MADA YA TATU: UHAKIKI WA KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi kama zilivyo kazi
nyingine za fasihi andishi hufanyiwa uhakiki. Uhakiki huu huzingatia vipengele
vya fani na maudhui ili kubainisha usanaa wa kazi husika pamoja na kile
ilichokusudia kufikishwa kwa hadhira.
Uhakiki wa Ushairi
Mashairi kama kazi nyingine za
kifasihi huhakikiwa kwa kutumia vigezo sawa na vinavyotumika katika kazi
nyingine za kifasihi. Vigezo hivyo ni kwa kuzingatia vipengele vyake viwili
yaani fani na maudhui.
Vipengele
vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Ushairi
Elezea vipengele vya fani na maudhui
katika kuhakiki ushairi
Vipengele vya fani
Uhakiki wa fani za ushairi ni
uchambuzi wa kina na kuziweka wazi mbinu za kisanaa alizotumia mshairi katika
kutunga kazi yake. Vipengele muhimu vya kuhakiki katika fani ya ushairi ni kama
vifuatavyo:
Mtindo
Jambo la kuonyesha hapa ni kwamba
iwapo shairi ni la kimapokeo ama ni la kisasa.
Muundo
Katika kuhakiki muundo wa shairi
mhakiki inatakiwa aweke wazi mambo yafutayo:
- Idadi ya beti
- Idadi ya mistari na aina ya vibwagizo
- Idadi ya vipande
- Idadi ya mizani
- Aina na mpangilio wa vina
Wahusika
Ikiwa shairi limehusisha wahusika ni
vema pia mhakiki awabainishe
Matumizi ya lugha
Katika kipengele hiki mhakiki
huchunguza:
- Mpangilio wa maneno. Mf. Wengi wari badala ya wari
wengi
- Matumizi ya : Mazida – kurefusha neno mfano,
kiwembe badala ya wembe; Ikisari – kufupisha neno mfano siombe
badala ya usiombe; Tabdila – kubadilisha mwendelezo wa neno mfano
kujitanuwa badala ya kujitanua.
- Matumizi ya methali, misemo na nahau
- Matumizi ya lugha ya picha
- Matumizi ya tamathali za semi kama vile takriri,
sitiari n.k
- Mbinu nyingine za kisanaa
Mhakiki anapochunguza vipengele vya
fani, jambo muhimu la kuzingatia ni jinsi vipengele hivyo vinavyosaidia
kuwasilisha maudhui.
Vipengele vya maudhui
Ili kuhakiki na kupata maudhui ya
shairi inatakiwa kulisoma shairi kwa kulielewa zaidi. Baada ya kupata picha
fulani kuhusu shairi na kutafakari maana za maneno muhimu, itatubidi tuelewe
vipengele vya maudhui, ambavyo ni dhamira, mtazamo, msimamo, falsafa ya
mwandishi, ujumbe na maadili, migogoro na muktadha.
Uhakiki wa Maigizo
Igizo huhakikiwa kwa namna lilivyo
katika maumbo yake yote mawili yaani fani na maudhui.
Vipengele vya Fani na Maudhui katika
Kuhakiki Maigizo
Elezea vipengele vya fani na maudhui
katika kuhakiki maigizo
Fani
Uhakiki wa fani katika maigizo
unajihusisha na ufundi uliotumiwa. Ufundi huu unajumuisha mambo kadhaa kama
ifuatavyo:
Mtindo
Mtindo ni sura ya maigizo
inayojitokeza kupitia mpangilio wa maneno na vitendo. Inabidi mhakiki achunguze
kama kazi ni:
- Mchezo wa jukwaani – wenye mpangilio wa mazungumzo
baina ya watu na matendo yao.
- Majigambo
- Vichekesho – mpangilio wa maneno yanayowasilisha ujumbe
kwa kuchekesha.
- Mazungumzo – maongezi ya kujibizana baina ya watu.
- Ngonjera – mpangilio wa tungo za kishairi ambapo watu
wawili au makundi mawili hukinzana.
- Miviga – sherehe za kitamaduni kama vile matambiko
Pamoja na haya, mtindo hutegemea
lengo la maigizo ambalo laweza kuwa kuelimisha, kukejeli, kuburudisha, kuonya,
kukosoa na kadhalika.
Mandhari
Mazingira ya kutendea ni kipengele
muhimu cha fani. Mhakiki hana budi kujiuliza iwapo utendaji unadhihirisha
wakati au mahali halisi. Jambo hili huweza kutekelezwa kupitia vifaa, maleba,
maneno n.k.
Wahusika
Maswali ya mhakiki kuuliza ni:
- Wamejitokeza kikamilifu?
- Wanaaminika?
Matumizi ya lugha
Vigezo anavyotumia mhakiki
kuchunguza lugha ni:
- Kama usemaji ni wa kisanaa, yaani unatumia picha,
tamathali za semi, methali, nahau n.k.
- Kama lugha imetumika vile inavyotumiwa katika jamii.
Mfano: kiimbo, mkazo, miguno, vihisishi n.k.
- Matumizi ya maneno ya ajabu kama yale yanayotumiwa na
waganga.
Maleba na vifaa
Hivi huakisi mandhari na husaidia
kuzua mukatadha. Kwa hiyo ni muhimu kuchunguza kama vimetumiwa ipasavyo.
Matumizi ya ala
Matumizi ya ala kama ngoma,
baragumu, au sauti zingine ili kuamsha hisia za hadhira ni jambo muhimu
kuchunguza.
Mbinu nyingine
Mhakiki anapaswa pia kuchunguza
matumizi ya nyimbo, uchezaji ngoma, usimulizi na mbinu nyingine katika kuibua
hisia za watazamaji.
Maudhui
Kwa upande wa maudhui, mhakiki wa
maudhui hutakiwa kuchunguza vipengele vyote vya kimaudhui ambavyo ni dhamira,
migogoro, maadili, mtazamo na msimamo wa fanani pamoja na ujumbe bila kusahau
kipengele cha falsafa. Yote hayo kwa pamoja ndiyo humsaidia mhakiki kubaini
ukinzani wa igizo na maisha halisi ya jamii ambayo huwa ndiyo hadhira ya igizo
hilo.
No comments:
Post a Comment