
MADA YA NNE: KUTUNGA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Utungaji wa Mashairi
Mambo ya Kuzingatia katika Utungaji
wa Mashairi
Utungaji/uandishi wa kubuni ni ule
unatokana na hisia ambazo zinamsukuma mtunzi ili atunge kazi yake. Hisia
zinaungana na wazo ambapo vitu hivyo vinamsumbua akilini na kumkosesha raha.
Mwandishi wa kubuni anataka aliwasilishe wazo lake ili hadhira ifahamu
kilichopo moyoni mwake. Mwandishi hukosa usingizi na hivyo hulazimika kuamka na
kuandika kile kinachomsukuma akilini mwake.
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi
atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo
ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
- Kuona:
je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la
kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni
makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?
- Kunusa:
pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je,
ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je,
ananuka mdomo?
- Kuhisi:
je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au
huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa
bega unajisikia nini?
- Kuonja:
je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina
pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi
au uchachu?
- Kusikia:
je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose
usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti
ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au
kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu.
Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa
kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana
nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha
yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu
waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama
yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na
mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya
udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu,
mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije,
anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya
ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue
kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata
hadhira yake.
Mwandshi baada ya kuzingatia mambo
haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika
utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua
dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata
maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi
kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi
hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo
yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao
huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo
nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa
Mashairi yana umbo ambalo huonekana
kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha
shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo
ni:
- Beti
– Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
- Vina
– Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni
mwa sentensi.
- Mizani
– Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
- Kituo
– Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha
bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika
kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho
maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni
mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama
ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila
mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele vya fani katika mashairi
Vipengele vya fani katika shairi ni
pamoja na:
- Jina / anwani
- Mandhari
- Wahusika
- Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia
n.k
- Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina,
kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti
unaofuatia.
Vipengele vya Maudhui kati mashairi
- Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe,
falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
- Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza,
kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza
kutunga shairi lako la kwanza.
MADA YA
TANO: ANDISHI
Uandishi wa Insha za Kiada
Insha ni kifungu cha maandishi
kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika kujadili juu ya mada
fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au kuishadidia mada hiyo.
Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za kisanaa) na insha za
kisanaa.
Insha za kaida ni insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo
mbalimbali katika jamii, mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia
n.k.
Muundo wa Insha za Kaida
Katika uandishi wa insha, muundo
wake unakuwa na vitu vifuatavyo:
- Kichwa cha insha;
kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa
mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k
- Utangulizi;
Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno
muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika
insha yako.
- Kiini cha insha;
katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika
insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya
hoja ulizonazo katika mjadala wako.
- Hitimisho;
hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha
au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.
Mambo ya kuzingatia katika uandishi
wa insha
Taratibu za uandishi zinapozingatiwa
insha pia itasomeka vizuri na pia itakuwa na mtiririko mzuri wa mawazo.
- Epuka kutumia vifupisho vya maneno visivyo rasmi.Uandishi wa insha ni suala rasmi, kwa hiyo katika
uandishi wake inatakiwa kuzingatia kuepuka kutumia vifupisho ambavyo sio
majumui yaani havijulikani. Kwa mfano maandishi kama, xamahani (samahani),
ckatai (sikatai) na mengine yafananayo kama hayo ni lazima yaepukwe katika
uandishi wa insha.
- Andika utangulizi unaovuta umakini wa msomaji. Hiki ni kipangele cha muhimu sana, msomaji anapoona
kwamba kwenye utangulizi hakuna kitu kinachomvutia hataendelea kuhangaika
kusoma insha hiyo.
- Andika kiini cha insha kwa mpangilio mzuri Unatakiwa kuandika insha yako katika mpangilio mzuri
huku kila wazo kuu likipewa aya yake na kuwepo na mtiririko mzuri wa
mawazo.
- Andika hitimisho la insha likiwa linahitimisha mawazo
yaliyokwishajadiliwa katika kiini.Hakikisha
unapofanya hitimisho epuka kudokeza wazo jipya ambalo linazua mjadala
mpya, hakikisha hitimisho lako linabeba mawazo uliyokwisha yajadili katika
insha yako na wala yasiwe mawazo yanayotoka nje ya kile ulichokijadili.
Uandishi wa Hotuba
Hotuba ni insha ambayo hutoa maneno
halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani.
Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi
kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake.
Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi
wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira
katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k
ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo.
Muundo wa Hotuba
Hutuba inakuwa na muundo ufuatao:
Anwani
Anwani, mada au kichwa cha hotuba
hurejelea mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.
- Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa
wananchi.
- Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
Utangulizi
- Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano
(hadhira).
- Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha
juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki
kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
- Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia
hadhira isiyokujua au wageni.
- Tanguliza mada yako.
Kwa mfano:
Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya,
Mhe. Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha Mazingira, mabibi na mabwana. Ni
matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi
cha Mazingira na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote
tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa …
Kiini
- Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi
mwisho
- Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia
wala si wa taarifa.
Tamati
- Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
- Unaweza kumaliza kwa shukurani
Uandishi wa Risala
Risala ni hotuba fupi inayosomwa
mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi,
wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa maelezo ya haja zao
mbalimbali na mahitaji yao au kuonyesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.
Muundo wa Risala
Utanguizi
- Cheo cha kiongozi anayehusika
- Kundi linalowakilishwa
Kiini
- Maelezo ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi
linalowakilishwa.
- Mapendekezso na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Hitimisho
- Shukrani
Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni hotuba fupi lakini
inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe huwa ni maelezo ya
muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika hotuba. Utungaji wa
risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo wazi kueleweka kwa
kiongozi.
Mfano wa risala:
Ndugu Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi
wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha
nne, tunayo heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika
siku hii muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo
yetu hapa shuleni.
Shukrani zetu za pekee na za dhati
ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa
kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema; kwasababu tupo tofauti
sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.
Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato
cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo
tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47.
Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali
zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu kidato cha nne.
Ndugu mgeni rasmi, elimu hii ya
kidato cha nne imetupatia msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia
imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na
kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo
mbalimbali kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu
ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla,
pia tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa, usalama katika mazingira
yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda. Vilevile
tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa
kuinua uchumi wetu wa taifa.
Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo
yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu
tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani
ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana
walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu ya Taifa ya
kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.
Ndugu mgeni rasmi, tumepata
changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama
ifuatavyo;
Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto
ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea
vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).
Ndugu mgeni rasmi, changamoto
nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii inapelekea kuchangia kifaa
kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.
Ndugu mgeni rasmi, pia kuna
changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea
kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.
Ndugu mgeni rasmi, pia kuna
changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya
wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi
wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.
Ndugu mgeni rasmi, maji ni changamoto
hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua
maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile
usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata
magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.
Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya
vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu
mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia
hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote
tunayocheza hapa shuleni.
Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru
uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika
kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule
imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna
upungufu mkubwa wa vifaa.
Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini
kwamba maombi yetu umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe
unaweza kupitia Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.
Mwisho tunaomba msamaha wa dhati
toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda
kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo,
tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.
Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru
sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi
ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.
Uandishi wa kumbukumbu za Mikutano
Kumbukumbu za mikutano ni rekodi
zinazowekwa na katibu wa mkutano wakati mkutano unapoendelea ili kuhifadhi
yanayojadiliwa na kukubaliana katika mkutano huo. Katibu anapaswa kufuatilia
mtindo maalum wa kuandika kumbukumbu hizo kulingana na mpangilio katika
mkutano.
Mambo
ya Kuzingatia katika Uchukuaji wa Kumbukumbu za Mikutano
Mambo ya kuzingatia katika uandishi
wa kumbukumbu ni kama yafuatayo:
- Kichwa cha kumbukumbu
– Kichwa cha kumbukumbu kinapaswa kutaja mambo yafuatayo: Ni mkutano wa
akina nani? Unaandaliwa wapi? Unaandaliwa lini? Unaanza saa ngapi? Mfano
wa Kichwa cha Kumbukumbu: Kumbukumbu za Mkutano wa Shirika la Msalaba
Mwekundu Shuleni ulioandaliwa tarehe saba Agosti 2001 katika Ukumbi wa
Mikutano kuanzia saa Tisa alasiri.
- Waliohudhuria
– Andika orodha ya wote waliofika kwenye mkutano huku kuanzia na yule mwenye
cheo cha juu zaidi hadi kwa wanachama. Pia onyesha vyeo vyao.
- Waliotoa Udhuru -Hawa
ni wale walioomba ruhusa kutohudhuria mkutano
- Waliokosa kuhudhuria -
Hawa ni waliokosa kuhudhuria mkutano, bila kutoa udhuru)
- Waalikwa -
Hawa ni wageni walioalikwa katika mkutano, k.v mlezi wa chama, afisa wa
kiutawala, n.k)
- Ajenda -orodhesha
hoja zitakazorejelewa katika mkutano huo
Kuandika kumbukumbu
KUMB 1
|
Kumbukumbu ya kwanza huwa ni
kufunguliwa kwa mkutano na ujumbe kutoka kwa mwenyekiti.
|
KUMB 2
|
Kusomwa kwa kumbukumbu za mkutano
uliotangulia na kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo kwa kutiwa saini.
|
KUMB 3
|
Maswala yanayoibuka kutokana na
kumbu kumbu zilizosomwa. (Kumbuka kutaja nambari ya kumbu kumbu hizo)
|
KUMB kuendelea
|
Maswala katika ajenda
|
KUMB ya Mwisho
|
Maswala mengineyo yasiyokuwa
kwenye orodha ya ajenda.
|
Tamati
|
Kufungwa kwa mkutano. Taja mkutano
ulifungwa saa ngapi; mkutano ujao utakuwa tarehe ngapi; kisha acha nafasi ya
kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo katika mkutano utakaofuatia.
|
Mfano
KUMBUKUMBU ZA MKUTANO WA CHAMA CHA
KISWAHILI ULIOANDALIWA KATIKA CHUMBA CHA MIJADALA TAREHE 24 JUNE 2013 KUANZIA
SAA TATU ASUBUHI
Waliohudhuria
- Teddy Mbogela – Mwenyekiti
- Vaileth Matiko – Mweka hazina
- Iliashibu Masatu – Mkuu wa utafiti
- Funk Kiduku – mwanachama
- Meta Mkorofi – katibu
Waliotuma Udhuru
- Bahatika Mashauri – Naibu Mwenyekiti
- Ponea Kamgazi – Msimamizi wa Mijadala
Waliokosa Kuhudhuria
- Zebedayo Chisege – Spika
- John Kumbikumbi – mwanachama
Waalikwa
- Mnoko Nokwe – Mwanahabari
- Dkt. Fikirini– Mlezi wa Chama.
Ajenda
- Uchapishaji wa jarida la Kiswahili
- Shindano la kuandika insha.
- Kusajili wanachama wapya
KUMBUKUMBU 3/04/14 – KUFUNGULIWA KWA
MKUTANO
Mwenyekiti aliwakaribisha wanachama
wote na baada ya kuwatambulisha wageni, akawaomba washiriki wawe huru kuchangia
katika ajenda mkutano huu ili kuboresha chama.
KUMBUKUMBU 7/04/14 – KUREJELEA
KUMBUKUMBU ZA MKUTANO ULIOPITA
Katibu alisoma kumbukumbu za mkutano
wa mwezi Machi. Kumbukumbu zilikubaliwa na wanachama wote na kuthibitishwa na
mwenyekiti pamoja na katibu kwa kutia saini.
KUMBUKUMBU 10/04/14 – MASWALA IBUKA
KUTOKANA NA KUMBUKUMBU ZILIZOSOMWA
Mweka hazina alifahamisha mkutano
kwamba aliongea na mkuu wa idara ya Kiswahili kuhusu ufadhili kama tulivyokuwa
tumekubaliana katika KUMB 9/03/10 ya mkutano uliopita.
KUMBUKUMBU 12/04/14 – HAFLA YA
KISWAHILI
Iliripotiwa kwamba hafla ya
Kiswahili ambayo wanachama walikuwa wamealikwa kuhudhuria katika Shule ya
Sakata Academy haingeweza kufanyika kutokana na tamasha la muziki lilizokuwa
linaendelea katika shule hiyo. Wanachama waliokuwa wamejitayarisha kwa mashairi
waliombwa kuendelea kujifunza ili wayawasilishe muhula wa pili.
KUMBUKUMBU 15/04/14 – UCHAPISHAJI WA
JARIDA LA KISWAHILI
Wanachama walikubaliana:
- Kwamba chama kitaanza kuchapisha jarida la Kiswahili
- Kwamba jarida litakuwa likichapishwa mara moja kila
muhula na kuuzwa shuleni
- Kwamba kila mwanachama atachangia katika kuandika
makala na kuuza nakala za jarida hilo.
- Kwamba paneli ya wahariri lingeundwa ili kuongoza idara
ya uchapishaji
- Kwamba hazina ya chama ina fedha za kutosha kuzindua
uchapishaji huo.
KUMBUKUMBU 17/04/14 – SHINDANO LA
KUANDIKA INSHA
Kila muhula wa pili, chama huandaa
shindano la kuandika insha ambalo wanafunzi wote hushiriki. Insha
zilizopendekezwa mwaka huu ni:
- “Jadili chanzo cha migomo shuleni na namna ya
kusuluhisha.”
- … … … … … … … … …
- … … … … … … … … …
- … … … … … … … … …
KUFUNGWA KWA MKUTANO
Mkutano ulifungwa saa kumi na nusu,
baada ya maswala yote kujadiliwa. Mkutano unaofuatia ulipoangwa kuwa tarehe
ishirini mwezi Mei, katika Ukumbi wa Muziki.
KUTHIBITISHWA KWA KUMBU KUMBU
______________
|
_____________
|
Mwenyekiti
|
Katibu
|
Tarehe:________
|
Tarehe:________
|
No comments:
Post a Comment