KIDATO:
CHA KWANZA
MADA YA KWANZA: MAWASILIANO
Katika mada hii unatarajiwa kuelewa
fasili ya mawasiliano na jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika. Utaelewa
dhana ya lugha na vipengele muhimu vinavyokamilisha fasili ya lugha. Utaelewa
dhima kuu za lugha, matumizi na umuhimu wake. Vilevile katika mada hii
utajifunza juu ya lafudhi na matamshi mbalimbali ya watumiaji wa lugha ya
Kiswahili.
Lugha kama Chombo cha Mawasiliano
Mawasiliano ni mchakato wa
kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa mawazo, hisia, malengo,
tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo, ishara na maandishi. Ni
ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo
zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake. Sasa hapa sisi tutajikita katika
mawasiliano yanayofanywa baina ya viumbe wanaotumia lugha (ambao kimsingi ni
binadamu).
Maana
ya Mawasiliano
Lugha ni nyenzo muhimu sana katika
mawasiliano ya binadamu. Ulishawahi kujiuliza kwamba mwasiliano yangekuwaje
pasipokuwepo lugha? Mwalimu angekua anatumia mtindo gani kukufundisha darasani
au wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako? (Unasema ungewasiliana kama wanavyowsiliana
watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao pia wanawasiliana hivyo kwa sababu wana
maarifa ya lugha.
Mafumbuzi ya kisayansi na
teknolojia, yote haya yasingewezekana pasipo kutumia lugha, usingeweza kusogoa
(kuchat) na marafiki zako kwenye facebook, usingeweza kumwandikia ujumbe rafiki
yako kupitia simu yako na kadhalika.
Umeona sasa jinsi lugha ilivyo
muhimu katika mwasiliano? Kabla hatujaona umuhimu huu hebu tuangalie
fasili/maana ya lugha.
Kuna mitazamo mbalimbali juu ya
fasili ya lugha lakini kwa ujumla lugha inaweza kufasiliwa kama mfumo wa
sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano
yao ya kila siku ili kuelezea hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.
Kulingana na fasili hii tunaweza
kubainisha maneno ya msingi yanayojitokeza katika fasili ya lugha, maneno hayo
ni pamoja na haya yafuatayo:
Lugha
ni mfumo
Kila lugha ya mwanadamu imeundwa
katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa
sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana
kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya.
Mfano; k+u+k+u – kuku
Mtoto + anatembea – mtoto anatembea
Katika muunganiko huu wa maneno na
miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila
kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu,
mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi. Kwa maana hiyo, lugha ya
mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa
basi kunakuwa hakuna utimilifu wa lugha husika. Sheria hizi zinazotawala
mpangilio wa viunzi vya lugha hiyo ndizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha
fulani kuelewana.
Lugha
ni mfumo wa sauti nasibu
Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba,
hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (kwa mfano jiwe) na kitu chenyewe
tunachotumia katika ujenzi na matumizi mengine (maana na kirejelewa). Hii ina
maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano
wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano neno “jiwe” hakuna watu waliokaa na
kusema kuanzia leo hili litaitwa jiwe. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya
neno “jiwe” na umbo linalorejelewa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na
hutofautiana kutokana na lugha moja na nyingine. Jiwe mnaliitaje katika lugha
yenu? Basi huo ndio unasibu wa lugha.
Lugha
ni maalumu kwa mwanadamu
Lugha ni chombo cha mawasiliano
ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si
binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa
fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule
isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana,
mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa
yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu
ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake na
kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano, ukimchukua paka wa china na kumleta
Tanzania atatoa sauti ile ile sawa na paka wa Tanzania kwa kueleza shida ile
ile au kutoa ishara ile ile.
Lugha
ni mfumo wa ishara
Uishara wa lugha unamaanisha kuwa
maneno huambatanishwa/huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa
makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni
ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo
basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na
kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa.
Lugha
hutumia sauti
Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti
ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu
ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia
lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba:
- Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na
kuandika.
- Mtoto hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri
kadiri anavyokuwa
- Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
- Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
- Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko
kuandika
Kuna mambo mengi ya muhimu katika
sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo
hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni muhimu katika mawasiliano
lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi
Lugha
ni kwa ajili ya mawasiliano
Kwa kutumia lugha binadamu anaweza
kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha
hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi
n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya
mawasiliano.
Mfumo wa Lugha
Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha
kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au
vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi
hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama
haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.
Dhima za Lugha katika Mawasiliano
Fafanua dhima za lugha katika
mawasiliano
Baadhi ya dhima za lugha ni pamoja
na hizi zifuatazo:
- Ujumi: ujumi
ni hali ya kutumia maneno ya lugha fulani kwa ufundi na ustadi wa hali ya
juu kwa lengo la kuburudisha na kuwavutia watu wengine. Baadhi ya watu
hutumia lugha kwa dhima hiyo, ili maksudi wasomaji au wasikilizaji wao
wavutike na kuburudishwa na Lugha hiyo. Maeneo yatumikamo lugha yenye ujumi
wa kiwango cha juu ni kwenye matangazo na kwenye fani ya utunzi wa
mashairi.
- Utambuzi: Ni
hali ya kufikiria kwa makini, kukokotoa na kutoa majibu ya maswali tofauti
ndani ya ubongo. Chombo kikuu kitumikacho kutoa majibu hayo ni lugha.
Kutokana na muktadha huo tunaweza kusema kwamba lugha hutumika kama chombo
cha utambuzi.
- Hisia: ni
fikra za ndani alizokuwa nazo kiumbe mwanaadamu. Tunapotaka kuonyesha hisia
zetu na vilevile kuwavuta wengine kwa maneno mazito yanayoweza
kumtoa msikilizaji machozi ya huzuni au ya furaha tunachagua maneno makali
yenye hisia.
- Kujielezea: Hali
ya mtu kudhihirisha mambo mbalimbali aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake.
Kwa mfano mtu anaposema nina furaha sana. Hapa mtu anatowa msisitizo wa
kuonyesha kiwango cha furaha alichonacho, hili linafanyika kwa kutumia
lugha. kwa ufupi tunachoweza kusema hapa ni kwamba lugha hutumika kwa
ajili ya kujielezea.
- Kuamuru: Ni
kutoa maelekezo kwa njia ya kuamrisha. Kwa mfano hakimu anamuhukumu
mshitakiwa kwa kumuamuru ‘Ninakufunga miaka mitatu jela’. Hapa
lugha inatenda kazi ya kuamuru.
- Kushirikiana: ni
hali ya kutenda kitu kwa pamoja au hali ya kuwa na ubiya kwenye jambo. Lugha
huwezesha watu kujenga mahusiano ya siri baina ya watu wawili au zaidi na
kuweza kujitengenezea njia zao za kuwasiliana pasipo wengine kuelewa.
- Kuonesha: kumuelekeza
mtu kitu kwa njia ya kuashiria. Unapotaka kuonesha jambo ni
lazima utumiye lugha kwa njia moja au nyengine.
Matumizi
na Umuhimu wa Lugha
Lugha hutumika kama chombo, zana,
kifaa au njia ya kufikia lengo fulani. Baadhi ya matumizi ya lugha ni pamoja na
haya yafuatayo:
- Kuwasiliana:- Lugha
hutumika kupashana habari
- Kuunganisha- Lugha
hupatanisha na kuleta uelewano miongoni mwa wanajamii. pia lugha huweza
kutofautisha jamii moja na nyengine.
- Kujenga jamii- lugha
huleta/huhimiza shughuli za maendeleo ya jamii, huleta amani na mshikamano
katika jamii.
- Kufundishia- Lugha
hutumika katika kufundishia elimu.
- Kutambulisha- Lugha
hutumika kutambulisha jamii ya watu fulani.
- Kuhifadhi- Lugha
ndicho chombo cha kuhifadhi na kueneza utamaduni
Matamshi na Lafudhi ya Kiswahili
Matamshi ni namna ambavyo mtu anatamka neno au jinsi mtu
anavyozungumza lugha. Unaposema fulani ana matamshi mazuri ya Kiswahili utakuwa
unamaanisha anazungumza Kiswahili fasaha.
Neno moja linaweza
kuzungumzwa/kutamkwa kwa namna tofauti na watu mbalimbali kutokana na sababu
mbali mbali, sababu hizo ni pamoja na eneo la kijiografia anakotoka huyo mtu,
kabila lake, kundi lake la kijamii mfano msanii au mwanasiasa, na elimu
aliyonayo. Hizi zote zinaweza zikawa ni sababu za kufanya watu watofautiane
katika matamshi.
Dhana ya matamshi huhusisha:
- Sauti za lugha husika
- Mkazo
- Kiimbo.
Sauti
za Lugha ya Kiswahili
Sauti za lugha ya Kiswahili
hujumuisha irabu na konsonanti, ambazo kwa ujumla huunda sauti 24, irabu tano
na konsonanti 19 (konsonanti x na q hazipo katika matamshi ya kiswahili). Sauti
za Kiswahili hutamkwa kama zilivyoandikwa, kwa mfano maneno “data” au “dengue”
wewe unayatamkaje? Wengi huyatamka kama yalivyo hata kama wakiwa wanazungumza
kiingereza, hii ni kwa sababu maneno ya Kiswahili hutamkwa kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo unapotamka maneno ya
Kiswahili ni sharti uzingatie sauti asilia za lugha ya Kiswahili. Kuna watu
huwa wanaandika hivi “xaxa”, hii huwa unaitamkaje? Au “ucjal” huwa unaitamkaje?
Kwa kufuata matamshi asilia ya Kiswahili “ucjal” itatamkwa “uchijal” sijui
itakuwa ina maana gani sasa. Na pengine umekuwa ukitumia maandishi ya namna hii
hata kwenye insha zako ukidhani upo sahihi au ni kwa mazoea tu, sasa kwa kuwa
umejua matamshi sahihi ya Kiswahili ni yapi, utajifunza kuyatumia kwa usahihi
katika maandishi rasmi na yasiyo rasmi.
Mkazo
Katika lugha ya Kiswahili kuna namna
ya kutamka maneno ili kuleta maana mbali mbali, kwa mfano neno “barabara”
litaleta maana husika kulingana na jinsi lilivyotamkwa. Hivyo, mkazo ni pale
silabi inapotamkwa kwa kukazwa. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo
hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa
mkazo, sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale
yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ba’bu, maya’i, rama’ni
(mimi nilikuwa nikitamka ra’mani), baraba'ra (njia).Baadhi ya maneno yenye
asili ya kigeni, huwa na mkazo katika silabi nyingine. Kwa mfano: bara'bara
(sawa sawa), Alha’misi
Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na
ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji, dhana
ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu ( yaani , kiwango
cha juu, cha chini au cha kati cha sauti katika usemaj), Kwa hivyo ni muhimu
hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina
maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya
kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au
kuwa chini.
Aina za viimbo
- Kiimbo cha maelezo: Kiimbo
cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye
kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa
takriban katika mstari ulionyooka. Mfano, Mwalimu anafundisha.
- Kiimbo cha maulizo: Kiimbo
cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana
na aina ya swali linaloulizwa. Mfano, mwalimu anafundisha?
- Kiimbo cha amri: kiimbo
cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo. Kiimbo cha amri,
mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha
maelezo. Mfano, njoo hapa!
Lafudhi
ya Kiswahili
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa
lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira. Mazingira hayo
yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, kiwango chake cha elimu,
tabaka lake la kijamii na kadhalika.
Lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili
kwa watumiaji wengi wa Afrika Mashariki, kwa hiyo hii inafanya kuwatambua
wazungumzaji wa Kiswahili kulingana na makabila yao au maeneo wanakotoka. Kwa
mfano, kwa hapa Tanzania tunaweza kuwatambua watu wa Mwanza kwa lafu dhi yao,
watu wa Mtwara kwa lafudhi yao, watu wa Pemba kwa lafudhi yao au watu wa Musoma
kwa lafudhi yao. Mifano:
- Usiniretee maswara ya ubaguzi wa kikabira hapa (Wakuria)
- Amemupiga mutoto ya watu juu amemuibia mafaranga makumi
mawili (Wakongo)
- Ukikaa nchale, ukichimama nchale (Wamakonde)
- Wewe unakamuaga mang’ombe tu moja kwa moja (Wasukuma)
- Mbona unakuwa kinganganizi, nilishakwambia sikupendi
lakini wewe bado unaningangania tu! (Wahaya)
MADA YA PILI:
AINA ZA MANENO
Katika lugha ya Kiswahili kuna
angalau aina nane za maneno ambazo wataalamu wengi wa lugha wanakubaliana
hivyo. Katika mada hii utaweza kujifunza na kubainisha aina zote nane za maneno
na jinsi zinvyotumika katika sentensi. Utaweza pia kujifunza namna ya
kutofautisha aina za maneno ambazo zimeleta ubishi miongoni mwa wataalamu wengi
hususani katika Viunganishi na Vihusishi.
Ubainishaji wa aina Saba za Maneno
Aina Saba za Maneno ya Kiswahili
Bainisha aina saba za maneno ya
Kiswahili
Aina za maneno katika lugha ya
Kiswahili ni pamoja na hizi zifuatazo:
- Nomino (N)
- Viwakilishi (W)
- Vitenzi (T)
- Vivumishi (V)
- Vielezi (E)
- Viunganishi (U)
- Vihusishi (H)
- Vihisishi (I)
Ufafanuzi wa aina za Maneno
Nomino (N)
Nomino ni maneno yanayotaja vitu,
watu, na hali kadhalika. Kuna aina mbali mbali za maneno ambazo ni pamoja na
hizi zifuatazo:
- Nomino za pekee:Nomino
za pekee hutaja na kutambulisha nomino mahsusi na za kipekee. Yaani kuwa
kitu ni hicho na wala si kingine chochote. Hizi ni nomino zinazohusisha
majina kama vile ya watu, nchi, miji, mito, milima, maziwa na bahari.
Herufi za kwanza za nomino za pekee huwa kubwa hata kama nomino hizi
zinapatikana katikati ya sentensi.
- Nomino za kawaida:Hizi
kwa jina jingine huitwa nomino za jumla. Nomino hizi hazibainishi wazi
wazi vitu ambavyo habari zake zinatolewa. Kwa mfano ikiwa ni mtu, mahsusi
hatambuliwi. Haituambii kama ni Bahati, Bite ama Neema. Ikiwa ni mlima
hautambuliwi kama ni Meru , Kilimanjaro au Evarest, yaani hutaja vitu bila
kutaja umahususi wake kama ilivyo katika nomino za pekee.Hizi
zinapoandikwa si lazima zianze na kwa herufi kubwa ispokuwa zimetumiwa mwanzoni
mwa sentensi au zimetumika kama anuani ya kutajia kitu kama vile Mkuu wa
Sheria. Katika mfano huu ‘sheria’ kwa kawaida ni nomino ya kawaida, lakini
hapa inaanza kwa herufi kubwa kwani inataja anuwani ya kipekee.
- Nomino za mguso:Nomino
za mguso hurejelea vitu vinavyoweza kuhusika na mwanadamu kupitia milango
ya hisia kama macho, mapua, masikio vidole na ulimi- yaani vitu
vinavyoweza kushikika, kuonekana, kunusika na kuonjeka.
- Nomino za jamii:Hizi
ni nomino ambazo zinawakilisha vitu vingi katika jina moja, yaani nimino
zinazotaja umla ya vitu vingi. Mfano; jozi ya viatu, umati wa watu,
bustani ya maua, bunga ya wanyama
- Nomiono dhahania:Kundi
hili la nomino hutumia kigezo cha uwezekano wa kuhesabika kuziainisha.
Hapa tunatofautisha kati ya nomino zinazowakilisha vitu vinavyohesabika
kwa upande mmoja, na vile visivyohesabika kwa upande mwengine. Nomino ya
vitu vinavyohesabikavitanda, nyumba,vikombe vitabu na kadhalika.Zile
zisizohesabika hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haviwezi
kugawika, kwa mfano maji, mate, makamasi, maziwa, moshi, mafuta. Aghalabu
nomino hizo huwa sawa katika umoja na wingi.
- Nomino za kitenzi jina:Hizi ni nomino zinazohusu vitenzi. Huundwa kwa
kuongezwa kiambishi {ku-} cha unominishaji kwenye mzizi wa kitenzi cha
kitendo halisi ili kukifanya kiwe nomino.
Vivumishi (V)
Vivimishi ni maneno yanayoelezea
zaidi juu ya nomino, aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino. Kuna aina kadhaa
za vivumushi, miongoni mwa hivyo ni pamoja na hivi vifuatavyo.
- Vivumishi:
vinaweza kujitokeza katika aina tatu ndogondogo.
- Vivumishi vya sifa: hutoa
sifa za nomino /kiwakilishi cha nomino. Sifa hizi huweza kuwa nzuri, mbaya
au yoyote ile.
- Vivumishi vya idadi; vivumishi
vya aina hii hutoa taarifa kuhusu idadi ya nomino. Kuna vivumishi vya
idadi vinavyoweza kuvumisha nomino kwa kutaja idadi ya nomino hizo
kiujumla jumla bila kudhihirisha idadi halisi.
- Vivumishi vya idadiambavyo
huonyesha nafasi iliyochukuliwa na nomino fulani katika orodha.
- Vivumishi vya kumiliki:-Ni vivumishi vinavyoonesha kuwa kitu fulani kina
milikiwa na mtu au kitu kingine.
- Vivumishi Vioneshi:vivumishi vya aina hii huonyesha mahali au upande kitu
kilipo. Vivumishi vya aina hii hujengwa na mzizi{h}kwa vitu
vilivyopo karibu na mzizi{le}kwa vitu vilivyo mbali.
- Vivumishi vya kuuliza:Hivi ni vivumishi ambavyo hufafanua nomino kwa kuuliza
habari zake. Hujibu swali “gani?ipi? ngapi?”
- Vivumishi vya A- unganifu:Vivumishi vya aina hii huundwa kwa mzizi wa kihusishi
a- unganifu. Kihusishi hiki huandamana na nomino kuunda kirai husishi
ambacho huvumisha nomino iliyotajwa awali.Vivumishivya aina hii
hutumika kuleta dhana za–Umilikaji, -Nafasi katika orodha.
- Vivumishi vya jina kwa jina:Hizi ni nomino zinazotumika kama vivumishi ambazo
hutumika kufafanua nomino
- Vivumishi vya pekee:Vivumishi
hivi huitwa vya pekee kwa sababu kila kimojawapo huwa na maana maalumu.
Pia kila kimojawapo huchukua upatanisho wake wa kisarufi kulingana na
ngeli ya nomino ambayo kinaivumisha.
Mizizi vivumishi hivi niote,
o-ote, -enye, -enyewe, -ingine, -ingineo.
- -ote:Huonyesha
ujumla wa kitu au vitu
- -o-ote:Kivumishi
cha aina hii kina maana ya “kila”, “bila kubagua”
- – enye:Kivumishi
cha aina hii hutumika kuleta dhanna ya umilikishaji nomino fulani.
- -enyewe:Kivumishi cha aina hii hutumika
kuisisitiza nomino fulani.
- – ingine:Kivumishi
cha aina hii huonyesha/huonesha ‘tofauti na’ au ‘zaidi ya’ kitu fulani
- – ingineo:Kivumishi
cha aina hii hutumika kuonesha/kuonyesha ziadi.
Vielezi (E)
Vielezi ni maneno yanayofafanua
vitenzi, vivumishi au vielezi vingine. Huweza kuarifu kitendo kilichotendeka
kilitendeka wapi, namna gani na hata mara ngapi.
Aina za vielezi
Vielezi vya Mahali
Vielezi vya mahali hutoa habari
kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa
kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno
linaloashiria mahali.Kwa mfano:nyumbani, kazini, shuleni
Example 1
- Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
- Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo
kinapofanyika; kwa mfano: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi.
Example 2
- Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
- Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
- Kisaka na Musa watakutana kesho
Vielezi vya Idadi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo
kilifanyika mara ngapi.
Idadi Kamili:Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi
kitendo kilifanyika. Kwa mfano:mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
Example 3
- Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia
- Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa
siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
Idadi Isiyodhihirika:Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho
kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili kwa mfano:chache, nyingi,
kadhaa, kidogo, wastani.
Example 4
- Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa
na polisi.
- Yeye hunipigia simu mara kwa mara.
Vielezi vya namna au jinsi
Vielezivya namna hii huonyesha jinsi
au namna kitendo kilivyotendeka. Vielezi vya namna vipo vya aina kadhaa.
Vielezi vya namna halisi
Hivi ni vielezi vinavyotumia maneno
ambayo kimsingi yana sura ya vielezi moja kwa moja katika uainishaji wa aina za
maneno.
Vielezi vya namna mfanano
Hivi ni vieleziambavyo hutumika
kufananisha vitendo na vivumishi au nomino mbalimbali. Hujengwa kwa kuongeza
kiambishi(ki-)au kiambishi(vi-).Viambishi hivi
hujulikana kwa jina la viambishi vya mfanano. Mfano; Ulifanyavizurikumsaidia
mwanangu.
Vielezi vya namna vikariri
Hivi ni vielezi ambavyo
hufafanua vitenzi kwa kurudiarudia neno moja mara mbili.
Vielezi vya namna hali
Hivi nivieleziambavyo
hufafanua juu ya kitendo kilichotendeka kimetendeka katika hali gani.
Vielezi vya namna ala/kitumizi
Hivi ni vielezi vinavyotaja
vitu ambavyo hutumika kutendea kitendo
Vielezi vya namna viigizi
Hivi vinaelezea zaidi jinsi tendo
lilivyofanyika kwa kuigiza au kufuatisha sauti inayojitokeza wakati tendo
linapofanyika au kutokea.
Vielezi vya wakati
Vielezivya namna hii huonyesha wakati wa kutendeka kwa
kitendo.Huweza kutokea kama maneno kamili au hodokezwa kwa kiambishi{po.}
Vitenzi
Kitenzi ni neno linaloeleza jambo
lililotendwa au lililotendeka. Kitenzi huarifu lililofanyika au lililofanywa na
kiumbe hai chochote kinachoweza kutenda jambo
Kitenzi cha Kiswahili huundwa na
mzizi pamoja na viambishi vyenye uamilifu wa aina tofauti
Aina za vitenzi
- Vitenzi vikuu:Vitenzi
vikuu ni vile ambavyo hubeba ujumbe muhimu wa kiarifu cha sentensi.
- Vitenzi visaidizi:Hivi
hutoa taarifa ya kusaidia vitenzi vikuu. Hutoa taarifa kama vile uwezekano
, wakati, hali n.k.Vitenzi visaidizi daima hutumika na vitenzi vikuu,
ndivyo vinavyobeba viambishi vya wakati.
- Vitenzi vishirikishi:
Hivi ni vitenzi vishirikishi ambavyo havichukui viambishi vya nafsi, njeo
ama hali. Vitenzi vishirikishi vipungufu ni vya aina mbili, ambavyo ni
kitenzi kishirikishi“ni” cha uyakinishina kitenzi shirikishi “si”
si cha ukanushi.
- Vitenzi vishirikishi vikamilifu:Hivi huchukuwa viambishi viwakilishi vya nafsi, njeo na
hata hali. Kwa mfano;ndiye, ndio, ndipo.
Kazi za kitenzi kikuu
- Kueleza tendo linalofanywa na mtenda/mtendwa.
- Kuonyesha wakati tendo linapotendeka
- Kuonyesha hali ya tendo
- Kuonyesha nafsi
- Kuonyesha kauli mbali mbali za tendo
- Kuonyesha urejeshi wa mtenda/mtendwa/ mtendewa/
kujitendea
Kazi za kitenzi kishirikishi
- Kushirikisha vipashio vingine katika sentensi
- Kuonyesha tabia fulani iliyopo au isiyokuwepo ya mtu
fulani au kitu fullani.
- Kuonyesha cheo au kazi anayofanya mtu.
- Kuonyesha sifa za mtu.
- Kuonyesha umoja wa vitu au watu
- Kuonyesha mahali
- Kuonyesha msisitizo
- Kuonyesha umilikishi wa kitu chochote.
Aina za wakati katika kitenzi
- Wakati uliopita
- Wakati uliopo
- Wakati ujao
Hali mbalimbali za kitenzi
- Hali ya masharti
- Hali ya kuendelea kwa tendo
- Hali ya kutarajia, kuamuru na kuhimiza
Viwakilishi
Viwakilishi ni aina ya neno
linaloweza kutumika badala ya jina/nomino .
Aina za viwakilishi
- Viwakilishi vioneshi au viwakilishi vya kuonesha:Viwakilishi vionyeshi hutumika badala ya nomino kwa
kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja. Kwa mfano; huyu,
yule, hapo, kule, humo. Huyu si mwenzetu kabisa; kule hakufai kwenda watoto.
- Viwakilishi vya nafsi: Kwa mfano:mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
- Viwakilishi vya kuuliza/viwakilishi viuliziambavyo huashiriwa na mofu /kiambishi{-pi}ambavyo
katika tungo hutanguliwa na kiambishi ngeli cha jina husika. Kwa mfano,
Wangapi wameondoka? Kipi kimekosewa?
- Wiwakilishi vya urejeshiambavyo vinajengwa na shinaambapamoja na
vipande vidogo vidogo –ye-, -o-, -cho-, vyo, lo, po, mo, kon.k
ambavyo vinachaguliwa kulingana na ngeli ya majina yanayorejeshwa navyo.
Mfano; aliyeondoko hatapewa chake.
- Viwakilishi vya idadi:Viwakilishi hivi hutuarifu kuhusu idadi ya nomino hiyo
huweza kuwa kamili (halisi) au ya jumla.
- Viwakilishi vya pekee/vimilikishi:-Hivi ni aina ya vivumishi vya pekee kuwakilisha nomino.
Hufuata sheria za upatanisho za nomino zinazowakilishwa. Mfano; '-angu,
-ako, -ake, -etu, -enu, -ao '. kwangu haingii megini, chako haikna
thamani.
- Viwakilishi vya A-unganifu:- Viwakilishi hivi huundwa kwa kihusishi chaA-unganifukusimamia
nomino iliyomilkiwa, inayochukuwa nafasi fulani katika orodha au nomino ya
aina fulani. Kihusishi a-unganifu huandamana na nomino kuunda kirai
husishi ambacho husimama mahali pa nomino. Mfano;ya kwakeyamemshinda,vya
wazeehaviguswi.
- Viwakilishi vya sifa:Haya
ni maneno ya sifa ambayo huchukua nafasi ya nomino katika setensi.
Kwa mfano -eupe, -janja, -tamu
- Viwakilishi vya Idadi;Idadi Kamili- hutumia namba kuelezea idadi ya nomino. 'saba, mmoja,
ishirini' -Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake. Idadi
Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili: 'chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani'
Viunganishi
Ni maneno, kikundi cha maneno au
kiambishi chenye kuunganisha maneno, kirai, kishazi au sentensi.Dhima ya
kiunganishi ni kuunga vipashio viwili au zaidi vyenye hadhi sawa kisarufi.
Aina za viunganishi
- Viunganishi huru:hivi
ni viunganishi vinavyosimama pekee katika tungo, katikati ya vipashio
vinavyoungwa.Viunganishi huru hujumuisha:
- Viunganishi nyongeza/vya kuongeza, kama vile, na, pia, pamoja. Baba na mwanae wanacheza
mpira, Alichukua chakula chote pamoja na akiba iliyokuwepo.
- Viunganishi vya sababu/visababishi, mfano, kwa sababu, kwa kuwa, kwa vile, madhali, ili.
Alimsogelea karibu ila ambusu, Atatumikia kifungo madhali amebainika kuwa
na hatia.
- Viunganishi vya uteuzi/chaguo. Mfano; au, Naweza kwenda nyumani au shuleni.
- Viunganishi vya kutofautisha/vya kinyume:ila, lakini, kinyume na, japokuwa, ingawa, ilihali.
Mfano; Mkumbatie lakini usimbusu.
- Viunganishi vya wakati.Wakati mfano; Mwalimu aliuliza swali wakati yeye
amesinzia.
- Viunganishi vya masharti;ikiwa, iwapo, hadi. Mfano; utaruhusiwa kuingia hapa
ikiwa umevaa mavazi yanaostahili.
- Viunganishi vihusishi;
miongoni mwa, kati ya; mfano: Jane alikuwa miongoni mwa washindi kumbi
bora kitaifa.
- Viunganishi tegemezi:ni
viambishi ambavyo hutiwa katika kitenzi cha kishazi tegemezi ili kukiunga
na kitenzi kikuu cha kishazi huru ambavyo kwa pamoja huunda sentensi
changamano au shurtia. Mfano; -po-, -cho-, -o- Nili-po-amka…,
Ali-cho-mwelez…, alizo-o-neshwa…n.k
Vihusishi
Ni maneno ambayo huonyesha uhusiano
uliopo baina ya neno moja na jingine. Vihusishi aghlabu huonyesha uhusiano kati
ya nomino au kirai nomino na maneno mengine.
Mambo yanayoweza kuonyeshwa na
vihusishi
- Huonyesha uhusiano wa kiwakati; Mfano, ni vizuri kupiga
mswakibaada yachakula.
- huonyesha uhusiano wa mahali: mfano, Ninaishikaribu
nakwa Mtogole
- huonyesha uhusiano wa kulinganisha: Amekulazaidi yauwezo
wake.
- huonyesha uhusiano wa umilikaji: Usiguse hicho kitabu
nicha kwangu
- huonyesha uhusiano wa sababu/kiini: nimerudi kwaajili
yakuonana na mkuu wa shule.
Aina za vihusishi
- vihusishi vya wakati
- vihusishi vya mahali
- vihusishi vya vya kulinganisha
- vihusishi vya sababu
- vihusishi vya ala/kifaa mfano; -kwa
- vihusishi vimilikishi
- vihusishi vya namna; Kichwacha mviringo
- vihusishi ‘na’ cha mtenda mfano, amepigwana Juma.
Matumizi ya kihusishi “kwa”
- huonyesha mahali au upande: Mfano, amekwenda kwa mjomba
wake.
- huonyesha sababu au kisababishi cha jambo: mfano;
ninaishi kwa ajili yako.
- huonyesha wakati: mfano; sina nafasi kwa sasa.
- huonyesha sehemu fulani ya kitu kikubwa, mfano: Mpira
umekwisha wakiwa wamefungana nne kwa tatu.
- huonyesha jinsi kitendo kilivyotendeka: Mfano; alimvuta
kwa nguvu sana ndo maana limevunjika.
Vihisishi/Viingizi
Ni maneno ambayo hutumiwa
kuwakilisha hisia fulani.
Vihusishi vinaweza kugawanywa katika
makundi yafuatayo:
Vihisishi vinavyoonyesha mhemko au
hisi kali
- vihisishi vya furaha
- vihisishi vya huzuni
- vihisishi vya mshituko
- vihisishi vya mshangao
Vihisishi vya maamrisho au msisitizo
wa jambo au tukio
- vihisishi vya maadili
- vihisishi vya mwiitiko
- vihisishi vya ombi
- vihisishi vya bezo
- vihisishi vya kutakia heri
- vihisishi vya kukiri afya/jambo
- vihisishi vya kiapo
- vihisishi vya salamu
Matumizi ya aina za Maneno katika Tungo
Matumizi ya Aina za Maneno katika
Tungo
Elezea matumizi ya aina za maneno
katika tungo
Aina za maneno hutumika katika tungo
kwa kutegemeana na lengo la msemaji. Kwa mfano kama lengo la msemaji ni
kuonesha aina fulani ya hisia atatumia vihisishi katika tungo yake. Vilevile
kama msemaji anahitaji kueleza kuhusu namna nomino inavyotenda, ilivyotendewa
au inavyotendwa, atatumia kitenzi.
No comments:
Post a Comment