KIDATO 3 $ 4-KISWAHILI-UCHAMBUZI WA RIWAYA

 WATOTO WA MAMANTILIE
Mwandishi –EMMANUELI MBOGO

UTANGULIZI
WATOTO WA MAMANTILIE” ni riwaya inayochambua kwa kina adha wanazozipata akina mamantilie.Hawa wakina mama wametapakaa mjini wakifanya biashara za kuuza vyakula ili kutafuta chochote cha kuweza kutunza familia zao.
Mwandishi anatueleza kuwa wakina mama hawa wanaishi maisha magumu,watoto wao ambao wangewasaidia hapo mbeleni hawapati elimu kutokana na kukosa mahitaji muhumu ya shule.Matokeo yake wanajiingiza kwenye vitendo viovu ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya,wizi na biashara za madawa ya kulevya.

MAUDHUI
DHAMIRA  KUU; UMASIKINI
Hili ni suala ambalo limeongelewa kwa kiasi kikubwa katika riwaya hii,takribani wahusika wote wameonekana wakiandamwa na umasikini.Kazi zao ni za kijungujiko (ndogo ndogo)kiasi ambacho hakiwezi kuwapatia kipato cha kumudu maisha yao.
    Mfano katika familia ya MAMA NTILIE ,mwandishi anasema maisha hayaendi bila mama ntilie kwenda kufanya biashara katika genge la Urafiki ,kilichopatikana kinaishia tumboni.
Ni umasikini huu ndio unawakatili kulwa na doto ,watoto mapacha walioachwa yatima baada ya mama yao kufariki .Hata hivyo Doto na Dani wanajiingiza katika ujambazi hatimaye wanapigwa risasi na kufa.
DHAMIRA NDOGONDOGO
1.   Suala la Malezi
            Mwandishi amejadili suala hili kwa kuwatumia Musa,Doto,Kulwa,Peter na Zitta anaonyesha umuhimu wa wazazi wote wawili katika malezi.Mfano Musa na Dani wamelelewa na mama tu bila baba hali kadhalika kwa Kulwa na Doto ambao hawakuwa na wazazi wote wawili.Hali hii pia inaonekana kwa akina Peter na Zitta ambao hawakupata malezi ya kutosha kutoka kwa baba kwani ambapo alikuwa anaondoka asubuhi kwenda kwenye pombe na kurudi usiku sana jambo ambalo limechangia kutoweza kutoa mahitaji muhimu kwa familia yake.
2.   Ulevi
Mwandishi amemtumia mzee Lomolomo ambaye alikuwa mlevi wa gongo tangu alipoachishwa kazi kule bandarini.Mzee huyo alikuwa akinywa pombe bila kufanya kazi yoyote ya kumletea kipato bali akiamka asubuhi anakwenda kwenye vilabu vya pombe na kurudi usiku akiwa amelewa .Ulevi wa namna hii huchangia umasikini katika jamii.
3.   Mapenzi
Katika tamthiliya hii mapenzi yamejitokeza katika pande mbili yaani yale ya kweli na yale ya uongo
v  Mhusika Peter ambaye alionyesha mapenzi ya kweli kwa Kulwa  na pamoja na misukosuko aliyoipata kutoka kwa dada yake Zitta.Peter anaonekana hakuwa na msaada .Peter anasema “Tungoje mama arudi lakini siwezi .....hatuwezi kumfukuza tutamwacha ateseke huko mitaani
v  Mamantilie anaonekana kuwa na mapenzi ya kweli kwa mumewe kwani pamoja na kwamba alikuwa mlevi wa kupindukia lakini bado aliweza kumfungulia mlango usiku aliporudi na kumpa chakula
v  Kwa upande mwingine mzee Lomolomo hakuwa na mapenzi ya kweli kwa mkewe na familia yote kwa ujumla kwani hakutoa mahitaji yoyote kama baba wa familia bali alijali pombe tu.
4 . Suala la Elimu
Elimu ni suala la muhimu sana kwa taifa lolote lile lenye mipango endelevu.Mwandishi anatueleza kwamba Peter alipenda sana kusoma shule hata baada ya kufukuzwa shule kwa kukosa ada na sare lakini jitihada hizo ziligonga mwamba na hivyo ndoto zake hazikutimia sababu ya umasikini.
4.   Nafasi ya Mwanamke katika jamii
Katika riwaya hii mwandishi amemchora mwanamke katika nafasi tofauti tofauti kama ifuatavyo;
v  Mwanamke amechorwa kama mhimili wa kiuchumi na kijamii katika jamii,mfano mamantiliye ameonyeshwa akijishughulisha katika biashara ndogondogo kama vile uuzaji wa vyakula na vinywaji baridi ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia yake, mwandishi anasema kila kukicha mamantilie na Zitta wanachukua maharage,unga sufuria na kuni hadi kiwanda cha Urafiki kwa ajili ya kazi na kurudi hadi jioni
v  Mwanamke amechorwa kama mwenye mapenzi ya dhati,mfano mamantilie alimhurumia mumewe wakati akirudi amelewa pamoja na kwamba mlevi kupindukia lakini alimfungulia mlango na kumpa chakula.
v  Mwanamke amechorwa kama mwenye upendo,huruma na roho ya kutoa msaada.Wanawake watatu wametumiwa na mwandishi kujadili suala hili,mmoja wapo ni Jane rafiki yake na Mama Kulwa huyu aliwahurumia watoto wa marehemu rafiki yake akawatunza hadi naye alipofariki.
        Mwingine ni kula aliyemhurumia Peter wakati Doto alipompiga kule kwenye jaa la taka bila sababu.
        Pia  Zenabu aliyempa Peter chai na kipande cha mhogo baada ya kuhisi Peter alikuwa na njaa.

5.   Wizi,Ujambazi na Biashara ya Madawa ya Kulevya
Vitendo hivi vimeonyeshwa na mwandishi kwa kutumia wahusika Dani,Kulwa na Doto ambao walijiingiza katika wizi na ujambazi baada ya kukumbwa na umasikini, waliendakuvunja duka la Mhindi matokeo yake Dani na Doto wanapoteza maisha kwa kupigwa risasi na mlinzi wa duka hilo.
Kwa upande mwingine Musa baada ya kufukuzwa shule kwa kukosa ada na sare anaamua kutorudi tena shuleni na hivyo anajiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya tena anamshawishi na Peter kushirikiana naye hatimaye wanakamatwa na polisi na kuishia jela

MIGOGORO
v  Mgogoro kati ya Peter na Doto chanzo ni Doto kumpiga Peter na kumfukuza alipokwenda kutafuta riziki kule jalalani,suluhisho ni Kulwa kumuonyesha kaka yake kwamba hakufurahishwa na kitendo cha yeye kumpiga na kumfukuza Peter.
v  Mgogoro kati ya Zita na Kulwa ,chanzo ni Kulwa kwenda kukaa kwa akina Zita na Peter suluhisho ni Peter kuingilia kati na kumueleza Zita habari za yeye kuhusiana na Kulwa.
v  Mgogora wa nafsi,Kulwa ameonyesha akiwa anawaza juu ya maisha yake ya shida na jinsi alivyokosa mapenzi ya wazazi,hii ni baada ya Kulwa kuwaona watoto wawili wadogo wakiongozana na mama yao na kila mmoja akieleza anachotaka mama amnunulie mwandishi anasema Kulwa alifumbua macho moyo wake ukitoa chozi nafsi yake ikimsimanga na kumuuliza mama yuko wapi?vicheko na tabasamu zao ziko wapi?alikaa pale kwa muda.
MTAZAMO /FALSAFA
Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu,ana upeo mpana wa kuangalia mambo mfano halidhiki na hali walizonazo wakina mama hapa nchini ambapo wanahangaika usiku na mchana kufanya biashara ndogondogo ili kutunza familia zao.

UJUMBE
v  Uhalifu haulipi mema hivyo mtu anayetenda uhalifu hata kama kuna matatizo yanayomchochea kufanya hivyo mwisho wake hauwezi kuwa mzuri ndivyo ulivyotokea kwa wahusika Dani,Doto,Peter na Musa wakati Dani na Doto wanapoteza maisha kwa ujambazi Musa na Peter wanaishia jela
v  Wakina mamantilie wanakazi kubwa ya kulea familia hivyo jamii lazima iwasaidie kubeba mzigo huo
v   Ni muhimu wazazi wahusike katika malezi ya watoto wao
v   Ulevi si kitu kizuri hivyo jamii inayohitaji maendeleo ni lazima kupiga vita ulevi
FANI
WAHUSIKA
WAHUSIKA WAKUU
     Mamantilie(mama zita)
*      Ni mke wa mzee Lomolomo
*      Mama mzazi wa Zita na Peter
*      Anajihusisha na biashara ya kuuza chakula katika genge la urafiki
Mzee Lomolomo
*      Mume wa mama Zita
*      Baba yao Zita na Peter
*      Alikuwa mfanyakazi wa bandari kabla ya kufukuzwa kazi kutokana na ulevi
*      Ni mlevi wa mataputapu na gongo
Peter
*      Ni mtoto wa kiume wa mamantilie
*      Alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Mapepele kabla ya kufukuzwa shule na mwalimu Chikoya kwa kukosa ada na sare
*      Anapenda kusoma na alihangaika kupata ada na sare ili arudi shuleni lakini hakufanikiwa
*      Aligeuza jaa kuwa sehemu yake ya kupa riziki
*      Ni mwenye kulipa fadhila
*      Mwishowe alikamatwa pamoja na Musa na Kulwa kwa kuhusika katika biashara haramu ya madawa ya kulevya
Zita
*      Ni mtoto mwingine wa mzee Lomolomo
*      Kama kaka yake naye alifukuzwa shule kwa kukosa sare na ada
*      Anashirikiana na mama yake kuuza chakula katika genge la urafiki
*      Aling’atwa na mbwa lakini hakupata matibabu yoyote jambo lililopelekea kifo chake
WAHUSIKA WENGINE
Mwalimu Chikoya
v  Ni mwalimu mkuu wa shule ya Nkurumla
v  Aliwafukuza wanafunzi wake wote kwa kukosa ada na sare za shule

Kulwa na Doto
§  Watoto mapacha ambao hawakumjua baba yao
§  Waliishi kisutu kwenye banda chakavu(mbavu za mbwa)
§  Wana bahati mbaya kwani mama yao alifariki wakiwa wadogo
§  Maisha yao ya dhiki kwani waliishi kwa kutegemea dampo
§  Doto anajiingiza katika vitendo vya ujambazi na kupoteza maisha kwa kupigwa risasi
§  Kulwa anakwenda kuishi kwa mamantilie na hata hivyo anaishia jela baada ya kukutwa nyumbani kwa Musa ambaye alikuwa anfanya biashara ya madawa ya kulevya
Zenabu
*      Ni msichana ambaye ni rafiki na jirani wa mamantilie
*      Ni mfanyakazi wa klabu ya pombe panapoitwa “Kilale bar”
*      Ana roho nzuri kwani alikuwa anawahurumia watoto wa mamantilie
*      Ni yeye aliyekodi taksi kumpeleka Zita hospitali ya Muhimbili baada ya kuzidiwa
Musa
v  Ni mmoja wa wanajamii waliofukuzwa shule ya msingi Nkurumla kwa kukosa ada na sare
v  Naye hamjui baba yake amelelewa na mama tu
v  Hapendi shule kwani anaona inapoteza muda
v  Anamshawishi Peter aingie kwenye biashara ya madawa ya kulevya mwishowe wanaishia jela
Muundo
riwaya ya mamantilie ina muundo “rukia” kwani mwandishi anatuonyesha kisa Fulani kisha anarukia kisa kingine kile cha kwanza kabla hajakimalizia,mfano katika sura ya tatu mwandishi anatueleza ugeni wa mjomba aliyeleta taarifa/habari za ugonjwa wa mama yake mamantilie,anatuonyesha mamantilie anavyoondoka kwenda Matombo kumuona mama yake kisha anarudisha na kueleza habari za kuzaliwa na kukua kwa Kulwa na Doto
 Riwaya hii ina sura tano zenye vijisehemu vidogovidogo
 Mtindo
Mwandishi ametumia nafsi ya tatu umoja na wingi pia matumizi ya nafsi ya kwanza naya pili katika vipengele vichache na ametumia dayalojia(UK 86na 87)
Anatumia mtindo wa fasihi simulizi ambao umetokana na matumizi ya nyimbo,mfano wimbo ulioimbwa na mzee Lomolomo wakati anarudi kutoka kwenye pombe na wimbo ulioimbwa na watu wa mdundiko(UK 9)
Mwandishi ametumia mtindo wa kuchanganya lugha ya kiswahili na kiingereza “empire” “chloroguinea” “those wine”, “queen Elizabeth”
Matumizi ya Lugha
         Tamathali za Semi
   Tashibiha
v  .....akamshika mumewe kwa mko mmoja kama bua (ni maneno ya mwandishi jinsi mamantilie alivyomshika mumewe)
v  Mate yenye harufu kali ya gongo yalimtoka mdomoni kama cheche za moto.Mwandishi anaeleza mate yaliyomtoka Lomolomo mdomoni wakati aliporudi nyumbani akiwa amelewa
v  Akaanguka chini kama mgonjwa mamantilie alimwachia mumewe naye akaanguka chini
v  Hizo nywele zimekuwa kama kinda la ndege
v  Aliona ile miguu iliyopekupeku yenye ngozi ya mamba
v  Mikono yake ilifanya kazi kama mashine
v  Baridi ilipenya ngozini kama msumari
v  Mdomo wake ulikaa kama bakuli la pombe
v  Mate yake yalisafiri na kutua kama roketi na kutua kwenye sikio la Peter pale chini
v  Aliinamisha shingo nayo ikapinda kama tawi la mforosadi
v  Maumivu makali yalisambaa kama cheche
v  Moyo ukamerimerima kama donge la barafu
v  Zita alianguka chini kama gunia
Tashihisi
*      “.......Miguuni alivaa raba zilizochakaa kwa huzuni. mwandishi anaeleza raba aluzokuwa amevaa Dani zilivyochakaa
*      Koo lilimsaliti ,mwandishi ameeleza pale Kulwa alipotaka kulia kwa sauti
*      Alirudisha kamasi ndani zikakataa
*      Harufu ile ilimvaa,mwandishi ameeleza harufu aliyoisikia Kulwa alipoingia ndani
*      Alisukuma mlango nao ukamwitikia labeka
Takriri
Ø  “Nakuacha,nakuacha mamantilie alimwambia Lomolomo wakati anamuinua aingie ndani (UK 12)
Ø  “Baba,baba,amka baba Kulwa alimuita mzee Lomolomo baada ya kuona haamki (UK 91)
Ø  Twende,twende mamantilie alimwambia mzee Lomolomo wakati aliporudi kwenye pombe akiwa amelewa
Ø  Kukuru,kakara,kukuru,kakara wakati Zita na Peter wanapigana (UK 61)
Ø  Nivione ,nivione nivione vinafanya kazi gani ?Zita alimwambia Peter alipomuomba pesa za kumnunulia Kulwa dawa ya vidonda
TANAKALI SAUTI
v  “Fyzoooio”dereva wa land river alifyonza baada ya kukwarua mkia wa mbwa aliyemuumiza Zita
v  Alikohoa ukolio,oklio Lomolomo alikohoa wakati mkewe anamsaidia aingie ndani
v  Peter aliitikia salamu hizo za ukarimu kwa kupiga chafya mbili tatu.tcha,tcha,tcha
v  Paa,paa,paa bastola ililia wakati Doto na Dani walipopigwa risasi walipokwenda kuiba kwenye duka la themfula
Nahau
ü  “Kupiga usingizi”mlinzi Simango alikuwa amelala
Mdokezo
ü  “Una.....una......”
ü  We maazita.......una......una(Lomolomo alipotaka kuongea na mama Zita)
UJENZI WA TASWIRA
Mwandishi ametumia taswira za aina mbili
·         Taswira zinazoonekana
·         Taswira za hisi
v  Taswira zinazoonekana zimetumika pale mwandishi pale anapotumia mbwa mweusi mwenye mkia mweupe aliyemuumiza Zita na kusababisha mauti yake.
v  Pia hii inasawiri barabara mazingira ya uswahilini ambako mbwa,mifupa na uchafu mwingi hutupwa ovyoovyo
v  Taswira hisi ni pale mwandishi anaposema “hatua chache mbele yake sufuria ,vikombe na vyombo vingine aliona nzi wakirukaruka juu ya vyombo vile vichafu”
   Msomaji anaposoma sehemu hii anahisi kichefuchefu kwani msomaji atapata picha ya mazingira halisi waishio wakina mamantilie MANDHARI
Mwandishi ametumia mandhari ya mjini katika jiji la Dar-es-salaam. .Hii inathibitishwa na majina ya maneno kama Kisutu,Kiwanda cha Urafiki,Manzese,dampo la Tabata


JINA LA KITABU

WATOTO WA MAMANTILIE kama ilivyo jina la riwaya linasadifu yaliyomo kwani mwandishi amejaribu kueleza jinsi wazazi hawa wanavyoishi maisha ya shida wao na watoto wao
Share:

No comments:

Post a Comment

ONLINE VISITORS


Labels

Blog Archive

Recent Posts