
MADA YA KWANZA: KUONGEZA MSAMIATI WA KISWAHILI
Uundaji
wa Maneno
Lugha hukua na kubadilika kila
wakati kulingana na maendeleo ya jamii. Kigezo kimojawapo cha kukua na
kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa msamiati. Ili msamiati uongezeke katika
lugha sharti maneno mapya yaundwe.
Njia
za Uundaji Maneno
Uundaji wa Msamiati hutokea kwa njia
mbalimbali zifuatazo:
- Kubadili mpangilio wa herufi.
- Kuambatanisha maneno.
- Kutohoa maneno ya lugha nyingine.
- Uambishaji wa maneno.
- Kufanikisha sauti, umbo, mlio na sura.
Kuunda
msamiati kwa kubadili mpangilio wa herufi
Neno hujengwa kwa vitamkwa au
herufi. Neno jipya lenye maana tofauti huweza kuundwa kwa kubadili mpangilio wa
neno lingine
Mfano
- Neno lima, lina herufi l, i, m, a, herufi hizi huweza
kujenga maneno kama mali, kumi,imla, mila.
- Neno tua lina herufi t, u, a, herufi hizi zina weza
kujenga maneno kama:- tatu, tua, viatu, tatua.
Njia
ya kuambatanisha maneno
Kuna njia tatu za kuambatanisha
meneno
Njia ya kurudufisha au kukariri neno
Mfano; barabara, sawasawa, polepole, katikati,
vilevile.
Njia ya uundaji wa Msamiati kwa
kuunganisha maneno mawili tofauti
Nomino na Nomino
- Punda + mlia unapata Pundamilia
- Bibi + Shamba unapata Bibishamba
- Afisa + Elimu unapata Afisaelimu
- Mwana + Siasa unapata Mwanasiasa
- Bata + maji unapata Batamaji
Kuunganisha kitenzi na Nomino/Jina
- Changa + moto changamoto
- Chemsha + bongo chemshabongo
- Piga + mbizi pigambizi
- Zima + moto zimamoto
Kuunganisha maneno mawili na
kudondosha baadhi ya herufi
Mfano
- Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA
- Mzaliwa wa mahali Fulani MZAWA
- Chama cha Mapinduzi CCM
- Nyamamfu NYAMAFU
Kutohoa maneno kutoka lugha nyingine
Kila lugha na tabia ya kuchukua
maneno lugha nyingine ili kukidhi mahitaji ya Msamiati. Maneno kutoka lugha
nyingine yanapoteuliwa hubadilishwa kimatamshiili ya fuate kanuniza Kiswahili.
Maneno yanayotoholewa kutoka lugha
nyingine husanifishwa na asasi za lugha ya Kiswahili ndipo ya ruhusiwe kutumiwa
rasmi.
Mfano
Neno la Kiswahili
|
Lugha ya Mwanzo
|
Neno Lililotoholewa
|
Kijerumani
|
Schule
|
|
Salama
|
Kiarabu
|
Salaam
|
Duka
|
Kihindi
|
Dukan
|
Karoti
|
Kiingereza
|
Carrot
|
Shati
|
Kiingereza
|
Shirt
|
Picha
|
Kiingereza
|
Picture
|
Papai
|
Kihispania
|
Papaya
|
Meza
|
Kireno
|
Mezi
|
Shukrani
|
Kiarabu
|
Shukran
|
Ngeli
|
Kihaya
|
Engeli
|
Ikulu
|
Kinyamwezi
|
Ikulu
|
Ng'atuka
|
Kizanaki
|
Ng'atuka
|
Ndafu
|
Kichaga
|
Ndafu
|
Namba
|
Kuunda maneno kwa njia ya uambishaji
wa maneno
Hii ni njia ya kubandika viambishi
awali na tamati kwe nyekiini. Ujenzi wa maneno hutokana na mzizi mmoja kuonesha
maana tofauti ingawa maana zina husiana.
Mfano mzizi: -lim-.Tukipachika
viambishi awali na tamati tunapata maneno kama lima, analima, walilima, kilimo,
limiana,halitalimwa na ukulima.
Kufananisha sauti, sura au tabia
Example 4
Mfano
- Kengele - utokana na sauti ya kengele inapo pigwa
- Pikipiki - hutokana na muungurumo wa pikipiki
- Ndizi mkono wa tembo – Ndizi inayo fananishwa na mkono
wa mnyama tembo
- Chubwi - Jiwe au chura atumbukiapo katika kina cha
maji.
Mazingira yanayoelezea Kuhitaji Maneno Mapya
Mabadiliko mengi yanatokea kila siku
katika nyanja mbalimbali za kimaisha-mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kisayansi
na kiteknolojia. Katika mazingira kama haya, watu watahitaji kuwasiliana, lugha
itahitaji kuunda maneno ili kuwasilisha dhana mpya zilizoibuka. Kwa mfano,
maneno kama vile nywila, kisakuzi, udukuzi, puku, talakirishi n.k yameundwa ili
kuwasilisha dhana za kiteknoljia kwa Kiswahili.
Undaji wa Maneno katika Miktadha mbalimbali
Mabadiliko ya kimaendeleo yanafanya
lugha ihitaji maneno ya kuyafikisha na kutumiwa na jamii. Ili kukidhi mahitaji
hayo, maneno mapya yanazuka. Maneno hayo yanaweza kuwa katika fani mbalimbali,
kama vile sayansi na teknolojia, siasa, utamaduni na uchumi kulingana na mkondo
wa maendeleo. Mfano wa msamiati ni kama vile fedha, ushuru, kumpyuta, ukoloni,
hospitali, suruali n.k
MADA YA PILI: UENEAJI WA KISWAHILI ENZI ZA WAINGEREZA NA
BAADA YA UHURU
Ukuaji na ueneaji wa Kiswahili katika enzi ya Waingereza
Mambo waliyochangia Waingereza
katika Ukuaji wa Kiswahili nchini Tanzania
Waingereza walipochukua koloni la
Tanganyika kutoka kwa Wajerumani walikuta Kiswahili kimeimarika na kinatumika
katika maeneo mengi ya nchi. Kwa kuwa nao walihitaji kutawala hawakupuuzia
matumizi ya Kiswahili katika utawala wao japo hawakutumia Kiswahili kwa lengo
la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila ya wao kukusudia.
Waingereza walitumia Kiswahili kama
nyenzo ya kusaidia shughuli zao za kiutawala. Hata hivyo kuna mambo waliyofanya
waingereza yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama
yafuatayo:
Shuguli
za kiuchumi
Shuguli za kiuchumi wakati wa
Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa klimo, Waingereza
waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali, na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua
kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua hao walijulikana kwa jina la manamba.
Katika mkusanyiko wa vibarua hawa
waliokuwa na usuli wa makabila tofautitofauti, lugha pekee iliyoweza
kuwaunganisha ni Kiswahili ikizingatiwa kwamba Kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha
rasimi katika mawasiliano ya kiutawala. Walilazimika kuzungumza Kiswahili kwani
bila hivyo mawasiliano yasingeweza kufanyika kwa urahisi.
Hata hivyo kupitia shuguli za kilimo
maneno mapya ya Kiswahili yaliweza kuzaliwa, kwa mfano: yadi, belo, belingi,
bani, mtama n.k, kwa hiyo kupitia shughuli hizi Kiswahili kilizidi kukua.
Shuguli
za kiutamaduni
Shughuli hizi ni kama vile uigizaji
wa tamthiliya za kigeni, uchezaji wa mziki wa kigeni hususani twisti.
Tamthiliya za kigeni zilikuwa zikiigizwa majukwaani kwa lugha ya Kiswahili na
hivyo ikasaidia kukua kwa msamiati wa Kiswahili.
Shughuli
za kidini
Wakati wa utawala wa mwingereza pia
kuliambatana na ujio wa wamishonari waliokuwa na lengo la kueneza dini ya
kikristo.
Katika harakati hizi walitumia lugha
ya Kiswahili ili kufanikisha malengo yao ikizingatiwa kwamba Kiswahili kilikuwa
kimeshaenea vya kutosha wakati wa utawala wa Mjerumani, kwa hiyo wamishonari wa
Kiingereza waliendelea kukiimarisha zaidi.
Pia shughuli za kidini zilipelekea
kutafsiriwa kwa vitabu mbalimbali vya kidini kama vile Biblia na vitabu
vingine. Tafsiri ya vitabu hivi ilikuwa ni kutoka katika lugha ya kiingereza
kwenda katika lugha ya Kiswahili. kwa kufanya hivi Kiswahili kiliweza kuingiza
msamiati mwingi sana na hivyo kukuza lugha ya Kiswahili.
Wamishonari walilazimika kujifunza
Kiswahili hukohuko kwao ili wanapokuja huku Afrika Mashariki wasipate tabu ya
kujifunza Kiswahili. Kwa sababu hii wamishonari waliokuwa wamekwishajifunza
lugha ya Kiswahili walitunga kamusi za Kiswahili – Kiingereza ili kuwasaidia
wenzao pia kujifunza Kiswahili; kwa njia hii waliweza kukikuza Kiswahili.
Shughuli
za kisiasa
Shughuli za kisiasa hasa katika
uanzishwaji wa vyombo mbalimbali vya kiutawala, jeshi, polisi, mahakama, boma
n.k. Kufuatia uanzishwaji wa vyombo hivi msamiati mwingi wa Kiswahili uliweza
kuzuka na hivyo kukuza Kiswahili.
Shughuli
za kiutawala
Makampuni ya uchapishaji
yalianzishwa (East African literature Bureau), na kamati ya lugha iliundwa
(Interterritorian language committee). Hatua hii iliimarisha matumizi ya lugha
ya Kiswahili hali iliyosaidia kukua kwa lugha ya Kiswahili.
Shuguli za ujenzi wa reli na
barabara
Shughuli hizi pia zilisaidia kuibuka
kwa msamiati mpya kama vile, reli, stesheni, tiketi n.k.
Usanifishaji
wa Kiswahili
Usanifishaji wa lugha ya Kiswahili
pia lilikua ni jambo jingine muhimu sana lililosaidia kukua kwa msamiati wa
Kiswahili. Lengo la usanifishaji wa Kiswahili lilikuwa ni kuleta ulinganifu wa
matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki.
UENEAJI WA KISWAHILI
Ukuaji na Ueneaji ni maneno mawili
yenye maana zinazokaribiana lakini zinazotofautiana. Ukuaji humaanisha ongezeko
la msamiati katika lugha na ueneaji ni uongezekaji wa matumizi ya lugha kieneo.
Kwa hiyo hapa tutaangalia yale mambo yaliyosababisha Kiswahili kitumike katika
eneo kubwa. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vilivyokuwepo kwa
wakati huo ni redio, magazeti na majarida mbalimbali. Kwa upande wa redio
kulikuwepo na redio Tanganyika iliyoanza kurusha matangazo yake kwa kutumia
lugha ya Kiswahili. Na magazeti yaliyokuwa yakichapishwa wakati huo ni pamoja
na: Mambo leo, Sauti ya Pwani, Kiongozi na Habari za leo. Magazeti haya yote
yalikuwa yakichapishwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kwa kutumia vyombo vya
habari (redio na magazeti) kiswahili kiliweza kuenea.
Kilimo
Kupitia kilimo watu waliweza
kukutana pamoja, watu wa makabila tofautitofauti. Kwa hiyo katika kipindi chote
walichokaa kwenye makambi ya mashambani waliweza kujifunza Kiswahili na
walipomaliza muda wao walirudi nyumbani wakiwa wamejifunza lugha mpya na hivo
kwa njia hii waliweza kuieneza lugha ya Kiswahili.
Muundo wa jeshi la kikoloni (KAR)
Jeshi la KAR liliundwa na watu
kutoka makabila mablimbali, na lugha iliyokuwa ikitumika jeshini ni Kiswahili,
askari hawa walisaidia kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kwani
kila walipokwenda walikuwa wakizungumza Kiswahili.
Mfumo wa elimu
Chini ya utawala wa Waingereza
Kiswahili kilitumika katika masomo yote kwa ngazi ya shule ya msingi, na pia
kilitumika kama somo kwa ngazi ya shule za sekondari. Kwa hiyo hii pia
ilichangia kuenea kwa lugha ya Kiswahili
Harakati za kudai uhuru
Chama cha TANU kilianzisha harakati
za kudai uhuru, harakati hizo ziliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo
kupitia harakati hizo Kiswahili kiliweza kuenea kwa kiwango kikubwa.
Tathimini ya maendeleo ya Kiswahili wakati wa Waingereza
Licha ya maendeleo ya lugha ya
Kiswahili katika utawala wa Waingereza, pia kulikuwa na changamoto
zilizoikabili lugha ya Kiswahili katika kupiga hatua ya maendeleo. Changamoto
hizo ni kama zifuatazo:
Kutofundishwa kwa Kiswahili shule
zote nchini
Wakati wa utawala wa Waingereza
Kiswahili kilifundishwa katika shule za watoto wa kiafrika tu, wakati katika
shule za watoto wa kizungu Kiswahili hakikufundishwa. Kwa hiyo suala hili
lilifanya Kiswahili kipewe msukumo mdogo sana na hivyo kuhafifisha ukuaji wake.
Kutotumika kwa Kiswahili kama lugha
ya kufundishia
Lugha ya Kiswahili ilitumika
kufundishia katika shule za msingi pekee ilihali lugha ya kiingereza ilitumika
kuanzia shule za sekondari hadi elimu ya juu. Hali hii ilisababisha watu
kujitahidi sana kujifunza kiingereza; kwa kuzungumza kiingereza ilikuwa na
ishara kwamba wewe ni msomi, na hivyo kutokana na hali hii Kiswahili kilendelea
kukua polepole sana.
Kukosekana kwa vyombo vya kizalendo
vya kukuza Kiswahili
Vyombo vilivyokuwa vinahusika na
masuala ya ukuzaji wa Kiswahili wakati wa ukoloni vilikuwa vimeanzishwa na
wakoloni wenyewe, kwa mfano Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki
(Inter-Territorial Swahili Language commitee) na Shirika la maandiko la Afrika
Mashariki (East African Literature Bureau). Katika hali kama hii ukuzaji wa
Kiswahili ulikosa msukumo mkubwa wa kizalendo.
Kasumba ya kuthamini Kiingereza
Wananchi walikuwa na kasumba kwamba
mtu anayezungumza Kiingereza alichukuliwa kuwa ni mtu mwenye maendeleo na
msomi, kwa hiyo hali hii ikapelekea watu kutothamini Kiswahili na hivyo
Kiswahili kudharaulika.
Ukuaji na Ueneaji wa Kiswahili baada ya Uhuru
Shughuli mbalimbali zinazowezesha
Kukua na Kuenea kwa Kiswahili nchini
Baada ya uhuru kuna harakati
mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kukiendeleza na
kukikuza kiswahili. Harakati hizo ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi
1962. Mkwaka 1964 kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na kuwa
kitatumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa mfano katika elimu
hususani elimu ya msingi.
Kuundwa kwa Chombo cha usanifishaji
ambacho kilikuwa na kazi ya kuhimiza maendeleo ya kiswahili, kutayarisha kamusi
na vitabu mbalimbali vya sarufi na fasihi ya lugha ya kiswahili na kuandaa
wataalamu watakaoshughulikia usanifishaji wa Kiswahili
Pia baada ya uhuru kulianzishwa
Taasisi mbalimbali zitakazoshughulikia lugha ya kiswahili. Mfano:- BAKITA,
TUKI, TUMI, UKUTA, UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaamu.
Baada ya uhuru nchini Tanzania
kiswahili kilienea kwa kasi kubwa sana. Kuna sababu mbalimbali ambazo
zilichangia kukua na kuenea kwa kiswahili hapa nchini. Baadhi ya sababu hizo ni
pamoja na kuteuliwa kwa kiswahili kuwa lugha ya Taifa, Kiswahili kitumike
katika Elimu, mfano kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi. Kuundwa
kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na kuneza kiswahili, Kiswahili kuwa Lugha
rasmi na lugha ya Taifa, shughuli mbalimbali za kidini, shughuli za kisiasa na
kiutawala na shughuli za kiutamaduni na uchapishaji wa vitabu na majarida
mbalimbali.
Kiswahili kuwa lugha ya taifa
Baada ya uhuru mwaka 1962 kamati
iliundwa ili kuangalia uwezekano wa kutumia kiswahili katika shughuli zote rasmi,
mfano bungeni na shughuli zote za kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha
ya taifa 1964 ambapo katika shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa kutumia
lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano
yote hasa katika shughuli za umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili
kiliendelea kupanda hadhi zaidi wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani
azimio hilo lilitungwa na kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
Kuundwa kwa vyombo vya ukuzaji na
uenezaji wa Kiswahili
Tanzania baada ya uhuru ilifanya
jitihada za kuunda vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza Kiswahili katika
nyanja mbalimbali mfano wa vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA, TUKI, Taasisi ya
Elimu, TAKILUKI na Chama cha Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Kutumika katika elimu
Kiswahili licha ya kutumika katika
shughuli mbalimbali za kiserikali, kilipendekezwa kutumika katika shule za
Msingi na kufundishwa katika elimu ya sekondari kama somo na katika vyuo vikuu
wanatoa shahada mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia katika Elimu ya watu
wazima ambao hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza masomo
mbalimbali kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua kusoma,
kuandika na kuzungumza lugha ya kiswahili fasaha. Kampeni hii ilikuwa kwa nchi
nzima ambapo walijifunza elimu ya Afya, Siasa, Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa
lugha ya Kiswahili na kuwafanya watu wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
Vyombo vya habari
Tangu uhuru ulipopatikana kuna
vyombo mbalimbali vya habari vilivyoanzishwa. Vyombo hivi hutumika kueneza
kiswahili kwa kiasi kikubwa na hufikiwa na watu wengi licha ya kuwepo kwa
changamoto za kiuchumi. Vyombo hivyo ni magazeti na majarida mbalimbali ambayo
huandikwa kwa lugha ya kiswahili lakini kuna redio na runinga ambazo matangazo
yake hutangazwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kukifanya kiswahili kuenea kote
ndani na nje ya nchi.
Biashara
Shughuli za kibiashara nchini
husaidia kuenea na kukua kwa kiswahili kutokana na kuwepo kwa makabila tofauti
tofauti ambapo wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa lugha ya kiswahili.
Hivyo kiswahili hudumishwa na kutumika katika biashara hizo.
Shughuli za siasa na utawala
Tangu wakati wa harakati za
kupigania uhuru kiswahili kimetumika kama nyenzo muhimu kuwaunganisha wananchi.
Shughuli za kisiasa zimetumia lugha hii katika kujiimarisha; mfano wakati wa
chama kimoja, Azimio la Arusha na Mfumo wa vyama vingi Kiswahili kimetumika
kama njia kuu ya mawasiliano. Pia katika utawala chama kinachotawala kimekuwa
na harakati za kukiendeleza kiswahilli katika nyanja zote. Ambapo kiswahili
kimekuwa kikitumika katika shughuli zote za kiutawala. Hivyo shughuli za
kisiasa na kiutawala zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza, kukieneza na
kukiendeleza kiswahili.
Uandishi na uchapishaji wa vitabu
Kuibuka kwa waandishi wa vitabu
mbalimbali vya kiswahili vya sarufi na fasihi ambavyo vilichambua kwa kina
mambo mabalimbali yahusuyo lugha ya kiswahili na utamaduni wake, mfano :- F
Nkwera, Shabani Robart, Mathias Mnyapala na Shaffi Adam Shaffi. Waandishi
wengine chipukizi walijitokeza na wanaendelea kujitokeza katika tasnia hii ya
uandishi wa vitabu.
Shughuli za kiutamaduni
Shughuli za kiutamaduni zimechangia
kueneza kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Shughuli hizo ni pamoja na
harusi, misiba, matanga na sherehe mbalimbali za kijamii ambazo zimesaidia
kukiendeleza Kiswahili kwa kuwa huwakutanisha watu tofautitofauti katika
shughuli hizo, ambapo huwalazimu kutumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano
na kufanya kiswahili kuendelea. Pia katika Sherehe mbalimbali vikundi vya sanaa
na muziki vinavyotumia lugha ya kiswahili kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa
nyimbo zao kwa ajili ya kukieneza Kiswahili.
Vyombo vya Ukuzaji na Uenezaji wa Lugha ya Kiswahili
Tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa
kuna vyombo kadha wa kadha vilivyoanzishwa kwa ajili ya kukuza na kueneza
Kiswahili baadhi ya vyombo hivyo ni hivi vifuatavyo:
BAKITA
Hii ni taasisi ya serikali iliyoundwa
kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza Kiswahili.
Kutokana na sheria hii Baraza ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala
wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
BAKITA imekuwa na mchango mkubwa
sana katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia majukumu yake.
Majukumu ya Baraza kama yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni haya yfuatayo:
- Kuratibu na kusimamia maendeleo na matumizi ya
Kiswahili nchini kote.
Katika kufanya hivi Baraza lina jukumu la kuhakikisha Kiswahili
kinaendelea na kuhakikisha kuwa matumizi ya Kiswahili yanakuwa sahihi.
- Kushirikiana na vyombo vingine nchini vinavyojihusisha
na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao. Vyama vya Kiswahili kama vile CHAKAMA, CHAWAKAMA vina
mchango mkubwa wa kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na
BAKITA. Ushirikiano wa BAKITA na vyama hivi waweza kuwa ni wa kuto
ushauri, au msaada wa kifedha, kwa mfano BAKITA imekuwa ikiwasaidia CHAWAKAMA
pale wanapokuwa wanataka kufanya makongamano nap engine wanahitaji msaada
wa kifedha, kwa hiyo BAKITA imekuwa ikiwasaidia kifedha.
- Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na
za kawaida. BAKITA imekuwa ikiandaa
vipindi mbalimbli redioni ili kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya
Kiswahili.
- Kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuthibitisha
tafsiri sanifu za istilahi.
Katiaka uundaji wa istilahi, BAKITA imekuwa ikichapisha vitabu mbalimbali
ikionesha istilahi sanifu zilizoingizwa katika lugha ya Kiswahili. kwa
hiyo kupitia jukumu hili Kiswahili kimekuwa kinakua.
- Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa serikali,
mashirika ya serikali na yasiyo yaserikali na asasi nyingine. Kupitia tafsiri zinazofanywa na BAKITA Kiswahili
kimekuwa kikikuwa na kuenea.
- Kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi
ya Kiswahili. Machapisho haya ya BAKITA
yanaendelea kukifanya Kiswahili kukua kwa kuongeza msamiati mpya na hivyo
watu wanaposoma machapisho hayo wanajifunza msamiati mpya na hivyo kufanya
Kiswahili kukua.
- Kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu
binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza
Kiswahili nchini Tanzania.
- Kutoa ushauri kwa waandishi na wachapishaji ili watumie
Kiswahili fasaha. Kwa kufanya hivi matumizi
bora ya Kiswahili yanakuwa yanaimarika.
- Kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kuthibitisha vitabu vya Kiswahili vitakavyotumika shuleni na vyuoni kabla
havijachapishwa. Hili pia ni jamabo
linaloimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.
TAKILUKI
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mwaka 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza lugha
ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar, ili kutimiza lengo hilo TAKILUKI
inajishughulisha na kazi zifuatazo:
- Kuratibu na kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili
visiwani Zanzibar, kuendesha mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa wazawa na
wageni, kuhariri miswada mbalimbali ili kuthibitisha ufasaha wa Kiswahili
na kufanya tafiti za Kiswahili katika Nyanja zake zote, hususani katika
uwanja wa sarufi na fasihi.
- Pia TAKILUKI wana kazi ya kuandaa istilahi za taaluma
mbalimbali, kutoa huduma za taaluma mbalimbali, kutoa huduma za tafsiri na
ukalimani kwa lugha mabalimbali kwa mashirika, idara, wizara, taasisi,
kampuni na watu binafsi, kufundisha lugha za kigeni na kuandika vitabu
mbalimbali vya Kiswahili.
- Pia hujishughulisha na utoaji wa ushauri wa kitaaluma
kwa watunzi wa vitabu ili waweze kuandika kazi zenye ubora, na
kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili kama vile, mashirika, wizara,
taasisi, vyuo na watu binafsi katika kuendesha shuguli za ukuzaji wa
Kiswahili, mathalani kuandaa na kuendesha semina, warsha na kozi fupifupi
za Kiswahili.
- Vilevile hujishugulisha na usimamizi na ufuatiliaji wa
matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari na katika
shughuli mbalimbali za serikali na za kawaida.
TUKI/TATAKI
Majukumu ya TUKI ni pamoja na kuunda
sera muafaka za kustawisha Kiswahili na pia kufanya utafiti katika lugha ya
Kiswahili.
Majukumu mengine ya TUKI ni
kuhariri, kuchapisha vitabu na kutawanya vitabu na majarida ya kitaaluma katika
Kiswahili.
Kwa sasa TATAKI inatoa shahada ya
awali na uzamili katika lugha ya Kiswahili, kwa njia hii inawaandaa wataalamu
wa lugha ya Kiswahili ambao watatumika sehemu mbalimbali za ulimwengu
kufundisha lugha ya Kiswahili.
CHAUKIDU
CHAUKIDU ni kifupi cha Chama cha
Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, makao makuu ya chama hiki kwa sasa yapo chuo
kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani
Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni:
Kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea
kasi ya malengo mahususi yafuatayo:
- Kukuza Kiswahili
katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na
kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa
ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu,
uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika
Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.
- Kusambaza habari na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya
mtandao wa kompyuta juu ya vipengele mbalimbali vya Kiswahili na masuala
yanayohusiana na Kiswahili.
- Kuwajumuisha wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao
katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.v. uboreshaji wa
ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa
kila mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya
mtandao.
- Kuelimisha umma
juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.
- Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa
kutambua thamani iliyobebwa na maliasili hii ili kuunda sera muafaka za
kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya serikali na
watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k.
CHAWAKAMA
CHAWAKAMA husimama badala ya Chama
cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki. Chama hiki kilianzishwa
mwaka 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika
Mashariki kupitia wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki
ni wale wanosoma Kiswahili na hata wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia
wanaweza kujiunga na chama hiki.
Chama hiki kina utaratibu wa kuandaa
makongamano ambapo wanachama wake kutoka nchi zote za Afrika Mashariki hupata
fursa ya kukutana mara moja kila mwaka. Pamoja na utaratibu wa chama kuandaa
makongamano pia uanzishwaji wake umeambatana na malengo kadhaa ambayo ndiyo
dira inayoiongoza chama kwa mujibu wa katiba, malengo hayo ni haya yafuatayo:
- Kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha,
kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili.
- Kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa lugha ya
kiswahili.
- Kueneza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
- Kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za
kuendeleza na kuimarisha lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi
wanachama.
- Kuwaunganisha wanafunzi wa kiswahili Afrika Mashariki
na kati katika kukikuza kiswahili.
- Kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na
ukuzaji na uenezaji wa kiswahili ndani na nje ya nchi kama vile BAKITA,
TATAKI, TAKILUKI, UWAVITA, CHAKAMA, BAKIZA n.k.
- Kuchapisha kijarida cha chama na machapisho mengine ili
kusaidia kueneza taaluma ya kiswahili.
- Kuweka kumbukumbu ya wataalamu wa kiswahili kwa nia ya
kuwatumia katika kufanikisha malengo ya chama na wadau wa Kiswahili.
- Kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali
inayohusiana na taaluma ya kiswahili.
Pamoja na malengo hayo, lengo kuu la
chama hiki ni kueneza Kiswahili lakini sasa wanakienezaje? Wanachama wa chama
hiki ambao ni nchi wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki wanakawaida ya
kuandaa makongamano kwa ngazi ya kitaifa na ngazi ya kimataifa.
Kwa ngazi ya kitaifa kila nchi
huandaa kongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote kutoka vyuo
mbalimbali katika nchi husika. Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinazohusu
lugha ya Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio
mbalimbali huchukuliwa juu ya maendeleo ya chama. Sasa katika mijadala kama hii
inatoa nafasi ya Kiswahili kukua kwani makala mbalimbali huandikwa ambazo pia
husomwa na watu mbalimbali. Makala hizi pia zimekuwa zikichapishwa katika
majarida ya chuo husika na pia zimekua zikichapishwa mtandaoni ambapo hutoa
fursa kubwa kwa watu wengi zaidi kuzifikia na kusoma, hivyo kwa njia hiyo
Kiswahili kinakua kimeenea.
Dhima ya kila Asasi inayokuza Kiswahili
Mafanikio na Changamoto
Zinazovikabili Vyombo vya Ukuzaji wa Kiswahili
Mafanikio
- Vyombo vya ukuzaji wa Kiswahili vimejitahidi sana
kukuza lugha ya Kiswahili, kwa hali ya Kiswahili ilivyo sasa ni matokeo ya
juhudi za vyombo hivyo. Mafanikio ya vyombo hivyo ni pamoja na haya
yafuatayo:
- Machapisho ya lugha ya Kiswahili ni mengi sana nchini
na nje ya nchi, kufanya mafunzo ya Kiswahili, kukua kwa matumizi ya
Kiswahili na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Kiswahili nchini.
- Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sehemu rasmi hasa
katika ofisi za serikali na ofisi za watu binafsi inadhihirisha mafanikio
ya jitihada za vyombo hivi kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili.
- Kufundshwa kwa lugha ya Kiswahili kama taaluma kwa
ngazi ya shahada ya awali, uzamili na uzamivu. Hizi ni jitihada za TATAKI
katika kuhakikisha kunapatikana wataalamu wa lugha ya Kiswahili, hivi sasa
TATAKI wanafundisha lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya shahada ya awali,
uzamili na uzamivu.
- Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo
mabalimbali vya kimataifa, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vikao vya
Umoja wa Afrika na pia ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika vyo
mabalimbali Duniani ni ishara tosha ya kuonesha mafanikio ya jitihada za
vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili.
Changamoto
- Vyombo hivi vinakabiliwa na upungufu wa wataalam.
Wataalamu wengi waliobobea katika taaluma za Kiswahili wanakimbilia nje ya
nchi wakidhani huko ndiko kuna maslahi mazuri zaidi.
- Upungufu wa fedha za kuendeshea shughuli za ukuzaji wa
Kiswahili katika vyombo hivi pia limekuwa ni tatizo sugu. Kwa hiyo
shughuli za ukuzaji wa Kiswahili zinakuwa zinakwenda taratibu.
- Taasisi hizi pia zinashindwa kujitangaza vizuri kutokana
na kwamba hazina vyombo vya habari binafsi ambavyo vingeweza kutumika
kutangaza shughuli zao. Jambo hili limesababisha vyombo hivi kushindwa
kutoa elimu ya Kiswahili kwa kutumia vyombo vya habari kutokana na kwamba
gharama za kufanya hivyo ni kubwa.
- Vyombo hivi baadhi havina ofisi za kudumu, na hivyo
kuhamahama jambo ambalo linaathiri utendaji kazi wa vyombo hivyo.
No comments:
Post a Comment