MADA YA
NNE: UHIFADHI WA KAZI YA FASIHI SIMULIZI
Ili kitu kidumu ni lazima
kihifadhiwe; fasihi simulizi kama sanaa kutokana na umuhimu wake katika jamii
nayo huhufadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Katika mada hii utaweza
kujifunza umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Utajifunza njia mbalimbali
zitumikazo katika uhifadhi wa fasihi simulizi pia utaweza kubainisha ubora na
udhaifu wa kila njia.
Njia za kuhifadhi Fasihi
Simulizi
Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Bainisha njia za kuhifadhi fasihi
simulizi
Umuhimu wa kazi za fasihi simulizi
Ingawa kila utanzu wa fasihi una
umuhimu wake, kwa pamoja tanzu zake zote zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Kwaza fasihi hutumika kama chombo
cha kuwaelimisha watu. Kupitia fasihi andishi na fasihi simulizi, watu hupata
maarifa ya kutambua mambo maovu na namna ya kuyakwepa. Licha ya haya, wanajamii
hujifunza njia za kujitawala, kuzalisha mali na kuishi kwa misingi ya haki,
usawa na demokrasia.
Pili, fasihi ni nyenzo ya kutoa
mafunzo kuhusu mambo kama vile historia, dini, siasa, jiografia na tiba. Kwa
hiyo watu hujifahamisha juu ya maumbile na asili yake, mazingira, utawala,
uchumi, sheria n.k.
Aidha fasihi huwapa watu mazoezi na
kuimarisha uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha, kuimba nyimbo kwa ufundi,
kuigiza mambo kwa ustadi, kucheza ngoma kwa umahiri, kughani mashairi kwa mvuto
na kusimulia matukio kwa mtindo ufaao.
Fasihi hufahamisha, huhifadhi na
hurithisha mambo kuhusu utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo
ni pamoja na mila, desturi, falsafa, imani na itikadi. Pia hudumisha maarifa ya
kijadi kama vile tiba, sayansi ya kilimo, uhifadhi wa mazingira na sayansi ya
utabiri wa hali ya hewa.
Umuhimu mwingine wa fasihi unatokana
na kutumika kwake kama chombo cha kuburudisha na kupumbaza. Watu wanaposoma
kazi mbalimbali za fasihi hupata, msisimko wa kimwili na kiakili. Kadhalika
fasihi hugusa hisia za watu na kuwafanya wafurahi au wahuzunike.
Istoshe fasihi hudumisha na kukuza
lugha. Watu hupanua msamiati wao na miundo ya lugha kupitia kazi zake. Hivyo
fasihi inakuwa kama hazina ya maneno na dafina ya kanuni za kisarufi.
Kutokana na umuhimu huu ndio maana
fasihi huhifadhiwa ili isipotee. Na uhifadhi huu hufanyika kwa njia
mabalimbali.
Ubora na Udhaifu wa kila Njia ya
Kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
Elezea ubora na udhaifu wa kila njia
ya kuhifadhi kazi za fasihi simulizi
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa
kwa njia zifuatazo:
Kichwani
Hii ndio njia ambayo imekuwa
ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo.
Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza
kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.
Ubora wake
- Uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati
wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.
- Hakuna gharama yoyote wakati wa uwasilishaji wa kazi ya
fashi. Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili waweze kuitoa
kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.
- Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai. Hii ni
kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na
matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti,
miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya
hadhira.
Udhaifu wake
- Uwezekano wa kazi kupotea au kuharibika hasa katika
fani ni mkubwa. Kwa mfano msanii anapokuwa amefariki dunia kazi anayokuwa
ameihifadhi kichwani nayo hupotea. Ndio maana katika baadhi ya jamii kazi
za kifasihi zimepotea. Hii ni kwa sababu wasanii wanapoondoka duniani
hondoka na fani hizo.
- Kazi inapohifadhiwa kichwani ni rahisi kubadilika. Hii
inatokea pale ambapo msanii anasahau baadhi ya maneno kutokana na umri
wake au sababu nyinginezo
Njia ya maandishi
Maandishi ni njia moja wapo
inayotumika kuhifadhia kazi za fasihi. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu
kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia
mbili kubwa. Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo; na hatua ya pili ni
kuliweka wazo hilo katika maandishi. Kazi za fasihi simulizi zinazoweza
kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo
n.k
Ubora wake
- Kazi iliyohifadhiwa inaweza kudumu kwa muda mrefu
- Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya
mbali na aliko msanii.
- Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake
na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii
atakapoamua kuibadilisha.
Udhaifu wake
- Hii njia ni kwa ajili ya watu wachache tu wanaojua
kusoma na kuandika.
- Wasanii wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua
kusoma na kuandika.
- Ni aghali sana kuhifadhi kazi za kifasihi kwa njia ya
maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika
maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza. Kwa hiyo ni aghali.
- Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa
ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya
msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
- Wahusika pia hawawezi kuonekana, endapo ni igizo mabalo
limehifadhiwa katika maandishi, hivyo ubora wa kazi ya msanii huchujuka.
Njia ya vinasasauti
Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo
vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea
kuliko ile ya maandishi.
Ubora wake
- Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali
na alipo mtunzi.
- Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au
CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa
vizuri.
- Sauti ya mtunzi unaiskia moja kwa moja
- Unaweza kusikia vionjo vya msanii
Udhaifu wake
- Njia hii ni aghali kutumia, kununua vinasasauti ni
gharama.
- Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya
msanii au wahusika lakini hahawezi kuonekana.
- Kazi yoyote ya kifasihi inapohifadhiwa katika
vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote
haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.
Njia ya kompyuta
Njia hii imeanza kutumika katika
miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua na mna ya kutumia kompyuta.
Ubora wake
- Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za
kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale
zinapokuwa zinahitajika.
Udhaifu
- Msanii au wasanii wanohusika hawawasiliani na hadhira
papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele
vinavyotatiza.
- Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni
sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta.
- Pia ni aghali sana, kuzingatia kwamba kununua komputa
ni gharama kubwa.
Njia ya kanda za video
Msanii huweza kutumia kanda ya video
kuhifadhi kazi yake.
Ubora wake
- Kwanza wasnii na vifaa wanavyotumia huonekana
- Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia
huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya
hadhira.
- Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video
iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.
Udhaifu wake
- Uhifadhi wa njia hii ni aghali, msanii atahitajika
kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
- Watu wanoweza kunufaika na njia hii ni wacheche mno na
wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi
hupatikana maeneo ya mijini.
- Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini
hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi
wanapohitaji kufanya hivyo.
Umuhimu wa kuhifadhi kazi
za Fasihi Simulizi
Faida ya Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Elezea faida ya kuhifadhi fasihi
simulizi
Njia zote za uhifadhi wa kazi za
fasihi simulizi zina umuhimu mkubwa katika ukuzaji na uendelezaji wa utamaduni
katika jamii. Kama ambavyo tumekwishaona, kazi za fasihi simulizi huelimisha,
huburudisha, hurithisha maarifa, maadili, pia ni vielelezo vya utamaduni wetu
wa asiili. Kwa ajili hiyo ni muhimu kuzihifadhi kazi hizo zisiharibike wala
kupotea ili ziendelee kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ni muhimu ziendelee kuwepo ili
kuhifadhi utamaduni wetu na huku vikitumika kama vivutio vya watalii.
Kazi za fasihi simulizi kwa upande
mwingine ni sehemu ya ajira. Kwa mfano, shughuli mabalimbali za kisanaa kama
vile ngoma, maigizo na utunzi wa vitabu, vinawapatia vipato baadhi ya wasanii.
Hivyo ni muhimu zihifadhiwe.
Kazi za fasihi simulizi pia ni
kichocheo cha umoja na maelewano miongoni mwa jamii. Yote hayo kwa ujumla wake
yanabainisha kuwepo na haja ya kuendelea kuzikusanya, kuzifanyia kazi,
kuziendeleza, na kuzihifadhi kazi za fasihi simulizi.