
MADA YA TATU: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Uhakiki wa Ushairi, Tamthiliya na Riwaya
Dhana ya Uhakiki
Fafanua vipengele vya uhakiki
Uhakiki ni kitendo cha kutathmini,
kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na
kaida maalum. Kwa kiwango cha elimu ya sekondari mhakiki anafanya kazi ya
uhakiki ili kuonesha mambo yanayojitokeza kama vile, dhamira, migogoro, ujumbe,
falsafa, mtazamo, msimamo n.k
Dhima ya Mhakiki na Nafasi ya Mhakiki
Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango
mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo:
- Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi;Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi
ya lugha na taswira, hivyo mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia
msomaji kuelewa vipengele hivi kwa kuvifafanua kwa lugha rahisi.
- Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi;Mhakiki anapoonesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi
fulani, watunzi wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora
zaidi.
- Uhakiki hukuza uelewa wa mhakiki; Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki
hujiongezea maarifa ya lugha pamoja na mambo yanayotokea katika jamii.
Nafasi ya Mhakiki
Mhahiki ana nafasi kubwa katika kazi
za fasihi, Mhakaki ndiye anafafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kumwelewa
vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo hapa mhakiki anasaidia kurahisisha mawasiliano
kati ya hadhira na mtunzi.
Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi
ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya
kazi bora zaidi.
Hatua za Kufuata wakati wa Kufanya
Uhakiki
Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi
ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya
kazi bora zaidi.
Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi;
hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya fasihi kwa kina na kuielewa
vizuri.
Pili ni kuainisha na kuchambua mambo
muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo katika vipengele vya fani na maudhui.
Tatu ni kutoa tathimini au kuelezea
ubora na udhaifu wa kazi inayohusika.
UHAKIKI WA MASHAIRI
Shairi ni utungo wa kisanaa wenye
mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu
mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani.
Mashairi yapo ya aina mbili:
- Mashairi huru
- Mashairi ya arudhi
Mashairi ya arudhi
Haya ni mashairi yanayofuata kanuni
za kimapokeo au arudhi za utunzi wa mashairi. Arudhi/kanuni hizi ni pamoja na:
- Kugawika kwa shairi katika beti
- Beti kuwa na idadi maalum ya mishororo.
- Mishororo ya ubeti kugawika katika vipande
- Mishororo kuwa na ulinganifu wa mizani
- Shairi kuwa na urari wa vina
- Shairi kuweza kuimbika / kuwa na mahadhi au mapigo.
- Kuwepo kwa kipokeo katika shairi
- Kuwa na mtiririko wa mantiki na mawazo au muwala
- hairi kuwa na utoshelezo wa beti / kujisimamia kimaana.
Mashairi huru
Pia hujulikana kama mashairi ya
kimapinduzi. Haya ni mashairi yasiozingatia lazima ya arudhi na hivyo huwa na
muundo huru. Sifa zake kuu huweza kuwa:
- Lugha ya muhtasari
- Lugha yenye mahadhi
- Lugha ya kisanii iliyo na mafumbo na taswira
- Mara nyingine hugawika katika beti.
- Mishororo kamilifu (inayojitosheleza) na ile isiyo
kamilifu (mishata)
Sifa za Mashairi
Mashairi huwa na sifa maalum
zinazoyatambulisha kama kazi ya kishairi, yawe ya kimapokeo au kimapinduzi.
Sifa hizi ni kama vile:
- Mashairi hutumia lugha ya mkato / muhtasari
- Ni sanaa au kazi iliyobuniwa kwa ufundi
- Huwa na mpangilio maalum kuanzia mistari hadi beti.
- Hutumia lugha teule na msamiati teule uliosheheni
tamathali, taswira na jazanda.
- Mashairi huwa na sifa ya kuweza kuimbika hivyo shairi
ni wimbo na wimbo ni shairi.
Dhima ya mashairi
- Kupasha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya upole na mvuto
- Kuelimisha na kuzindua jamii.
- Kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi.
- Kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na Sanaa ya
fasihi.
- Kuburudisha hadhira na wasomaji.
- Kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo
Hatua za uhakiki wa mashairi
- Soma shairi polepole na kwa makini kupata maana ya
jumla.
- Soma shairi tena kwa utaratibu ukizingatia maneno na
vipande mbalimbali na kuchunguza maana ya kila mojawapo
- Pitia maswali yote kwa makini ukitilia maanani aina ya
majibu yanayotarajiwa.
- Soma shairi tena ukipigia mstari kwa penseli sehemu
zinazoelekea kujibu maswali.
- Toa majibu kamilifu kulingana na swali kwa lugha ya
mtiririko.
Vipengee vya Uchambuzi Wa Mashairi
- Anwani/kichwa cha shairi – Huwa ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi
moja. Anwani ni kidokezo muhimu cha kinachozungumziwa katika shairi.
Anwani huweza kuwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya
kibwagizo. Ikiwa shairi halina anwani, basi lipewe anwani inayoafikiana na
maudhui au dhamira kwasentensi isiyozidi maneno 6.
- Maudhui
– Haya ni masuala makuu au mambo muhimu yanayohusu mwanadamu au mazingira
yake yanayozungumziwa katika shairi. Kwa mfano: malezi, siasa,
usalama, unyanyasaji, ufisadi n.k. Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi
kutokana na kisa kilichomo katika shairi.
- Dhamira / shabaha -
Ni lengo kuu la mshairi katika kusanifu utungo wake. Dhamira ya mtunzi
huwa ni ujumbe kwa kifupi anaoutambua msomaji kutokana na mwelekeo wa
usemaji wa mtunzi katika shairi. Mfano: Baada ya kusoma shairi,
unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli kuwa uongozi mbaya
haufai, misitu ni uhai n.k. Dhamira hutokana na
mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.
- Mbinu na tamathali za lugha - Ni mbinu za uandishi na tamathali za usemi
zilizotumiwa na mshairi katika shairi. Mfano:Mazda / ziada / zidi -
kurefusha maneno;enda kuwa enenda. Inksari / muhtasari - Ni
kufupisha maneno;aliyefika kuwa alofika. Utohozi – Mbinu ya
kugeuza msamiati / maneno ya lugha geni ili yaandikike na kutamkika kana
kwamba ni ya Kiswahili. Mfano: Time - taimu; One – Wani. Mbinu hii
vilevile huitwa ukopaji au uswahilishaji.
Taarifa Muhimu za Mwandishi wa kila Kitabu
Mwandishi wa fasihi ni mtu anaeweza
kubuni kazi ya fasihi na kuiweka katika maandishi. Unaposoma kazi za fasihi ni
lazima ujue taarifa muhimu za mwandishi wa kazi hiyo, ambazo ni jina, kwa
sababu kila utakapokua unajibu swali ni lazima utaje jina la mwandishi wa
kitabu. Falsafa na utamaduni kujua msimamo wake, na muundo kujua mpangilio wa
matukio, mtindo kujua upekee wake na matumizi ya lugha.
No comments:
Post a Comment