KIDATO 3 $ 4-KISWAHILI- UCHAMBUZI WA RIWAYA


UHAKIKI WA RIWAYA
 RIWAYA YA TAKADINI
Mwandishi : BEN HANSON
Mchapishaji : Mathews bookstore

UTANGULIZI
TAKADINI ni riwaya inayoeleza maisha ya jamii za kiafrika na tamaduni zake.Riwaya hii  inaeleza namna jamii nyingi za kiafrika zinavyowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye ulemavu kutokana na mila potofu.Katika riwaya hii mwandishi amemtumia kijana Takadini aliyezaliwa sope alivyowakilisha waathirika wa mila hizo potofu.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU ; UKOMBOZI
Mwandishi ameeleza kuwa ili tuweze  kupata ukombozi wa kweli na kujenga jamii mpya tunapaswa kuachana na mila potofu na kukomboka kifikra na kiutamaduni.Miongoni mwa mila hizo ni mauaji kwa watu wenye ulemavu.Takadini alizaliwa sope aliamriwa auawe  siku ya pili tu toka atoke tumboni mwa mamaye Sekai.
  Aidha makwati anasikitika baada ya kuletewa taarifa kuwa mtoto aliyezaliwa ni sope anasema.....hilositalielewa......itakuwaje....aliuliza maswali mengi (uk 12).Bila ngozi?,Sope?ni nini ulichokileta hapa kwetu?  maswali haya yanaonyesha namna walemavu wasivyothaminiwa.Suala hili lilimsononesha sana Sekai inaonyesha dhahiri mtoto sope katika jamii ya Makwati hakustahili kuishi.
  DHAMIRA NDOGO NDOGO
1.   MAPENZI
Mwandishi anaonyesha mapenzi katika sura mbili tofauti yale ya dhati na ya uongo.Mapenzi ya dhati hayachagui hali wala mali pia kabila dini wala rangi.Kila mtu ana haki ya kupendwa na kupenda ,
v  Mapenzi ya dhati kati ya Sekai na mwanae ,Sekai alikuwa radhi auawe ilimradi furaha yake itimie ya kubaki na mwanawe sope,hakuogopa kufa alimlinda takadini na kuamua atoroke baada ya makwati kuruhusu wazee wamwangamize
v  Mapenzi ya dhati kati ya Sekai na Tendai  hawa ni marafiki wa kweli  walifarijiana baada ya kuelezana matatizo yao,Tendai mke mdogo wa mtemi masasa aliyelazimishwa kuolewa na mzee wa rika la baba yake.
v  Mapenzi ya dhati  kati ya Mzee Chivero na Sekai,mzee Chivero alimpokea Sekai na mwanawe Takadini na kuwachukulia kama wanawe (familia yake) licha ya wanakijiji wengine kuwatenga
Mapenzi ya dhati baina ya Takadini na Shingai ,Shingai alimpenda Takadini licha ya kuwa na ulemavu wa ngozi (sope) pia mlemavu wa mguu (alitembea kwa msaada wa gongo) kama anavyokiri mwenyewe “huyu ndiye mwanaume ninayetaka anioe”
Mapenzi ya uongo ni baina ya Makwati na Takadini ,Nhamo na Shangai ,Sekai na wake wenza isipokuwa Pindai
2.   NDOA ZA MITARA
Mwandishi ameeleza athari za ndoa za mitara kuwa ni pamoja na chuki baina ya wanawake na hivyo kusababisha migogoro ndani ya familia.Mfano Sekai anasengenywa na wake wenza wake Dedirai,na Rumbidzai na kudai ni mchawi
 Aidha wake wa Mtemi Masasa wanamdharau Tendai na kuchukulia kama mtoto wao na si mke mwenzao kwa sababu ya umri wake mdogo
3.   MILA POTOFU
Dhamira hii imetazamwa katika sura tofauti kama vile:-
v  Wazazi kuwachagulia watoto wao wenza (wake/waume)Tendai na Shingai wanalazimishwa kuolewa na watu wasiowataka,hii ni mila potofu zilizopitwa na wakati.
v  Mauaji kwa walemavu ,mwandishi anaonyesha kuwa watu wenye ulemavu hawakustahili kuishi katika himaya  ya akina Makwati na mtemi Masasa na ndiyo maana kuzaliwa na kuishi kwa Takadini kulileta mzozo.
4.   NAFASI YA MWANAMKE
Jamii nyingi za kiafrika zinamkandamiza mwanamke na kumfanya mtu duni katika Nyanja mbalimbali za maisha,kama ifuatavyo;
·         Mwanamke hana maamuzi yake binafsi,watoto wa kike hawapati haki sawa na watoto wa kiume.mfano Tendai anaonekana kutofurahishwa na tendo la kuolewa na mume mwenye umri mkubwa (mzee Masasa)alisema “ni heshima kuwa mke wa mtemi mwenye nguvu kama Masasa lakini namchukulia kama baba yangu kuliko mume wangu”.......’’(uk 47) hapa inaonyesha mwanamke hana nafasi ya kuongea kama mtu mwingine.
·          Mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe,hili linaonyeshwa kwa mzee Makwati na Mtemi Masasa kuwa na wanawake wengi kwa ajili ya kujifurahisha na hili linajitokeza bayana pale(uk 40) aliletwa mtoto kumpa joto mzee angehisi msisimko wowote ule wa mapenzi.
·          Mwanamke anachorwa kama mwanamapinduzi ,haya yanajionyesha wazi kwa Sekai na Shingai ni wanawake walioleta mabadiliko katika jamii.mfano Sekai alikuwa wa kwanza kuvunja mila na desturi kwa kukataa Takadini asiuawe na kuamua kutorokea kijiji cha jirani pia alileta mabdiliko akiwa uhamishoni
Shingai naye mwanamapinduzi kwani alipingana na suala kuchaguliwa mchumba aliamini kuwa ndoa ya kweli inahusisha watu wawili waliopendana na waliochaguana alisema “ Si kwamba ninamchukia Nhamo ,la hasha isipokuwa sidhani kama nitakuwa furaha ya kuishi naye”(UK 110)  mwisho mwandishi anaonyesha Shingai ameolewa na Takadini na wamezaa mtoto asiye sope.
5.   UMOJA NA MSHIKAMANO
Umoja na mshikamano ni moja kati ya nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko na ukombozi wa kiutamaduni,mshikamano mzuri ulionyeshwa na mzee Chivero,Tendai,mtemi Masasa ulisaidia kumlinda Takadini dhidi ya unyanyapaa na hatari ya kupoteza maisha katika mapambano yoyote yenye umoja na nguvu utengano ni udhaifu
6.   UJASIRI
Mwandishi ameonyesha kuwa Sekai ni mwanamke jasiri aliepambana kufa na kupona kumlinda mwanae Takadini dhidi ya mila na desturi za kikatili hatima yake kuleta ukombozi katika jamii.
·         Shingai naye ni mwanamke aliyepambana na matatizo ya kuchaguliwa mchumba,mila zinazokandamiza wanawake.
7.   SUALA LA MALEZI
Malezi ya watoto yanapaswa kusimamiwa kwa pamoja yaani baba na mama.Katika kitabu hiki malezi yanaonekana ya upande mmoja mfano Sekai ndio mlezi mkuu wa familia hususani malezi ya Takadini
·         Shingai naye anapata malezi kwa mama,shangazi na bibi hata anapokata shauri la kutorokea kwa Takadini ,anaulizwa kuwa ndivyo ulivyolelewa?mzee Nhariswa anampiga mkewe na kusema “umefanya nini wewe mwanamke tangu mwanao alivyopeleka maji kwa Sekai umefuatilia kujua anachokifanya ...uliona dalili kwanini hukutafuta dawa?
UJUMBE
Ø  Walemavu wana haki sawa ya kuishi kama watu wengine hivyo wathaminiwe.
Ø  Malezi yanahusisha pande zote mbili yaani baba na mama hivyo kila mmoja awajibike.
Ø  Wanawake wawe na maamuzi katika jamii hiyo ili wasinyanyaswe
Ø  Ndoa ni baina ya watu wawili wapendanao hivyo haipaswi kuingiliwa na mtu yoyote
Ø  Umoja na mshikamano ni jambo muhimu katika ukombozi wa jamii yeyote ile.
MTAZAMO WA MWANDISHI
Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu,anaona kuwa matatizo yanayotokana  na mila na desturi yanaweza kukataliwa na watu wengine kwa kuchukua hatua za kujikomboa kama alivyofanya Sekai na wenzake.
MSIMAMO WA MWANDISHI
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameeleza udhaifu wa baadhi ya mila na desturi zinazokandamiza watu hivyo anataka jamii ijikomboe dhidi ya mila desturi hizo.


FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa binadamu wote ni sawa hata kama kuna tofauti za kimaumbile lakini kila mtu ana haki ya kuishi .
MIGOGORO
Migogoro imejitokeza sehemu mbalimbali katika  riwaya hii ya TAKADINI kama ifuatavyo;
Ø  Mgogoro kati ya Makwati na Sekai,chanzo cha mgogoro huu ni  (mila na imani potofu) baada ya Sekai kuzaa mtoto sope,mtoto huyo alipaswa auawe ,mwandishi anasema suala hili halikuungwa mkono na Sekai,suluhisho sekai aliamua kutoroka kijijini ili kunusuru maisha ya mtoto Takadini.
Ø  Mgogoro wa Shingai na wazazi wake,Chanzo cha mgogoro huu ni mila potofu wa kuchaguliwa mchumba ambaye ni Nhamo ambapo  wazazi walikasirika hata kumtolea maneno mabaya,suluhisho ni  Shingai anaamua kutorokea kwa Takadini.
Ø  Mgogoro kati ya Sekai na wake wenzake,chanzo cha mgogoro huu ni Makwati kuzidisha upendo kwa Sekai hivyo waliamini kuwa Sekai ni mchawi
Ø  Mgogoro wa nafsi huu unajitokeza kwa Tendai ambaye aliozwa kwa mzee Masasa ambaye alikuwa na umri mkubwa
Ø  Mgogoro wa kijamii,chanzo cha mgogoro ni kuzaliwa mtoto mlemavu(sope)kulizuka mgogoro baina ya wanajamii ,wao walitaka Sekai na mtoto wake wafukuzwe.
FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa msago (moja kwa moja).Mwandishi ameanza mwanzo kuonyesha mimba ya Sekai ambayo inazua chuki kwa wake wenza pia anapozaa mtoto wa kiume (sope)
v  Sekai anaamua kutoroka ili kuokoa maisha ya mtoto,anaishi ugenini siku nyingi hata sope anakuwa mkubwa na kupata mke na mwisho kabisa mwandishi anaonyesha Sekai akipanga kurudi kwao.
MTINDO
Mwandishi anatumia mtindo wa masimulizi vilevile kuna matumizi ya dayalojia (UK 4)Dadirai na Rumbidzai wanajibizana
Je na yule mbuzi wako uliepewa na baba mzee Makwati amekupa watoto wangapi?
Tangu nimepata ni miaka miwili sasa na tayari ana watoto wawili nabado anatarajia mwingine.
Pia mwandishi ametumia nyimbo (UK 2)
Mashamba yote yamelimwa mbegu zote zimepandwa zimechipua na kumea,sisi watatu tumepata mavuno yetu.,Mheshimiwa wetu amemiliki mavuno kwa mikono yake halisi kutoka mashamba yetu yote lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi ile isiyomea kitu?...........
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha rahisi inayotumika kwa watu wengi,pia ametumia tamathali za semi,nahau,misemo na mbinu nyingi za kisanaa.
MISEMO NA NAHAU
Misemo na nahau imetumika katika riwaya hii ili kuipamba kazi yake
·         “Habari njema kuchechemea kwa mguu mmoja lakini mbaya kukimbia kama sungura.Msemo huu unamaanisha kwamba habari njema hazienei haraka ila mbaya huenea haraka sana
Pia kuna misemo mingi kama
·         Pokea upewacho
·         Maosha ni matamu
·         Kanga hawezi kutua kwenye bua la mtama
·         Mume ni kiungo kwa mwanamke
TAMATHALI ZA SEMI
  Tashibiha
Matumizi ya tashibiha yamejitokeza sehemu mbalimbali
v  Giza jepesi lilibakia ukutani kama mgeni asiyekaribishwa na asiyetaka kuondoka
v  Muda huenda polepole sana mithili ya mwendo wa kakakuona (UK 6)
Tashihisi
Mwandishi wa riwaya ya Takadini ametumia tashihisi sehemu mbalimbal; kama vile’
·         Ubongo wake uliathiriwa kwa mawazo yaliofukuza usingizi wake
·         Fikra zilizopingana zilijichomeka katika nafsi yake
·         Mwanga wa jua ungaavu za novemba uliingia ndani na kulifukuza giza totoro.
Dhihaka
Mwandishi ametumia tamathali iliyoonyesha dharau na yenye lengo la kumweka mtu katika hali duni kupita kiasi lakini kwa mbinu ya mafumbo (uk 2)
v  “Naamini ulichobeba sasa ni mtoto na si dubwasha”
    Haya maneno yalimlenga Sekai kwakuwa siku zote waliamini hazai Tafsida
Mwandishi ametumia tamathali hii kuficha ukali wa maneno (uk 83)
v  Akashambulia hata sehemu za siri (UK 17)walifanya tendo la ndoa
v  Akajivuta karibu zaidi naye chini ya guza hawakuzungumza wakafanya kile ambacho kilitokea kwa asili ya maumbile ,wakakata kiu ya hisia zilizowavuta pamoja miezi mingi (uk 117)
Takriri
v  Wewe ni sope,sope,sope
v  Najua ,najua (UK 79)
Mdokezo
v  Siku moja sijui lini ....lakini hivi (UK 75)
v  Sukuma mara moja tena ....(UK 125)
v  Mtu mzima kama watu wengine na ameoa
WAHUSIKA
 Takadini
·         Huyu ndiye mhusika mkuu wa riwaya hii
·         Ni mtoto wa Sekai
·         Ni mlemavu wa mguu na ngozi (zeruzeru )
·         Kijana wa kiume
·         Ni mchapakazi na anayependa kujituma
·         Ni mtiifu
·         Ni jasiri
·         Ni mwathirika wa mila na desturi mbaya au zilizopitwa na wakati
·         Anafaa kuigwa na jamii
Sekai
v  Ni mhisika mkuu
v  Ni mama yake Takadini
v  Ni mke wa kwanza wa Makwati
v  Mwanamapinduzi
v  Mwathirika wa mila na desturi zilizopitwa na wakati
v  Jasiri
v  Ni mwenye huruma
v  Ni mwenye upendo
Makwati
*      Mume wa Sekai
*      Baba wa Takadini
*      Ni mkali
*      Anapendana na mke wake
*      Anashiriki mila za kale
Chivero
*      Ni mzee wa makamo
*      Ni mganga wa kienyeji
*      Mwenye upendo
*      Mwenye huruma
*      Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa
*      Mpenda mabadiliko
*      Alimpokea Sekai na Takadini
Mtemi masasa
*      Mzee wa makamo
*      Mtemi wa kijiji
*      Mwenye heshima
*      Ni mpole
*      Mwenye huruma
*      Mwenye wake wanne
Shingai
*      Ni binti wa mzee Nhasriswa
*      Mke wa takadini
*      Ni jasiri
*      Mwanamapinduzi
*      Ni msichana mwenye msimamo
*      Mwenye mapenzi ya kweli na takadini
*      Mpenda mabadiliko
*      Ana huruma
*      Anafaa kuigwa

Tendai
*      Mke mdogo wa mzee Masasa
*      Ni mke mkarimu
*      Mwanamapinduzi
*      Ni mpole
*      Rafiki kipenzi wa Sekai
Dadirai
*      Mke wa tatu wa Makwati
*      Ni mwenye roho mbaya
*      Mpenda majanga
*      Ana wivu
*      Ana mawazo potofu
MANDHARI
Mwandishi ametumia mandhari ya kijijini.Mandhari hii inawakilisha vijiji mbalimbali hapa Tanzania na Bara la Afrika.Kwa ujumla mahala ambapo hakuna elimu kuhusu ulemavu wa ngozi haijaeleweka vema au hakuna kabisa.Pia vijiji ambavyo huduma kama shule hakuna
JINA LA KITABU
TAKADINI linasanifu yaliyomo kuwa kuna neno TAKADINI lina maana ya sisi tumefanya nini?Swali ambalo wahusika wengi wanajiuliza mfana Sekai na wanawake wasiozaa na hata vijana au watu wenye ulemavu



Share:

KIDATO 3 $ 4-KISWAHILI-UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA

NGOSWE -PENZI KITOVU CHA UZEMBE
MTUNZI: EDWINI SEMZABA
MCHAPISHAJI:THE GENERAL BOOKSELLERS LTD
CHAPA YA 1-1988

UTANGULIZI
Ngoswe-penzi Kitvu cha Uzembe  inaonyesha namna jamii inapaswa kushiriki mipango mbalimbali ikiwepo ya kisiasa kiuchumi na kiutamaduni.Mafanikio ya mipango hiyo inategemea na kujulikana kwa idadi ya watu utayari,uelewa wa watu hao kuhusu mipango husika
Tamthiliya hii inaonyesha kazi ya kuhesabu watu ilivyokwama kijijini kwa mzee mitomingi ngengemkeni kutokana na uzembe wa afisa wa kuhesabu sensa Ngoswe.
DHAMIRA
1.    MAPENZI
Mwandishi Edwin semzaba ameonyesha jinsi mapenzi yalivyo kitovu cha uzembe,wahusika Ngoswe na Mazoea wametumiwa na mwandishi kufafanua dhamira hii
Ngoswe baada ya kufika kwa mzee Mitomingi anashindwa kuitawala nafsi yake mara anapomuona Mazoea,Ngoswe aliamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Mazoea hali iliyomfanya ashindwe kuimudu kazi yake na mapenzi kwa wakati mmoja.
Ngoswe anamtorosha Mazoea kitendo hiki kinamuudhi balozi Mitomingi Ngengemkeni (baba mzazi wa mazoea)na kuamua kuchoma moto karatasi muhimu za serikali.Ngoswe anaonekani ni mzembe kwa kuwa alishindwa kutofautisha kazi na mapenzi kama msomi (afisa wa sensa )alitakiwa ajue umuhimu wa kazi iliyompeleka kijijini.
2.   ULEVI NA ADHARI ZAKE
Katika tamthiliya ya ngoswe penzi kitovu cha uzembe mwandishi  anaonyesha namna ulevi ulivyoleta madhara,mfano kuchelewesha kazi.Wahusika Mitomingi na Ngoswe wanashindwa kukamilisha kazi kwa vile wahusika (wahesabiwa)wapo kwenye Pombe kama maneno haya yanavyothibitisha;
Mitomingi:Haya ni matatizo yote hii shauri ya pombe nadhani yupo kilabuni
Ngoswe :hawezi kwenda kuitwa?
Mitomongi:haitosaidia mkewe tu hana habari ya kuhesabiwa sembuse hao wengine kwa leo haitowezekana
Licha ya kuchelewesha kazi ulevi huaribu kazi.Mfano:ngoswe anaunguza karatasi za sensa baada ya kulewa pombe ya mnazi.
3.    ELIMU
Elimu ni chombo cha ukombozi kama itatumiwa vizuri ipaswavyo,mwandishi wa tamthiliya hii amemuonyesha kijana Ngoswe (msanii)alivyoshindwa kutumia elimu yake hususani katika kujua namna ambavyo  maisha ya mjini yanavyotofautiana na maisha ya kijijini,Ngoswe anajikuta akiharibu kazi yake kwa kukosa maarifa.
       Mwandishi ameonyesha elimu katika familia ya mito mingi haikupewa thamani yoyote ile wananchi wengi hawakuwa na elimu kwa kisingizio cha shule kuwa mbali,ukosefu wa elimu ulichangia ukosekanaji wa huduma muhimu kama vile hospitali ,miundo mbinu na maji ili kupata maendeleo,suala la elimu lazima litiliwe maanani watu wakieleweshwa wataweza kujua wajibu wao :-
Mfano:kujali kazi na kuacha ulevi “kutumia vema hospitali badala ya kutegemea mitishamba
4.    UCHAWI NA USHIRIKINA
Mwandishi wa tamthiliya hii ameonyesha jinsi watu wengi ndani ya jamii walivyo na imani juu ya uchawi,wanajamii hawa wameweka vikwazo kuhusu sensa wakiamini kuwa mtu anayewahesabu wenzake ni mchawi
Mfano:mama anasema mchawi ndiyo huhesabu watoto wa wenzake ili awaroge sasa wewe ni mchawi? hata kama si mchawi siwezi kukubali unihesabu maana sijui nia yako kama ni mbaya au nzuri.Imani hizo ni za kishirikina zinachangia kukwama kwa zoezi la sensa pia maendeleo kwa ujumla kuwachini,watu wakiugua hawapelekwi hospitali badala yake wanapelekwa kwa mganga wa kienyeji wakidhani kuwa amerogwa.
5. NAFASI YA MWANAMKE
  Katika tamthiliya hii mwanamke ametazamwa katika mitizamo tofauti kama ifuatavyo;
Ø  Mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe,mwandishi amemuonyesha mzee mitomingi kuwa na wake wengi (mitala)bila kuoyesha bayana kazi zao.
Ø  Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na sauti
mfano:Mazoea na mama yake hawakushirikishwa katika mipango ya kutaka kuolewa mazoea kwa vile walionekana hawana mchango wowote katika maamuzi hayo
Ø  Mwanamke amechorwa kama mlezi,
katika tamthiliya hii inamchora mwanamke kama mtu mwenye majukumu ya malezi ya watoto,baada ya Mazoea kuwa na mahusiano na Ngoswe mzee Mitomingi anamlaumu mama yake Mazoea kuwa hakuona dalili ya mahusiano ya kimapenzi kwa kuwa ni jukumu la mama kumwangalia binti yake.
5.   NDOA NA MALEZI
Mwandishi wa tamthiliya hii ameonyesha suala la ndoa ni suala la hiyari na si kufuata matakwa ya wazazi,Mazoea alichaguliwa mchumba na wazazi wake (baba yake)hali iliyomfanya kutoroka na ngoswe
Hali kadhalika katika tamthiliya hii wanaume wengi wana mke zaidi ya mmoja hali hii inapelekea familia kuwa kubwa na kushindwa kuzitunza.
Mfano:Mzee Mitomingi ana wake wawili ambao ni mama Mazoea na mama Mainda,wazazi hawa wanatofautiana katika malezi hasa kwa Mazoea hali iliyopelekea kuwa na tabia mbaya.
 Kwa upande mwingine ndoa zenye mke zaidi ya mmoja haziwi na upendo ndani ya familia hivyo kuwa kikwazo kwenye malezi.
6. UVIVU NA ATHARI ZAKE
   Wanakijiji wa Ngengemkeni mitomingi wengi ni wavivu muda mwingi wanautumia kwenye ulevi na uvuvi,unawafanya wakose huduma muhimu kama shule,barabara na hospitali huduma hizi zingepatikana kama wananchi wenyewe wanajitolea.
   Siku zote wavivu wanatafuta visingizio,vifo vingine vinatokea sababu ya uzembe na uvivu kisha sababu hutafutwa.
   Mfano:wanawake wawili walidai mume wao amerogwa ili hali wenyewe hawakumpeleka hospitali
 MIGOGORO
Ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili zenye mitazamo tofauti Katika tamthilia ya Ngoswe penzi kitovu cha uzembe kuna migogoro mingi ambayo imeweza kujitokeza kama ilivyoonyeshwa na mwandishi
Ø  Mgogoro kati ya Ngoswe na wazazi wa Mazoea chanzo cha  mgogoro huu umetokana na Ngoswe kumtorosha Mazoea,suluhisho wazazi kumfukuza Ngoswe na Mazoea kuchoma karatasi na kumwadhibu Mazoea
Ø  Mgogoro kati ya Mazoea na wazazi wake,chanzo cha mgogoro huu ni baada ya Mazoea kutoroka na Ngoswe ili hali Mazoea tayari ana mchumba wake,suluhisho ni mitomingi kumchapa mazoea na kuchoma karatasi za sensa.
Ø  Mgogoro kati ya Ngoswe na serikali,chanzo cha mgogoro huu ni Ngoswe kuharibu kazi ya sensa na hivyo kusababishia serikali ishindwe kupanga mipango ya maendeleo,suluhisho halijapatikana hadi mwisho.
UJUMBE
Ø  Si jambo zuri kuchanganya suala la kazi na starehe au mapenzi,wakati wa kazi uwe wa kazi na wakati wa starehe uwe wa starehe
Ø  Wavulana wanaovuruga wasichana siku moja watakamatwa na wasichana wenyewe wanapewa tahadhali wasiwe na maamuzi bila kufikilia.
Ø  Elimu ni kitu cha muhimu sana katika jamii na jamii isipokuwa na watu walioelimika hawawezi kuwa na maendeleo maana ili tuwe na maendeleo tunatakiwa tutupilie mbali ulevi na uvivu katika jamii yoyote
Ø  uchawi na ushirikina ni kikwazo kikubwa katika maendeleo
 FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa ni rahisi jamii kuingia kwenye matatizo kama itachanganya mambo mengi kwa wakati mmoja hivyo ikumbukwe kuwa kila jambo na wakati wake.
FANI
Vipengele vya fani katika kazi ya fasihi ni muundo ,mtindo,madhari ,wahusika na matumizi ya lugha
 MUUNDO
Muundo uliotumika katika tamthiliya ni wa muundo wa moja kwa moja ambapo kazi nzima ipo katika sehemu tano ambazo mwandishi amezipa majina ya kitwasira kulingana na ukubwa wa tatizo linalozungumziwa ,yaani ameonyesha kuingia kwa Ngoswe kijijini mazingira yanayoashiria hali ngumu ya maisha(kijito)
Ø  Sehemu ya pili inaonyesha kazi ya kuhesabu watu imeanza na watu hawana utayari na uelewa juu ya sensa (vijito)
Ø  Sehemu ya tatu inaonyesha Ngoswe ameanza kujihusisha na mapenzi na ulevi,ambavyo ni viashiria vya kuharibu kazi yake (mto)
Ø  Sehemu ya nne inaonyesha kazi aliyopewa Ngoswe tayari imekosa mwelekeo,Ngoswe amebobea kwenye mapenzi na ulevi, karatasi zinachomwa moto baada ya kumtorosha Mazoea (jito)
Ø  Sehemu ya tano inaonyesha serikali ikimuhukumu Ngoswe juu ya takwimu zilizoungua moto na Ngoswe asingizia kuwa kijijini kuna shida ya kuhesabu kwani nyumba zimejitenga na watu wenyewe kutoelewa (baharini)
MTINDO
Mtindo uliotumika ni wa kidayalojia ambapo wahusika wake wanazungumza kwa kujibizana
Pia kuna matumizi ya nafsi zote tatu na nafsi hizo zimetumika katika sehemu mbalimbali.Mfano sehemu ya tano kwa matumizi ya nafsi ya kwanza pale Ngoswe anapoulizwa na serikali kuhusu takwimu akajibu “usemi sinao”
 MANDHARI
Kitabu hiki kimejengwa katika mandhari ya kijijini,hii inadhihirishwa na ukosefu wa huduma muhimu kama vile shule hospitali na miundo mbinu
Tabia za wahusika pia zinaonyesha mandhari ya kijijini mfano,ulevi wa pombe za mnazi,watu kutojali elimu,kun’gan’gania mila zilizopitwa na wakati
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha nyepesi na yenye kueleweka pia mwandishi ametumia tamathali za semi,misemo na mbinu nyingi za kisanaa.
Tamathali za semi
Hizi ni semi au kauli zitumiwazo na mwandishi katika kazi ya fasihi ili kuongeza ladha katika kazi husika
Tashibiha
Ni  tamathali ilinganishayo vitu viwili au zaidi kwa kutumia viunganishi kama mithili ya ,kama,mfano wa
Mfano,Ngoswe anaposhangaa ardhi ya kijijini kwa balozi Mitomingi anasema
·         Udongo mwekundu kama ugoro wa sabiani
·         Tazama suruali yake kama kengele ya bomani
·         Nikitoka hapa najitupa kitandani kama gogo
Tafsida
Ni tamathali itumiwayo kupunguza ukali wa maneno
mfano Mainda anasema labda anajisaidia(Uk 21)
Takriri
ni tamathali inayorudiarudia neno ili kuweka mkazo juu ya kile kinachosemwa
Mfano; karibu,karibu(pale Ngoswe alipokuwa akikaribishwa)
Mdokezo
Ni tamathali ambayo hueleza jambo kwa kukatakata maelezo
Mfano Mazoea anasema sijui......sijui......siwezi namwogopa baba (Uk 22)
Tanakali za sauti
Ni tamathali inayoiga mlio wa vitu
mfano Ngoswe alishindwa kujizuia akacheka ha ha ha ha
Methali
Ngoswe anamwambia Mazoea
v  “Penye nia pana njia” (uk 22)
Misemo
v  Hebu keti tutupe mawe pangoni
v  Kupeleka chakula ndio unafanya makambi
Taswira/Jazanda
Taswira mbalimbali zimetumiwa na mwandishi katika tamthiliya hii. Msanii ametumia taswira ya mtu kwa kuhusisha na matukio ya wahusika.Mwandishi analinganisha mwanzo wa mchezo ni kijito ni mto mdogo sana hivyo maelezo ya sehemu hii yanategemewa kuwa madogo sana
v  Sehemu inayofuata ya vijito,sehemu ya vijito inaonyesha kuwa masuala yanashughulikiwa na kujadiliwa hapa yanaongeza uzito ingawa sio mazito sana
v  sehemu  ya mto inaonyesha ukubwa wa shughuli ya Ngoswe yuko kazini (yuko mtoni)tayari yupo ndani ya jukwaa bila shaka maji ya mto ni mengi (matatizo mengi)na hivyo yeyote atakayeingia mtoni yampasa awe mwangalifu
v  sehemu ya jito inaashiria kuna hatari, kuna matatizo mengi, katika jito kulivika si kazi rahisi hatimaye tunaonyeshwa Ngoswe amezama baharini ambapo kuzama kwa Ngoswe ni baada ya makaratasi kuchomwa moto.
WAHUSIKA
Wahusika ni watu walioshiriki katika mchezo au tamthiliya husika.
Mwandishi amegawa wahusika katika makundi mawili yaani mhusika mkuu na wahusika wasaidizi
MHUSIKA MKUU
NGOSWE
Ni msomi anayependa kazi ya kuhesabu watu lakini kutokana na tamaa ya mwili wake anaharibu kazi baada ya takwimu zote kuchomwa moto na Mitomingi kutokana na kitendo cha kujaribu kumtorosha mazoea .
WAHUSIKA WADOGO
Mazoea
v  Msichana mwenye umri wa miaka 18-20
v  Ni mtoto wa balozi (Mitimingi)
v  Anawakilisha wanawake wasio na msimamo katika mapenzi
Ngengemkeni mitomingi
v  Huyu ni balozi
v  Baba yake Mazoea
v  Anachoma karatasi za takwimu kutokana na Ngoswe kutaka kumtorosha Mazoea
v  Ni mzee aliyeshikilia ukale na anapenda ndoa za mitara
JINA LA KITABU
Ngoswe penzi kitovu cha uzembe jina hilo la kitabu linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu ,kwani msanii kwa kiasi kikubwa amejaribu kujadili na kuonyesha matatizo yanayoikumba jamii katika shughuli za kijamii,matatizo hayo ni kama uchawi ulevi uzembe na dhana nyingine potofu



KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Mwandishi katika tamthiliya hii amefeli kwa kuwa ameonyesha matatizo yaliyomo katika jamii bila kuonyesha mbinu mbadala ya kuyatatua.


Share:

ONLINE VISITORS


Labels

Recent Posts