
MADA YA SITA: UFAHAMU
Ufahamu wa Kusikiliza
Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya
kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya
maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano
mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa
hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake
mwenyewe.
Kujibu Maswali ya Habari
Uliyosikiliza
Ufahamu wa kusikiliza unahusisha
michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa.
Michakato hii inahusisha:
- Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa
- Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza
- Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa
namna zinavyowasilishwa.
Katika ufahamu wa kusikiliza,
msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo:
- Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili
kuweza kusikia kila anachokisema.
- Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo
msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha
hoja.
- Msomaji anatakiwa kuandika baadhi ya mambo anayoona
kuwa ni ya muhimu ili kumasidia kukumbuka hapo baadae.
- Kuwa makini na ishara mbambali za mwili kama vile
kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho.
Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika
mazungumzo.
Kufupisha Habari
Ili kuandika ufupisho mzuri wa
habari uliyoisikiliza yafuatayo hayana budi kuzingatiwa; kusikiliza habari kwa
makini ili kuielewa vizuri, kuandika mawazo makuu yanayojitokeza katika kila
aya, kuyaunganisha mawazo makuu na kuiandika habari kwa maneno yako, kuhesabu
idadi ya maneno kama inazidi na kuandika idadi hiyo mwisho wa ufupisho upande
wa kulia chini kidogo.
Zoezi
Soma habari kisha toa ufupisho wake
Ufahamu wa Kusoma
Ufahamu wa kusoma ni ule mtu
anaoupata kwa njia ya kusoma makala, kifungu cha habari, kitabu au gazeti.
Kujibu Maswali kutokana na Habari
ndefu uliyosoma
Kuna vipengele viwili vinavyounda
mchakato wa ufahamu wa kusoma:
- Uelewa wa msamiati na
- Uelewa wa matini
Ili kuilelewa habari/matini ni
lazima msomaji awe na uwezo wa kuelewa msamiati uliotumika katika matini hiyo.
Endapo maneno yaliyotumika hayataeleweka vilevile matini yote hataeleweka.
Katika ufahamu wa kusoma, msomaji
anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
- Kubaini mawazo makuu;
msomaji anaposoma habari fulani au kitabu inatakiwa ajiulize, Je,
kinachoongelewa hapa ni nini? Ni jambo gani hasa analolizungumzia
mwandishi? Msomaji akiwa na maswali haya akilini mwake basi itakuwa rahisi
kwake kuielewa habari hiyo.
- Kuzingatia alama za uakifishi; msomaji ni lazima azingatie alama za uakifishi, kwa
kufanya hivyo itamsaidia kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo
hatazingatia alama za uakifishaji anaweza kupotosha maana ya mwandishi.
- Kubaini maana ya maneno na misemo mbalimbali; habari nyingine huwa zina maneno ya kisanaa hivyo ni
muhimu msomaji kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari
hiyo, hii itamsaidia kuelewa vyema maana ya mwandishi.
- Vilevile msomaji anatakiwa kumakinikia kile
anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.
Kwa kuzingatia haya yote msomaji
atakuwa na uelewa mzuri juu ya habari aliyoisoma na pia anaweza kufupisha
habari hiyo aliyoisoma.
Kufupisha habari
Kufupisha habari ni kuandika upya
habari uliyoisoma kwa maneno machache lakini bila kupotosha ujumbe wa habari ya
kwanza.
Ufupisho wa habari huwa na sifa
hizi:
- Huwa ni mfupi kuliko habari ya mwanzo
- Huwa na ujumbe uleule uliokuwa katika habari ya mwanzo
- Hujumuisha mawazo makuu yaliyodondolewa kutoka kwenye
habari ya mwanzo
- Mawazo haya sharti yapangwe katika mtririko wenye
mantiki
Hatua za kufuata katika kuandika
ufupisho
Ili kuweza kufanikiwa kufupisha
habari kwa ufanisi hatua zifuatzo sharti zifuatwe:
- Kuisoma au kuisilikiza habari kwa makini ili kuielewa
vizuri
- Kutambua na kubaini mawazo makuu yanayojitokeza katika
kila aya
- Kuyaunganisha mawazo makuu na kuandika au kuelezea
ufupisho wa habari hiyo kwa maneno yako mwenyewe bila kupostosha maana ya
habari ya kwanza.
- Kuhesabu idadi ya maneno ya ufupisho ili kuyapunguza
ikiwa yanazidi idadi iliyotakiwa.
- Kama muda unaruhusu pitia tena habari ya mwanzo na
pitia tena ufupisho ili kujiridhisha kuwa hujaacha taarifa yoyote ya
muhimu.
Kufupisha Habari ndefu uliyosoma
Ili kuweza kuandika ufupisho wa
habari ndefu uliyoisoma hatua zifuatazo sharti zifuatwe, kusoma habari kwa
makini na kuielewa vizuri, kubaini mawazo makuu, kuandika ufupisho wa habari
kwa maneno yako, kuhesabu idadi ya maneno na kupunguza yaliyozidi na kupitia
tena habari ya mwanzo na ya mwisho kama muda unaruhusu. Aidha ufupisho wa
habari huwa ni mfupi na una ujumbe uleule wa habari ya mwanzo.
No comments:
Post a Comment