KISWAHILI KIDATO CHA PILI








MADA YA SABA: USIMULIAJI WA MATUKIO
Usimuliaji wa Matukio
Njia za Usimulizi wa Matukio
Fafanua njia za usimulizi wa matukio
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea kwa namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.
Taratibu za usimulizi wa matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
  2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
  3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
  4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
  5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
  6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
  7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
  • Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi yasiyozodi aya moja.
  • Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
  • Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano, yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.



Share:

KISWAHILI KIDATO CHA PILI

                                    






MADA YA SITA: UANDISHI
Insha za Hoja
Insha za hoja ni insha zinazoelezea jambo fulani katika hali ya kujenga hoja ambazo zinatetea msimamo fulani alionao mwandishi wa insha hiyo juu ya jambo analolizungumzia. Hoja ni maelezo bayana yanayotolewa na mwandishi kutetea msimamo wake.
Katika uandishi wa insha za aina hii, mwandishi hutakiwa kuonesha ni jambo gani ambalo analiunga mkono na ni lipi ambalo hakubaliani nalo.
Ili hoja zote zipate kueleweka ni sharti zipangwe katika mtiririko wa mawazo ulio sahihi kiasi kwamba mtu aisomapo anapata kuelewa ni mada gani mwandishi anaijadili na ana msimamo gani kuhusu mada hiyo.
Muundo wa Insha za Hoja
Elezea muundo wa insha za hoja
Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
  1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
  2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.
  3. Kiini cha insha;katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.
  4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.




Barua Rasmi
Dhima ya Barua Rasmi
Elezea dhima ya barua rasmi
Barua rasmi ni barua zinazohusu mambo rasmi ya kiofisi. Dhima za barua rasmi ni kutoa taarifa, kuomba kazi au huduma, kuagiza vitu na kutoa mwaliko kwa mfano kwa kiongozi fulani wa nchi, kutoa malalamiko na kuweka kumbukumbu au marejeo.
Muundo wa Barua Rasmi
Elezea muundo wa barua rasmi
Barua rasmi au barua ya kiofisi/kibiashara huzingatia mtindo rasmi wa barua. Kwa kawaida huwa na sehemu zifuatazo:
  1. Anwani ya mwaandishi -huwekwa juu kabisa na huwa katika upande wa kulia wa karatasi.
  2. Tarehe ya barua hiyo- tarehe huandikwa chini ya anwani ya mwandishi
  3. Anuwani ya mpokeaji- Anwani ya anayeandikiwa huwa katika upande wa kushoto wa karatasi, na huwekwa msitari mmoja chini ya tarehe.
  4. Salamu- Chini ya anwani ya mpokeaji, barua huanza kwa kumrejelea mpokeaji kama bwana au bi. Ni makosa kumsalimia mpokeaji wa barua rasmi au kumwuliza hali yake.Ndugu Bwana Meshaki, => taja jina lake ikiwa mnajuana na unayemwandikia. Kwa Bw/Bi, => Ikiwa humjui mpokeaji wa barua, tumia bw/bi
  5. Mada- Kichwa cha barua rasmi huja pindi tu baada ya salamu. Hutangulizwa na maneno kama vile YAH:(yahusu). Ni sharti kichwa kiandikwe kwa herufi kubwa na kipigiwe mstari. Kichwa kinapaswa kuwa kifupi na kinachoelezea mada ya barua kiukamilifu.
  6. Utangulizi– Hukaa chini kidogo ya mada ya barua. Haya ni maelezo mafupi yasiyozidi aya moja ambayo huelezea kusudi kuu la barua kama kidokezo.
  7. Ujumbe- Ujumbe wa barua rasmi lazima uwe mfupi na unaotumia lugha rasmi.
  8. Tamati– mwandishi humalizia kwa maneno ya hitimisho kama vile: Wako mwaminifu, [jina], Sahihi
Simu
Dhima ya Simu ya Maandishi
Elezea dhima ya simu ya maandishi
Simu za maandishi ni aina ya barua fupi ambazo husafirishwa kwa haraka sana kuliko barua za kawaida.
Simu hizo huandikwa kwenye fomu maalumu ambazo hutolewa na shirika la posta. Simu za maandishi hujulikana kama telegram.
Kwa kawaida simu za maandishi hutumika kutuma ujumbe wa dharura. Kuandika simu za maandishi ni njia ya haraka ya kufikisha ujumbe kwa sababu, baada ya kuandika simu yako ujumbe humfikia huyo unayemtumia katika muda usiozidi siku tatu.
Gharama za simu za maandishi hutozwa kulingana na idadi ya maneno yaliyotumika. Kwa hiyo ujumbe unaotumwa huandikwa kwa maneno machache ili kuepuka kutozwa gharama kubwa.
Example 1
Mfano wa simu ya maandishi:
MUSA KINGAMBE SLP 5299 DSM
NJOO HARAKA
DADA MGONJWA LINGIDO
Kuandika Simu za Maandishi kwa Kuzingatia Muundo na Taratibu za Uandishi
Andika simu za maandishi kwa kuzingatia muundo na taratibu za uandishi
Muundo wa kuandika simu za maandishi una mambo yafuatayo ya kuzingatia ambayo ni anwani ya mpelekewa taarifa, ujumbe na jina la mwandishi au mtuma simu. Mambo mengine ya kuzingatia ni kuandika maneno yote kwa herufi kubwa ili kurahisisha usomaji na kuandika simu ya maandishi katika karatasi maalumu ambayo hutolewa na posta.
Activity 1
Andika simu za maandishi kwa kuzingatia muundo na taratibu za uandishi
Kadi za Mialiko
Kadi za mialiko ni aina ya karatasi ngumu zinazopeleka taarifa fupi za kumwomba mtu ahudhurie katika sherehe fulani kama vile harusi, ubatizo mahafali n.k
Muundo wa Kadi ya Mialiko
Fafanua muundo wa kadi ya mialiko
Mambo muhimu yanayotakiwa kuonyeshwa katika kadi ya mwaliko:
  1. Jina la mwandishi au mwalikaji
  2. Jina la mwalikwa, ni muhimu kuandika cheo chake kama vile: Profesa, Bi., Bw. Bw&Bi n.k
  3. Lengo la mwaliko
  4. Mahali pa kufanyika shughuli
  5. Tarehe ya mwaliko
  6. Wakati wa shughuli
  7. Jina na anwani ya mtu atakayepelekewa majibu.
Mialiko huweza kuandikwa kwa namna mbili yaani kama barua au kadi. Jina la mwalikwa katika kadi ya mwaliko hutakiwa kuanza na maneno ya heshima kama vile Bwana….Bi…..au Ndugu…ikiwa waalikwa ni mume na mke kadi itaanza na Bwana na Bibi.
Example 2
Mfano wa Kadi ya Mwaliko
Familia ya Manyama na Joseph
Wanapenda kukualika/kuwaalika Profesa/Dkt/Shekhe/Padri/Bi/Bw/Bw&Bi……… kwenye harusi ya kijana wao mpendwa Benny Joseph itakayofanyika huko Kiabakari katika ukumbi wa simba siku ya Jumapili tarehe 9/12/2016 sasa 8.00 mchana hadi saa 3.00 usiku
Kufika kwako ndio mafanikio ya sherehe hii.
Majibu kwa (wasiofika tu)
Emmanuel Joseph
Simu: 0786 67 54 62
Uandishi wa Dayalojia
Dhana ya Dayolojia
Elezea dhana ya dayolojia
Dayalojia ni mazungumzo au majibizano baina ya watu wawili au zaidi wanaozungumza kwa kupokezana. Kama zilivyo kazi nyingine za utunagaji, dayalojia inaweza kuwasilishwa kwa nijia ya mazungumzo au maandishi.
Katika kutunga dayalojia mtunzi hana budi kujifanya kama mhusika katika dayalojia hiyo. Kwanza anapaswa kutafakari kwa makini mada anayokusudia kuandikia dayalojia, kutayarisha na kupanga mawazo kimantiki na kwa mtiririko na kufikiria wahusika na kuwapangia majukumu kulingana na matendo yao. Kwa mfano kama mhusika ni mkulima, lugha anayopewa, vifaa anavyosemekana kuvitumia na mandhari aliyomo ni lazima vifanane na hali ya mkulima halisi.
Mambo ya kuzingatia katika dayalojia ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Kutoa maelezo ya ufafanuzi katika mabano ili kumfahamisha
  2. Kuwa na mazungumzo ya mkato na yasiyozidiana sana kati ya wahusika. Mhusika mmoja asitawale mazungumzo kupita wengine.
  3. Kutumia vihisishi ili kufanya dayalojia iwe ya kusisimua
  4. Pawepo mwingiliano wa mazungumzo ya wahusika na kudakia maneno ili dayalojia iwe na uhalisia.
Example 3
Mfano wa dayalojia
Wambura:
(Anaonekana mwenye furaha,anamwita rafiki yake, Anna)Wow, Anna! Tumekutana tena, siamini macho yangu! (wanakumbatiana wote wakiwa na nyuso za furaha).
Anna:
(Anatabasamu huku ameshikilia mkono wa kulia wa Wambura, anaonesha shauku kuu)Wambura! Bado unanikumbuka? Nina furaha sana kwa kweli, ni muda mrefu sana.
Wambura:
(Anachekelea)Aaaah, nahisi kama naota Neema, siamini kama nimekutana na wee leo hii ni muda mrefu sana, nimefurahi kwa kweli.
Anna:
(Anachekelea)
Wambura:
Mbona wachekelea tu….




Share:

KISWAHILI KIDATO CHA PILI









MADA YA TANO: UTUNGAJI WA KAZI ZA KIFASIHI
Kazi za fasihi simulizi hazikutokea tu, zilitungwa. Mtu fulani alikaa na akatunga kazi fulani ambayo inajulikana katika jamii. Katika mada hii utajifunza kanuni mbalimbli zinazohusika na utunzi wa kazi za fasihi simulizi. Pia utapata fursa ya kujifunza jinsi ya kutunga kazi mbalimbali za fasihi simulizi kama vile ngonjera, methali , nahau, vitendawili na kazi nyingine. Utajifunza pia kanuni zinazoongoza utunzi wa kila kazi ya fasihi simulizi.

Mashairi
Kanuni za Utungaji wa Mashairi
Fafanua kanuni za utungaji wa mashairi
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
  • Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?
  • Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je, ananuka mdomo?
  • Kuhisi: je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa bega unajisikia nini?
  • Kuonja: je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi au uchachu?
  • Kusikia: je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu. Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu, mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira yake.
Mwandishi baada ya kuzingatia mambo haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa.
Mashairi yana umbo ambalo huonekana kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo ni:
  1. Beti – Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
  2. Vina – Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni mwa sentensi.
  3. Mizani – Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
  4. Kituo – Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele vya fani katika mashairi
Vipengele vya fani katika shairi ni pamoja na:
  • Jina / anwani
  • Mandhari
  • Wahusika
  • Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia n.k
  • Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti unaofuatia.
Vipengele vya Maudhui kati mashairi
  • Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
  • Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza, kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza kutunga shairi lako la kwanza.
Kuigiza Ngonjera
Igiza ngonjera
Katika kuigiza ngonjera muigizaji hana budi kuzingatia fani yenye kanuni zifuatazo; mtindo wa mashairi ya kimapokeo, muundo wa mashairi ya kimapokeo wenye mizani, vina, vipande, mishororo na beti, kuteua mandhari kutegemeana na mada, kuwepo kwa wahusika wawili au zaidi au makundi mawili au zaidi na matumizi ya lugha ya kishairi.

Maigizo
Kanuni za Utungaji wa Maigizo
Elezea kanuni za utungaji wa maigizo
Maigizo ni tendo la kuiga sura, tabia, matendo na mazungumzo ya watu au viumbe wengine yaani kuiga jinsi walivyoumbwa, wanavyotembea, wanavyovaa, wanavyosema n.k
Kanuni na hatua za kutunga maigizo
  1. Kuchagua wazo, tendo, visa au tukio la kuigizwa:Ni lazima jambo hilo liwe na uzito, umuhimu au athari fulani katika jamii. Matukio hubainika kutokana na utafiti. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni kama vile matumizi mabaya ya simu za mkononi, mitindo ya mavazi, madhara ya uganga wa kienyeji, madhara ya UKIMWI n.k.
  2. Kuchagua muktadha au mahali pa kutendeka kwa jambo:Muktadha waweza kuwa ofisini, shuleni, kijijini, mjini, barabarani, kwenye daladala n.k
  3. Kuamua mtindo wa kuwasilisha jambo la kuigizwa:Hapa mtunzi anaweza kutumia fumbo, vichekesho, historia, tanzia n.k. Inashauriwa mtunzi kuchanganya mbinu ili kuongeza mvuto.
  4. Kupanga hoja kuu zinazojenga maudhui ya igizo:Maudhui hujikita katika migogoro au mivutano. Suluhisho la mivutano hupatikana pale migogoro inapofikia kilele. Kwa mfano jamabazi sugu anapokamatwa.
  5. Kuweka mpangilio wa maonyesho:Maonyesho hujumuisha vitendo na hoja zinazokamilisha sehemu inayobeba aina moja au zaidi ya maudhui. Sehemu kadhaa nazo hukaa zikajenga kitendo ambacho hubeba jambo mojawapo muhimu. Katika migawanyo hii yapasa mtunzi atunge kauli na vitendo vinavyoandamana navyo.
  6. Kubuni wahusika na kuweka aina au idadi yao kulingana na matukio:Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika wanaohitilafiana. Kwa mfano wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi n.k. Mtunzi akishawateua anaweza kuwatungia kauli na zamu za matendo katika sehemu mbalimbali.
  7. Ni muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua maleba yao:Uamuzi huu yapasa ufanywe kwa kuzingatia mazingira. Kwa mfano siku hizi sio lazima wahusika wazee kuvaa ngozi, kutumia mkongojo na kuvuta mtemba.
  8. Urefu wa maigizo ni suala la kuamliwa kutegemea tukio
  9. Kutunga maelezo kuhusu mandhari:Maumbile ya wahusika na vitendo vyao, ni muhimu kuelezwa katika mabano.
  10. Kuandika maigizo na kuhariri:Ni muhimu kutumia lugha ya kimazungumzo inayovutia, yenye kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleza maadili kwa mnato. 


Share:

KISWAHILI KIDATO CHA PILI










MADA YA NNE: UHIFADHI WA KAZI YA FASIHI SIMULIZI
Ili kitu kidumu ni lazima kihifadhiwe; fasihi simulizi kama sanaa kutokana na umuhimu wake katika jamii nayo huhufadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Katika mada hii utaweza kujifunza umuhimu wa fasihi simulizi katika jamii. Utajifunza njia mbalimbali zitumikazo katika uhifadhi wa fasihi simulizi pia utaweza kubainisha ubora na udhaifu wa kila njia.

Njia za kuhifadhi Fasihi Simulizi
Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Bainisha njia za kuhifadhi fasihi simulizi
Umuhimu wa kazi za fasihi simulizi
Ingawa kila utanzu wa fasihi una umuhimu wake, kwa pamoja tanzu zake zote zina umuhimu mkubwa katika jamii.
Kwaza fasihi hutumika kama chombo cha kuwaelimisha watu. Kupitia fasihi andishi na fasihi simulizi, watu hupata maarifa ya kutambua mambo maovu na namna ya kuyakwepa. Licha ya haya, wanajamii hujifunza njia za kujitawala, kuzalisha mali na kuishi kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia.
Pili, fasihi ni nyenzo ya kutoa mafunzo kuhusu mambo kama vile historia, dini, siasa, jiografia na tiba. Kwa hiyo watu hujifahamisha juu ya maumbile na asili yake, mazingira, utawala, uchumi, sheria n.k.
Aidha fasihi huwapa watu mazoezi na kuimarisha uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha, kuimba nyimbo kwa ufundi, kuigiza mambo kwa ustadi, kucheza ngoma kwa umahiri, kughani mashairi kwa mvuto na kusimulia matukio kwa mtindo ufaao.
Fasihi hufahamisha, huhifadhi na hurithisha mambo kuhusu utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo ni pamoja na mila, desturi, falsafa, imani na itikadi. Pia hudumisha maarifa ya kijadi kama vile tiba, sayansi ya kilimo, uhifadhi wa mazingira na sayansi ya utabiri wa hali ya hewa.
Umuhimu mwingine wa fasihi unatokana na kutumika kwake kama chombo cha kuburudisha na kupumbaza. Watu wanaposoma kazi mbalimbali za fasihi hupata, msisimko wa kimwili na kiakili. Kadhalika fasihi hugusa hisia za watu na kuwafanya wafurahi au wahuzunike.
Istoshe fasihi hudumisha na kukuza lugha. Watu hupanua msamiati wao na miundo ya lugha kupitia kazi zake. Hivyo fasihi inakuwa kama hazina ya maneno na dafina ya kanuni za kisarufi.
Kutokana na umuhimu huu ndio maana fasihi huhifadhiwa ili isipotee. Na uhifadhi huu hufanyika kwa njia mabalimbali.
Ubora na Udhaifu wa kila Njia ya Kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
Elezea ubora na udhaifu wa kila njia ya kuhifadhi kazi za fasihi simulizi
Fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:
Kichwani
Hii ndio njia ambayo imekuwa ikitumiwa kuhifadhi kazi za fasihi tangu kale na inaendelea kutumika hadi leo. Kwa kutumia njia hii kazi ya msanii hukaa kwenye ubongo wa msanii, naye huweza kuiwasilisha kazi hiyo, wakati wowote bila gharama yoyote.
Ubora wake
  • Uwasilishaji wa kazi hiyo unaweza kufanyika wakati wowote bila kuhitaji kufanyika maandalizi yoyote, hususani ya kiufundi.
  • Hakuna gharama yoyote wakati wa uwasilishaji wa kazi ya fashi. Msanii hahitaji kugharimia kitu chochote ili waweze kuitoa kichwani, ni uamzi wake tu, anaweza kuimba papo kwa papo.
  • Kazi ya fasihi iliyohifadhiwa kichwani ni hai. Hii ni kwa sababu msanii anakuwa ana kwa ana na hadhira yake. Kutokana na matumizi ya mbinu tofauti za kisanaa kama vile kucheza, kubadili sauti, miondoko na mengineyo mengi, kazi yake inapata uhalisia zaidi mbele ya hadhira.
Udhaifu wake
  • Uwezekano wa kazi kupotea au kuharibika hasa katika fani ni mkubwa. Kwa mfano msanii anapokuwa amefariki dunia kazi anayokuwa ameihifadhi kichwani nayo hupotea. Ndio maana katika baadhi ya jamii kazi za kifasihi zimepotea. Hii ni kwa sababu wasanii wanapoondoka duniani hondoka na fani hizo.
  • Kazi inapohifadhiwa kichwani ni rahisi kubadilika. Hii inatokea pale ambapo msanii anasahau baadhi ya maneno kutokana na umri wake au sababu nyinginezo
Njia ya maandishi
Maandishi ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhia kazi za fasihi. Njia hii imeanza kutumika baada ya watu kujua kusoma na kuandika. Uhifadhi wa kazi za fasihi kwa njia hii hupitia njia mbili kubwa. Hatua ya kwanza ni kubuni kisa au wazo; na hatua ya pili ni kuliweka wazo hilo katika maandishi. Kazi za fasihi simulizi zinazoweza kuhifadhiwa katika maandishi ni hadithi, nyimbo, mashairi, ngonjera, majigambo n.k
Ubora wake
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kudumu kwa muda mrefu
  • Kazi iliyohifadhiwa inaweza kufikia hadhira hata ya mbali na aliko msanii.
  • Kazi iliyohifadhiwa katika maandshi haipotezi fani yake na maudhui yake bali huendelea kuwa katika asili yake ya awali hadi msanii atakapoamua kuibadilisha.
Udhaifu wake
  • Hii njia ni kwa ajili ya watu wachache tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Wasanii wanaoweza kutumia njia hii ni wale tu wanaojua kusoma na kuandika.
  • Ni aghali sana kuhifadhi kazi za kifasihi kwa njia ya maandishi. Msanii atalazimika kununua vifaa vinavyohitajika katika maandishi ambavyo ni kalamu, karatasi, meza. Kwa hiyo ni aghali.
  • Uwasilishaji wake si hai kwani hakuna kuonana ana kwa ana kati ya hadhira na fanani. Kwa hiyo msomaji hawezi pata vionjo vya msanii hivyo itambidi ajibunie yeye mwenyewe.
  • Wahusika pia hawawezi kuonekana, endapo ni igizo mabalo limehifadhiwa katika maandishi, hivyo ubora wa kazi ya msanii huchujuka.
Njia ya vinasasauti
Vinasasauti ni miongoni mwa vyombo vinavyotumika kuhifadhi kazi za fasihi simulizi. Hii ni njia iliyoendelea kuliko ile ya maandishi.
Ubora wake
  • Kazi ya msanii huweza kuwafikia watu hata walio mbali na alipo mtunzi.
  • Ikihifadhiwa katika vinasasauti kama vile tepurekoda au CD ubora wake huwa haupotei wala kuharibika endapo vifaa hivyo vitatunzwa vizuri.
  • Sauti ya mtunzi unaiskia moja kwa moja
  • Unaweza kusikia vionjo vya msanii
Udhaifu wake
  • Njia hii ni aghali kutumia, kununua vinasasauti ni gharama.
  • Uwasilishaji wake si hai, ingawa unaweza sikia sauti ya msanii au wahusika lakini hahawezi kuonekana.
  • Kazi yoyote ya kifasihi inapohifadhiwa katika vinasasauti, kwa mfano nyimbo, huwa ni mali ya msanii husika, mtu yeyote haruhusiwi kuitumia kama mali yake binafsi bila kuruhusiwa na msanii.
Njia ya kompyuta
Njia hii imeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni baada ya watu kuanza kujua na mna ya kutumia kompyuta.
Ubora wake
  • Njia hii ni ya uhakika zaidi kwa vile shuguli za kisanaa zinazohusika huhifadhiwa katika kompyuta na hutolewa pale zinapokuwa zinahitajika.
Udhaifu
  • Msanii au wasanii wanohusika hawawasiliani na hadhira papo kwa papo. Hivyo hadhira hukosa kuuliza maswali katika vipengele vinavyotatiza.
  • Ili kuhifadhi kazi ya fasihi kwa kutumia njia hii ni sharti msanii awe anajua kutumia kompyuta.
  • Pia ni aghali sana, kuzingatia kwamba kununua komputa ni gharama kubwa.
Njia ya kanda za video
Msanii huweza kutumia kanda ya video kuhifadhi kazi yake.
Ubora wake
  • Kwanza wasnii na vifaa wanavyotumia huonekana
  • Sauti zao na milio ya ala wanazotumia husikika na pia huonekana kwa hadhira. Hii angalau huipa uhai kazi ya msanii mbele ya hadhira.
  • Huweza kudumu kwa muda mrefu endapo kanda ya video iliyotumika kuhifadhi kazi ya msanii itatunzwa vizuri.
Udhaifu wake
  • Uhifadhi wa njia hii ni aghali, msanii atahitajika kununua, kanda ya video, kumlipa mpiga picha na mzalishaji pia.
  • Watu wanoweza kunufaika na njia hii ni wacheche mno na wengi wao ni wale wenye uwezo wa kumiliki televisheni ambao kimsingi hupatikana maeneo ya mijini.
  • Ingawaje hadhira wanaweza kumwona msanii lakini hawawezi kuwasiliana nae ana kwa ana, hivyo kukosa kuuliza swali pindi wanapohitaji kufanya hivyo.
Umuhimu wa kuhifadhi kazi za Fasihi Simulizi
 Faida ya Kuhifadhi Fasihi Simulizi
Elezea faida ya kuhifadhi fasihi simulizi
Njia zote za uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi zina umuhimu mkubwa katika ukuzaji na uendelezaji wa utamaduni katika jamii. Kama ambavyo tumekwishaona, kazi za fasihi simulizi huelimisha, huburudisha, hurithisha maarifa, maadili, pia ni vielelezo vya utamaduni wetu wa asiili. Kwa ajili hiyo ni muhimu kuzihifadhi kazi hizo zisiharibike wala kupotea ili ziendelee kutumika kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ni muhimu ziendelee kuwepo ili kuhifadhi utamaduni wetu na huku vikitumika kama vivutio vya watalii.
Kazi za fasihi simulizi kwa upande mwingine ni sehemu ya ajira. Kwa mfano, shughuli mabalimbali za kisanaa kama vile ngoma, maigizo na utunzi wa vitabu, vinawapatia vipato baadhi ya wasanii. Hivyo ni muhimu zihifadhiwe.
Kazi za fasihi simulizi pia ni kichocheo cha umoja na maelewano miongoni mwa jamii. Yote hayo kwa ujumla wake yanabainisha kuwepo na haja ya kuendelea kuzikusanya, kuzifanyia kazi, kuziendeleza, na kuzihifadhi kazi za fasihi simulizi.



Share:

ONLINE VISITORS


Labels

Recent Posts