MADA
2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI
UWASILISHAJI NA
UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa,
kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji wake.
AU
Ni sanaaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika
kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa watazamaji au wasikilizaji.
Mazungumzo hayo huwa katika mfumo wa masimulizi kwa kuumbwa,
kutambwa, kuganwa au kutongolewa.Fasihi simulizi hueleza jamii kiutamaduni,
kiuchumi na kisiasa. Fasihi huzungumzia juu ya yale mambo ambayo huzunguka
jamii husika na huathiriwa sambamba na
mabadiliko ya jamii na kwa hiyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia
mabadiliko ya mifumo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.Fasihi simulizi ni utanzu
wa Sanaa ambao hukua na kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mifumo
ya jamii.
VIPENGELE MUHIMU VYA FASIHI SIMULIZI
(a)
Msimulizi (fanani),Huyu huwa ni mtu ambaye anaitamba
hadithi, kuimba wimbo, kusimulia au kutoa vitendawili au methali.
(b)
Wasikilizaji au watazamaji (Hadhira),Hawa ni washiriki katika kutazama au
kusikiliza fani ya fasihi simulizi na mara nyingine huwa wanatumiwa na fanani
kama wahusika katika kazi yake
(c)Mandhari, Hili
ni jukwaa au mahali ambapo tukio la kifasihi (fasihi simulizi)
litatendeka.Pahali au mahali hapo yaweza kuwa nyumbani, uwanjani, kuzunguka
moto, baharini n.k.
(d)
Tukio/Dhana inayotendeka,Hili huwa ni tendo linalotendeka katika
jukwaa la fasihi simulizi. Tendo hili laweza kuwa ni usimulizi wa hadithi,
kutega vitendawili, kuimba nyimbo au wimbo au kutoa methali.
SIFA ZA FASIHI SIMULIZI.
Ø Fasihi simulizi hushirikisha fanani na hadhira katika
utendaji kwa wakati mmoja.Hii humfanya fanani aweze uonyesha baadhi ya
matendo katika usimulizi wake kama vile kutumia viungo vya mwili kwa kuchezesha
midomo, kukunja uso, kubinya macho, kuchezesha mabega n.k.
Ø Fasihi simulizi ina sifa ya kuwepo
kwa fanani ambaye huweza kusimulia kwa kuimba, kusoma kwa sauti au kubadilisha mtindo wa usimuliaji
wake,fanani huweza kufanya yote hayo kama akiona hadhira yake imechoka
kusikiliza.Pia ana uwezo wa kuona kama ujumbe wake umeeleweka au la!
Ø Fasihi simulizi zina sifa ya kwenda
na wakati na mazingira, tabia hii inatokana na jinsi fasihi simulizi inavyoenea wasikilizaji
huwa wengi na hata kama baadhi tanzu za fasihi simulizi zilipitwa na wakati
zinaweza kubadilishwa na fanani ili zisadifu mazingira maalumu ya wakati huo.
Ø Fasihi simulizi huzaliwa, hukua,
huishi hata kufa hii inasababishwa na mabadiliko ya mazingira
ambayo hufuata mfumo wa kihistoria wa jamii, mfano kutokana na maendeleo ya
sayansi na teknolojia ya kuhifadhi fasihi simulizi katika maandishi ya fasihi
simulizi huonekana chapwa kwa sababu ya mambo kama vile miondoko au ngoa,
vinakuwa havimo.
Ø Fasihi simulizi ina uwanja maalumu wa kutendea, Fasihi simulizi huwa na sehemu inayochaguliwa kwa ajili ya
aina fulani ya fasihi simulizi itakayofanywa na wahusika. mfano tambiko huwa na
sehemu maalumu ya kutambikia kama vile sehemu yenye pango,kwenye mti mkubwa kama
vile mbuyu, njia panda, makaburini n.k.Hivyo ni wazi kwamba fasihi simulizi
inahitaji uwanja wa kutendea yenye kuhusisha vitendo.
Ø Fasihi simulizi ni mali ya jamii
nzima.Tanzu zake
zote zikishatendwa humilikiwa na jamii kwa pamoja na hii ndiyo inayopatiwa
uwezo wa kurithishwa kizazi kimoja hadi kingine.Hivyo huwafikia watu wengi hata
wale wasiojua kusoma na kuandika.
MCHANGO WA FASIHI SIMULIZI KATIKA FASIHI ANDISHI
Fasihi simulizi ina mchango mkubwa sana katika fasihi Andishi kifani n
kimaudhui
A.Kimaudhui,Dhamira nyingi ambazo ndicho kiini cha maandishi mengi katika Fasihi Andishi zilikwishajadiliwa katika fasihi simulizi.Dhamira hizo ni kama
vile Mapenzi,Siasa,Matabaka,Uhuru,Ukombozi,Usawa,Unyonge wa mwanamke,Uchawi na
Ushirikina n.k Fasihi simulizi haijavumbua dhamira mpya kabisa bali
maudhui/dhamira zote za kale.
B. Kifani,Vipengele mbalimbali vya fani ya fasihi simulizi katika
kufikisha ujumbe kwa jamii zao.Vipengele hivyo ni;
1. Muundo,Fasihi simulizi muundo wake ni wa
moja kwa moja pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi ambao wametumia
muundo wa moja kwa moja.Mfano Riwaya ya Kuli (1979) ya Shafi A. Shafi Ametumia
muundo wa moja kwa moja.
2. Mtindo,Fasihi simulizi
hutumia mtindo wa masimulizi pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi
hutumia mtindo wa masimulizi.Mfano Riwaya ya Shida (1975) ya Balisdya
3. Wahusika,Waandishi wa Fasihi andishi hutumia wahusika wasio binadamu
katika kazi zao ambao kwa kawaida hupatikana katika fasihi simulizi tu.Mfano Mashetani
(1971),Pambo (1975),Adili na Nduguze (1952) Kusadikika (1951) na Kufikirika
(1967) wametumia wahusika mashetani ambao
hupatikana katika fasihi simulizi tu. Wahusika kama wanyama,majini,mazimwi
hupatikana katika fasihi simulizi tu.
4. Matumizi ya hadithi
ndani ya hadithi,hapa
wahusika husimulia hadithi mbali mbali katika fasihi andishi .Hawa husimuliana
hadithi za kimapokeo ambapo hadithi ni kipera cha fasihi simulizi.Mfano Njozi
iliyopotea (1980),Lina Ubani (1984), Mashetani (1971)
5 . Matumizi ya mtambaji hasa katika tamthiliya,Waandishi wengi wa tamthiliya
wametumia mbinu ya utambaji ambapo wanakuwa na mtambaji anayetamba hadithi
fulani.Mfano, Lina Ubani (1984),Nguzo mama
(1980),Pambo (1975)
6.Matumizi ya mianzo ya hadithi za Fasihi simulizi,Mfano tamthiliya ya Jogoo
kijijini na ngao ya jadi(1970) Kilio Chetu (1995) ,Kivuli kinaishi (1990),Riwaya hizi zimetumia mianzo maalum ya
fasihi simulizi mfano paukwa……,pakawa.
7. Matumizi ya Semi mbali mbali,Fasihi andishi hutumia semi mbalimbali ambazo ni ni
tanzu za fasihi simulizi.Semi ambazo hutumiwa sana ni
misemo,nahau,methali,tamathali ,vitendawili na tanzu nyingine
8. Matumizi ya Ushauri na nyimbo,Waandishi wengi hutumia sana nyimbo
katika kazi zao ili kuzipa mvuto,mfano Riwaya ya Njozi iliyopotea
(1980),tamthiliya ya Kilio chetu wametumia sana nyimbo
katika kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
MADA NDOGO-1; UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI
SIMULIZI
(a)
UWASILISHAJI WA FASIHI SIMULIZI
Uwasilishaji
hutumiwa kuelezea njia au mtindo unaotumiwa kufanya kazi ya kifasihi iwafikie
walengwa .Mfano uwasilishaji wa maigizo ni kutendwa kwake jukwaani mbali ya
hadhira ya watazamaji.Tangu zamani, uzalishaji wa tanzu za mbalimbali za fasihi
simulizi huwasilishwa kwa masimulizi ya mdomo na matendo.Fasihi simulizi hubuni
hadithi, nyimbo, methali n.k. zinazobaini hisia zao mbalimbali kuhusu maisha na
mazingira yao.Fasihi simulizi pia inaweza kuzungumzia historia ya watu wa
jumuiya Fulani itikadi zao na mambo mengine mengi wanayoyathamini katika kuishi
kwa pamoja.
Kwa kuwa fasihi simulizi haiandikwi kuhifadhiwa kwake
kunategemea kurithishana kwa mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia
hii kizazi kimoja kinaweza kurithisha kizazi kingine yale mambo muhimu ambayo
kinataka yaendelee katika jamii hiyo mambo ambayo yamefungamana na mazingira
yao maisha yao utamaduni wao na itikadi zao.
(b)UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
UENEZAJI:
Hutumiwa kueleza
uhusianokati ya hadithi na jamii mbali mbali.Nadharia hii huonyesha kuwa inawezekana kuwa jamii zinazohusika
ziliingiliana kihistoria au kutokana na ukaribu wao wa kijiografia n
zilihusiana kihistoria. kuingiliana huku kunaweza kuwa msingi wa kuwako kwa
hadithi zinazosimuliwa ambazo zinafanana katika jamii mbalimbali.
Mfano;utenzi wa Fumo Liyongo unapatikana
katika jamii kadhaa za pwani ya Kenya kama waswahili, wapokomo, wabajuni n.k.
Inawezekana kuwa kupatikana huku ni tokeo la ueneaji hasa kwa kuwa hizi ni
jamii zinazokaribiana kijiografia za zilizohusiana kihistoriau
SABABU ZA KUENEA KWA FASIHI SIMULIZI.
a)
Kuanzishwa kwa vikundi vya Sanaa na muziki,Vikundi
mbalimbali vya Sanaa na muziki vilianzishwa ambavyo kazi yake ni kuendeleza
tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hapa nchini.Vikundi vya Sanaa za maonyesho,
Vikundi vya taarabu na muziki mfano, Ottu Jazz Band,Kilimanjro orchestra,Kilwa
Band n.k vinafanya kazi kubwa ya kueneza na kuendeleza fasihi simulizi hapa
nchini.
b) Muingiliano na fasihi andishi,Kuenea kwa kazi ya fasihi simulizi
kwa asili ni kwa mdomo na masikio yaani usimulizi, hata hivyo maendeleo ya watu
yamefanya baadhi ya kazi za fasihi simulizi zienee kwa maandishi.Maandishi ni
jitihada za kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi na kuifikisha mahali ili
ikatambuliwe au isimuliwe.Hadithi mbalimbali kama vile Hekaya za Abunuasi (1915),Hadithi
za Esopo (1890),Fasihi simulizi ya mtanzania.Hadithi (1977) ,Hizi zote
zimehifadhiwa na kuenezwa kwa maandishi.
Fasihi andishi inatumia vipengele
mbalimbali vya fasihi simulizi katika uandishi wake na hivyo kuviendeleza.
vipengele hivyo kama vile ,Matumizi ya semi mbalimbali,Matumizi ya nyimbo,Matumizi
ya hadithi ndani ya hadithi,Matumizi ya mianzo na mishilizo ya hadithi za
fasihi simulizi,Matumizi ya majigambo, utani n.k.
Kwa sasa methali, vitendawili, nahau,
vimewekwa katika maandishi kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye na hivyo
vinaenezwa kwa njia ya maandishi.
c) Ufundishaji shuleni na vyuoni,mfumo wa Elimu nchini nao umesaidia
kueneza fasihi simulizi kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwa sasa fasihi simulizi
ni somo linalofundishwa toka darasa la kwanza hadi ngazi za juu (chuo kikuu).Vile
vile kuna vyuo hapa nchini vinavyofundisha baadhi ya tanzu mbalimbali za fasihi
simulizi kama vile Sanaa za maonyesho na muziki. Mfano chuo cha Bagamoyo,
Butimba, Nyegezi na chuo kikuu cha Dar-es-salaam.
d) Mabadiliko ya kiteknolojia,Kutokana na
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa sasa fasihi simulizi inaenezwa kwa
vyombo vya habari kama vile kaseti, redio, video, luninga, mitandao ya kijamii
n.k.Mfano Redio Tanzania (TBC) kupitia kipindi chake cha “Mama na Mwana” “Watoto Wetu”
vimesaidia sana kueneza fasihi simulizi hapa nchini Tanzania. Luninga nazo
zimesaidia sana kueneza fasihi simulizi nchini kupitia vipindi mbalimbali vya
michezo ya kuigiza.Hivyo mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hayawezi kuwa
fasihi simulizi
E)Mwingiliano wa mataifa mengine.Katika mwingiliano muziki umesaidia
sana kukuza fasihi simulizi.Hali hii imesaidia kuleta muziki wa kizazi kipya
(muziki wa kufoka foka) pamoja na Rege
vijana wa kizazi kipya wamechota miundo na mitindo ya muziki kutoka nje
na kuendeleza muziki wao ingawa madhui bado wanajadili yale yale yaliyojadiliwa
na wanamuziki wa zamani.Matumizi ya fasihi simulizi katika Sayansi na
Teknolojia yamesaidia sana kuenea kwa fasihi simulizi kwani fasihi simulizi
inapata hadhira kubwa kwa wakati mmoja lakini hadhira hiyo haionani ana kwa ana
na fanani wao kwa kutumia vyombo hivyo vya Sayansi na Teknolojia.
ATHARI ZA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA UWASILISHAJI NA
UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Mwanzo fasihi simulizi iliwasilishwa na kuenezwa kwa njia ya
masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walionana ana kwa ana wakati wa
uwasilishaji lakini zama hizi za Sayansi na Teknolojia, uwasilishaji na
uenezaji unatumia vyombo vya habari kama vile redio, video, televisheni, kanda
kunasia sauti, mtandao na hata kompyuta, mara nyingi hasa hadhira haiwi ana kwa
ana na fanani hutokea hadhira ikawa inaangalia luninga au sinema au tamthiliya
jukwaani kwenye mazingira kama hayo si rahisi hadhira kushiriki kikamilifu
katika utendaji.Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia fasihi inaathiriwa
katika vipengele vifuatavyo:-
·
Uwasilishaji. Mwanzoni fasihi simulizi iliwasilishwa
kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walikuwa wanaonana ana
kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini katika kipindi hiki cha sayansi na
teknolojia, uwasilishaji wa fasihi
simulizi unatumia vyombo kama, vile redio, luninga, video, kanda,
mtandao na hata kompyuta na sio lazima msanii awepo.
·
Uhifadhi, kutokana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia sasa fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa vizuri Zaidi kuliko
inavyofikiriwa na wanamapokeo kwani leo
hii fasihi simulizi inaweza kuwekwa katika mkanda wa kompyuta (flash disc) CD,
DVD, Maandishi n.k na ikaendelea kuwepo kwa miaka mingi sawa sawa na fasihi
andishi hata zaidi.Kwa upande wa video na DVD, uhifadhi wake huendelea
kuonyesha vitendo na sauti huweza kudumu hata zaidi ya maandishi.
·
Wakati na mahali, zamani fasihi simulizi ilifanyika
sana saa za jioni, kando ya moto au barazani. Aidha kwa vile fasihi simulizi
hutolewa redioni inaweza kusimuliwa wakati wowote na mahali popote ambapo
kipindi kinasikika na kwa saa na wakati huo. Majumbani, mijini watoto
hawazunguki moto tena, bali husubiri wakati kipindi kinaporushwa kwa siku
maalumu na wanaizunguka luninga au redio.
·
Hadhira au ushirikishwaji wa hadhira, zamani hadhira ya fasihi simulizi
ilikuwa inaonana ana kwa ana na fanani wake wakati wa uwasilishaji wake. Hadhira
iliweza kuchangia kazi ya fasihi hiyo na hata kuathiri uumbwaji wake, ikaitwa
hadhira tende. Lakini katika muktadha wa maendeleo ya sayansi si lazima fanani na hadhira waonane ana
kwa ana .
MADA NDOGO-2 ;UHIFADHI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Kwa sasa fasihi simulizi inaweza kukusanywa na kuhifadhiwa
kwa njia zifuatazo:-
Ø Kichwa,uhifadhi wa fasihi simulizi ni
katika vichwa vya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Jambo hili limekuwa likifanyika
kwa muda mrefu sana.Hivyo kutokana na kuhifadhiwa katika vichwa ndio maana
fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Ø Maandishi, Tangu maandishi yagunduliwe baadhi
ya kazi za fasihi simulizi zimekuwa zikihifadhiwa kwenye maandishi kwa ajili ya
kumbukumbu ya baadaye. Kazi za fasihi simulizi zikihifadhiwa katika maandishi
inaweza kufanya watu wasijue ni simulizi au andishi. Hata hivyo vidokezo kadhaa
husaidiakujua kazi za fasihi simulizi kama
vile kuwa na mianzo maalum,mfano “Paukwaa!
Pakawa! Au hadithi…….hadithi njoo” n.k.
Aghalabu fasihi simulizi huwa na mtiririko(muundo) wa moja kwa moja usio na
urejeshi.
Ø Kanda za kunasia sauti (tepu rekoda),Hii ni njia moja wapo inayotumika
kuhifadhi tanzu mbali mbali za fasihi simulizi. Kanda hizo hushika sauti pamoja
na vidokezo vyake, kwa hiyo wasikilizaji ili wapate wanachokitaka lazima
wanunue kanda hizo.
Ø Kanda za video, luninga na filamu z sinema CD, DVD
na Kompyuta/Tanakilishi.Mtandao, picha za video hurekodi sura na
sauti,Picha hizo hutembea na kuonyeshwa kwenye skirini ya video na
lunnga. Picha za sinema hupigwa kwa aina maalumu za kamera ambazo hupiga picha
za mfululizo katika utepe maalumu. Picha hizo huonyeshwa kwa mashine na
huonekana zinatembea, kamera nyingi za
sinema za siku hizi zina mitambo ya kurekodi sauti pia. Hivyo kwa kutumia
filamu za sinema na video tunaweza kuhifadhi na kuonyesha kazi za fasihi
simulizi.
ATHARI ZA MBINU MBALI
MBALI ZA UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI
KICHWANI
Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi
kichwani una matatizo yafuatayo:-
·
Kumbukumbu
za akili zinaweza kupungua au kufifia au fanani kufa kabisa. Hali hii ikitokea
fasihi simulizi hupotea.
·
Mtu
anayehifadhi kichwani anaweza kubadilisha mambo muhimu katika simulizi na hivyo
kugeuza kiini cha masimulizi hayo.
·
Kutokana
na mazingira pamoja na mabadiliko kuna tatizo la kupata watu wanaoweza
kuhifadhi kazi hiyo.
MAANDISHI
Uhifadhi
kwa kutumia maandishi una matatizo yafuatayo:-
Ø Baadhi ya mambo hayawezi kuhifadhiwa katika maandishi. Mambo
hayo ni yale yanayohusiana na utendaji, sauti, vitendo, toni, kuimba,
muziki n.k. Matokeo ya kukosekana kwa vitu hivi ni kwamba ladha au
athari ya kazi inayowasilishwa hupungua.
Ø Kukosa sauti kwa hiyo msomaji anapaswa atie sauti na
mahadhi yake mwenyewe.Shughuli hii inaweza kuharibu au kufanya kazi ya fasihi ipungue ubora
wake.
Ø Hakuna ushirikishwaji kati ya fanani
na hadhira, kwa
hiyo hadhira inashiriki kwa kuona maandishi.
Ø Haibadiliki kulingana na wakati na
mazingira. Hivyo
huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi andishi.
Ø Inakuwa ya ubaguzi au watu wachache yaani wale wanaojua kusoma na
kuandika. Wale wasiojua kusoma na kuandika itawawia vigumu kuelewa fasihi hiyo
iliyoko katika maandishi.
Ø Ni gharama kubwa,kuhifadhi masimulizi katika
maandishi, hii ni kwasababu uandishi hutumia kalamu na karatasi. Hivyo hapa
zinahitajika pesa za kununulia kalamu na karatasi na gharama za uchapaji.
KANDA ZA KUNASIA SAUTI
Uhifadhi kwa kutumia
maandishi una matatizo yafuatayo:-
Ø Kanda za kunasia sauti husikika sauti
tu, Matendo hayawezi kushikwa na hii kuathiri tena uhifadhi na utoaji wa kazi
za fasihi simulizi.
Ø Hakuna ushirikishwaji wa hadhira kwani fanani na hadhira hawaonani
ana kwa ana kwa hiyo hadhira inashiriki kwa kusikiliza kanda tu, sikio
huathirika lakini jicho halioni.
Ø Ni gharama, kuhifadhi fasihi simulizi kwa njia
hii kwani kununua tepurekoda pamoja na kanda zenyewe, betri, spea hupatikana
kwa shida na kwa bei ghali licha ya hiyo si wote wenye uwezo wa kununua
tepurekoda hivyo ni watu wachache sana wenye uwezo wa kuhifadhi fasih simulizi
kwa kutumia chombo hiki.
Ø Haitabadilika kulingana na wakati au
mahitaji ya hadhira, Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi
andishi.
KANDA ZA VIDEO, LUNINGA, FILAMU ZA
SINEMA, CD, DVD, VCD NA KOMPYUTA
Njia hii ina matatizo yafuatayo:-
v Upungufu wa ushirikishwaji wa hadhira,Hadhira haiwezi kushiriki ila
inasaidia kufanya fasihi simulizi kupata hadhira kubwa ingawa hadhira hiyo
haionani ana kwa ana na fanani wao.Kanda hizo huwa zinatazamwa na watu wengi
hivyo kupata hadhira wengi kwa wakati mmoja ambao hawawasiliani na fanani wao.
v Ni gharama,kwani vitu hivyo vinahitaji pesa
nyingi za kununulia vifaa hivyo ambapo ni watu wachache wenye uwezo wa kununua vifaa
hivyo.
v Haibadiliki kulingana na mahitaji ya
jamii au hadhira au wakati,Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo
fasihi andishi
v Vifaa hivyo vinahitaji mahali pazuri
ambapo panaweza kutunza vyombo hivyo kwa muda mrefu, endapo havitahifadhiwa hivyo kuna hatari ya kupoteza kilichohifadhiwa
katika vyombo hivi.
MADA NDOGO-3; KUHAKIKI KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI.
Kazi za fasihi simulizi zinaweza kupimwa na kuonekana kama
zinafaa au hazifai. Kazi hizi hupimwa kwa kuzingatia uhusiano wake na hali
halisi ya jamii.Katika upimaji vipengele
vya fasihi simulizi huangaliwa jinsi
vilivyotumika.Upimaji wa ubora wa kazi ya fasihi simulizi hujumuisha umuhimu wa
mambo yaliyosemwa katika jamii inayohusika au namna mambo hayo yanayosemwa
Hivyo mhakiki atajiuliza maswali kama:-
Ø Ujumbe utolewao hapa ni wa kweli na
una manufaa au la!
Ø Je maadili yatolewayo hapa
yanalingana na wakati tulionao?
Ø Je nahau, misemo, methali na
tamathali za semi zinalingana na jambo linalosemwa au la!
Ø Je mtiririko wa matukio unasaidia
msikilizaji kuelewa kisa au unamchanganya?
Maswali ya namna hiyo yanamsaidia mhakiki kuelewa ubora wa
kazi ya fasihi simulizi.Pia yaweza kutumiwa na mtunzi wa kazi ya fasihi
simulizi ili kurekebisha kazi yake na kuifanya iwe bora Zaidi.
FANI KATIKA FASIHI SIMULIZI
FANI
Fani ni ustadi au
ubingwa au mbinu ambazo msanii wa kazi ya fasihi hutumia katika kuwasilisha
ujumbe wake kwa hadhira yake.
AU
Fani ni Sanaa na jumla ya vipengele vya lugha
vilivyowekwa katika mpangilio mahususi ili kutoa maana fulani kwa hadhira.
VIPENGELE VYA FANI
1.Tukio,Katika tanzu za fasihi simulizi mara nyingi ni lazima pawe na
jambo au tukio ambalo huchukuliwa kama kiini au chanzo cha utanzu
utakaohusishwa fani au utanzu unaotumiwa na msanii hauibuki tu hivi hivi.Tukio
huwa ndio kishawishi cha fanani wa fasihi simulizi .Mfano: Nyimbo za unyago
huibuka katika mazingira yake, methali za kutuliza zaweza kutumiwa pale ambapo
pana majonzi ya aina fulani, kwa hiyo ni lazima pawe na tukio ambalo litachukua
chemichemi ya utanzu utakaotumiwa na fanani kuwasilisha ujumbe wake kwa
hadhira.
2.Mazingira/mandhari, Mazingira ni pale ambapo matukio ya fasihi simulizi
yaliibuka ama yalitokea.Ufundi wa kuchora mazingira unatoa picha halisi, picha
inayoonekana waziwazi juu ya mazingira yaliyohusika.Fasihi simulizi hutegemea
sana muktadha au mazingira maalumu hivyo tungo za fasihi simulizi huwa
zimejikita katika utamaduni wa jamii zinamoibukia vifaa ambavyo vinatumika
katika fasihi simulizi vinategemea mazingira yanayohusika, mfano msanii
anapodhaminia kutoa picha ya kuogofya anatumia mazingira ambayo yanaogofya kama
vile mazingira ya misituni na wahusika kama majitu ili kuleta dhana ya hofu
katika mazingira yake.
3.Muundo,Katika fasihi simulizi muundo ni mpangilio na mtiririko wa
kazi ya fasihi simulizi kwa upande wa visa na matukio.Katika muundo kinachozingatiwa
ni jinsi fanani alivyofuma na kuunda
hata alivyounganisha tukio moja na lingine kimoja na kingine, wazo na wazo,
ubeti na ubeti na mstari wa beti na mwingine.Kuna miundo mbalimali katika tanzu
mbalimbali za fasihi simulizi, kama vile
muundo
wa moja kwa moja na kuna muundo changamano,pia upande wa ushairi
Katika mashairi kuna miundo mbalimbali ambayo hutumiwa
kuainisha mashairi kwa kufuata idadi ya mistari katika kila ubeti, miundo hii
ndiyo hutupa mashairi ya tarbia, tathilitha, takhmisa na n.k.Katika hadithi na hata
katika tamthiliya waweza kuwa na muundo ambao fanani ameanza kutoka mwanzo
akaenda katikati na baadae kumalizia kisa chake aina hii ya muundo
unaitwa mtiririko shanga.Mtirirko wa namna hii hujengwa kwa kutumia visa au
vitukio mbalimbali na vinaweza kuongezwa na kupunguzwa bila kupoteza maana ya
hadithi au tamthiliya.
1. Mtindo,Katika kazi ya fasihi mtindo ni ile
namna ambayo msanii hutunga kazi yake na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui
huainisha kanuni au kaida zilizofuatwa kama zilizopo ni za kipekee. Mtindo ni upangaji wa fani na
maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye huonyesha nafsi na labda
upekee wa mtunzi wa kazi hiyo.
Katika tamthiliya na
riwaya katika mtindo kinachotazamwa ni
matumizi ya nafsi,matumizi ya monolojia,masimulizi na dayalojia,matumizi ya
hadithi ndani ya hadithi,matumizi ya barua n.k
Upande wa mashairi
kuna mitindo mbalimbali kama vile Mtindo wa Pindu,mtindo wa kuhoji,mtindo wa
beti kubadilishana vina,mtindo wa kidato n.k na shairi linaweza kuwa la
vina na mizani au la kisasa ambalo halifuati kanuni za urari wa vina na mizani.
2. Matumizi ya lugha.
Ni kipengele muhimu cha fani ya fasihi, lugha ndiyo malighafi
ya fasihi.Lugha inayotumika katika kazi ya fasihi ni lugha ya kisanaa
inayopambwa na inayokusudiwa kuibua hisia fulani kwa hadhira yake.Inaweza
kuathiri moyo ya hadhira na kulingana na jinsi inavyotumiwa kwa lengo la
kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia hamasa au kushawishi
‘’
Fani lazima iwe na utanashati na ulimbwende wa kipekee wenye mvuto na mnato wa
kuteka na kusisimua hisi za wasikilizaji wasomaji au watazamaji’’(khatibu
1981:16)
Matumizi ya lugha fasaha, uteuzi wa misamiati na matumizi ya
misemo na methali zinazosadifu mazingira ya jaini inayohusika kufanya kazi hiyo
ya fasihi simulizi kuwa sumaku ya kuvutia msomaji, msikilizaji au
mtazamaji.Tamathali za semi za aina mbalimbali hutumika kujenga picha mfano ya
tamathali za semi ni kama vile sitiari, tashihisi, kejeli, kijembe,
tabaini,
tuniaba, tashibiha n.k.Taswira ni lugha ambayo huchora picha za watu,
vitu au mahali kwa kutumia ishara katika taswira unaweza kubainisha maelezo
ambayo jinsi yanavypangwa na msanii huweza kufanya hadhira zipate aina
mbalimbali za hisi za kunusa, kusikia, kuona na kugusa.Mara nyingi hutumiwa na
wasanii ili kunasa hisia zao kwa hadhira.Hivyo wasanii hutumia maneno ambayo
huumba picha kamili ya kitu, hali, wazo, dhana au uzoefu fulani wa jamii
inayohusika.Mara nyingi matumizi ya picha huenda sambamba na ishara mbalimbali
ili kuwakilisha vitu, dhana au mawazo mengine.
3. Upeo
Katika
fasihi simulizi upeo ni kama kilele cha kazi yenyewe, kuna upeo wa aina mbili
Upeo wa juu ,ni zile sehemu za kazi hiyo ambazo
hutosheleza haja za wasikilizaji au watazamaji. Katika sehemu hii hadhira
hupata majibu muhimu ambayo kazi hiyo imechelewesha kwa kutumia taharuki mbinu
rejeshi, mtindo wa kiutelezi n.k.Mara nyingi watunzi wa kazi za fasihi
huweka kipeo cha juu mwishoni mwa kazi zao ingawa si lazima kuwa na kipeo kimoja tu
wakati mwingine waweza kupata kazi ya fasihi simulizi ambayo haina kipeo kabisa
Katika kazi mbalimbali za fasihi wasanii hujenga mgogoro ambao hujtokeza na
kukua, jinsi kazi hizo zinavyokua, kipeo cha juu hutokea pale ambapo msanii
hujaribu kutoa suluhisho kwa mgogoro uliojengwa katika kazi yake.
Upeo wa chini ,ni sehemu ambayo matatizo yaliyounda
kazi ya fasihi yanatatuliwa.Upeo wa chini ni pale ambapo haja na mataajio ya
hadhira hayakukidhiwa, katika baadhi ya kazi za fasihi vipeo vya chini hudhihirisha
udhaifu wa kazi hiyo lakini katika kazi nyingine upeo wa chini huwa umekusudiwa
hivyo na mtunzi.Hali hii ya pili hujitokeza hasa katika kazi ya fasihi ambayo
upeo wa chini hutumiwa kwa lengo la kushangaza hadhira.
4. UCHESHI KATIKA KAZI ZA FASIHI
Ucheshi ni kipengele muhimu cha kifani katika kazi ya fasihi
hasa fasihi simulizi.Ucheshi ni mbinu ya kifani ambayo watunzi hutumia katika
kazi zao za fasihi kwa lengo la kuchekesha na kuburudisha hadhira na kuondolea
uchovu.
Wasanii mbalimbali hutumia mbinu tofautitofauti kuleta
vichekesho katika kazi zao.Baadhi yao hutumia vitendawili ili kujenga,
kejeli, dhihaka, n.k. vichekesho pia huweza kutumiwa ili kujenga
maudhui.
5. WAHUSIKA.
Ni viumbe ambavyo hutumiwa na wasanii katika mtiririko wa
matukio kuelezea visa vyake.Wahusika wanaweza kuwa watu, miti, wadudu, mizimu, misitu
na wanyama.Wahusika huwa ni viumbe ambavyo vinatenda na kutendewa wanatumwa na
msanii kusimamia hali mbalimbali za binadamu katika jamii wanamoishi.
Hawa ndio uti wa mgongo wa fani ya fasihi simulizi, Bila wahusika
mtiririko wa matukio au visa hukosa pahali pa kujishikiilia.Wahusika si viumbe
maalumu wa mtunzi kwa vile ndiyo wanaotumia kutoa picha au kuwasilisha mawazo
na fikra zake kwa jamii inayowakilishwa na wahusika hao.Katika Fasihi
simulizi wahusika wanaweza kuwa binadamu
,wanyama,au vitu fulani vilivyopewa fursa ya mandhari na kauli kama binadamu.
VIPENGELE VYA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI
Ø MAUDHUI
Ni jumla ya mambo yote yanayosemwa na msimuliaji au mwandishi
katika kazi yake.Vipengele vya maudhui au umbo la ndani la kazi ya fasihi ni
kama vile
Ø Dhamira, Ni
kusudio la mtunzi wa kazi ya fasihi.Kazi ya fasihi inaweza kuwa na dhamira kuu pamoja na dhamira
ndogo ndogo.Ubainishaji wa dhamira hufanywa na hadhira,hivyo dhamira hufahamika
kutokana na fasili za wasikilizaji au wsomi wa kazi ya fasihi.
Ø Ujumbe: Ili
dhamira ya mtunzi itimie, msanii hutoa taarifa fulani fulani kwa hadhira
yake.Taarifa hizo huitwa ujumbe.
Ujumbe unaweza kutamkwa wazi au kwa uficho. Kwa mfano methali ya “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” ina ujumbe huu ukidharau maonyo ya wakubwa utapatamatatizo,Siku za mwizi ni arobaini ujumbe wa methali hii chenye mwanzo kina mwisho kwa kawaida
kazi moja ya fasihi inaweza kuwa na taarifa Zaidi ya moja.
Ø Mafunzo: Ni
mafundisho au nasaha za mtunzi katika kazi ya fasihi.Mafunzo pia huwa na maana kulingana
na fasili ya hadhira. Mafunzo humfikirisha msikilizaji au msomaji kwa njia ya ujumbe.Mfano
katika ujumbe huu akaiba akafungwa hapa
funzo ni tusiibe wakati mwingine kazi za fasihi inaweza kutoa mafunzo mabaya
(maadili) mtunzi anaweza kukusudia hivyo au kutokusudia hivyo.
Ø Migogoro: Hii
huelekeza kisa lakini hujizatiti juu ya migogoro ya maisha anayosimulia
fanani.Baadhi ya kazi za fasihi huonyesha ukinzano uliopo baina ya makundi ya
watu au hali ya aina moja dhidi ya hali nyingine kuna aina nyingi za migogoro
lakini Zaidi ni ile ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni au ile ya kibinafsi
mfano: matatizo yanayosababishwa na uzembe dhidi ya watetezi wa kazi (viongozi)
dhidi ya usasa katika mila na desturi husababisha mgongano wa kiutamaduni.
Ø Falsafa: Ni mafunzo
makuu ya msanii (mtunzi) kuhusu maisha. Mawazo haya hutokana na uchanganuzi wa
kimantiki na huwa ndio hekima na busara za msanii (mtunzi) huyo.Ni Imani ya
mwandishi au fanani katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii.
UMUHIMU NA UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
SIMULIZI.
Fani ni jumla ya mambo mengi yanayoijenga kazi ya
fasihi.Mambo haya ni kama vile muundo, mtindo, mandhari,wahusika na matumizi ya
lugha na maudhui ni jumla ya mawazo au dhamira, msimamo, mtazamo, falsafa na
ujumbe katika kazi ya fasihi.
Kwa ujumla fani na maudhui ni vitu vya muhimu sana katika
fasihi simulizi kwa sababu mtunzi hutumia vipengele hivi katika kujenga kazi
yake anayotaka kuwasilisha kwa jamii husika.Maudhui ni kila kina kinachosemwa
na fani ni namna kinavyosemwa.
Fani na maudhui ni vitu vinavyohusiana, vinaathiriana,vinategemeana na
kukamilishana katika kujenga kazi ya fasihi simulizi na kila kipengele kimo
ndani ya kingine
Mudhui hujumuisha viungo mbalimbali vya kazi ya fasihi
simulizi na fani ni mbinu za kisanaa zinazotumiwa na msanii ili kuvifanya
viungo hivyo viyasawili maisha kwa njia ivutiayo hadhira.kila kigezo (fani na
maudhui) kimo ndani ya kingine huku vikishirikiana na kuathiriana katika
kujenga au kubomoa kazi ya fasihi simulizi.
MADA NDOGO-4 ; KUTUNGA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Utungaji ni uundaji wa mawazo na kuyapanga maneno
yakuwasilisha ama kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi.Utungaji unweza
kutolewa kawa njia mdomo aqu kwa njia ya maandishi.
Mambo ya kuzingatia
katika kutunga kazi ya fasihi simulizi.
·
Kuwa na jambo la kueleza (tukio).Mtunzi anapaswa kuwa na jambo ambalo anaona kuwa
linasababisha mivutano katika jamii.Jambohilo lazima litoke katika jamii
inayohusika na isiwe nje ya jamii hiyo.
·
Kuteua utanzu utakaotumia.Mtunzi ni vyema kujua
ni utanzu upi atakaotumia katika kuwasilisha jambo hilo kwa jamii.Kwa kawaida
fasihi simulizi ina tanzu nne ambazo ni hadithi, ushauri, semi na Sanaa za maonyesho
(maigizo).
·
Kuteua vipengele vya maudhui, mtunzi anapaswa aangalie nini dhamira yake, kuna ujumbe gani
kwa hadhira, hadhira itapata maadili gani na je migogoro ipi na iwasilishwe
vipi ili isipotoshe lengo zima la kazi yake.
·
Kuteua kipera kitakachotumika katika uwasilishaji wa kazi yake kwa
hadhira, mfano
kama mtunzi ameamua kutumia utanzu wa hadithi; hanabudi kuchagua kipera kimoja
wapo kati ya ngano, soga, vigano, visasili au tarihi (visakale)
·
Uteuzi wa vipengele vya fani. Baada ya kubaini vipengele vya maudhui, msanii anapaswa
aangalie namna atakavyowasilisha maudhui hayo kwa jamii.Hapa atatumia au atashughulika
na vipengele vya fani ambavyo atavitumia katika kuwasilisha ujumbe
wake.Vipengele hivyo ni muundo, mtindo, wahusika, matumizi ya lugha na
mandhari.Sehemu hii ndiyo ambayo mtunzi anatakiwa kutumia ufundi na ubunifu wa
hali ya juu ili kazi yake ieleweke, ielimishe na kusisimua hadhira.
Utungaji wa hadithi za fasihi
simulizi
Katika kutunga hadithi yoyote, vipengele vifuatavyo
vinastahili kuzingatiwa;
Ø Maudhui
Haya ni masuala yanayowasilishwa na
hadithi kwa ujumla wake.Katika utungaji wa kipengele cha maudhui tutazingatia
mambo yafuatayo:-
a)Dhamira – Hili ni lengo kuu analowasilisha mtunzi kwa hadhira.
Dhamira lazima zitokane na jamii inayohusika. Katika dhamira, kuna dhamira kuu
na dhamira ndogo ndogo zinazojenga dhamira kuu. Mtunzi wa hadithi ni lazima
azingatie kipengele hiki.
b) Ujumbe na maadili – Hadithi lazima
iwe na ujumbe fulani kwa hadhira yake. Mtunzi lazima azingatie hilo. Vile vile
hadithi lazima itoe maadili fulani kwa jamii na maadili yanayotakiwa kutolewa
lazima yaendane na jamii husika pamoja na wakati.
Ø Fani
Fani ni jumla ya
mambo yote yanayofanywa katika kazi za sanaa ili kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. Katika utungaji wa hadithi mtunzi
anatakiwa azingatie vipengele vifuatavyo kifani:-
·
Ploti/visa ,ni mtiririko wa matukio ya hadithi
kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kila hadithi ina mwanzo – kati – mwisho. Aghalabu
hadithi zina ploti moja nyepesi ya moja kwa moja. Mtunzi katika kipengele hiki
cha ploti, lazima azingatie hadithi yake itakayokuwa na mwanzo – kati – mwisho.
·
Wahusika ,Hivi ni viumbe vinavyoshiriki katika
hadithi. Hadithi huwa na mhusika mmoja mkuu anayehusishwa na matukio makuu
katika hadithi nzima. Wahusika ni wachache na huwa bapa (wasiobadilika) .
Mtunzi wa hadithi katika kipengele hiki cha wahusika lazima azingatie ubapa wa
wahusika wake katika kuwajenga wahusika wake.
· Mazingira – Katika kipengele hiki, mtunzi anapaswa kuangalia
muktadha kijiografia na kuonyesha:-Mazingira ya kijamii yanayojadiliwa,Majukumu
ya mhusika mkuu anayoyatekeleza katika jamii/ familia, n.k,Mahali tukio
linapotokea (mahali pa kazi pa mhusika – msikitini, kanisani, ofisini,
nyumbani, kijijini, mjini, n.k)Mandhari yakichorwa vizuri husaidia kulisukuma
gurudumu la wakati na kwapambanua wahusika.
a) Kilele –
Kilele cha hadithi huwa pale suluhisho la maswali ambayo msikilizaji amefanywa
ajiulize hupatikana.
b) Mtindo wa usimulizi – Hadithi nyingi hutumia nafsi ya kwanza au ya tatu. Zingine hutumia
chuku maelezo na kutumia takiriri – mambo ambayo mtunzi anatakiwa kuyazingatia
wakati wa utunzi wake.
· Matumizi ya lugha,Katika kutunga kazi za mtunzi anapaswa kutumia lugha yenye mvuto iliyojaa
Taharuki,Tamathali za semi kama vile
tashihisi, tashibiha, sitiari, n.k
UTUNGAJI WA MASHAIRI/TENZI/NGONJERA WA FASIHI SIMULIZI
Kabla ya kuanza kutunga shairi lolote,
mtungaji anawajibika kuvifahamu kwanza vipengele vinavyojenga shairi,
vinginevyo utungaji wake utapwaya sana.Vipengele muhimu vinavyojenga shairi ni
vya aina mbili: vya kifani na, vya kimaudhui.
Fani
Shairi lolote lile ni muungano wa fani,
maudhui na muktadha.Kwa kawaida, mashairi
hutunga ili kueleza maudhui fulani kutokana na, au kwa ajili ya muktadha
fulani. Shabaha hiyo ya mshairi hutimizwa kwa kutumia fani na hudhihirika
kifani. Ingawa maudhui hutawala fani kwa maana ya kuwa mtunzi huanza na wazo
ambalo hulitafutia fani ya kulielezea, lakini fani vilevile huathiri maudhui
hayo, maana maudhui yamo ndani ya fani na hudhihirika kifani. Hivyo tukitaka
kutunga shairi sharti kwanza tuviainishe na kuvielewa vipengele vya kifani
vitakavyotumika. Vipengele muhimu vya kifani ni lugha, muundo, wahusika na
mtindo.
(a)Lugha,ushairi hutumia lugha yenye mpangilio na maneno maalumu
yaliyoteuliwa ili kuwasilisha ujumbe wake. Kwa hiyo, vipengele vya kuzingatia
upande wa lugha ni ;Utenzi wa maneno na
semi,Mpangilio wa maneno katika
sentensi,Matumizi ya picha (Jazanda)
na tamathali: Picha (taswira) ni uwakilishaji wa jambo kutumia kauli maneno
yanayosawiri picha au hali ya jambo hilo na kuibua hisia au vionjo kuhusu jambo
hilo katika akili ya msomaji/msikilizaji. Picha huweza kumfanya msomaji au
msikilizaji, katika mawazo yake, aone, asikie aonje, anuse, apende au achukie
kile kinachosawiriwa.
Tamathali ni aina ya picha. Ni ufananisho wa vitu kisanii kwa kusudi
maalumu. Baadhi ya tamathali zinazotumika sana ni tashibiha, sitiari, tashihisi, metonomia (kutumia sehemu ya kitu
kuwakilisha kitu kamili, au kutumia kitu kidogo kuwakilisha kitu kikubwa
kinachohusiana nacho), mubalagha na kejeli.
Picha na tamathali hutumiwa sana na
washairi ili kuyasawiri mawazo yao. Baadhi ya picha na tamathali hizo huwa na
viwango mbalimbali vya maana na kuhitaji akili pevu na uzoefu kuzifumbua.
(b)Muundo,mashairi ya
Kiswahili yana miundo mingi. Baadhi ya vipengele vya kimuundo vinavyotumika
zaidi ni mistari,beti,mizani na vina. Urefu wa wa mistari hutofautiana
kutegemea mizani ya shairi linalohusika, au kutegemea mtiririko wa wazo/hisia
kama ni shairi huria. Urefu wa beti hutegemea idadi ya mistari katika kila
ubeti: zipo tungo za utatu(tathlitha),unne(tarbia), utano (takhimisa), n.k.
Kwa kweli miundo inayotokana na
mpangilio wa vina na mizani haina idadi, inategemea matakwa na ubunifu wa
washairi wanaohusika.
(c)Wahusika,mashairi ya
kawaida hayategemei sana wahusika ili kuwasilisha ujumbe wake. Hata hivyo,yapo
mashairi ya masimulizi,kwa mfano, tendi, ambayo hutumia wahusika kujenga
maudhui yake. Utungaji wa mashairi ya aina hiyo lazima uzingatie pia dhima na
taswira ya wahusika hao katika ujenzi wa matukio na maudhui ya utenzi huo.
(d)Mtindo,mtindo ni tabia
ya utungaji ambayo humpambanua mtunzi mmoja na mwingine. Mtindo hubainika
katika namna mtunzi anavyotumia maneno yake (Kama anaendelea kutumia maneno
magumu au rahisi, kuchanganya lugha, kutumia methali, n.k.) Jinsi anavyozipanga
semi zake (kama anatumia sentensi fupifupi au ndefu, takiriri (vibwagizo,
n.k.), na namna anavyoumba tungo zake. Mtindo wa mtunzi humwezesha msomaji
kubainisha upekee na uasilia wa mtunzi huyo,na pia athari za watunzi wengine
kwenye usanii wake.
Mambo
muhimu ya kuzingatia katika utungaji wa ushairi wa kimapokeo
Hapa yanaingia mashairi ya tenzi za
kijadi zenye kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho
au kati. Katika ushairi wa kimapokeo,kuna mambo ya msingi yanayosemekana kuwa
ni uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili. Kwa mujibu wa wanamapokeo, shairi la
Kiswahili lazima liwe na vina, mizani, mstari, ubeti na kituo. Katika utenzi
(aina pia ya ushairi wa kimapokeo) kunakuwa na bahari katika mstari wake wa
mwisho. Hapa tutaelezea kwa ufupi juu ya vipengele hivyo.
·
Vina, ni silabi za namna moja zinazotokea
baada ya kila mizani kadhaa katika mstari wa shairi. Mashairi ya mistari minne
ya mizani 16 huwa na vina katika silabi ya 8 na ya 16 katika mistari mitatu ya
kwanza. Kwa kawaida, vina vya silabi 16 huwa vya namna moja katika beti zote za
shairi zima, na vina vya silabi 8, kwa desturi inayotumika sana, huwa tofauti
ubeti na ubeti. Kwa kawaida tuna vina vya kati na mwisho. Mfano:
Kuna
utesi uzushi, nchi ina maongezi,
Pembeni twaona
moshi, moshi haujitokezi,
Shairi
kuzinakishi, kugeuza maongezi,
Mashairi na
utenzi, sanaa tusipotoshi.
Katika ubeti
huu,kuna vina vya kati na mwisho ambavyo hufanana.
·
Mizani ,ni jumla ya silabi zilizomo katika
kila mstari wa ubeti.katika ushairi, hizi ndizo ziletazo urari wa mapigo, kwani
kila mstari unatakiwa uwe na mizani sawa na mistari mingine. Kwa kawaida
mashairi ya kimapokeo huwa na mizani 16, sehemu ya kwanza mizani 8 na sehemu ya
pili mizani 8.
Mfano
Ku
na u te si u
zu shi, n chi i na ma o nge zi
8
2 3 4 5 6
7 8
9 10 11 12 13 14 15
16
·
Kituo,Huu ni mstari wa mwisho katika kila
ubeti wa shairi. Kituo huweza kuwa kimalizio au kiini.Kinakuwa ni kimalizio
kinapokuwa kinatumika kama kitu cha kulifunga na kulikamilisha wazo moja katika
kila ubeti. Kinakuwa ni kiini kinapokuwa kikitumiwa na kinajitokeza katika kila
mwisho wa ubeti na kinataja kwa muhtasari jambo muhimu linalozungumzwa.
·
Muwala (kutosheleza),Muwala ni ile
hali ya utoshelevu katika ubeti hadi katika utungo mzima. Yaani kila ubeti
uweze kujitosheleza katika maana, lakini wakati huo huo ukawa hausigani na beti
nyingine.
·
Ubeti.,Hiki ni kifungu chenye kuleta maana
kamili katika jumla ya vifungu vilivyomo katika utungo.
·
Kipande,Hiki ni kisehemu kimojawapo katika visehemu
viwili au zaidi vya kila mstari kwa tungo zenye kugawanyika katika sehemu mbili
au zaidi katika kila mstari.
HATUA/Mambo ya kuzingatia katika utungaji wa mashairi
Ø Kuteua maudhui na dhamira
Katika
kipengele cha maudhui, mtunzi wa mashairi anatakiwa kuzingatia vipengele
vifuatavyo ili aweze kufanikisha lengo lake.
· Kuweka lengo maalumu – Kabla ya kuanza kutunga hairi lazima ujue nini unataka kueleza. Hapa
lazima ujue sababu inayokufanya utake kueleza hayo uliyonayo. Lengo laweza kuwa
kupinga mauaji ya albino, ajira kwa watoto au unyanyasaji wa wanawake.
· Kuteua wazo kuu la shairi – Hili ndilo wazo utakalolikuza na kuliendeleza. Wazo kuu
linaweza kuwa “ athari za ugonjwa wa UKIMI” katika jamii. Hivyo mwandishi
ataliendeleza wazo hilo kutoka mwanzo hadi mwisho.
· Kuoanisha dhamira na wakati – Ni muhimu mtunzi wa ushairi kuhakikisha kwamba
anazungumzia mambo ambayo anafikiri jamii inayahitaji katika wakati huo. Kwa
mfano, leo Tanzania imekabiliwa na matatizo kama vile ugonjwa wa UKIMWI , ajira
kwa watoto, mauaji ya albino, madawa ya kulevya, n.k. Haya ndiyo mambo ambayo
mtunzi hupata hadhira kubwa. Kama taongea mambo ambayo yako nyuma ya wakati,
atakuwa haitendei haki jamii yake kwa kujadili mambo ambayo hayako katika jamii
yake kwa wakati uliopo.
· Kupanga vizuri mawazo yako – Panga mawazo yanayojenga maudhui kimantiki kutegemea
uzito, upya, ugumu na umuhimu wake kwa jamii inayohusika.
Ø Kuteua vipengele vya fani
Maudhui pekeehayatoshi kulipa shairi mvuto. Mtunzi ni lazima
azingatie fani, yaani mbinu za kisanii anazotumia mtunzi kulipa shairi mvuto.
Mbinu hizi ni pamoja na:-
·
Kutumia mitindo inayofaa – Shairi linaweza kuwa la kimapokeo
au kisasa. Uteuzi wa mtindo untegemea sana dhamira inayokusudiwa pamoja na
lengo alilonalo mtunzi mwenyewe. Kwa mfano, tukio la kihistoria utatumia
“utenzi” badala ya “wimbo”, mawaidha fulani huwezi kutumia “utenzi” bali
utatumia “ushairi” au “wimbo”.
·
Kutumia miundo inayofaa,Kuamua muundo wa shairi kutategemea
idadi ya mistari. Mtunzi anaweza kutumia muundo wa tathnia (mistari miwili),
Tathlitha (mistari mitatu), Tarbia (mistari mine), Tkhimisa (mistari mitano) au
sabilia (mistari sita na kuendelea). Katika kipengele hiki ni muhimu vile vile
mtunzi kuzingatia idadi ya mizani, aina ya vina, vipande, kituo msisitizo,
muwala, ubeti na urari. Vitu hivi ni muhimu sana hasa kwa ushairi wa kimapokeo.
·
Uteuzi wa lugha – Ushairi una lugha yake ya tofauti
na kazi nyingine. Mtunzi hana budi kutumia lugha yenye sifa zifuatazo:- Lugha
ya mkato, -Matumizi ya picha, Matumizi ya tamathali za semi, Matumizi ya
methali, misemo, nahau na mbinu nyingine za kisanaa
UTUNGAJI WA MAIGIZO YA FASIHI SIMULIZI
Katika utungaji wa maigizo kuna vipengele mbali mbali ambavyo
lazima vifuatwe ili utungaji ukamilike. Vipengele hivyo ni :-
·
Kuchagua tendo au tukio la kuigiza ,Mtunzi achague matendo yale tu
ambayo lazima yatasaidia kujenga wazo lake. Ni lazima jambo hilo liwe uzito au
athari fulani kwa jamii. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni
kama vile ufisadi, malezi ya watoto, unyanyasaji w mwanamke, mauaji ya albino,
ujambazi, madhari ya UKIMWI, n.k
·
Kuchagua mahali pa kutenda jambo ,Mahali pa kutenda panaweza kuwa
ofisini, nyumbani, barabarani kwenye
basi, mjini, kijijini, n.k.
·
Kuteua mtindo na kuteua jambo la
kuigizwa,Hapa mtunzi
anaweza kutumia fumbo, vichekesho, tanzia, ramsa (futuhi), n.k. Ni vizuri
mtunzi achanganye mbinu ili kutdumisha mvuto.
·
Kupanga hoja zinazojenga maudhui ya
igizo,Maudhui
hujikita katika migogoro. Masuluhisho ya migogoro hupatikana pale migogoro
inapofikia kilele. Kwa mfano, mwanamke anapojikomboa kutokana na manyanyaso ya
mwanaume.
·
Kuweka mpangilio wa maonesho,Maonesho ambayo hujumuisha vitendo
na hoja zinazokamilisha sehemu inayobeba
maudhui ni muhimu sana. Maonesho yapangwe kwa utaratibu maalumu ili yaweze
kufikisha ujumbe kirahisi kwa hadhira. Maonesho yakipangwa ovyo, mvuto wa kazi
ya sanaa huwa ovyo pia.
·
Ujengaji wa wahusika- Wahusika wajengwe kutokana na
misukosuko ya migongano. Matendo, maneno na mawazo ya wahusika yapate chanzo
kutokana na misukumo hiyo. Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika tofauti tofauti.
Kwa mfano, wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi, wembamba, n.k. Ni
muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua mavazi yao na vifaa
vingine. Uamuzi huu yafaa ufanywe kwa kuzingatia mazingira.
·
Uteuzi wa maneno – Maneno ya kusema wahusika
yanapaswa kuwa yale tu ambao yanajenga tendo. Maneno yanajengwa ili
kudhihirisha tendo liwe wazi zaidi. Kuweka maneno mengi hudhoofisha nguvu ya
matendo, katika kuleta maana inayokusudiwa kwa vile huwa vigumu hupatanisha
maneno hayo na matendo. Kwa hiyo, mtunzi wa maigizo anapaswa kuwapa wahusika
wake maneno machache jinsi iwezekanavyo, na tena yale tu ambayo yanaoana na
vitendo.
·
Baada
ya yote hayo, mtunzi anawezakuandika maigizo na kuhariri – Ni muhimu kutumia lugha ya
kimazungumzo (dayolojia) inayovutia na kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleze
maadili kwa mnato.
M
W I S
H O
No comments:
Post a Comment