika. Pia katika utambaulisho wa kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu
hutambulika katika jamii kulingana na namna anavyoongea kulingana na hadhi,
tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza kusababisha mshikamano au mwachano
katika mazungumzo. Kwa mfano jamii itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi
kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo anaoutumia, au ni mtu wa mtaani
kulingana na lugha anayotumia.
Rejesta, ina nafasi kubwa sana
katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hii ni
kutokana na kwamba, madhumuni makuu ya mawasiliano katika biashara ni kuwavutia
wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma wanazouziwa ni za kiwango
cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha ya biashara (rejesta), kwa
kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au huduma, huwa na sentensi au
vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu” pia huwa na lugha ya kupumbaza
na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia rejesta inasaidia sana
kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika masuala mbalimbali ya
kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii. Mfano hospitalini
“mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni “kata nusu” na maeneo
mengine.
Baadhi ya rejesta hutumika kupunguza
idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe mafupi na yanayoeleweka kwa
urahisi mfano rejesta za hotelini kama vile:- Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja:
hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa.
Pia katika kutolea elimu ya dini
kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa katika kujenga maadili.
Vilevile rejesta ina nafasi ya
kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza hapa na pale hupenda
kutumia maneno tofautitofauti ili kufanya mazungumzo yawe ya kuvutia. Mfano
mazungumzo miongoni mwa vijana:
Kijana 1: Niaje? Nakuona umechili
Kijana 2: mzuka jembe. Kama kawa…
kama dawa!
MISIMU
Kuwasiliana kwa Kutumia Misimu
Misimu ni semi za muda na mahali
maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. misimu inayodumu
huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya lugha ya jamii hiyo.
Chanzo cha misimu
- Misimu huzuka kulingana na mabadiliko ya kihistoria
yanayoikumba jamii husika katika nyakati mbalimbali.
- Misimu huzuka kutokana na haja ya watu kuelezea hisia
zoa juu ya matukio mbalimbali yaliyotokea katika vipindi fulani kwa mfano,
njaa, mafuriko, vita n.k.
Aina za misimu
- Misimu ya pekee.
Hii ni misimu ambayo huelezea mahusiano ya kikundi kimoja kutoka katika
utamaduni mmoja, na hujulikana miongoni mwao pekee.
- Misimu ya kitarafa.
Misimu hii hujulikana na watu wengi katikia eneo kubwa, yaweza kuwa ni
kata, wilaya au tarafa.
- Misimu zagao.
Ni misimu iliyoenea nchi nzima au pengine kuvuka mipaka ya nchi, misimu
hii husikika redioni, magazetini na hata kwenye vitabu. Msimu uliokita
mizizi sana huweza kusanifishwa na kuwa msamiati rasmi.
Sifa za misimu
- Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya
jamii
- Ni lugha isiyo sanifu
- Ina chuki
- Ni lugha ya mafumbo
- Ina maana nyingi
Dhima ya misimu
- Hutumika kupamba lugha
- Hutumika kukuza lugha
- Hutumika kutunza historia ya jamii fulani
- Hutumika kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji
- Hufurahisha na kuchekesha
Lugha ya Kimazungumzo na ya Kimaandishi
Sifa ya Lugha ya Kimazungumzo
Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya
watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo
lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha
mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo
ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo
kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za
kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.
Faida ya lugha ya mazungumzo
- Mzungumzaji anaweza kukaa ana kwa ana na msikilizaji,
hivyo hukuza uhusiano.
- Mzungumzaji anaweza kutumia ishara za mwili katika
kusisitiza maelezo yake.
- Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kuuliza au
kuulizwa maswali.
- Mzungumzaji anaweza kuonesha hisia zake kwa kulia,
kupaza sauti, kupunguza sauti, kuonyesha furaha huzuni au hasira.
- Mzungumzaji anaweza kuuliza maswali, kuona hisia za
mzungumzaji kwa kusikiliza lugha zinazotolewa na kuangalia ishara za mwili
zinazotumika.
- Mzungumzaji anaweza kupata nafasi ya kufuta usemi wake,
kuongezea jambo au kutoa maelezo ya ziada.
- Mzungumzaji anaweza kubadilisha lugha yake kulingana na
mazingira aliyomo.
- Mzungumzaji anao uhuru wa kutumia lugha ya mitaani,
misimu kulingana na muktadha.
Matatizo ya lugha ya mazungumzo
- Maelezo lazima yahifadhiwe kichwani, hivyo kama mtu
hana kumbukumbu, taarifa zilizotolewa hupotea na kusahaulika.
- Mtumiaji wa lugha ya mazungumzo anaweza kurudiarudia
vipengele fulani na hivyo kuichosha hadhira.
- Ujumbe unaweza usieleweka kama unatolewa kwenye kelele
nyingi
Lugha
ya maandishi
Hii ni lugha inayowasilishwa kwa
njia ya maandishi. Lugha ya maandishi huzihusiha pande mbili, mwandishi na
msomaji. Lugha ya maandishi sharti iwe fasaha ili msomaji anaposoma maandishi
hayo, apate kuelewa kila kitu, yaani asibaki akijiuliza maswali.
Lugha ya maandishi huambatana na
alama za uakifishaaji, hii husaidia maandishi kusomeka vizuri na kueleweka kwa
urahisi
Ubora wa lugha ya maandishi
- Lugha ya maandishi huwawezesha watu walio mbali
kuwasiliana.
- Lugha ya maandishi hustawisha sarufi ya lugha na
misingi yake, kwa sababu mwandishi anahakikisha kwamba anazingatia vizuri
kanuni za kisarufi ili msomaji wake aweze kumwelewa.
- Ili kuhakikisha maelezo yake yanaeleweka mwandishi
analazimika kuandika kwa uwazi na kwa kuzingatia kanuni na miiko yote ya
uandishi.
Udhaifu wa lugha ya maandishi
- Lugha hii hutumiwa na wale tu wanaojua kusoma na
kuandika.
- Lugha ya maandishi haina msisimko uletwao na lafudhi na
matamshi.
- Msomaji hukosa vidokezo vingi ambavyo katika lugha ya
mazungumzo huchangia katika mawasiliano.
- Lugha ya maandshi inamnyima mwandishi nafasi ya kupima
welewa wa msomaji kwa kuwa hamwoni.
Dhima
ya lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi
Lugha ya mazungumzo na lugha ya
maandshi zote zina umuhimu wa pekee katika maisha ya kila siku kwa sababu ndizo
zinzaowezesha watu kuwasiliana kwa namna mbalimbali.
Umuhimu wa lugha ya maandshi pia
hutokana na dhima yake kwa watu. Maandishi yanaweza kuhifadhiwa na kusambazwa
kwa watu wengi hata walio mbali. Maandishi yanahifadhi kumbukumbu na kwa muda
mrefu. Kwa hali hii, watu wa vizazi vingine wanaweza kusoma na kujua mambo
yaliyofanyika karne nyingi zilizopita.
Tofauti kati ya lugha ya mazungumzo
na lugha ya maandishi
- Lugha ya mazungumzo huwezesha mawasiliano ya ana kwa
ana lakini lugha ya maandishi haiwezeshi mawasiliano ya ana kwa ana.
- Lugha ya mazungumzo haihitaji maandalizi wakati lugha
ya maandishi huhitaji maandalizi. Mwandishi atalazimika kupata muda wa
kuandika pamoja na kuandaa vifaa kama vile kalamu, karatasi n.k
- Lugha ya mazungumzo hailazimiki kuzingatia kanuni za
kisarufi, lakini lugha ya maandshi hutakiwa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Tofauti nyingine kati ya lugha ya
maandishi na lugha ya mazungumzo huweza kuonyeshwa katika jedwali lifuatalo.
Kipengele
|
Mazungumzo
|
Maandishi
|
Muktadha
|
|
|
Mada
|
Hazina uzito mkubwa
|
Huelekea kuwa na uzito mkubwa.
|
Mpangilio
wa mada na mawazo
|
Hautabiriki. Unaelekea kutokuwa na
mtiririko.
|
Hutabirika. Huelekea kuwa na
mtiririko.
|
Mjadala
wa mada
|
Hauelekei kuwa na kina. Hazichujwi
kwa uaangalifu.
|
Unaelekea kuwa na kina. Huchujwa.
|
Dhima ya matumizi ya lugha
Dhima kuu ya lugha ni kupashana
habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano
mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara,
kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama
inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha.
Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa
umetumia lugha kwa mujibu wa mila na desturi za jamii inayohusika.
Mambo ya kuzingatia katika matumizi
ya lugha
- Mada inayozungumziwa: Mada za mazungumzo zipo nyingi. Kuna mada za kijamii,
kwa mafano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani, muziki n.k.
Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara,
faida n.k. Kwa hiyo, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji
wanatakiwa kuzingatia mada husika.
- Muktadha wa mazungumzo: Mazungumzo yanaweza kuathiriwa na miktadha tofauti. Kwa
mfano kuna miktadha ya kidini, kiganga, huzuni, sherehe, kisiasa, kielimu,
kibiashara n.k. Mazungumzo yanaweza kufanyika mjini, kijijini, ugenini,
shuleni, dukani, hotelini n.k
- Malengo ya mazungumzo hayo: Malengo ya mazungumzo nayo yanaathiri matumizi ya
lugha. Kwa mfano, lengo linaweza kutoa taarifa, kuhoji, kukejeli, kutia
moyo n.k. Sasa jinsi lugha itakavyotumika katika kutoa taarifa ni tofauti
na itakavyotumika katika kutia moyo au kukejeli.
- Uhusiano uliopo baina ya wazungumzaji: Matumizi ya lugha huweza kuathiriwa pia na mahusiano ya
wazungumzaji. Kuna mazungumzo baina ya watoto, wanafunzi, wazee, viongozi,
marafiki n.k. Upo uhusiano wa daktari na mgonjwa, mwalimu na mwanafunzi,
mnunuzi na muuzaji. Kwa hiyo mazingira baina ya pande hizi mbili
yatategemea uhusiano wao, kwa hiyo kaida za uhusiano huu utapaswa kuzingatiwa.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia mambo haya manne, itawafanya wazungumzaji wawe
makini katika uteuzi wa maneno, miundo, mifano na kina cha ufafanuzi wa
maelezo au habari inayozungumzwa.
Dhima
ya Lugha ya Kimazungumzo na ya Kimaandishi
Lugha ya kimazungumzo na ya
kimaandishi zina dhima kuu ya kupasha habari, ujuzi, na maarifa mbalimbali,
husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu, kufikisha ujumbe unaotakiwa
vizuri bila kupotosha, kufundishia ujuzi, kuchochea maendeleo, kuhifadhi historia
ya jamii na kueleza mawazo au hisia za watu.
Lugha ya Kimazungumzo na ya
Kimaandishi katika Miktadha Sahihi
Tumia lugha ya kimazungumzo na ya
kimaandishi katika miktadha sahihi
Matumizi ya lugha ya kimazungumzo na
ya kimaandishi katika muktadha sahihi huongozwa na mambo yafuatayo, ambayo ni
mada inayozungumzwa, muktadha au mahali mazungumzo hayo yanapofanyika, malengo
ya mazungumzo hayo na uhusiano uliopo kati ya wazungumzaji.
Zoezi 1.
Tumia lugha ya kimazungumzo na ya
kimaandishi katika miktadha sahihi.
Matamshi na Lafudhi ya Kiswahili
Matamshi ni namna ambavyo mtu
anatamka neno au jinsi mtu anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi
mazuri ya Kiswahili utakuwa unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza
kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu
mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu,
kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu
aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane
katika matamshi.
Lafudhi Mbalimbali za Kiswahili
Dhana ya matamshi huhusisha
- Sauti za lugha husika
- Mkazo
- Kiimbo
Sauti za lugha ya Kiswahili
Sauti za lugha ya Kiswahili
hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano
na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti
za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue”
wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza
kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo unapotamka maneno ya
Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha ya Kiswahili. Kuna watu
huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au “ucjal” huwa unaitamkaje?
Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal” itatamkwa “uchijal” sijui
itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa ukitumia maandishi ya namna hii
hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa
umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi, utajifunza kuyatumia kwa usahihi
katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
Mkazo
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna
ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara”
litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale
silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo
hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa
mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale
yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni
(mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).
Baadhi ya maneno yenye asili ya
kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara (sawa
sawa), Alha’misi
Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na
ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana
ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu ( yaani , kiwango
cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu
hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina
maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya
kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au
kuwa chini.
Aina za viimbo
- Kiimbo cha maelezo: Kiimbo
cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye
kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa
takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
- Kiimbo cha maulizo: Kiimbo
cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana
na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
- Kiimbo cha amri: kiimbo
cha amri hakitofautiyani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri,
mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha
maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi
ya Kiswahili
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa
lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo
yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu,
tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili
kwa watumiaji wengi wa afrika mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua
wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa
mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa mwanza kwa lafudhi yao,
watu wa mtwara kwa lafudhi yao, watu wa pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma
kwa lafudhi yao.
Mfano 3.
Mifano
- Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa
(Wakuria)
- Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mfaranga makumi
mawili (Wakongo)
- Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
- Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
- Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi
lakini wewe bado unaningangania tu! (Wahaya)
Utata katika Mawasiliano
Utata ni hali ya neno au sentensi
kuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo tungo tata ni tungo ambayo inaweza kuwa
na maana zaidi ya moja.
Sababu za Utata
Utata katika tungo hutokea kwa
sababu zifuatazo:
- Neno kuwa na maana zaidi ya moja, kwa mfano neno mbuzi,
kata n.k.
- Kutozingatia taratibu za uandishi, Mfano; Tulimkuta
Nyammy na rafiki yake, Mazala vs Tulimkuta Nyammy na rafiki
yake Mazala. Katika sentensi hizi alama (,) ndio huleta tofauti,
sentensi ya kwanza inamaana kulikuwa na watu wawili Nyammy na rafiki yake
aitwaye Mazala na sentensi ya pili isiyo na alama (,) inamaanisha kulikuwa
na watu wawili Nyammy na mtu mwingine ambaye ni rafiki yake Mazala
- Kutumia maneno bila kuzingatia muktadha wa matumizi ya
maneno hayo.
- Utamkaji wa maneno. Wakati mwingine utata unaweza
kujitokeza katika matamshi tu, ili hali katika maandishi utata hauonekani.
Kwa mfano; Mimina wewe, katika maandishi linaweza kuandikwa mimi na wewe,
na hivyo kuondoa utata.
- Mjengo wa maneno. Utata huu huzuka katika vitenzi kama pigia.
Chanzo cha utata katika kitenzi hiki ni kiambishi –i-.
Kiambishi hiki kinaweza kumaanisha: kwa ajili ya…, kwa sababu ya.., kwa
kutumia chombo fulani.., au mahali fulani.
Mfano 4
Mfano:
- Alimpigia ukorofi wake (kwa sababu ya)
- Alimpigia kiatu (kifaa)
- Alimpigia ndani (mahali)
Mfano 5
Mifano ya utata katika tungo
- Patience amemwandikia Lilian barua: Sentensi hii huweza kuwa na maana kuwa Patience
ameandika barua kwenda kwa Lilian au Patience ameandika barua kwa niaba ya
Lilian
- Umefanikiwa kununua mbuzi? Sentensi hii huweza kumaanisha ununuzi wa mbuzi mnyama
au mbuzi kifaa cha kukunia nazi.
- Alimkuta amelala kwenye nyumba ya wageni: Sentensi hii huweza kumaanisha, nyumba ya mtu lakini
inatumika kwa ajili ya wageni kwa malipo au ni nyumba inayomilikiwa na
watu ambao ni wageni katika eneo lile.
- Attu ametumwa na Aritamba: Sentensi hii inaweza kueleweka kumaanisha, Aritamba
amemtuma Attu au Attu na Aritamba wametumwa wote kwa pamoja
No comments:
Post a Comment