MADA YA
TANO: UTUNGAJI WA KAZI ZA KIFASIHI
Kazi za fasihi simulizi hazikutokea
tu, zilitungwa. Mtu fulani alikaa na akatunga kazi fulani ambayo inajulikana
katika jamii. Katika mada hii utajifunza kanuni mbalimbli zinazohusika na
utunzi wa kazi za fasihi simulizi. Pia utapata fursa ya kujifunza jinsi ya
kutunga kazi mbalimbali za fasihi simulizi kama vile ngonjera, methali , nahau,
vitendawili na kazi nyingine. Utajifunza pia kanuni zinazoongoza utunzi wa kila
kazi ya fasihi simulizi.
Mashairi
Kanuni za Utungaji wa Mashairi
Fafanua kanuni za utungaji wa
mashairi
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi
atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo
ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
- Kuona:
je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la
kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni
makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?
- Kunusa:
pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je,
ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je,
ananuka mdomo?
- Kuhisi:
je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au
huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa
bega unajisikia nini?
- Kuonja:
je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina
pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi
au uchachu?
- Kusikia:
je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose
usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti
ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au
kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu. Mwandishi ana uzoefu (uzoevu)
wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana
nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha
yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu
waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama
yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na
mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya
udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu,
mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje,
analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali
muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu
anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira
yake.
Mwandishi baada ya kuzingatia mambo
haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika
utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua
dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata
maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika
mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho
mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao
huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo
nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa.
Mashairi yana umbo ambalo huonekana
kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili
hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu
shairi, nayo ni:
- Beti
– Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
- Vina
– Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni
mwa sentensi.
- Mizani
– Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
- Kituo
– Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha
bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika
kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho
maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni
mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama
ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila
mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele vya fani katika mashairi
Vipengele vya fani katika shairi ni
pamoja na:
- Jina / anwani
- Mandhari
- Wahusika
- Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia
n.k
- Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina,
kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti
unaofuatia.
Vipengele vya Maudhui kati mashairi
- Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe,
falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
- Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza,
kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza
kutunga shairi lako la kwanza.
Kuigiza Ngonjera
Igiza ngonjera
Katika kuigiza ngonjera muigizaji
hana budi kuzingatia fani yenye kanuni zifuatazo; mtindo wa mashairi ya
kimapokeo, muundo wa mashairi ya kimapokeo wenye mizani, vina, vipande,
mishororo na beti, kuteua mandhari kutegemeana na mada, kuwepo kwa wahusika
wawili au zaidi au makundi mawili au zaidi na matumizi ya lugha ya kishairi.
Maigizo
Kanuni za Utungaji wa Maigizo
Elezea kanuni za utungaji wa maigizo
Maigizo ni tendo la kuiga sura,
tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine yaani kuiga jinsi
walivyoumbwa, wanavyotembea, wanavyovaa, wanavyosema n.k
Kanuni na hatua za kutunga maigizo
- Kuchagua wazo, tendo, visa au tukio la kuigizwa:Ni lazima jambo hilo liwe na uzito, umuhimu au athari
fulani katika jamii. Matukio hubainika kutokana na utafiti. Matukio
yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile matumizi mabaya
ya simu za mkononi, mitindo ya mavazi, madhara ya uganga wa kienyeji,
madhara ya UKIMWI n.k.
- Kuchagua muktadha au mahali pa kutendeka kwa jambo:Muktadha waweza kuwa ofisini, shuleni, kijijini, mjini,
barabarani, kwenye daladala n.k
- Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa:Hapa mtunzi anaweza kutumia fumbo, vichekesho,
historia, tanzia n.k. Inashauriwa mtunzi kuchanganya mbinu ili kuongeza
mvuto.
- Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo:Maudhui hujikita katika migogoro au mivutano. Suluhisho
la mivutano hupatikana pale migogoro inapofikia kilele. Kwa mfano jamabazi
sugu anapokamatwa.
- Kuweka mpangilio wa maonyesho:Maonyesho hujumuisha vitendo na hoja zinazokamilisha
sehemu inayobeba aina moja au zaidi ya maudhui. Sehemu kadhaa nazo hukaa
zikajenga kitendo ambacho hubeba jambo mojawapo muhimu. Katika migawanyo
hii yapasa mtunzi atunge kauli na vitendo vinavyoandamana navyo.
- Kubuni wahusika na kuweka aina au idadi yao kulingana
na matukio:Mtunzi anashauriwa kutumia
wahusika wanaohitilafiana. Kwa mfano wazee, vijana, wanawake, wanaume,
wanene, wafupi n.k. Mtunzi akishawateua anaweza kuwatungia kauli na zamu
za matendo katika sehemu mbalimbali.
- Ni muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na
kuamua maleba yao:Uamuzi
huu yapasa ufanywe kwa kuzingatia mazingira. Kwa mfano siku hizi sio
lazima wahusika wazee kuvaa ngozi, kutumia mkongojo na kuvuta mtemba.
- Urefu wa maigizo ni suala la kuamliwa kutegemea tukio
- Kutunga maelezo kuhusu mandhari:Maumbile ya wahusika na vitendo vyao, ni muhimu
kuelezwa katika mabano.
- Kuandika maigizo na kuhariri:Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo inayovutia,
yenye kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleza maadili kwa mnato.
No comments:
Post a Comment